Katika mkutano wa tatu wa Bunge kikao cha kwanza leo tarehe 5 Aprili 2011 niliuliza swali la nyongeza kutokana na swali la msingi namba 4 kwa ofisi ya Rais Wizara ya utawala bora.
Katika swali hilo niliiuliza serikali itoe kauli kuhusu hatua zilizochukuliwa kuhusiana na Kampuni ya Kagoda Agricultural Limited na kukumbusha kwamba serikali imekuwa ikitoa kauli za mara kwa mara bungeni kuwa uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na vyombo vya kimataifa; niliuliza ni lini uchunguzi huo utakamilika.
Katika majibu yake serikali ilitoa kauli kwamba uchunguzi bado unaendelea. Pamoja na kuwa sikuridhishwa na jibu hilo la serikali, hakukuwa na fursa kwa mujibu wa kanuni kuuliza swali lingine.
Hivyo natoa kauli ya kuitaka serikali itoe tamko la kina kuhusu uchunguzi huo kwa kuwa miaka takribani mitatu imepita toka uchunguzi huo uanze.
Itakumbukwa kwamba Kagoda inatuhumiwa kuchota jumla ya dola za Kimarekani 30,732,658.82 (Sh. 40 bilioni) katika Akanuti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT) mwaka 2005.
Serikali imekuwa ikijichanganya kuhusu ufisadi wa Kagoda mathalani tarehe 15 Septemba 2006 Waziri wa Fedha wa wakati huo Zakhia Meghji aliandika barua kwa wakaguzi wa mahesabu wa kampuni ya Deloitte& Touche ya Afrika Kusini kuwa fedha za Kagoda zilitumika kwa kazi ya usalama wa taifa na kutaka usiri na busara katika ukaguzi wa mahesabu ya kampuni hiyo. Baadaye Waziri Meghji alifuta barua hiyo.
Nyaraka mbalimbali zinaonyesha kwamba cheti cha usajili wa Kagoda kilichotolewa na ofisi ya Wakala wa Usajili wa Leseni za Biashara na Makampuni (BRELA) kinaonyesha Kagoda ilisajiliwa 29 Septemba 2005.
Mpaka sasa siri za ufisadi wa Kampuni hiyo na wa kampuni zingine zilizohusika kwa wizi wa Kagoda zimebaki kwa Rais Jakaya Kikwete na wajumbe watatu wa timu uliyoiunda wakati huo ikiwemo idadi na majina ya watuhumiwa wanaodaiwa kurejesha sehemu ya fedha.
Wakati serikali imekuwa ikieleza kwamba haiwajui wamiliki wa Kagoda; taarifa mbalimbali zimekuwa zikimtaja Rostam Aziz (Mb) na wengine.
Baadhi ya vyombo vya habari vimewahi kuandika kwamba Wakili Bhyidinka Sanze wa kampuni ya mawakili ya Malegesi (Malegesi Law Chambers) ya Dar es Salaam katika maelezo yake kwa Kamati ya Rais ya kushughulikia wizi kwenye akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) alikiri kwamba alishuhudia mkataba wa Kagoda na mikataba mingine iliyohusu ufisadi huo.
Wakili huyo alieleza kwamba mkataba huo ulishuhudiwa na Caspian Construction Limited (inayomilikiwa na Rostam Aziz) iliyopo Dar es salaam na kwamba alielezwa kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuiwezesha CCM kugharamia uchaguzi na kwamba maelekezo hayo yalitolewa kwa aliyekuwa gavana wakati huo (marehemu Daudi Balali) na Rais wakati huo Benjamin Mkapa.
Hata hivyo, pamoja na serikali kwa wakati wote kuendelea kusisitiza kutowajua wamiliki wa Kagoda; Taarifa za hivi karibuni zimemtaja mfanyabiashara Yusuph Manji kupitia kampuni ya familia yake ya Quality Finance Corporation Limited (QFCL) anadaiwa na serikali kurejesha fedha za Kagoda.
Katika mazingira haya ya utata ndio maana natoa kauli ya kuitaka serikali kutoa tamko la kina kuhusu kashfa hii ya Kagoda.
John Mnyika (Mb)
Jimbo la Ubungo
05/04/2011
No comments:
Post a Comment