Monday, September 8, 2008

Undumilakuwili wa UVCCM

Baada ya waandishi kadhaa kuniomba nitoe maoni kuhusu suala la Nape kuchufukuzwa unachama wa UVCCM niliwaandikia ifuatavyo:

“Awali ya yote nianze kwa kusema kwamba si kawaida yangu kutoa maoni kuhusu masuala ya kawaida ya kiutendaji ndani ya vyama vingine. Hata hivyo, nalazimika kulitolea maoni suala hili kwa kuwa lina mwelekeo wa kuvuka mipaka ya CCM na kugusa maslahi ya vijana wengi nchini na watanzania kwa ujumla. Hii ni kwa sababu, mosi- asili ya mjadala ni Jengo linaloitwa na UVCCM ambalo kimsingi ni jengo liliopaswa kuwa la vijana wote bila kujali itikadi. Pili, uamuzi umechukuliwa wakati ambapo tayari mjadala wa kitaifa ukiwa umeibuka kuhusu tuhuma za ufisadi katika mkataba wa Jengo hilo. Na tatu kauli za Makamba, Kingunge nk ambazo zinaibua mjadala kuhusu aina ya ushiriki wa vijana katika siasa ndani ya chama chao na hata katika taifa kwa ujumla.

Si lengo la maoni yangu kutetea aina yoyote ya ukiukwaji wa maadili na nidhamu ndani ya chama chochote cha siasa iwe ni kwa kusema uwongo, kutokutumia vikao wala kwa kutokuwa na uwajibikaji wa pamoja. Na wala sina nia ya kujiingiza katika mijadala ya makundi yaliyomo ndani ya CCM. Mimi ni mwanachama wa CHADEMA, chama cha demokrasia na maendeleo. Rangi nyeupe katika bendera yetu inawakilisha ukweli, uwazi na uadilifu; hivyo wakati wote hii ndio misingi ambayo wanachama wa Baraza la Vijana wa CHADEMA(BAVICHA) tunasimamia na tuko tayari kuhakikisha misingi hii inasimamiwa popote pale bila kujali itikadi.
Bwana Nape amesimamishwa kwa tuhuma za kusema uwongo, kuhusu mchakato wa Mkataba wa Jengo la UVCCM. Mimi binafsi nimeona nakala ya makubaliano ya mradi wa Jengo ambayo yanamaudhui ya kimkataba. Na kwa maoni yangu, naungana na Bwana Nape makubaliano hayo ni bomu na kwamba yana sura ya mkataba mbovu kama mikataba mingine ambayo Viongozi wa chama chake ikiwemo waliomo katika serikali wamekuwa wakiingia kwenye sekta mbalimbali nchini ikiwemo madini. Na kwa ujumla kuingia makubaliano hayo ni ufisadi na kuendelea kuwaibia vijana wa Tanzania ambao kimsingi jengo lile ni lao kwa kuwa lilijengwa na kodi za watanzania wote bila kujali itikikadi wakati wa mfumo wa chama kimoja na kuporwa na UVCCM baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi. Katika mazingira hayo, kwa maoni yangu badala ya vikao vya UVCCM na CCM ya chama hicho kuendelea kujadili mradi huo, wanapaswa kupitisha azimio la kurudisha jengo hilo serikalini ili litumiwe na vijana wote bila kujali itikadi. Inasikitisha kwamba wakati Idara ya Vijana ya Serikali ikiwa kwenye jengo dogo na bovu, huku vikundi na taasisi nyingi za vijana zikiwa hazina ofisi; UVCCM wanaendelea kung’an’gania mikataba na makubaliano mabovu kuhusu mradi wa Jengo hilo.

