MUSWADA BINAFSI WA BARAZA LA VIJANA LA
TAIFA KUJADILIWA BUNGENI TAREHE 31 MACHI 2015
Nashukuru wote ambao
mmekuwa mkifuatilia hatma ya muswada binafsi wa Baraza la Vijana la Taifa
niliouwasilisha tarehe 31 Oktoba 2013.
Vijana na wadau wa
maendeleo ya vijana mzingatie kwamba muswada huo hatimaye umepangwa kusomwa kwa
mara ya pili na kujadiliwa Bungeni Jumanne tarehe 31 Machi 2015 katika Mkutano
wa 19 wa Bunge.
Muswada huo ulisomwa
kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa 14 wa Bunge tarehe 21 Disemba 2013. Maoni
kutoka kwa wadau yalikusanywa Oktoba 2014 na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Maendeleo ya Jamii.
Baraza la Vijana la
Taifa pamoja na malengo mengine litawezesha vijana kuanzia kwenye vijiji/mitaa
mpaka taifa kuweza kuwa na vyombo vya kuwaunganisha vijana kwa kike na wa kiume
kwa ajili ya maendeleo yao na ya taifa.
Aidha, Baraza hilo
litafuatilia pia kwa karibu utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya vijana ikiwemo
kuhusu ajira, elimu na sekta zingine katika Halmashauri, Serikali kuu, katika
vyombo mbalimbali vya maendeleo na wadau wa maendeleo.
Pia, Muswada huo
utawezeshwa kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na kulipa jukumu Baraza
la Vijana kufuatilia kwa karibu utendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana; kuhakikisha
kwamba fedha zinatengwa za kutosha na kufika kwa walengwa kuwawezesha vijana
kujiajiri, kukuza vipaji vyao na kushughulikia maendeleo yao kwa ujumla.
Kujadiliwa kwa
muswada huo ni hatua ya pekee katika historia ya harakati za vijana nchini kwa
kuzingatia kuwa Sera ya zamani ya maendeleo ya vijana ya mwaka 1996 ilitamka
kwamba kutaanzishwa Baraza la Vijana na
suala hilo kurudiwa katika Sera mpya ya mwaka 2007.
Hata
hivyo Serikali imekuwa ikikwepa kuhakikisha kwamba matakwa hayo ya sera tajwa
yanatekelezwa kwa wakati pamoja na kuwa suala hilo linahusu mustakabali wa
maendeleo ya vijana nchini.
Natambua
mchango wa vijana na taasisi zote za vijana mlioshiriki katika maandalizi ya
muswada huu, unaitwa binafsi kwa sababu tu ndio neno linalopaswa kutumika kwa
mujibu wa Kanuni za Bunge lakini ukweli ni kwamba huu ni muswada wenu; mimi ni
mwakilishi.
John
Mnyika (Mb)
Machi
2015
Kuupitia muswada utakaojadiliwa ingia hapa:
No comments:
Post a Comment