Viti Maalum: Msekwa na Makamba wapuuzwe Tarime
Na John Mnyika
Mama yangu aliwahi kuniasa kwamba uongo ukisemwa sana huaminika kuwa ukweli. Lakini baba yangu aliwahi kunieleza pia kuwa siku ukweli ukijitokeza uongo huweza kutahayari, kujificha na wakati mwingine kutoweka. Tutafakari! Hii ni mara yangu ya kwanza kuandika makala ya mtizamo wangu kuhusu suala la viti maalum. Mjadala huu ulikuwa mkali, mwaka 2006 mwanzoni. Mashambulizi yakielekezwa kwa CHADEMA. Wakati huo, nikiwa nauguza majeraha ya ushiriki wangu katika uchaguzi wa 2005 kama mgombea ubunge katika Jimbo la Ubungo.
Halafu ukazuka tena mwaka 2007 mwanzoni; kwa ari, nguvu na kasi mpya wakati huo ukipigiwa debe na makada wa CCM wakiongozwa na Katibu Mkuu wao Bwana Yusuph Makamba, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum kwa kuteuliwa na Rais Kikwete. Ukanyamaza kidogo, na ukarudi tena, wakati wa Uchaguzi wa kuziba pengo la Makamu Mwenyekiti CHADEMA, hii ilikuwa mwishoni mwa mwaka 2007.
Mjadala ukanyamaza tena. Ukaibuka tena 2008 baada ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, kusimamishwa na Kamati Kuu kutumikia nafasi hiyo na kubaki akiitumika CHADEMA akiwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara na Mbunge wa Tarime. Akashika kasi zaidi baada ya Kamanda Chacha kufariki dunia Julai 28, Mungu amlaze mahali pema. Safari hii, ukipigiwa upatu zaidi kwa mara nyingine na Makada wa CCM na wachambuzi wachache hata kufikia hatua ya wanaCCM kusambaza kile walichokiita- Waraka wa Marehemu aliyekuwa kiongozi wa CHADEMA! Katikati ya mjadala huo ambao kitovu kilikuwa CHADEMA palijitokeza pia mijadala mingine ya viti maalumu ambayo haikushika kasi sana. Ule uliotokana na ripoti ya wanaharakati kuhusu miaka kumi ya viti maalum Tanzania. Ule wa kuziba, kiti ya marehemu Amina Chifupa- Mungu amlaze mahali pema. Na ule ulioshikiwa bango hata na Rais Kikwete, kuhusu uwiono wa hamsini kwa hamsini(50-50) bungeni. Nitaeleza sababu katika makala zangu zijazo!
Lakini kilichonisikuma leo, kujitokeza kutoa mtizamo wangu kuhusu suala hili; ni kauli ya Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mzee Pius Msekwa kuwa wanaTarime wainyime kura CHADEMA kwakuwa haina shukrani! Kwamba Mbowe alipewa kura elfu thelathini Tarime, lakini CHADEMA ikafanya ubaguzi na kuacha kuteua Mbunge wa viti maalum mwanamke kutoka Jimbo hilo. Ukistajaabu ya Musa!
Awali uongo kama huu ulikuwa ukisemwa na watu wa jamii ya Mzee Makamba, ambao walifikia hatua ya kutangaza kwamba CHADEMA ni chama cha wachagga. Eti makao makuu ya CHADEMA imejaa wachagga! Wakati Makamba na wenzake wakitoa kauli hizo, kati ya wakurugenzi wa CHADEMA tisa miaka hiyo ya 2005/07 Mchagga alikuwa mmoja tu, Antoni Komu. Huku wasukuma tukiwa wengi zaidi. Baadaye wakaongezeka wachagga wawili, walioteuliwa si kwa uchagga wao wao, bali uwezo wao na utumishi wao; John Mrema aliyekuwa Waziri Mkuu Chuo Kikuu cha Dar es salam, mara baada ya kuhitimu kwake akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri. Na Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Lyimo akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Rasilimali. Hata hivyo, makao makuu ya CHADEMA imeendelea kuwa na wasukuma wengi zaidi. Kwa bahati mbaya, mwaka 2008 propaganda za kikabila zikaendelea kufanywa zaidi, ikafikia hatua hata sisi wasukuma wengine, kubatizwa kabila na kuitwa wachagga. Huku CHADEMA ikiwa na dereva mmoja tu mchagga kati ya madereva wote wa CHADEMA wanaozunguka nchini kufanya kazi za kisiasa, nikashangaa kusoma kwamba madereva wote CHADEMA ni wachagga. Na vyombo vya habari, vichangia kueneza uzushi, ukabila na ubaguzi dhidi ya wachagga. Hakuna mchambuzi aliyekwenda mbali zaidi, kuchunguza na kujua kwamba mtu kama John Mnyika wa CHADEMA ni msukuma aliyezaliwa na familia ya Dalali, ni Mjukuu wa Masalu wa ukoo wa “Inkhamba”! Tuyaache hayo, turudi kwenye mtizamo wangu wa leo.
Wangeendelea kusema wakina Makamba, ningeendelea kunyamaza! Lakini sasa, wamejiingiza katika athari za Lucifer, hata wazee tunaowaheshimu, kama Mzee Msekwa. Kweli sasa CCM imekuwa kokoro. Vijana kama sisi, wanasiasa wa kizazi kipya; kwa kweli hatustahili hata kufungua gidamu za viatu vya kina Mzee Msekwa. Lakini sasa kwa kisingizio cha siasa, wazee wetu hawa wamejishusha na kufikia hatua sasa wanatusukuma kuwapandia vichwani.
Mzee Msekwa niliyemsoma mimi katika vitabu vya historia ya nchi yetu kama mwanasiasa mkongwe na mweledi wa masuala ya kisheria; siamini kama kauli aliyoitoa Tarime amekosea. Nionavyo mimi ni kuwa amedhamiria kupotosha kwa malengo ya kisiasa.
Huyo Mzee Msekwa, aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyepitisha Sheria ya Uchaguzi yenye kuvilazimisha vyama kupeleka Orodha ya majina ya Wateule wake wa Viti Maalum kabla ya kura za Uchaguzi Mkuu kupigwa. Leo anaibuka na kusema uwongo kuwa CHADEMA ilikuwa inajua kuwa Mbowe amepewa kura elfu thelathini Tarime, lakini bado CHADEMA ikaamua kuwanyima wananchi wa Tarime kiti hata kimoja cha Wabunge wa Viti Maalum. Yeye anajua, kuwa CHADEMA ililazimishwa na Sheria kufanya uteuzi kabla ya kujua matokeo, na ikumbukwe kwamba mwaka 2000, CHADEMA haikufanya vizuri Tarime kama ilivyokuja kufanya maajabu Mwaka 2005. Wakati CHADEMA inajua matokeo iliyoyapata Tarime, tayari uteuzi wa Viti Maalum ulishafanyika. Msekwa analijua hilo, mintaarafu mjadala ndani ya CCM na UVCCM kuziba nafasi ya Amina Chifupa aliyekuwa akiwakilisha Vijana; nafasi yake ikaja kuzibwa na Dr Ishengoma wa UWT kwa kuwa tayari CCM nayo ilishalazimishwa kisheria kufanya uteuzi toka kabla ya matokeo ya uchaguzi 2005 na majina yalikuwa Tume ya Uchaguzi(NEC) tayari. Nitaendelea na mjadala huu, nitaachana na wakina Msekwa na Makamba na kujikita katika kujadili hoja kuhusu viti maalumu Tanzania; mpaka kieleweke. Ila ninachoweza kusema kwa sasa, wana Tarime; wapuuzeni watu ambao wako tayari kusema chochote ama kufanya chochote kwa sababu ya uchaguzi. Watu hawa hugueza uchaguzi kuwa uchafuzi, na demokrasia kuwa domo-ghasia!
Mwandishi ni mwanasiasa kijana anayepatikana kupitia 0754694553 na http://mnyika.blogspot.com
No comments:
Post a Comment