Sunday, January 2, 2011

Kauli yangu juu ya tamko la Rais Kikwete kuhusu Katiba Mpya

Mara baada ya hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ya tarehe 31 Disemba 2010 nikiwa safarini nimepokea simu na ujumbe wa simu pamoja na barua pepe toka kwa vyombo mbalimbali, baadhi ya viongozi wa kada anuai na wananchi kadhaa wakitaka kujua msimamo wangu kuhusu kauli ya Rais Kikwete kukubali hoja ya kuandikwa kwa katiba mpya na kutangaza kuunda Tume ya mchakato husika.

Aidha baadhi ya simu na barua hizo zimetaka kujua hatma ya hoja binafsi ambayo nilipanga kuiwasilisha kwenye Mkutano wa Bunge wa Mwezi Februari kuhusu mchakato husika; hoja ambayo nimeshawasilisha taarifa yake ya hoja kwa Katibu wa Bunge.
Katika simu hizo na barua pepe wako baadhi ya watu ambao wamekwenda mbele zaidi kwa kutoa maoni wengine wakitaka bado hoja binafsi iwasilishwe bungeni na wengine wakishauri kwamba sasa nguvu zielekezwe katika Tume iliyotangazwa kuundwa na Rais kuhusu mchakato husika.

Katika muktadha huo nimeona ni vyema nitoe kauli rasmi kuhusu suala husika ili msimamo na maoni yangu kuhusu suala husika ufahamike wa wananchi wa Ubungo na Watanzania wenzangu kwa ujumla kuhusu suala hili nyeti linalogusa mustakabali wa taifa letu.

Natambua tofauti aliyoionyesha Rais Kikwete kwenye jambo hili kwa kutambua haja ya katiba mpya kinyume na kauli za watendaji wake ndani ya serikali za hivi karibuni ( Waziri Kombani, Waziri Mkuu Pinda na baadaye Mwanasheria Mkuu Werema) ambao wote walitaka marekebisho ya katiba kwa kuwekwa viraka mbalimbali.

Aidha natambua kuwa kauli ya Rais Kikwete kukubali kuandikwa kwa katiba mpya inaashiria mabadiliko ya kimtazamo kwa upande wake pia ukilinganisha na kauli zake mbalimbali katika kipindi cha kuanzia mwaka 2005 mpaka mwaka 2010 kuhusu suala la mabadiliko ya mfumo wa utawala katika taifa hali inayoashiria kwamba ametambua kuwa hitaji la katiba mpya ni la watanzania waliowengi ambalo limetolewa kauli na wadau mbalimbali.

Pamoja na kukubali kuandikwa kwa katiba mpya bado watanzania wanahitaji kujadili kwa kina na kwa haraka kuhusu mchakato uliopendekezwa ili taifa liende katika mkondo sahihi wa kuanza kutoa maoni.

Ni muhimu kwa wadau wote kutaka kufahamu muundo wa Tume pamoja na hadidu rejea kwa kina ili kuepuka taifa kuanza mchakato kwa njia isiyo kamili; kinyume na hapo watanzania tunaweza ‘kuuziwa mbuzi kwenye gunia’.

Suala hili ni la msingi kwa kuwa Historia ya Taifa letu inaonyesha kwamba Tume zilizoundwa na Marais na kushughulika na masuala yanayogusa Katiba hazikuweza kukidhi matakwa ya wananchi kwa sababu mbalimbali.

Mathalani, taifa linajadili sasa kuhusu mabadiliko ya katiba kutokana na kasoro katika hatua za awali za kuandikwa kwa Katiba ya Kudumu ya Tanzania ya mwaka 1977 ambayo ndiyo tunayoitumia hivi sasa pamoja na marekebisho yake.
Mchakato uliotumiwa na Rais wa wakati huo, Hayati Julius Nyerere ndio ambao unajitokeza sasa kwenye Hotuba ya Rais Kikwete kwa kueleza kwamba Rais anaunda tume na baadaye mapendekezo ya tume yanakwenda moja kwa moja kwenye vyombo vya kikatiba bila kwanza kuwa na .

Matokeo ya utaratibu huu ni wananchi kutoshirikishwa kwa ukamilifu wake katika maamuzi yanayohusu katiba. Tume ya Rais ya wakati huo iliyokuwa chini ya Thabiti Kombo ilifanya kazi ya kukusanya kwa muda mfupi, matokeo yake yakaenda kujadiliwa kwenye Halmashauri Kuu ya chama tawala wa siku moja, na hatimaye yakapelekwa bungeni na kupitishwa baada ya majadiliano ya muda mfupi sana (kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha kwa saa tatu tu).

Matokeo ya mfumo huo ni kuandikwa kwa katiba isiyokubalika na umma kwa uwingi wake na kusababisha mpaka sasa marekebisho (viraka) mara kumi na nne na bado kuna mapungufu mengi kwa kiwango cha sasa kukubaliana kuandika katiba mpya.
Natambua kwamba Rais Kikwete amesema kwamba Tume itakwenda kukusanya maoni kwa umma, lakini jambo la muhimu sio kupatikana kwa maoni tu, suala la msingi na maamuzi kuhusu ni maoni ambayo ndiyo yanatumika kama msingi wa katiba mpya na makubaliano ya pamoja kuhusu misingi muhimu ya katiba mpya.

Katika mazingira hayo, ndipo panapojitokeza umuhimu wa kuwa na Mkutano Mkuu wa Taifa Katiba kabla ya mapendekezo ya katiba kupelekwa kwenye mamlaka za kikatiba ambazo kwa mujibu wa katiba ya sasa ibara ya 98 ni Bunge pekee. Kauli ya Rais Kikwete inaashiria kwamba wananchi hawatahusishwa moja kwa moja kwenye kuamua katiba badala yake tume itachukua maoni yake na baadaye maamuzi yatafanywa na bunge kwa niaba yao kama ilivyo kwenye marekebisho ya kawaida ya katiba kwa mujibu wa ibara ya 98 ya katiba.

Izingatiwe kuwa kwa sasa Tanzania haifanyi marekebisho ya Katiba bali tunakwenda kufanya mapitio (review) na hatimaye kuwa na katiba mpya; hivyo suala la ushirikishwaji wa umma sio katika kutoa maoni tu bali kuamua misingi muhimu ya katiba ni suala lenye umuhimu wa pekee ili tuwe na katiba inayokubalika na umma mpana isije yakajirudia tena yaliyojitokeza kwenye kuandikwa kwa katiba ya mwaka 1977.
Kutokana na mapungufu yaliyopo kwenye Katiba hii tunayotumia sasa kwenye ibara ya 98 ambapo haijaweka bayana mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya bali mabadiliko ya katiba, ni muhimu kutumia mamlaka ya ibara hiyo ya katiba kifungu cha pili kuwezesha Bunge kutunga sheria itayosimamia na kuwezesha mchakato wa mapitio (review) ya katiba ili kupata katiba mpya.

Sheria hiyo itawezesha kuwekwa utaratibu wa Kongamano/Mkutano wa Taifa, Tume ya Katiba, Bunge Maalum la Katiba na hata kutafakari uwezekano wa kufanya kura ya maoni (referendum) katika masuala nyeti kama Muungano.

Kutokana na kujitokeza bayana kwa mahitaji ya kisheria kuhusu mchakato inaonekana bayana kwamba bado iko haja ya suala hili la mchakato wa katiba mpya kupata uhalali wa umma kwa kurejea ibara 8 ambayo inatamka kwamba madaraka na mamlaka ni umma serikali inafanya kazi kwa niaba na Bunge ndicho chombo kikuu cha kusimamia wajibu huo kwa kutokana na mamlaka ya kikatiba yaliyopo kwenye ibara ya 63(2) na (3) na ibara ya 98 inayohusika na mabadiliko ya katiba.

Katika mazingira hayo nasubiri kwanza ufafanuzi wa serikali kuhusu mchakato husika ikiwemo kujua kwa kina muundo wa tume, hadidu rejea na kama serikali itapeleka bungeni mapendekezo kuhusu mchakato kabla ya kutoa kauli kuhusu hatma ya hoja binafsi ambayo nilitoa taarifa kuwa nitaiwasilisha bungeni katika mkutano wa mwezi Februari.

