Aprili Mosi 2011 Rais Jakaya Kikwete alilihutubia taifa na kuzungumzia masuala matatu: shughuli ya kutembelea Wizara na Idara za serikali, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Katiba Mpya.
Katika hotuba hiyo Rais Kikwete alizungumzia kuhusu hali ya umeme nchini na gharama za kuunganisha umeme kama sehemu ya mambo aliyoyatolea maelekezo wakati wa ziara yake katika Wizara ya Nishati na Madini.
Katika hotuba hiyo Rais Kikwete amekiri kwamba serikali yake haina suluhisho lolote la umeme wa dharura kwa ajili ya kupunguza mgawo wa umeme katika kipindi cha sasa mpaka Julai zaidi ya kutegemea kudra ya mvua kuendelea kunyesha. Katika hali hiyo Rais alipaswa kuwawajibisha wote waliochelewesha maandalizi ya kukabiliana na dharura ambayo yalijulikana toka mwaka 2008 na Rais Kikwete amekuwa akiyatolea maelezo na maelekezo toka wakati huo bila kusimamia kikamilifu utekelezaji.
Aidha kauli ya Rais Kikwete kwamba mchakato wa kukodi mitambo ya kufua umeme wa megawati 260 uko kwenye hatua ya zabuni kutangazwa imedhihirisha uzembe kwa upande wa serikali kwa kuwa toka mwezi Februari kauli hiyo hiyo imekuwa ikijirudia hali ambayo inaashiria kwamba mpango huo hautakamilika mwezi Julai mwaka 2011 kama inavyodaiwa. Uamuzi wa kukodi mitambo hiyo ulifikiwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri cha tarehe 15 Februari 2011 ambacho Rais Kikwete alikuwa mwenyekiti wake, Rais baada ya kikao hicho alipaswa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maazimio husika badala ya kusubiri mpaka kutoa maagizo mengine kwenye ziara ya wizarani mwezi Machi mwishoni. Hali hii itapelekea taifa kulipia baadaye mitambo ambayo haitatumika kikamilifu katika kipindi chote cha dharura kama ilivyotokea katika kashfa ya Richmond/Dowans.
Kadhalika kauli ya Rais Kikwete imedhihirisha kuwa serikali yake imeshikilia msimamo wa kukodi mitambo ambayo itatumika kwa kipindi cha miezi sita pekee kwa gharama za zaidi ya bilioni 400 badala ya kuweka mkazo katika kununua mitambo kama ambavyo imeshauriwa na wadau mbalimbali. Ni muhimu kwa Wizara husika kuueleza umma kiwango cha fedha ambacho kitatumika katika mpango huu ambacho kimsingi kitazidi kuongeza mzigo wa madeni kwa TANESCO.
Pia, serikali ieleze maandalizi ambayo yamekwishafanyika mpaka hivi sasa kukabiliana na tatizo la upatikanaji, usafirishaji na uhifadhi wa mafuta mazito (HFO) ambayo yatahitajika kwa kiwango kikubwa katika kuendesha mitambo hiyo katika mikoa itakayowekwa mitambo hiyo. Jambo hili ni muhimu kwa kuwa katika mazingira ya sasa serikali inashindwa kukabiliana vya kutosha na mahitaji ya mafuta mazito kwa mitambo ya megawati 100 ya IPTL iliyopo Dar es salaam ambayo hutumia takribani bilioni 15 kwa mwezi kwa mafuta pekee.
Kwa upande mwingine, naunga mkono kauli ya Rais ya kuwataka TANESCO kuangalia kwa haraka namna ya kupunguza gharama kubwa za kuwaunganishia umeme wateja jambo ambalo nimekuwa nikitoa mwito kwa serikali kulifanya toka mwaka 2010. Natambua kwa Rais Kikwete amekubaliana na pendekezo la kuwaunganishia watu umeme na kuingiza gharama hizo katika bili ya umeme kidogo kidogo hata hivyo ni muhimu pendekezo hilo likaambatana pia na utaratibu ambapo wananchi wanapogharamia wenyewe vifaa kama nguzo za umeme basi gharama hizo warejeshewe kupitia punguzo katika malipo ya bili zao kama umeme uliolipiwa kabla kwa kuwa miundombinu hiyo hubaki kuwa mali ya TANESCO.
Hatahivyo, pamoja na kutoa kauli kwa TANESCO Rais Kikwete alipaswa kuwaeleza watanzania namna serikali yake ilivyojipanga kuipunguzia mzigo wa madeni TANESCO kutokana na madeni ambayo serikali inadaiwa na pia mzigo mkubwa ambao TANESCO inaubeba kutokana na mikataba mibovu ya kifisadi ambayo serikali iliingia. Kuwepo kwa gharama kubwa ya kuunganisha umeme na bei ya umeme wenyewe ni matokeo ya mzigo wa madeni na ufisadi katika mikataba kubebeshwa wateja waliopo. Sekta ikiwemo umeme imegubikwa na rushwa na ufisadi mkubwa ukihusisha viongozi wa juu wa Serikali tangu mwaka 1991, wakati wa IPTL ambayo inaendelea kuitafuna nchi hadi leo. Pamoja na kashfa ya Dowans/Richmond mwaka 2006 serikali iliingia mkataba na Alstom Power Rentals kuzalisha umeme wa dharura Mkoani Mwanza na kampuni hiyo kulipwa bilioni takribani 40 bili kuzalisha umeme wowote. Hivyo natoa mwito kwa Serikali kupitia upya haraka mikataba ya umeme hapa nchini ambayo imeliingiza taifa katika fedheha na hasara kubwa, ikiwemo mikataba ya IPTL na Songas,Artimas,Tanpower Resources /Kiwira, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kishera na kinidhamu patakapobainika uzembe au ufisadi wowote kwa wote wanaohusika, kwa mikataba iliyoisha lakini ambayo iliingiza nchi katika hasara kubwa kama sehemu ya mkakati wa kupunguza gharama za umeme nchini Tanzania.
Nilitarajia pia Rais Kikwete angetumia hotuba hiyo kueleza kwa umma maelekezo ambayo ameyatoa kwa Wizara ya Nishati na Madini kuhusu sekta ndogo ya mafuta hususani yanayohusiana na ubora na bei ya mafuta ikiwemo mkakati wa kupunguza tozo na kodi ili kupunguza gharama ambazo zinaongeza ugumu mkubwa wa wananchi hivi sasa. Kwa ujumla, maagizo ambayo Rais Kikwete ameyatoa mengi ni yale yale ambayo amekuwa akiyatoa kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2006 mpaka 2010, hivyo wakati umefika sasa kwa Rais kusimamia kikamilifu utekelezaji wa masuala ambayo baraza la mawaziri ambalo yeye ni mwenyekiti wake ndicho chombo cha haraka zaidi kinachopaswa kuongeza ufanisi. Mfumo wa utawala unaotumiwa na Rais Kikwete wa kuzunguka (Management By Walking Around-MBWA) hauwezi kuleta tija ya kutosha ikiwa Rais Kikwete hataweka mkazo katika mifumo ya kiutawala inayozingatia malengo na matokeo (Management by Objectives and Results).
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli-Nishati na Madini
02/04/2011
No comments:
Post a Comment