Sunday, November 28, 2010

Ujumbe wa Mbunge: Shukrani, Twende Kazi!

Nakushukuru kwa kuniunga mkono katika uchaguzi na kuniwezesha kuwa mbunge wa wote wa Jimbo la Ubungo. Tuendelee kushirikiana kutimiza wajibu katika kipindi cha mwaka 2010-2015 tukitekeleza ahadi jimboni kwa kuweka kipaumbele kwenye Akili, Ajira, Miundombinu, Maji, Uwajibikaji, Usalama, Ardhi na Afya (AMUA) kama ifuatavyo:

AKILI:

Akili na vipaji ambavyo kila mwanadamu amejaliwa ndiyo mtaji mkuu wa kujikwamua kimaisha. Kwa hiyo, tushirikiane kuwezesha elimu bora:

• Tuhakikishe ruzuku ya bajeti ya elimu kwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari, inafika na kuboresha upatikanaji wa vifaa vya elimu na huduma zingine za muhimu.
• Tutumie sehemu ya fedha za mfuko wa kuchochea maendeleo ya jimbo(CDCF) kutoa elimu maalum ya kuwawezesha wananchi kujua haki zao, fursa zilizopo na namna ya kujiendeleza, haswa kwa akina mama, vijana na walemavu. Mfano; haki za mirathi kwa wajane na kukuza vipaji kwa vijana.
• Tuendelee kupigania haki na maslahi ya wanafunzi wote wakiwemo wa elimu ya juu.



AJIRA:

• Tuwezesha kupatikana mitaji, mafunzo ya ujariliamali na kutetea wafanyabiashara na wazalishaji wadogo wadogo wawe na maeneo ya biashara.
• Tuhakikishe vitega uchumi vilivyopo kama kituo cha mabasi Ubungo, Kiwanda cha Urafiki, Songas na kituo cha kiuchumi cha “EPZ”, vinatoa ajira kwa wakazi wa jimbo la Ubungo na kuchangia miradi ya maendeleo.
• Tuchochee uwekezaji na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo ili kupunguza hitaji la ajira hasa kwa vijana.
• Tutetee ujira bora na stahili za wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi kama walimu, manesi, polisi, madereva nk.


MIUNDO MBINU:

• Ili kupunguza msongamano katika barabara kuu, pamoja na mbinu zingine tuhakikishe barabara za pembezoni zinajengwa. Mfano: barabara ya Mbezi-Goba, Kimara-Makuburi n.k. Pia turahisishe usafiri wa maeneo ya pembezoni kwa ukarabati wa barabara na madaraja. Mfano: Golani, Mburahati Kisiwani, Msakuzi, King’ong’o, Kwembe, Makoka n.k

• Tupiganie kupunguzwa kwa gharama za kuvuta umeme kwa kujenga hoja bungeni ili gharama za nguzo na nyinginezo ziwekwe kwenye bili ya mteja kama umeme uliolipiwa. Hii itasaidia wengi kuvuta umeme kwa gharama nafuu.
MAJI:
• Tusimamie uwekaji mabomba katika maeneo yaliyorukwa na kuhakikisha DAWASCO inatimiza wajibu wake wa kuhakikisha maji yanatoka wakati wote.

• Tuhamasishe ujenzi wa visima kwenye maeneo ambayo hayafikiki kirahisi na mtandao wa maji ya bomba kama suluhisho la muda, huku tukifuatilia ufumbuzi wa kudumu katika maeneo hayo.
• Tuhakikishe bei ya maji inayotozwa kwenye Viosk inaendana na viwango vilivyopangwa na mamlaka husika (EWURA).


UWAJIBIKAJI:

• Tupambane na ufisadi kwenye Halmashauri na kuhakikisha fedha nyingi zinazopatikana kila mwaka zinatumika kuwahudumia wananchi, ikiwemo kushughulikia mapungufu yaliyoanishwa na mkaguzi mkuu wa serikali katika vipindi vilivyopita.

• Tuhamasishe wafadhili wa ndani na nje ya nchi kuchangia fedha na rasilimali nyingine za kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wakazi wa Ubungo.