Na katika kipindi ambacho nasubiria ufafanuzi wa serikali ambao inapaswa kuuweka hadharani nitaendelea na hatua ambazo nilizitangaza nilipokwenda kuwasilisha taarifa ya hoja tarehe 27 Disemba 2010.

Hata hivyo, kutokana na kauli ya Rais Kikwete na hatua za ziada ambazo natarajia kutoka kwa serikali nitatumia wiki ya kwanza ya mwezi Januari kukutana ana kwa ana na baadhi ya viongozi wa asasi za kiraia, taasisi za dini na vyama vya siasa ikiwemo CHADEMA kuweza kushauriana hatua za ziada za kuchukua.

Kimsingi, kama nilivyoeleza awali, hoja hiyo pamoja na kuwa inaitwa hoja binafsi kwa kanuni za bunge ni mimi ni mwakilishi lakini hoja ya umma kutokana na kuwa katiba mpya ni hitaji la wananchi hivyo maamuzi kuhusu hatma ya hoja husika yatafanywa kwa kushauriana na wananchi na wadau wengine baada ya kupata ufafanuzi wa serikali.
Aidha kabla ya wananchi kuanza kutoa maoni kuhusu maudhui (nini kiwemo ndani ya katiba mpya) natoa mwito kwa wadau wote kujadili kwa kina mchakato (taratibu gani zifuatwe) wa katiba mpya; kwa kuwa mchakato usipokuwa sahihi hata maoni mazuri yakitolewa yanaweza yasifikie hatua ya kufanyiwa kazi kwa ukamilifu na hatimaye tukakosa tija ambayo tunaikusudia kwa kuandikwa kwa katiba mpya miaka 50 baada ya uhuru.

Tukumbuke kwamba mwaka 1991 Rais wakati huo Ali Hassan Mwinyi aliunda tume ya kuhusu mfumo wa vyama Tanzania (maarufu kama Tume ya Nyalali) na kwamba tume hiyo ilikuja na mapendekezo mengi ikiwemo la kutaka kuandikwa kwa katiba mpya, lakini serikali ilichukua machache ikiwemo la kuanza kwa mfumo wa vyama vingi. Mchakato tunaotaka kuuanza sasa ungeshakamilika miaka mingi kama mapendekezo ya wakati ule yangetekelezwa kwa ukamilifu wake.

Kadhalika tukumbuke kwamba mwaka 1998 Rais wa wakati huo Benjamin Mkapa aliunda Tume ya marekebisho ya Katiba (Maarufu kama Tume ya Kisanga aliyoratibu maoni kwa kutumia White Paper), hata hivyo sehemu kubwa ya mapendekezo ya Tume hayakutekelezwa. Na Rais wa wakati huo aliikataa hadharani sehemu kubwa ya taarifa yao na kutangaza kuwa tume imefanya kazi kinyume na hadidu rejea. Wakati huo tume ilielezwa kuwa ilikwenda kinyume na maoni ya wananchi lakini kimsingi ni kwamba mapendekezo ya tume yalikwenda tofauti na misimamo ya serikali ambayo ilianishwa bayana kwenye White Paper. Suala hili lilijitokeza kwa kuwa kuwa kwa mujibu wa Katiba ibara ya 37 Rais katika kufanya kazi zake halazimiki kufuata ushauri wa mtu yoyote; hivyo suala la kuwa na mfumo ambao mapendekezo yake yatakubalika na kuheshimika ni la muhimu sana kabla ya kuanza kutoa maoni ya kuingizwa kwenye katiba mpya.

Ndio, maana ni muhimu kwa mchakato wa sasa kufanyika kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na kuwekewa utaratibu bayana ikiwemo kuitaka tume yoyote itayoundwa kutumia mfumo wa Green Paper ili wananchi wenyewe kuanza kutoa maoni yao kuhusu masuala wanayoyaona kipaumbele badala ya kuathiriwa kimsimamo na serikali au tume yenyewe.