Bwana Nape amesimamishwa akiwa ameibua mjadala wa ufisadi ndani ya UVCCM, hali ambayo inabua maswali kuhusu dhamira ya CCM katika vita dhidi ya ufisadi. Nirudie tena, kuna haja ya kutofautisha madai ya uwongo dhidi ya ukweli. Na nimesema wazi kuwa ni kweli kuwa uporaji wa jengo la UVCCM toka kwa wananchi na makubaliano hayo yaliyosainiwa baada ya uporaji huo, ni ukweli wa ufisadi ambao haupaswi kufumbiwa macho na wapenda demokrasia na maendeleo. Lakini kinachosikitisha zaidi ni kuwa Baraza Kuu la UVCCM limekaa katika kipindi ambacho Orodha ya Mafisadi imetolewa na mjadala wa ufisadi umeshamiri katika taifa letu, badala ya UVCCM kutoka na Azimio la kutaka watuhumiwa wa ufisadi kama wakina Lowassa, Chenge nk kuvuliwa uanachama katika chama hicho au walau kuvuliwa nafasi za uongozi kama walivyopendekeza kwa Kamati Kuu kuhusu Bwana Nape. Uamuzi huu wa UVCCM umeendeleza vitendo vya jumuia hiyo kutumika kuwalinda na kuwasafisha mafisadi. Kama hali hii haitabadilika, wasiwasi wa watanzania mbalimbali kuwa chama hicho kinageuka kuwa chama cha mafisadi utazidi kushamiri na hatma ya taifa itakuwa mashakani kama chama kilicho madarakani kwa wakati huu kitakuwa kinaelea vijana wake katika malezi, fikra na maamuzi ya utamaduni wa ufisadi.
Kwa maoni yangu, uamuzi wa UVCCM ni shinikizo toka katika kundi la kina Kingunge, Lowassa, Makamba na Nchimbi ndani ya chama hicho; kwa kuzingatia kauli ambazo viongozi hao wamezitoa kuhusu mradi wa jengo hilo na/ama Bwana Nape. Kauli za Wazee wa chama hicho kama Makamba, Kingunge nk kuwataka vijana wa chama hicho wawe wapole inatishia uhuru, udadisi na ushiriki makini wa vijana katika medani ya siasa. Kauli hizo zinapingana kabisa na dhamira ya Mwalimu Nyerere na misingi ya zamani ya ushiriki wa vijana wakati huo chini ya TANU Youth League(TYL) ambapo vijana walikuwa mstari wa mbele kuhoji. Ni dhahiri kuwa wanasiasa hao wamepitwa na wakati. Lakini kauli zao zinadhihirisha wazi kuwa vijana wadadisi na wapenda mabadiliko hawapaswi kuwa wala kujiunga katika UVCCM. BAVICHA inawakaribisha vijana wote wenye moyo wa uadilifu na kutetea rasilimali za taifa kujiunga na CHADEMA ili kuendeleza mapambano dhidi ya ufisadi na kuleta maendeleo nchini. Aidha kusimamishwa kwa Bwana Nape kumetanguliwa na kauli ya Mzee Kingunge ya hivi karibuni(ambayo hakuitoa ndani ya vikao vya chama chake, lakini hakuitwa kuhojiwa na kuadhibiwa kwa kutoa kauli nje ya vikao kama Bwana Nape); ya kuwakemea wanaokosoa chama hicho na viongozi wake dhidi ya ufisadi. Kusimamishwa kwa Bwana Nape kunapaswa kuwa mwito wa kuamka(wake up call) kwa wapuliza filimbi wote(whirstle blowers) ndani ya chama hicho na serikali juu ya ufisadi ikiwemo baadhi ya wabunge kuwa wanaweza kuchukuliwa hatua; hivyo, ni wakati sasa wa kuchukua hatua zinazovuka mipaka ya CCM. CCM imeanza kujidhihirisha wazi kuwa kina uongozi wenye kulinda ufisadi. Haki za binadamu ndani ya CCM zinalindwa zaidi kwa mafisadi lakini inapokuja suala la kukemea ufisadi wanaokemea haki zao hazilindwi kikamilifu.

Tunapenda kuwakumbusha UVCCM na watanzania kauli ambayo CHADEMA tuliitoa mwaka 2005 kuwa ‘Mabadiliko ya Kweli, hayawezi kuletwa na mafisadi wale wale, wa chama kile kile, chenye uoza ule ule, wakiendeleza yale yale, eti kwa Ari, Nguvu na Kasi mpya. Kwa falsafa ya chukua chako mapema(ccm), Tanzania yenye neema haiwezekani.’
Maoni yametolewa 8/9/2008:

John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana
0754694553

PS: Nimeandika kwa haraka, utafanya uhariri kama kuna makosa ya uchapaji, unaweza pia kushauri itolewe kama makala




No comments: