Friday, January 14, 2011

Mnyika ataka Maji yafunguliwe Mbezi

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika amefanya ziara ya ghafla tarehe 3 Januari 2010 ya kutembelea visima na maghati ya maji katika jimbo la Ubungo na kubaini mapungufu katika maghati hayo hususani kuuza maji bei juu tofauti na ile iliyopangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA).

Mbunge Mnyika ameeleza kuwa kwa mujibu wa agizo la EWURA na: 10-017 la tarehe 10 Juni 2010 bei ya maji katika mabomba ya jumuiya au maghati ya maji inapaswa kuwa shilingi 20 kwa kila lita 20, sawa na shilingi moja kwa lita lakini maghati mengi yanatoza kati ya mia moja mpaka mia tatu hali inayoongeza gharama za maisha na kusababisha ugumu wa maisha kwa watanzania wa kipato cha chini.

Mbunge Mnyika ametoa mwito kwa EWURA kukagua visima na maghati yote ili kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa ikiwemo la bei husika kubandikwa kwenye kila eneo ili wananchi watambue haki yao wasitozwe kinyume na viwango vinavyostahili.

Hata hivyo Mbunge Mnyika amesema kwamba katika kufanya hivyo lazima EWURA iwahusishe kwanza wananchi na viongozi wa kuchaguliwa ili hatua zozote zinazochuliwa ziweze kulinda maslahi ya umma.

Mbunge Mnyika alisema kwamba amepokea taarifa toka kwa wananchi kwamba yapo maghati yamefungwa kwa maagizo ya EWURA kutokana na mivutano baina ya DAWASCO, DAWASA na wafanyabiashara binafsi wanaoendesha maghati hayo kuhusu bei ya maji hali ambayo imesababisha baadhi ya wananchi kukosa maji kwa takribani wiki moja.

Mbunge Mnyika ameitaka serikali iingilie kati na kuagiza vioski husika vya maji vifunguliwe ili wananchi waweze kupata huduma hii muhimu ya msingi.

Mbunge Mnyika amesema wananchi hawapaswi kuhukumiwa kwa kunyimwa maji kwa makosa yasiyokuwa ya kwao hivyo serikali kupitia DAWASA na DAWASCO inapaswa kutuma wafanyakazi wake kusimamia vioski husika ili huduma za msingi za maji zikiendelea kutolewa kwa wananchi wakati suala la ongezeko la bei ya maji kinyemela likiendelea kushughulikiwa.

Mbunge Mnyika ameeleza kuwa kwa mujibu wa takwimu za Bajeti ya Kaya asilimia 38 ya wananchi wa Jimbo la Ubungo sawa na wastani wa watu wanne katika kila wakazi kumi wanategemea maji ya vioski na maghati hayo hivyo usimamizi mzuri zaidi unahitajika ili wananchi wasikose huduma za msingi na wasipate kwa gharama nafuu kama ilivyopangwa.

Chanzo: Global Publishers (04/01/ 2011

1 comment:

Unknown said...

Habari mbunge wetu.Mimi ni mwananchi wako toka jimbo la ubungo eneo la kimara VYUMBA VINANE(MAVURUNZA A).Nasikiitika kukujulisha kuwa eneo letu hatuna maji kwa mwaka mzima sasa ilihali tuna mabomba tayari(mabomba ya mchina).chakushangaza ni kwamba,wenzetu eneo hilohilo ng'ambo ya barababara wanapata maji bila zengwe.Kilio changu ni hiki kwa nini wengine wapate maji na wengine tusipate sababu nini?Tunaomba utusaidie mbunge wetu.mimi binafsi nilishaenda pale maji ubungo kuulizia kulikoni wakasema watakuja lakini hakuna mtu aliyekuja.simu yangu ni 0754284492/0732201460,email susan.ngwegwe@gmail.com,susan.ngwegwe@ttcl.co.tz