• Tufungue ofisi mbili za Mbunge wa Jimbo la Ubungo, ili kila ofisi ihudumie kata saba. Hii itasaidia wananchi kukutana kwa urahisi na mbunge wao kabla ya kwenda kuwawakilisha kwenye vikao vya bunge.
• Tuzisimamie mamlaka za serikali kutekeleza wajibu wake, mathalani EWURA katika nishati/mafuta, SUMATRA katika usafiri, TANESCO katika umeme, TBS katika ubora wa bidhaa nk



USALAMA:

• Tuhamasishe ujenzi wa vituo vya polisi katika maeneo yasiyokuwa na vituo kama Goba na kupanua vituo vya polisi vilivyopo ili kuviongezea uwezo na hadhi katika kuwahudumia wananchi.
• Tushirikiane polisi na viongozi wa kata/mitaa kuhakikisha doria inakuwepo ili kupunguza vitendo vya wizi, ukabaji na ujambazi hususani kwenye maeneo yenye vitendo vingi vya uhalifu


ARDHI:

• Tuhakikishe wananchi wanapewa fidia wanazostahili katika maeneo yote yenye migogoro ya ardhi kama Kwembe,Kibamba,Ubungo Maziwa n.k
• Tuhakikishe viwanja vya umma vilivyouzwa kinyemela na viwanja vya wazi vilivyovamiwa, vinarejeshwa. Mfano: viwanja vya Makurumla, Sinza, Ubungo, Makuburi, Mbezi nk.
• Tusimamie mpangilio mzuri wa makazi na kuhamasisha upimaji wa viwanja ili wananchi wapate hati na leseni za makazi kwa urahisi na kwa bei nafuu.
AFYA:
• Tuhakikishe wanaoishi na UKIMWI/VVU, Wazee, Walemavu na wagonjwa wa kifua kikuu, wanapata huduma za matibabu kwa wakati na kwa fedha za serikali na wadau wengine wa maendeleo.

• Tusimamie vizuri fedha za bajeti ya afya kwa kuhakikisha zinatumika kuboresha huduma katika zahanati za kata na hospitali ya Mwananyamala inayohudumia pia wakazi wa jimbo la Ubungo.
• Tupiganie ujenzi wa zahanati mpya kwenye uhaba wa zahanati.

Inawezekana, Ungana nami -Shiriki Sasa!! Tuwasiliane; johnmnyika@gmail.com au 0784222222

2 comments:

Anonymous said...

Mheshimiwa Mbunge,

Salaam sana. Ama baada ya salamu niende moja kwa moja kwenye hoja yangu ili nisikuchoshe kwa maneno mengi.

Kuna eneo la kibamba ccm, ni kata ya Ubungo, ila linasomeka kama Mloganzila, wilaya ya Kisarawe. Eneo hili ni kushoto mwa barabara ya morogoro kuanzia kibamba kwa mangi hadi kibamba mwisho. Tafadhali hebu mtupatie ufafanuzi, MPAKA KATI YA KIBAMBA NA KILUVYA UPO SEHEMU GANI?

Shukrani

Anonymous said...

Mh.Mnyika,
Tunashukuru sana kwa mwanzo huu unao uonyesha ni dalili njema.
Lakini naomba sana hoja yangu hii kufanyiwa kazi ni kuhusu kusahaulika kwa Chuo kikuu kiomoja nacho ni Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.Kila mara viongozi wakuu wanapoongelea masuala ya elimu ya juu mara nyingi chuo hiki kinsahaulika kutajwa SI hivyo tu hata bajeti yake ni aibu kwa kweli Pia wanachuo wake upatikani wa mikopo umekuwa wa kutilia mashaka sio wote wapatao ukitilia maanani ada yake ni ndogo sana ukilinganisha na vyuo vingine.
LAKINI wanasahau kuwa chuo hiki kinaweza kudahili wanafunzi wengi sana kwa wakati mmoja na hata kuondoa kabisa tatizo la watu kukosa nafasi za kusoma but hakina walimu wa kutosha na vitabu vimekuwa haba sana JARIBU kutembelea kituo chake kipo UBUNGO hapo pembeni ya Ubungo Plaza.Kuna watu wamelipa ada but hawajapata vitabu kumbukeni kuwa Chuo hiki kiko kila mahali mikoani...HEBU KITUPIE MACHO NA SIE WANACHUO WA CHUO HIKI....OPEN UNIVERSITY OF TANZANIA