Thursday, September 25, 2008

Toka Ubungo-Mwito wa kuchukua hatua

Hii imetolewa na Katibu wa CHADEMA Jimbo la Ubungo. Nathibitisha kuwa nitakuwepo kwenye mkutano huo:



25 Septemba, 2008

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
HATUJARIDHIKA NA HATUA ZA SERIKALI KUHUSU KERO ZA WANANCHI

Fedha zilizolipwa Dowans zirudishwe, wahusika wapelekwe mahakamani

Serikali itoe tamko kuhusu madai ya Wafanyakazi kiwanda cha Urafiki ufisadi na maslahi/mishahara duni

Ulipaji wa Fidia Luguruni bado una mapungufu, Serikali itangaze hatua zilizofikiwa kutokana na orodha ya mafisadi ardhi aliyopewa Waziri Magufuli.

Mkutano wa Hadhara kueleza haya kufanyika Kimara 27 Septemba, 2008

Kuzindua kipeperushi cha “Mwito wa Kuchukua Hatua”

Taarifa inatolewa kwa umma kwamba CHADEMA Wilaya ya Kinondoni Jimbo la Ubungo inakusudia kufanya mkutano wa hadhara siku ya Jumamosi tarehe 27 Septemba, 2008 kuanzia saa 9 alasiri katika Kata ya Kimara, Dar es salaam uwanja wa Kimara Matangini Stendi ya Mabasi. Mpaka sasa Mbunge wa Viti Maalum Suzan Lyimo, Mkurugenzi wa Vijana, John Mnyika na Afisa Mwandamizi wa Habari, David Kafulila wamethibitisha kuhudhuria na kuhutubia katika Mkutano huo wa hadhara.

Kama sehemu ya mchakato wa mkutano ya mchakato wa Hadhara na Maandamano, kesho ijumaa 26 Septemba, 2008; Mwenyekiti wa Kamati ya Msukumo Jimbo la Ubungo-Joseph Maserere atazindua kipeperushi maalum cha kutoa mwito kwa wananchi kushiriki kwenye maandamano hayo. Kipeperushi hicho kitakuwa maadhui ya kupinga ufisadi na kutetea rasilimali za Taifa. Uzinduzi huo utafanyika katika ofisi za CHADEMA Jimbo la Ubungo iliyopo Kimara eneo la KONA.

Mkutano huu umepangwa mahususi wa kutoa shinikizo kwa serikali kuhusu masuala mbalimbali yanayowakabili wananchi wa Jimbo la Ubungo na Wilaya ya Kinondoni kwa ujumla kama yalivyojadiliwa na kuazimiwa katika Kongamano la Maendeleo Ubungo lililofanyika Ukumbi wa Kilato, Kimara Jumamosi tarehe 14 Juni, 2008. Mgeni rasmi katika Kongamano hilo alikuwa Mh. Zitto Kabwe(Mb), Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA. Katika Kongamano hilo wananchi kutoka kata mbalimbali za jimbo la Ubungo na maeneo ya jirani katika mkoa wa Dar es salaam walijadili kuhusu kero mbalimbali zinazowakabili wakazi na kufikia maazimio mbalimbali. Taarifa ya kufanya mkutano huo imeshatolewa kwa Serikali za Mitaa, Kata na Polisi na hapajatolewa na pingamizi lolote. Awali mkutano huo ilikuwa ufanyike tarehe 3 Agosti, 2008 lakini uliahirishwa kutokana na msiba wa kitaifa wa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wetu, na Mbunge wa Tarime, Chacha Zakayo Wangwe.

Kongamano hilo lilijadili bajeti ya halmashauri ya Kinondoni 2008/09 na kubaini kwamba bajeti hiyo imeshindwa kukabiliana na kero nyingi za msingi za wakazi, hivyo Kongamano likaazimia kwamba bajeti hiyo ifanyiwe uchambuzi zaidi na ukweli kuhusu bajeti hiyo uweze kusambazwa kwa wakazi wengi zaidi ili waweze kuiwajibisha serikali. Kati ya mambo yaliyojadiliwa katika Kongamano hilo ni pamoja na kuongezeka kwa bei ya umeme kunakochangiwa na mikataba mibovu katika sekta hiyo. Kwa kuwa kampuni ya Dowans iliyorithi mkataba feki wa Richmond ipo katika jimbo la Ubungo, wakazi wa jimbo hilo walioshiriki Kongamano waliazimia mkataba huo uvunjwe, malipo ya milioni 152 yasitishwe, fedha zilizokwishalipwa zirejeshwe, mitambo iondolewe, watendaji wa serikali waliohusika wachukuliwe hatua ikiwemo kupelekwa mahakamani kama sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu suala hilo baada ya ripoti ya Kamati Tuele ya Bunge. Kadhalika Kongamano lilijadili kuhusu migororo mbalimbali ya ardhi na kuweka hadharani tuhuma za ufisadi katika ulipaji wa fidia kwa wananchi wa Eneo la Luguruni Kata ya Kibamba mkoani Dar es salaam. Kongamano liliazimia kuwa serikali iwachukulie hatua watuhumiwa wote wa ufisadi huo na kufanya upya mchakato wa tathmini na ulipaji fidia ili kuhakikisha wananchi wanalipwa haki yao ili kupitisha utekelezaji wa mradi wa maendeleo ya mji katika eneo hilo. Pia Kongamano lilijadili kuhusu haki za wafanyakazi katika wilaya ya Kinondoni hususani jimbo la Ubungo, na katika Kongamano hilo tuhuma za ufisadi katika uuzaji wa nyumba za wafanyakazi, ukodishaji kibiashara badala ya makazi wa maghorofa ya wafanyakazi na mishahara/maslahi duni ya Wafanyakazi wa Kiwanda cha Nguo cha Urafiki ziliwekwa bayana na kujadiliwa. Kongamano liliazimia kuwa kiwanda hicho ni Ubia kati ya serikali ya Tanzania na watu wa China, serikali izifanyie kazi tuhuma hizo na kutoa kauli. Ili kuishinikiza serikali kushughulikia kero hizo Kongamano liliazimia kwamba maandamano ya wananchi yaandaliwe na hivyo Kongamano liliunda Kamati ya Kuandaa Maandamano hayo.

Tarehe 20 Julai, 2008 katika ofisi za CHADEMA jimbo la Ubungo, Kamati ya Kongamano ilikutana na viongozi wa Wilaya ya Kinondoni na Jimbo la Ubungo chini ya uenyekiti wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano, John Mnyika ambaye pia ni Mkurugenzi wa Vijana Taifa kutathmini hatua ambazo serikali imechukua baada ya Kongamano hilo. Pamoja na serikali kutangaza kusitisha mkataba na Dowans, Kikao kilibaini kuwa serikali haijavunja mkataba husika. Bali ilifanya usanii. Hii ni kwa sababu mkataba wa awali uliingiwa Agosti 2006 kwa miaka miwili hivyo, mkataba huo muda wake wa kuisha ni Agosti 2008. Hivyo, kwa kuwa serikali imetangaza kusitisha mkataba kuanzia Agosti, 2008 maana yake ni kwamba serikali itakachositisha ni kuendelezwa kwa mkataba mpya; ndio maana mpaka sasa serikali imeendelea kulipa milioni 152 kwa kampuni ya Dowans. Kadhalika, pamoja na Waziri wa Viwanda, Mh. Mary Nagu kutembelea kiwanda cha urafiki siku chache baada ya Kongamano hakujibu madai ya msingi ya wafanyakazi kuhusu tuhuma za ufisadi na/ama matumizi mabaya ya madaraka katika uuzaji na ukodishaji nyumba za wafanyakazi wala kushughulikia tatizo la mishahara na maslahi duni ya wafanyakazi. Kwa upande mwingine, mara baada ya Kongamano serikali ilianza kufanya uthamini upya kuhusu fidia za wananchi wa eneo la Luguruni lakini mchakato huo bado una mapungufu mbalimbali ikiwemo kutokushirikishwa kikamilifu kwa wananchi, kutokutangazwa kwa kiwango cha fidia kwa mujibu wa bei ya soko, na kutokuelezwa kwa hatua zilizochukuliwa baada ya aliyekuwa Waziri wa Ardhi Mh. John Magufuli kukabidhiwa orodha ya watuhumiwa wa ufisadi katika ulipaji wa fidia katika eneo hilo ambao unahusisha fedha za umma shilingi bilioni tatu. Kwa upande mwingine, pamoja na Meya wa Kinondoni, Mh. Salum Londa kutoa kauli ya kumjibu Mgeni Rasmi wa Kongamano, Mh. Zitto Kabwe, majibu yake hayakujibu mapungufu ya bajeti ya wilaya yake yaliyojadiliwa na wananchi na wala hakujibu hoja ya msingi ya mgeni rasmi ya kutaka aeleze umma ni kwanini bajeti ya wilaya hiyo iliwasilishwa na yeye Meya badala ya Mkurugenzi mtendaji. Suala hili ni la muhimu kwa sababu linahusisha dhana nzima ya mgawanyo wa madaraka(kati madiwani na utendaji) na kuhakikisha uwajibikaji kama sehemu ya mihimili muhimu ya uwajibikaji. Hivyo Kamati ya Maandamano pamoja na Viongozi wa wilaya ya Kinondoni na Jimbo la Ubungo kwa pamoja walikubaliana siku hiyo kwamba kabla ya kufanya maandamano paandaliwe Mkutano wa Hadhara wa tarehe 3 Agosti 2008( ambao sasa utafanyika Jumamosi tarehe 27 Septemba, 2008) katika Kata ya Kimara kuzungumza na Wananchi kwa kina kuhusu masuala hayo ili kuunganisha nguvu ya umma katika maandamano ambayo yatapangwa kufanyika baadaye. Mambo mengine ambayo yaliyokubaliwa kuzungumzwa katika mkutano huo wa hadhara ni pamoja na kupanda kwa gharama za maisha ikiwemo nishati, chakula, nauli nk na haja ya kujenga matatu katika barabara kuu ya Morogoro kupunguza kugongwa kwa wananchi kama ilivyo katika maeneo mengine ya barabara hiyo.

Katika hatua nyingine; tunapenda kuutarifu umma kuwa Jumapili 21 Septemba, 2008 ambayo ilikuwa ni Siku ya Amani na Duniani na pia ni Siku ya Michezo Tanzania; CHADEMA Jimbo Ubungo iliadhimisha siku hiyo kwa kukabidhi Mpira kwa Jumuia ya Waganga wa Tiba Asilia Mburahati. Mpira huo ulikabidhiwa na Kaimu Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Ubungo, Martin Mng’ong’o kwa niaba ya Mkurugenzi wa Vijana, Bwana John Mnyika. Mpira huo ulitolewa na Bwana Mnyika kama sehemu ya kutimiza ahadi yake ya kuchangia vifaa vya michezo kwa jumuia hiyo. Itakumbukwa kwamba katika Kongamano la Juni 14, 2008 Jumuia hiyo ilishiriki, na kutoa mwito kwa umma kuwapatia mpira kwa ajili ya kushiriki kukuza michezo.

Akituma salamu za mshikamano katika kuadhimisha siku hiyo, Bwana Mnyika alisema “ Mpira huo ni ishara ya kwamba kila mdau ana wajibu wa kuunga mkono jitihada za kuboresha michezo. Hata hivyo, pamoja na kuwa na vifaa kuna haja ya kuongeza jitihada za kupata viwanja vya michezo. Hivyo, natoa rai kwa serikali itumie maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Michezo Tanzania. Kutafakari kurudisha kwa umma viwanja vya michezo na maeneo mengine ya wazi ambayo yamejengwa kiholela katika jimbo la Ubungo na maeneo mengine ya mijiji ili kutumika kuweka misingi mizuri ya oganizesheni ya soka. Hii ijumuishe pia kurudisha kwenye halmashauri ama vyama vya michezo, viwanja vya michezo ambavyo vimehodhiwa na CCM vilivyojengwa na michango ya watanzania wote bila kujali itikadi kabla ya mfumo wa vyama vingi kuanza”. CHADEMA Jimbo la Ubungo imefarijika kuwa katika siku hiyo hiyo, ujumbe wa Waziri wa michezo nchini uligusia suala hilo hilo ambalo lilitolewa mwito na Mkurugenzi wa Vijana. Hivyo, tunatarajia hatua za haraka zitachukuliwa kurekebisha hali hiyo.

Wenu katika ujenzi wa Taifa,

Michael Aweda-0754583330
Katibu wa CHADEMA
Jimbo la Ubungo na Wilaya ya Kinondoni

No comments: