Wosia wa Nyerere na Viti Maalum: Wanaoeneza ukabila wamefilisika kisiasa
Na John Mnyika
Wiki iliyopita nilianza kutoa mtazamo wangu kuhusu suala la ubunge wa viti maalumu. Katika makala yangu iliyopita nilijenga hoja “Viti Maalum:Msekwa na Makamba wapuuzwe Tarime”. Katika mtazamo huo, nilikosoa Sheria yetu ya Uchaguzi ambayo ilitungwa na bunge lililokuwa na wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), chini ya Msekwa kama Spika wa wakati huo. Sheria ambayo inavinyima fursa vyama ya kujua matokeo ya uchaguzi ili kugawa viti hivyo kwa kutoa kipaumbele katika kukubalika kwa chama husika katika maeneo mbalimbali. Hii ni kwa sababu sheria hiyo, ina kifungu kinacholazimisha vyama vya siasa kutangaza wateule wake wa viti maalum kwa kuwasilisha majina Tume ya Uchaguzi kabla ya kura za uchaguzi mkuu kupigwa na matokeo ya ujumla kutangazwa. Dhamira ya sheria hiyo inajichanganya yenyewe, wakati ambapo viti hivyo maalum vinagawiwa kwa vyama kutokana na uwiano wa kura na uwingi ya wabunge wa majimbo, vyama vinalazimika kufanya uteuzi bila kuzingatia uwiano na uwingi huo; hata kama vyama hivyo, vingependa kuweka mambo hayo kama sehemu ya vigezo vyake. Ndio kikwazo kimojawapo ambapo Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) ilikumbana nacho wakati wa uteuzi wa wabunge wa viti maalum mwaka 2005.
Katika mtazamo wangu wa leo, kama nilivyoahidi wiki iliyopita- nitajikita katika kuchambua masuala badala ya kuwajadili wakina Msekwa na Makamba, na kauli zao za kizushi dhidi ya CHADEMA. Masuala ambayo yameibuliwa katika mijadala mbalimbali kuhusu suala hili pamoja na mambo mengine ni tuhuma za uwepo wa ubaguzi, ukabila na upendeleo katika mgawanyo wa viti hivyo. Lakini masuala mazito zaidi, ni mjadala kuhusu dhana na dhima ya viti maalum hususani vya wanawake katika taifa letu katika muktadha wa mfumo wa uwakilishi wa kidemokrasia nchini.
Kwa kuitwa ‘viti maalum vya wanawake’, hakika tayari nafasi hizi zinabeba sura ya upendeleo kabla hata ya uteuzi wenyewe. Na kwa ujumla, vinaweza kutafsiriwa kuwa ni ‘ubaguzi’ kama tutachukua maana pana zaidi ya maneno hayo. Kwa mantiki hiyo, viti hivyo, vinaweza kuonekana kama ni ‘maalumu’, vya ‘upendeleo’ na kwa ujumla vinagawiwa ‘kibaguzi’ kwa wanawake dhidi ya makundi vingine. Vinapatikana kwa ushindani ‘uliofungwa’ miongoni mwa wanawake wengine. Ni watu wenye mtizamo huu mpana ndio ambao wanamsimamo kuwa viti hivyo ‘vifutwe’. Watetezi wa viti hivi wamekuwa wakijenga hoja wakati wote kuwa viti hivyo ni muhimu, kwa kuwa wanawake wamekuwa wakishindwa kushindana na kushinda majimbo na hivyo kufanya uwakilishi wao kuwa duni. Na wanatoa sababu za kihistoria na sababu za vikwazo vya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kama vikwazo vya wanawake kupata nafasi za ubunge. Katika hali hiyo, watatezi hao wanaamini kama uwepo wa viti maalum, ni tiba na daraja la kuwawezesha wanawake kupata nafasi katika siasa.(Affirmative action). Lakini Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) na Wanaharakati wa Haki za Wanawake(FEMACT) wao wamefanya tathmini ya miaka kumi toka viti maalum viazishwe, wakati wa mapitio ya miaka kumi toka tamko la Beijing na kubaini kwamba viti hivi; havijasadia masuala ya wanawake kupewa kipaumbele katika vyombo vya maamuzi, wala havijasaidia kuwezesha wanawake wengi zaidi kuingia katika siasa na kushinda majimboni. Kwa ujumla, viti hivi vinaonekana kuzua ‘upendeleo’, ‘ubaguzi’ nk miongoni mwa wanawake wenyewe na kunufaisha tabaka la wachache. Wapo wenye mtizamo mkali zaidi, kuwa kwa kutengewa ‘viti maalum’, wanawake wanazidi kusukumwa pembezoni mwa mkondo na mfumo wa uwakilishi. Hivyo, mjadala huu unapaswa kuwa mpana zaidi ili kuhakikisha mfumo wa uwakilishi wa uchaguzi na kisiasa mwaka 2010 na kuendelea unatoa tija inayostahiki kwa makundi yote ya kijamii. Nitajadili suala hilo kwa undani wakati nachangia mtizamo wangu kuhusu mjadala wa uwakilishi wa uwiano mintaarafu 50 kwa 50 ulioibuka katika taifa letu.
Nimeacha leo kuingia kwenye mjadala huo mpana zaidi wa kitaifa kwa wasomaji wa mtazamo wangu wa wiki iliyopita, wamenirudisha katika mjadala wa kuhusu Viti Maalumu ndani ya CHADEMA. Wametaka kujua vigezo na mchakato gani ulitumika, na kama kwa maoni yangu palikuwa na upendeleo na ubaguzi wa kikabila wa kuwapendelea wachaga katika uteuzi huo.
Nasikitika kwamba mijadala ya ukabila na udini na kutazamana kwa vigezo hivyo inaanza kushamiri katika taifa letu. Mijadala ambayo isipojadiliwa kwa umakini wake ni chimbuko la kuteteresha misingi ya undugu, umoja na pengine hata amani katika taifa letu. Katika muktadha wa mjadala huu wa viti maalum, nimekuwa nikosoma mitazamo ya wachambuzi magezetini; wengine wakiandika wabunge wa viti maalum CHADEMA wote ni wachagga, wengine wakiandika watano ni wachagga nk.
Ieleweke wazi, ukabila si uwepo wa makabila; maana kama ukabila ungekuwa ni hali hiyo, basi tusingekuwa na haja ya kujadili suala la ukabila katika nchi yenye makabila takribani120. Ukabila, ni uwepo wa ubaguzi kwa misingi kabila. Neno kabila hapa, kila mtu analijua kwa kuwa analo!
Katika hali hii, wengine tunalazimika kuingia katika mijadala ya kutaja watu na matukio; badala ya mijadala ya masuala. Lakini ni muhimu kwa sasa, katika kukabiliana na uzushi na propaganda zenye kuchochea ukabila. CHADEMA ina wabunge sita wa viti maalamu. Halima Mdee, mpare aliyeteuliwa kutoka Dar es salaam, mkazi wa Jimbo la Ubungo. Maulidah Anna Komu, aliyeteuliwa toka Zanzibar; mzaliwa wa Kwabijokha-Tanzania visiwani. Suzan Lyimo, mchagga aliyeteuliwa toka Dar es salaam akiwakilisha Vyuo Vikuu nchini. Lucy Owenya, mchagga aliyeteuliwa toka Kilimanjaro. Grace Kiwelu, mchagga aliyeteuliwa toka Kilimanjaro. Mhonga Said toka Kigoma. Kati mazingira hayo, tunaona kuna wachagga watatu, wao pamoja na wenzao wengine; wameteuliwa si kwa uchagga wao, ama kwa makabila yao; bali kwa vigezo mbalimbali. Ni katika mazingira kama hayo, wengine hatukutia neno pale ambapo Baraza la kwanza la mawaziri la Kikwete lilijaa wachagga wengi na manaibu wenye asili ya Kilimanjaro. Wala siwashangai wananchi wa mikoa mingine tofauti na Kilimanjaro ambayo wabunge wake wa Viti Maalum wa CCM wana asili ya Kilimanjaro. Kwa sababu naamini, sisi sote ni watanzania!
Katika mchakato wa uteuzi wa mwaka 2005 ulianzia kwenye ngazi ya wilaya zao na baadaye kupitia kwenye Kamati Kuu ya chama. Mchakato huu uliongozwa na vipengele vya Katiba ya CHADEMA toleo la mwaka 2004 ambayo ilikuwa ikitumika wakati huo. Vigezo hivyo vilijikita katika kuangalia sifa za uongozi na mchango wa kila mwombaji katika kutimiza wajibu kwa CHADEMA na taifa. Katika mtizamo wangu wa wiki ijayo, nitachambua vigezo hivyo kwa undani, na kuibua pia masuala ya kitaifa; kwa lengo la kutoa mtazamo wangu katika kuboresha mfumo, vigezo na mchakato uwakilishi wa wanawake na makundi mengine katika taifa.
Jambo moja ambalo watanzania ni vyema wakalifahamu; CHADEMA kama chama kinachokuwa. Mwaka 2006 kilifanya tathamini ya chama, na kuandaa Mpango Mkakati wa chama 2006 mpaka 2010. Na kati ya mambo ambayo chama kiliyatazama ni mfumo wa uteuzi wa wanawake wa viti maalum. Pamoja na mafanikio yaliyopatikana, na mchango mzuri wa wabunge wetu bungeni ikiwemo wa viti maalum, palionekana changamoto- namna kati ya kuwianisha mfumo wa uteuzi kwa vigezo na mfumo wa uteuzi kwa kugombea pekee. Chama kiliona kuna haja ya kuboresha zaidi mfumo wake wa uteuzi wa wabunge hawa, na hivyo, CHADEMA ikabadili katiba yake. Sasa katiba imetoa fursa ya kuanzishwa kwa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA), na pamoja na mambo mengine- BAWACHA ndio itayosimamia uteuzi wa wabunge wa viti maalum mwaka 2010, kupitia ushindani wa wanawake wenyewe. Mambo hayo yote yalifanyika kwa uwazi, Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa chama uliofanyika Agosti 13 mwaka 2006, wanaCHADEMA waliungana pamoja mbele ya umma kwa kuwa mkutano huo ulikuwa wazi kwa vyombo vya habari. WanaCHADEMA walikubaliana kutazama mbele kwa Tumaini jipya, ikiwemo katika suala hili la uteuzi wa viti maalum. Mjadala huu, unapoendelezwa mwaka 2008, katika sura ya kuituhumu CHADEMA kwa ukabila, katikati ya harakati za CHADEMA za kupambana na ufisadi na kutetea rasilimali za Taifa. Inanikumbusha maneno ya Mwalimu Nyerere, kwamba ukiona watu waanza kutumia dini au kabila kujihalalisha; ujue wamefilisika kisiasa.
0754694553 na http://mnyika.blogspot.com