Natambua kwamba Rais Kikwete amedokeza kuwa Tume anayotaka kuiunda itahusisha wadau hata hivyo ni muhimu tume ikaundwa katika mfumo ambao ni shirikishi, sio tu wajumbe kuteuliwa kutoka sekta au kada Fulani bali pia kuwe na mashauriano (consultation) kati ya kada au sekta husika kabla ya uteuzi ili kuwe na uwakilishi badala ya wahusika kujiwakilisha wenyewe au kumwakilisha aliyewateua. Ndio maana katika mazingira hayo, tume inayoundwa kwa sheria ya bunge ingekuwa na uzito zaidi na kazi yake kupata kuungwa mkono. Jambo hili ni muhimu kwa kurejea yaliyojiri katika mchakato wa kuundwa kwa Kamati ya Rais ya kupitia upya mikataba ya madini (maarufu kama Kamati ya Bomani); hali hiyo haipaswi kujitokeza sasa katika mchakato wa kuunda Tume ambayo inashughulika na suala tata na tete la katiba mpya ambalo kukubalika kwa mchakato na chombo kinachoratibu ni hatua ya msingi sana katika kuwa na katiba inayokubalika na umma.

Pamoja na njia ya kibunge ambayo niliidokeza wakati naeleza kusudio la hoja binafsi, Rais Kikwete na serikali yake kwa dhamira ya kuhusisha umma katika kuandika katiba mpya kuanzia katika hatua za awali ingeweza kuitisha Kongamano la Kitaifa (National Congress) kujadili tunu za taifa kitaifa, misingi ya kikatiba, muundo/majukumu ya tume ya katiba, kutoa mwongozo wa bunge la katiba na namna ya kufanya kura ya maoni (referendum). Hivyo, kama serikali haitatoa maelezo yanayokidhi haja na hoja bado Bunge litawajibika kutimiza wajibu wake wa kikatiba kwa niaba ya wananchi kwa kurejea ibara ya 63(2) na (3) ili kuweka mchakato muafaka zaidi wa katiba mpya kama sehemu ya kuisimamia na kuishauri serikali inayoongozwa na Rais Kikwete katika hatua hii muhimu ya kuandika katiba mpya- ambayo ni sheria mama na mkataba kati ya wananchi na serikali.

4 comments:

Anonymous said...

ni vyema kuwa na watu makini kama wewe mh. ambaye utawatoa watu kizani na kuwaleta kwenye mwanga!

Msafiri said...

Kwanza nmeridhishwa sana na hoja yako juu ya hili suala.

Pili wakati mwingine ni changamoto za kukabiliana wimbi la mabadiriko ya upepo wa kisiasa. Na wenzetu nyinyi wanasiasa wajanja wajanja kama anavyojaribu kufanya Rais wa NEC.

Kuna mikakati katika ngazi tofauti tofauti. Kiu yetu wengine ni kupata taarifa za maendeleo (development) ili kama tunaweza kutoa michango yetu tutoe yaani tushirikishwe.

Vijana manasema "NAKUAMINIA" na mimi nasema "NAWAAMINIYA" hoja isitekwe nyara

Relief said...

We got your back as long as you lead us through the right path, its not only about constitution its about everything that has to do with this nation's affairs. We invested so much trust on leaders who moved our hearts and minds at the beginning but proved us failure in the end, We do not expect the same from you. May GOD leads you to lead us.

Barton Willilo said...

Kaka nimepitia maoni yako na muongozo wa awali kuhusu mchakato mzima wa kuandika katiba mpya. Umeeleza kwa lugha nyepesi na elekezi. Nashauri taarifa hii uipublish kwenye local news papers ili iweze kuwafikia wengi zaidi. Kwa bahati nzuri mjadala huu tayari tumeshaanza kuujadili katika platform mbalimbali hasa facebook na katika blog mbalimbali. Hata hivyo kutokana na mijadala inayoendelea katika media hizi inaonyesha elimu kubwa itahitajika kuwaelimisha watanzania juu ya swala hili mhimu. Hivyo naomba report yako uipublish magazetini ili na wale wasio na access ya mtandao waweze kupata taarifa hii.