Monday, January 10, 2011

Mnyika alia na usimamizi wa maji

MBUNGE wa Jimbo la Ubungo John Mnyika (CHADEMA) amesema usimamizi mbovu wa nishati ya maji unachangia huduma hiyo kutopatika kwa watu wengi zaidi.

Mnyika alitoa kauli hiyo juzi mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea visima na maghati ya maji ambapo alibaini uuzaji wa maji kwa bei kubwa tofauti na ile iliyopangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA).

Alisema asilimia 38 ya wananchi wa jimbo hilo sawa na wastani wa watu wanne wanategemea maji ya vioski na maghati hivyo ni vema kuanzia sasa kukawepo na usimamizi mzuri ili wananchi wengi waweze kuipata huduma hiyo kwa bei nafuu.

Alibainisha kuwa kwa mujibu wa agizo la EWURA, namba 10-017 la Juni 10, 2010 bei ya maji katika mabomba ya jumuiya au maghati ya maji inapaswa kuwa shilingi 20 kwa kila lita 20.

Alisema amepata taarifa kuwa wananchi wanatozwa lita moja kwa shilingi mia moja hadi mia tatu hali inayochangia ugumu wa maisha hasa kutokana kuwa na kipato kidogo.

Aliishauri EWURA kukagua visima na maghati yote ili kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa ikiwemo bei husika kubandikwa kwenye kila eneo ili wananchi watambue haki yao wasitozwe kinyume na viwango vinavyostahili.

Mnyika alisema katika kufanya hivyo lazima EWURA iwahusishe kwanza wananchi na viongozi wa kuchaguliwa ili hatua zozote zinazochukuliwa ziweze kulinda maslahi ya umma.


Chanzo- Tanzania Daima (04/01/2011)

No comments: