Friday, July 15, 2011

Hotuba Mbadala Wizara ya Nishati na Madini

HOTUBA YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI NA MADINI MHE. JOHN JOHN MNYIKA (MB) KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2010/2011 NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012 UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika; awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwasilisha maoni haya ya kambi rasmi ya upinzani kuhusu makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012 kwa mujibu wa kanuni za Bunge (Toleo la mwaka 2007) kifungu cha 99 (7) ikiwa ni sehemu ya kuchangia katika wajibu wa bunge wa kuishauri na kuisimamia serikali.

Mheshimiwa Spika; Nawashukuru wananchi wenzangu wa jimbo la Ubungo kwa kuniamini bila kujali tofauti zingine na kunituma kuwawakilisha kwa kunitunuku heshima ya kuwa mtumishi wa umma. Nawashukuru pia kwa kunipa madiwani wa kufanya nao kazi. Asanteni wazee kwa busara zenu, wanawake kwa sala zenu na vijana wenzangu tuliokuwa pamoja kipindi cha kampeni na kukesha wote Loyola katika kulinda ushindi.

Tumeandika historia kwamba hakuna hujuma inayoweza kudhibiti nguvu ya umma (people’s power) mabadiliko yameanza kuonekana na kwa pamoja tuendelee kutimiza wajibu kwa kurejea dira yetu: A.M.U.A; Maslahi ya Umma Kwanza.

Mheshimiwa Spika; Nawashukuru wanafamilia yetu ya Dalali; wazazi wangu na ndugu zangu kwa upendo wenu ambao umechangia katika furaha yangu na motisha ya kuendeleza ujasiri na uadilifu katika kusimamia ukweli, haki na ustawi.

Mheshimiwa Spika; Natambua kwa shukrani mchango wa viongozi wenzangu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) makao makuu, Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum Dar e salaam, Jimbo la Ubungo na wa kambi rasmi ya upinzani bungeni katika hatua ambayo tumefikia; mahitaji na matumaini ya watanzania yanatutaka tuendelee kuongoza kwa umoja, umakini na uwajibikaji mpaka kieleweke dhidi ya ubinafsi, uzembe na ufisadi ambao unazidi kushamiri katika taifa letu.

Mheshimiwa Spika; Nawashukuru wote katika mamlaka ambao mmenipa ushirikiano kwenye serikali kuu, manispaa ya Kinondoni, katika kamati ya nishati na madini na wabunge wengine kwa ujumla katika kutekeleza majukumu ya kibunge kwa manufaa ya taifa letu na watu wote.

Mheshimiwa Spika; Wizara ya Nishati na Madini ambayo tunatolea maoni bajeti yake leo ni wizara nyeti sana katika taifa letu nyakati za sasa na kwa vizazi vijavyo. Sekta ya nishati ni moyo wa taifa wakati madini ni mtaji wa nchi yetu.

Tanzania imejaliwa rasilimali nyingi watu, ardhi yenye rutuba , maji (bahari, mito na maziwa), kuwa katika eneo la kimkakati la kijiografia kwa biashara, mali asili ikiwemo za utalii na madini. Hata hivyo, tunaelekea kuwa na laana ya rasilimali hali ambayo inafanya wananchi walio wengi kuendelea kuwa katika lindi la umasikini na wakiendelea kusukumwa pembezoni nje ya urithi ambao taifa linao.

Mheshimiwa Spika; Tishio la usalama na amani katika taifa letu kwa sasa sio migomo wala maandamano bali ni migogoro inayoendelea ya kirasilimali maeneo mbalimbali ya nchi ambayo ni bomu la wakati litakalolipuka iwapo kasi ya ukuaji wa uchumi wenye kutoa fursa kwa wengi haitaongezwa. Sekta ya nishati ni moyo wa kurekebisha hali hii na sekta ya madini ni mtaji wa kufanikisha dhamira hiyo.

Mheshimiwa Spika; tunakutana leo ikiwa ni miezi michache kuelekea kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru taifa likiwa gizani kutokana na mgawo wa umeme unaoendelea, idadi ndogo ya watanzania waliounganishwa kwenye gridi ya taifa na matatizo ya sekta ya nishati kwa ujumla. Tunakutana wakati ambao urithi wetu mkuu ambao mababu zetu waliupigania wakati wa kudai uhuru; ardhi na rasilimali zake ikiwemo madini ukiwa mashakani kutwaliwa na kutawaliwa kwa ubeberu mamboleo.

Mheshimiwa Spika; Mnamo tarehe 21 Juni 2011 Bunge lilipitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2011/2012 ambapo wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani tulipiga kura ya HAPANA; lakini ikapita kutokana na uwingi wa wabunge wa upande wa pili bila kuzingatia maslahi ya umma.

Tulipiga Kura ya HAPANA kwa kuwa ilikuwa ni bajeti yenye maneno matupu bila matendo katika mipango na utekelezaji; athari za bajeti hiyo zimeshaanza kudhihirika kwenye uchumi wa nchi na maisha ya wananchi wa kawaida. Bajeti ya mwaka 2011/12 ilielezwa kwa maneno matupu kuwa imeweka nishati kuwa ni kipaumbele cha kwanza. Hata hivyo vitabu vya Bajeti ya Serikali iliyopitishwa vinadhibitisha ukweli mchungu kwamba jumla ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya nishati na madini ni bilioni 539.3 tu.

Kwa mujibu wa Vitabu vya Bajeti ya Serikali 2011/2012 iliyopitishwa, Wizara ya Nishati na Madini imetengewa jumla ya shilingi 402.4 bilioni kwenye Fungu 58. Fedha hizo zimegawanywa katika mafungu ya Matumizi shilingi 76,953,934,000 na bajeti ya Maendeleo zimetengwa shilingi 325,448,137,000 tu. Fedha nyingine kidogo za maendeleo bilioni 126.6 zipo kwenye Fungu la 50 miradi ya MCC kwa kutegemea wahisani.

Hivyo; bajeti hii haijaichukulia kwa uzito unaostahili sekta za nishati na madini hususani umeme hali ambayo inaibua maswali iwapo serikali ina dhamira ya dhati ya kukabiliana na changamoto za msingi zinazolikabili taifa hivi sasa.

Mheshimiwa Spika; kambi rasmi ya upinzani imepitia kitabu cha pili cha matumizi ya kawaida ya Wizara ya Nishati na Madini ( Volume II Supply Votes) Fungu la 58 vifungu 1001-1009, 2001-2012 na 3001 na kubaini kwamba hii ni bajeti ya mgawo mkubwa wa posho na ufujaji. Mathalani Idara ya Kitengo cha Mawasiliano katika kulipana posho zitatumika Sh. Milioni 405.62 sawa na asilimia 63% ya fedha yote iliyotengwa Sh. Milioni 641.99 kwa idara hii.

Idara ya fedha na uhasibu itatumia Sh milioni 598.49 sawa na asilimia 42% ya fedha yote iliyotengwa. Kanda ya Ziwa – Mwanza kulipana posho inatumia Sh. milioni 389.68 sawa na asilimia 40% ya fedha yote iliyotengwa. Kuna posho kuwanunulia mavazi wafanyakzi wanao safiri nje ya nchi, sherehe na maonesho, chakula na vinywaji, huduma kwa wageni, posho za kukaimu nafasi na posho nyingine.

Kwa ujumla Wizara ya Nishati na Madini inakadiriwa kutumia Sh. Bilioni 7.9 kulipana posho na matumizi mengine ya kawaida ya anasa. Kwani jumla hii ni nje ya posho za msingi kama vile; posho za uhamisho, posho za mafunzo, nyumba, maji na umeme.

Kambi Rasmi ya Upinzani inataka serikali ifanye marekebisho kwenye bajeti ili fedha hizi zipunguzwe ziweze kuongezwa kwenye kuongeza ujenzi wa miundombinu wa Chuo Cha Madini Dodoma na na kuongeza kiwango cha fedha katika mfuko wa wachimbaji wadogo wa madini. Aidha yako matumizi mengine ya ujenzi wa maofisi na gharama kubwa za kisheria ambayo yanapaswa kuhamishiwa katika miradi muhimu ya maendeleo ikiwemo ya umeme vijijini.

Mheshimiwa Spika, Ikumbukwe kwamba tarehe 15 Juni 2011 Kambi ya upinzani iliwasilisha bajeti mbadala ambayo ilitenga fedha za kutosha katika kukabiliana na changamoto za sekta za nishati na madini. Bajeti mbadala ilitenga fedha za maendeleo Sh. Bilioni 977 kwa ajili ya Wizara ya Nishati na Madini ukilinganisha na ile serikali iliyotenga Sh. Bilioni 452 kwa maendeleo (Fungu 58 na 50); ambayo ni sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 100 (100 %).

Kambi rasmi ya upinzani inataka kiwango cha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kuongezwa ili vipaumbele vifuatavyo viweze kuzingatiwa kwa uzito unaostahili: · Kuwekeza fedha za kutosha kwenye sekta ya umeme na Gesi ili kumaliza kabisa tatizo la nishati ya Umeme na kupunguza gharama za maisha. Hatua hizo ziambatane kuwekeza katika Bomba la Gesi kutoka Mtwara, pamoja na ujenzi wa mtambo wa kutengeneza Gesi (LPG extraction Plant) ili kuwezesha gesi kutumika kwenye magari, viwandani na majumbani. ·

Kuhakikisha tunazalisha 360MW za umeme kila mwaka ili kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo wa miaka Mitano na kumaliza tatizo la mgawo wa umeme. Kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya usafirishaji na usambazaji wa umeme vijijini ili kuchangia katika ukuaji wa uchumi vijijini.

Mheshimiwa Spika; Tunatambua kwamba wakati wote serikali imekuwa ikitoa visingizio kuwa kiasi cha fedha kilichopo ni kidogo na hivyo kutegemea zaidi fedha za wahisani. Hivyo, kambi rasmi ya upinzani imewasilisha vyanzo vya mapato ambavyo vinaweza kutumika kuongeza kiwango cha bajeti kwa ajili ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini. Baadhi ya misingi muhimu ya mapato ambayo tumeiwasilisha ni pamoja na: · Kupunguza misamaha ya Kodi ikiwemo kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta Kampuni za Madini peke yake kutaongeza mapato ya shilingi bilioni 59. ·

Kutoka Vyanzo vipya vya mapato tulivyovianisha; kwa upande wa sekta ya madini kwa Kurekebisha Kodi Sekta ya Madini peke yake tunaweza kukusanya shilingi bilioni 240 katika mwaka wa fedha 2011/2012. · Kupunguza fedha kwenye Wizara zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida yasiyokuwa ya lazima na kuelekeza fedha katika miradi ya maendeleo hususani ya umeme na gesi.

Mheshimiwa Spika; katika muktadha huo pamoja na kifungu cha 106 cha Kanuni za Bunge kutenguliwa kuruhusu sheria ya fedha 2011 kupitishwa tarehe 22 Juni 2011; ni muhimu mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini uhusishe pia kupitia kitabu cha kwanza cha mapato (Volume 1- Revenue Estimates) ili kuongeza wigo wa mapato.

Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuzingatia maoni na mapendekezo yanayoendelea kutolewa na kuwasilisha marekebisho (amendments) ya sheria ya fedha ili kuongeza wigo wa mapato. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka kuwasilisha bajeti ya Nyongeza (Supplimentary budget) kwa ajili ya Wizara ya Nishati na Madini ili kuwa na makadirio ya nyongeza ya matumizi kwa mujibu wa kanuni 107 kwa ajili ya miradi ya umeme na gesi asilia.

Umeme Mheshimiwa Spika; Tatizo sugu la mgawo wa umeme ambalo sasa limekomaa na kuwa janga la taifa limetokana na ufisadi na udhaifu wa kiuongozi na kiutendaji ambao umeikabili sekta ya nishati nchini kuanzia awamu ya pili, likaongezeka katika awamu ya tatu na kukomaa katika awamu ya nne ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ufisadi na udhaifu huo wa kiutendaji unajidhihirisha zaidi katika maamuzi mbalimbali yaliyofanyika awamu ya pili hususani 1990 mpaka 1995; awamu ya tatu hususani 1996 mpaka 2004 na awamu ya hususani 2006 mpaka 2011 kwenye maamuzi na mikataba mbalimbali mathalani kashfa ya IPTL, hasara ya mchakato wa ubinafsishaji wa TANESCO, uzembe wa Net Group Solution, ufisadi wa Kiwira, kashfa ya Alstorm Power Rentals, sakata la Songas/Pan African Energy, ufisadi wa Richmond, madhara ya Dowans (ambayo sasa mitambo yake iko chini ya Symbions bila serikali kutoa kauli, kashfa kuhusu mitambo hiyo zimekwisha baada ya umiliki kuhamia kwa kampuni ya Marekani na iwapo taratibu za zabuni zilifuatwa) ambapo mkazo haukuwekwa katika mipango ya muda mrefu ya kuondokana na tatizo la mgawo wa umeme nchini ambayo imetajwa bayana katika nyaraka mbalimbali za mipango ya kiserikali.

Mheshimiwa Spika, Pamoja na maamuzi ya Bunge la tisa ya kuhusu masuala hayo bado kambi ya upinzani inataka hatua kamili kuchukuliwa kwa wahusika wa kashfa hizo kama walivyotajwa kwenye orodha ya mafisadi ili kujenga msingi wa kuepusha hali kama hiyo kujirudia katika uwekezaji unaondelea hivi sasa.

Mheshimiwa Spika,athari za upungufu wa umeme kwenye uchumi wa nchi na maisha ya wananchi ni makubwa sana. Taarifa za Serikali zinaonyesha kwamba Mamlaka ya Mapato inapoteza mapato ya Bilioni 840 kwa mwaka kutokana na mgawo wa umeme na ripoti za wadau wengine zimeeleza bayana upungufu wa ajira unaosababishwa na mgawo wa umeme.

Mheshimiwa Spika; Ikumbukwe kwamba katika mkutano wa pili wa Bunge kikao cha sita tarehe 15 Februari 2011 Waziri wa Nishati na Madini alitoa kauli bungeni kuhusu mipango ya dharura ya serikali kupunguza tatizo la mgawo wa umeme. Kati ya hatua ambazo zilielezwa ni ukodishaji wa mitambo ya dharura ya MW 260 na kuongeza matumizi katika mitambo ya IPTL.

Kambi rasmi ya upinzani imefadhaishwa na taarifa iliyotolewa kwa umma na TANESCO wakati wa kuanza kwa mgawo wa umeme unaoendelea hivi sasa kuwa umechangiwa na mitambo ya IPTL kuzalisha chini ya kiwango kutokana na upungufu wa mafuta mazito (HFO) suala ambalo linatosha kwa serikali kuwajibika kutokana na uzembe wenye kulitia hasara taifa kwa sababu suala hili lilikuwa likijulikana kwa miezi mingi bila hatua stahili kuchukuliwa.

Mheshimiwa Spika; Tarehe 1 Aprili 2011 Rais Jakaya Kikwete alitoa ahadi kupitia hotuba yake kwa taifa kwamba mitambo ya MW 260 ingekodishwa na kuanza kufanya kazi mwezi Julai kukabiliana na mgawo wa umeme.

Kambi ya Upinzani haijaridhika na visingizio ambavyo vimekuwa vikitolewa na serikali kwa kutumia sababu za matatizo ya nje ya nchi kuelezea uzembe wa kiutendaji wa kushindwa kusimamia maamuzi ya ndani na inaitaka Wizara ya Nishati na Madini ieleze kwa uwazi na ukweli sababu za kuchelewa kwa mpango huo na hivyo kuongeza kwa kiwango kikubwa muda na kiwango cha mgawo wa umeme unaoendelea hivi sasa.

Mheshimiwa Spika; kwa upande mwingine mgawo wa umeme unaoendelea hivi sasa ni matokeo ya serikali kushindwa kutekeleza kwa wakati mpango wa kuweka mitambo ya MW 100 Ubungo (Dar es salaam) na MW 60 Nyakato (Mwanza) ambayo iliwekwa kwenye mpango wa umeme wa mwaka 2009 ambao ulicheleweshwa na hatimaye wakati wa Bajeti ya mwaka fedha 2010/2011 Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na Madini wote waliahidi kukamilisha uwekaji wa mitambo hiyo mapema mwaka 2011. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ieleze sababu za kuchelewa kutekelezwa kwa mpango huo na hatua za uwajibikaji zilizochukuliwa kutokana na udhaifu huo.

Mheshimiwa Spika; Ni aibu kwa taifa kuendelea kutegemea vyanzo ambavyo vilianzishwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza iliyoongozwa na Hayati Mwalimu Nyerere na awamu zilizofuata sio tu kushindwa kuongeza kasi ya kuzalisha umeme bali pia kushindwa kukarabati mitambo hiyo na hivyo kuzalisha chini ya kiwango. Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2010 inaonyesha kuwa vituo vyetu vya umeme vinazalisha 3694.74 jigawati kwa saa yaani MW 421.8 sawa na asilimia 53.5 ya uwezo wa vituo hivyo MW 788.68.

(Rejea Kielelezo cha Pili). Sababu zinazotolewa za uzalishaji kidogo ni uchakavu wa mitambo na ukame unaoliathiri taifa. Kambi ya Upinzani inaishauri serikali kuacha kuwalaghai wananchi kwa sababu zisizo za msingi kwani ikumbukwe kwamba zipo nchi zilizo katika hali ya jangwa lakini vituo vya kuzalisha umeme vina uwezo wa kuzalisha umeme wa wastani wa zaidi ya asilimia 90.

Mheshimiwa Spika; Mwaka 2010 Serikali ilieleza kupitia taarifa ya hali ya uchumi kwamba mahitaji ya umeme yalifikia MW 791 na Waziri wa Nishati na Madini akatoa matumaini hewa kwa wananchi kupitia bajeti ya mwaka 2010/2011 kuelekea uchaguzi kwa kutaja miradi ambayo jumla yake iliahidi uzalishaji wa MW 2,960; hata hivyo serikali haikutenga fedha za kutosha kufanikisha mipango husika au walau kuweka mazingira wezeshi kwa taasisi zingine na sekta binafsi kwa ujumla kufanikisha utekelezaji hali ambayo imejirudia tena katika bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012.

Mheshimiwa Spika; Kutokana na hali hiyo ya mgawo wa umeme unaoendelea na kasi ndogo ya usambazaji wa umeme vijijini na majibu yaliyotolewa na Serikali kupitia kwa maswali ya papo kwa papo ya Waziri Mkuu tarehe 14 Julai 2011 yameonyesha kwamba serikali halichukulii tatizo la umeme kwa udharura na uzito unaostahili. Hivyo, kambi rasmi ya upinzani inatoa hoja kwa bunge kupitisha azimio la kutangaza kwamba ukosefu wa nishati ni janga la taifa na kupitisha maamuzi ya hatua za haraka ambazo serikali inapaswa kuzichukua kwa uwajibikaji wa pamoja.

Bunge lichukue nafasi yake kwa niaba ya wananchi kwa mujibu wa katiba ibara ya 63 (2) (3) ili kuisimamia serikali kuondoa janga hili la taifa; maazimio ya bunge yatawezesha taarifa za mara kwa mara kutolewa bungeni kuhusu hatua za utekelezaji na adhabu kutolewa kwa mawaziri wa serikali watakaozembea katika kuchukua hatua za haraka.

Mheshimiwa Spika, Mpango wa Taifa wa miaka mitano (2011/2012-2015/2016) umelenga kuongeza uzalishaji wa umeme mpaka kufikia MW 2780 kwa kuongeza MW 1788 kwa mujibu wa miradi iliyotajwa kwenye mpango. Lengo hili ni dogo ukilinganisha na rasilimali ambazo zipo katika taifa letu; hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kufanya mapitio ya mpango huo na kuongeza miradi mingine mikubwa ukiwemo wa Stiggler Gorge ambao una uwezo wa kuzalisha MW 2100 na kuingiza pia makadirio ya ujumla ya MW zinazotokana na miradi midogo midogo itakayoanzishwa katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani imebaini kwamba hata lengo hili dogo la MW 1788, ambalo ni sawa na ongezeko la wastani wa MW 360 kila mwaka; halijaanza kutekelezwa kwa ukamilifu. Hii ni kwa sababu katika mwaka wa fedha 2011/2012 serikali imepanga katika bajeti kuongeza MW 160 ambazo kimsingi zilipaswa ziwe zimekamilika mwaka wa fedha 2010/2011.

Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kueleza mradi mwingine wa MW 200 ambao unapaswa kukamilika katika mwaka huu wa fedha na rasilimali zilizotengwa kwa ajili ya kufanikisha mradi husika. Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza kwamba mradi wa Kiwira wa MW 200 awamu ya kwanza upewe kipaumbele maalum katika mwaka huu wa fedha ili kuweza kuziba pengo lililopo. Kambi rasmi ya Upinzani inataka kauli ya serikali kuhusu pendekezo letu la kutenga fedha za ndani kutekeleza mradi wa njia za kusafirisha umeme huo kutoka Kiwira mpaka Mbeya katika mwaka wa fedha 2011/2012 .

Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza miradi iliyosalia kwa wakati Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Wizara ya Nishati na Madini kueleza mazingira wezeshi ambayo yanakusudiwa kuandaliwa ili miradi ifuatayo iweze kupata rasilimali kwa wakati na makubaliano kukamilishwa mapema: Dar es salaam-Kinyerezi (Gesi Asilia MW 240), Iringa-Mchuchuma na Ngaka (Makaa ya Mawe-300), Mtwara – Somanga Fungu (Gesi Asilia-MW 300) na Morogoro/Iringa- Ruhudji (Maji- MW 358).

Mheshimiwa Spika, Uchambuzi wa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu Taarifa ya Utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2010/2012 na makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 unaonyesha uwezo mdogo na kasi ndogo ya kufikisha umeme vijijini. Mathalani katika bajeti yake ya mwaka huu Wizara imetenga Sh Bilioni 1.1 kupeleka umeme katika vijijini 4 tu ( Kijiji cha Magindi, kijiji cha Mbwewe, Kijiji cha Mgwashi, kijiji cha Kiwanga) kati ya vijiji 12,176 vilivyosajiliwa kutokana na taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Kwa hali hiyo itachukua karibu miaka elfu mia mbili sawa na karne mbili kufikisha umeme katika vijiji vyote; kama ambavyo tumetumia miaka 50 ya uhuru kuunganisha umeme kwa 14% tu kwenye gridi ya taifa. Kasi ndogo ya kusambaza umeme inadhihirishwa na idadi kubwa ya maombi ya wananchi wanaotaka kufungiwa umeme huku Shirika la Umeme (TANESCO) likiwajibu kuwa halina uwezo kwa sasa mpaka lipate miradi.

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2010/2011 Serikali iliahidi kutekeleza Mradi wa MCC (Millenium Challenge Cooperation) wa kuvipatia umeme vijiji 289 katika mikoa 6. Mwanza (42), Tanga (129), Dodoma (45), Mbeya (18), Iringa (17) na Morogoro (38). Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutoa taarifa ya kina ya utekelezaji kutokana na malalamiko ya kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi kwa kulinganisha na kiwango cha fedha kilichotumika. Aidha tathmini ifanyike kuhusu utekelezaji wa mradi husika ili kuwezesha umeme kuweza kufika vijijini kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani tulieleza kwenye bajeti mbadala 2011/2012 kwamba Kipaumbele chetu cha muhimu ni Kuwezesha Ukuaji wa Sekta za Uzalishaji na hasa ukuaji wa uchumi vijijini ili kuboresha kilimo, kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kuongeza thamani za bidhaa, kuongeza ajira na kupunguza umasikini kwa wananchi walio wengi.

Mkakati huu ambao utapunguza vijana wengi kukimbilia mijini na kuliokoa Tanzania kuwa taifa la wachuuzi unahitaji uwekezaji wa kutosha kwenye miundombinu ya vijijini ikiwemo ya umeme. Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kutenga bilioni 150 kwa ajili ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ili kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya kwa ajili ya uzalishaji wa umeme toka vyanzo vidogo vya maeneo mbalimbali pamoja na usambazaji wa umeme katika maeneo ya vijijini.

Chanzo cha nyongeza ikiwa ni fedha ambazo zinaendelea kutozwa hivi sasa kutokana na ongezeko katika kodi ya mafuta ya taa ambayo ikiendelea kwa mwaka mzima serikali kukusanya kiasi kisichopungua bilioni 70. Mheshimiwa Spika; tunatambua kwamba utekelezaji wa mradi kabambe wa kusambaza umeme katika mikoa 16 unasuasua kutokana na serikali kutokupeleka fedha kwa REA kwa mujibu wa bajeti zinazopitishwa na serikali.

Mpaka mwezi Mei mwaka 2011 serikali ilikuwa imepeleka bilioni 23.3 tu kwa ajili ya malipo ya wakandarasi wakati ambapo fedha zinazohitajika ni shilingi bilioni 78.3. Kwa mwaka wa fedha 2008/2009 fedha ambazo hazikutolewa na hazina ni bilioni 25.3 huku mwaka wa fedha 2010/2011 mpaka mwezi Mei zikiwa zimetolewa bilioni 13.6 tu ambazo ni sawa na chini ya robo (23%) ya bajeti iliyopangwa.

Aidha kambi ya upinzani inashauri mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali (CAG) afanye ukaguzi wa ufanisi wa miradi inayoendelea kutekelezwa ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa mapema kuwezesha wananchi wa vijijini kupata umeme.

Mheshimiwa Spika; kambi rasmi ya upinzani hairidhiki na kasi ya kuboresha utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO) na tunataka serikali ieleze hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mpango maalum wa kurekebisha hali ya kifedha ya shirika (2006-2010). Kambi rasmi ya upinzani inaitaka serikali iwaeleze watanzania ni lini mapitio ya mikataba ambayo inaipa mzigo mkubwa wa kifedha TANESCO na kusababisha bei ya umeme kupanda itafanyiwa mapitio.

Aidha, serikali imekuwa ikiidhamini TANESCO kupata mikopo ambayo kwa sehemu kubwa imekuwa ikitumika kwenye kukodi mitambo ya dharura; hivyo kambi rasmi ya upinzani inashauri kuwe na udhibiti wa kutosha ili mikopo hiyo isigeuke kuwa mzigo kwa taifa baadaye. Kwa upande mwingine, TANESCO imekuwa ikizidai wizara, idara na taasisi za serikali Ankara za umeme zinazofikia bilioni 76; hivyo serikali inapaswa ionyeshe mfano kwa kufanya malipo kwa wakati.

Mheshimiwa Spika; Pia pamekuwepo malalamiko mbalimbali kuhusu mazingira ya kupitishwa kwa zabuni za ununuzi wa nguzo, transforma na nyaya za umeme kwa kiwango kikubwa toka nje ya nchi huku viwanda vya ndani mathalani TANALEC ABB, East African Cables (hususani kampuni tanzu ya Tanzania Cables) na vingine vikididimia.

Hali hii imesababisha pia kukwama kwa utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya kusambaza umeme kutokana kwa kile kinachoelezwa kuwa ni vifaa kutokupatikana kwa wakati toka nje ya nchi. Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali kuandaa mkakati wa kupunguza gharama za manunuzi na pia kupunguza kiwango cha uagizaji wa nguzo na vifaa vingine kutoka nje ili kutumia rasilimali za ndani ili kuchangia katika kukuza uzalishaji na uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika; kambi rasmi ya upinzani hairidhiki na hatua ambazo serikali inachukua katika kupunguza gharama wanazotozwa wananchi za kuunganishiwa huduma ya umeme suala ambalo linapunguza kasi ya uunganishwaji wa umeme. Tumepokea malalamiko toka kwa wananchi wanaotakiwa na TANESCO kulipia nguzo na gharama nyingine za kuunganishwa umeme kwa kiasi kinachozidi milioni moja ambacho ni vigumu kwa wananchi wa kawaida kumudu.

Hivyo, serikali itoe kauli ya hatua inazopanga kuchukua ikiwemo za kubadili mfumo wa Ankara ili kuruhusu kuingiza kwa mteja gharama hizo kidogo kidogo katika kipindi hiki cha mpito. Aidha, TANESCO inahimizwa kutangaza kwa umma Kanuni za Sheria ya Umeme zilizotolewa kwenye gazeti la Serikali tarehe 4 Februari 2011 (GN 63) ambazo kifungu cha nne kinaeleza namna mteja atakavyofidiwa na kampuni ya usambazaji pale ambapo mteja anajigharamia mwenyewe kuvutiwa umeme ili fursa hiyo iweze kutumika ipasavyo.

Mheshimiwa Spika; kutokana na kasi ndogo ya usambazaji wa umeme, pamoja na kuondoa kodi katika vifaa vya umeme wa jua; serikali ieleze hatua ilizochukua katika kuweka mazingira wezeshi kwa vifaa vya umeme wa dharura kuweza kupatikana kwa urahisi mathalani vifaa vya kuhifadhia umeme (invetors). Aidha, serikali iongeze kasi ya kutekeleza miradi ya kuhamasisha nishati mbadala hususani vijijini kwa kufanya marekebisho ya msingi katika sheria ya fedha na sheria ya umeme.

Gesi Asilia Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imejaliwa utajiri wa gesi asilia katikati ya lindi la umasikini wa wananchi. Gesi asili iligunduliwa nchini mwaka 1974, ikaanza kutumika kuzalisha umeme viwandani 2004 mpaka sasa inatumika kuzalisha MW 440 sawa na 60% ya matumizi yote ya umeme kila siku na inatumiwa na takribani viwanda 25 kwa uzalishaji.

Kwa mujibu wa tafiti tuna zaidi ya 12 tr cf za gesi na uko uwezekano wa kugundua zaidi kutokana na utafutaji unaoendelea. Taifa letu lina fursa ya kuwa nchi kiongozi katika gesi Afrika na kushindana kimataifa ikiwa tutaweka mstari wa mbele upeo, umakini na uadilifu katika sekta ya nishati kuepusha laana ya rasilimali. Hata hivyo kwa mwelekeo wa ufisadi na udhaifu wa kiuongozi unaoendelea hivi sasa rasilimali hii inaweza kuwa chanzo cha migogoro na kuhatarisha pia usalama wa nchi.

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kwamba mradi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara kupitia Dar es salaam mpaka Tanga uwekwe kipaumbele katika Bajeti ya nyongeza ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012. Hivyo, serikali itenge bilioni 200 kwa ajili ya kuchangia kwenye mradi wa Bomba la Gesi na kuchangia katika ujenzi wa Kiwanda cha Gesi kama sehemu ya mkakati wa kushughulikia upungufu wa nishati kama janga la taifa.

Aidha usiri katika majadiliano ya mradi wa bomba la gesi ni muhimu ukaondolewa kwa wakati nyaraka rasmi za kiserikali zinaonyesha majadiliano yanayoendelea kati ya Tanzania na China kuhusu mradi husika; kambi rasmi ya upinzani inayo mawasiliano baina ya watendaji wakuu wa kampuni ya Orca Exploration Limited na baadhi ya maofisa wa ikulu kutaka kupatiwa mradi husika; wakati kampuni yao tanzu ya Pan African Energy Tanzania (PAT) imekuwa ikilalamikiwa kuhusu mradi mwingine wa gesi.

Mheshimiwa Spika; kambi ya rasmi ya upinzani inasisitiza mradi kwa kujenga kiwanda cha kujaza gesi kwenye mitungi (LPG) na mradi wa usambazaji wa gesi Dar es salaam pamoja na mradi matumizi ya gesi kwenye magari inayotekelezwa na Shirika la Petroli Nchini (TPDC) inapaswa kuongezewa rasilimali katika mwaka wa fedha 2011/2012.

Hatua hii itapunguza pia matumizi ya umeme katika maeneo yenye kuweza kutumia gesi na kubakiza umeme mwingine utakaoweza kutumika kwenye maeneo ikiwemo ya viwandani yenye upungufu wa nishati mbadala. Uamuzi huu utawezesha pia kupunguza gharama za uzalishaji na za maisha zinazotokana na kupanda kwa bei ya mafuta ambayo pamoja na mizigo ya kodi na gharama zinazotokana na mfumo mbovu wa uingizaji inasababishwa pia na kupanda kwa bei katika soko la dunia.

Aidha ili kuongeza mapato kwa serikali na TPDC kambi rasmi ya upinzani inataka mrabaha wa asilimia 12 kwenye gesi uanze kutozwa kwa mujibu wa sheria na isitishe mara moja utaratibu wa baadhi kuachiwa kutokulipa malipo husika kwa mujibu wa wa sheria. Mapitio ya kitabu cha mapato yameonyesha kwamba wakati kwenye kifungu cha 2001 cha madini kuna mrabaha hakuna kasma hiyo kwenye kifungu 3001 kinachohusika na gesi na mafuta.

Mheshimiwa Spika; ili kujiandaa kitaaalumu kama taifa kwa mipango kabambe ya gesi, kambi rasmi ya upinzani itekeleze mkakati wa kuwaambatanisha wataalamu wazawa na makampuni makubwa yenye uzoefu wa sekta husika. Aidha, kambi rasmi ya upinzani inataka Wizara ya Nishati na Madini iharakishe kukamilisha mtaala wa uhandisi wa gesi na mafuta ili fani hizo ziweze kutolewa kwenye Chuo Cha Madini Dodoma. Aidha, kwa kuwa serikali wakati wa kuhitimisha mjadala wa mpango wa mpango wa taifa wa miaka mitano; serikali ilikubali pendekezo la kuanzisha Chuo Kikuu cha Mtwara.

Kambi rasmi ya upinzani inaitaka Wizara ya Nishati na Madini kueleza maandalizi ambayo inakusudia kuyafanya kwa kushirikiana na mamlaka zingine husika ili kuwezesha uanzishwaji wa chuo kikuu hicho muhimu ambacho kitatoa mchango mkubwa kwa taifa katika masuala ya gesi na bidhaa zitokanazo na gesi.

Mheshimiwa Spika; kwa muda mrefu sasa taifa letu limekuwa likitegemea mradi mkubwa wa Songo Songo kwa shughuli za uendelezaji, uzalishaji, usafishaji na usafirishaji ambao uko chini ya Kampuni ya Songas. Hata hivyo, kampuni ya Songos imeiajiri Kampuni ya PanAfrican Energy Tanzania (PAT), ambayo ni mshirika wa TPDC katika uzalishaji, usambazaji na ugavi wa gesi asili. PAT imepewa pia Mradi wa Kusambaza Gesi Asili (Ring Main and CNG Project) jijini Dar es Salaam. Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa Kampuni ya PAT ililipwa kiasi kikubwa cha fedha zaidi gharama ilizoingia wakati wa kujenga mtandao wa usambazaji wa gesi asili.

Mheshimiwa spika, Aidha upo mwenendo usioridhisha wa kampuni hii ambao unapelekea upungufu wa gesi unaosababisha mgawo wa umeme, mfumo wa bei kubwa unaoongeza mzigo wa watumiaji na pia upotevu wa mapato ya serikali. Hivi karibuni kampuni hii ilipewa na TPDC mabilioni ya fedha kinyume cha taratibu mpaka sasa serikali inadai; ni muhimu serikali ikawaeleza watanzania ni viongozi gani walinufaika na malipo hayo na kiasi gani mpaka sasa hakijarejeswa.

Kutokana na uzito wa tuhuma na usiri katika mikataba; Kambi Rasmi ya Upinzani inashauri kuundwe kamati teule ya bunge itayofanya mapitio ya mikataba, sheria, kanuni pamoja na tuhuma za upungufu wa mgawo wa mapato na ufisadi kutokana na mauzo ya gesi kuanzia mwaka 2004 mpaka 2010.

Mafuta Mheshimiwa Spika; Taarifa za Hali ya Uchumi nchini zinaeleza kuwa mfumuko wa bei unaombatana na kupanda kwa gharama za maisha unazidi kuongezeka katika taifa letu kutoka asilimia 4.2% Oktoba mpaka 6.4% Aprili, na kama utaendelea kupanda hivi kwa ari, nguvu na kasi zaidi kwa miezi michache ijayo utakuwa zaidi ya tarakimu moja.

Kambi rasmi ya upinzani inatambua kwamba ukiondoa kupanda kwa bei ya chakula kunakutokana na kushuka kwa uzalishaji, chanzo kikuu cha hali hii ni ongezeko la bei ya nishati hususani mafuta, umeme na gesi hali ambayo isipodhibitiwa kwa mikakati makini ni tishio kwa utulivu wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Juni 2011 kambi rasmi ya upinzani iliishukuru serikali kwa kutoa kauli ya kukubali matakwa ya umma na pendekezo la kambi rasmi ya upinzani la kupunguza kodi na tozo kwenye bidhaa za mafuta ili kupunguza bei na mzigo mkubwa wa gharama za wananchi na kuonyesha mashaka kuhusu kiwango ambacho kitaondolewa na serikali.

Mheshimiwa Spika, Mashaka hayo yalidhihirisha kwenye kupitishwa kwa muswada wa sheria ya fedha tarehe 22 Juni 2011 ambapo serikali haikuonyesha kivitendo dhamira ya kupunguza kodi kwenye mafuta kwa kiwango cha kuwapunguzia ugumu wa maisha badala yake ikajikita kwenye kupunguza tatizo la uchakachuaji pekee ambalo limedumu kwa sababu ya serikali kushindwa kusimamia utawala wa sheria. Ushahidi ni kwamba katika marekebisho ya kodi; serikali haikupunguza hata senti moja katika mzigo wa kodi kwenye petrol. Aidha, serikali ilipunguza kodi ya dizeli kwa shilingi 99 tu huku ikiongeza kodi ya mafuta ya taa kwa shilingi 358.

Mheshimiwa Spika; kambi rasmi ya upinzani ilikuwa na dhamira ya kuwianisha bei ya mafuta ya taa na dizeli ili kupunguza tatizo la uchakachuaji; lakini si kwa kuongeza kwa kiwango kikubwa kodi ya mafuta kama ilivyofanya serikali. Matokeo ya uamuzi huu ni kwamba wakati bei ya petroli na dizeli zikibaki bila kupungua au zikipanda katika maeneo mengi ya nchi; bei ya mafuta ya taa imepanda kwa ari, nguvu na kasi zaidi.

Kambi rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuleta marekebisho ya sheria ya fedha ili kurekebisha hali hiyo na kueleza mkakati wa kweli wa kupunguza gharama za maisha kwa wananchi. Aidha, serikali ijieleze bungeni kutokana na udhaifu ulionyeswa na taasisi zake ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) katika kusimamia bei elekezi na kupunguza bei za mafuta ambazo serikali iliahidi bungeni kuwa zingepungua kuanzia Julai 2011.

Aidha kama sehemu ya mchakato wa kupunguza gharama za mafuta kufuatilia mabadiliko ya kodi, tozo na mfumo wa uingizaji wa mafuta serikali ifanye mapitio ya mkataba baina ya EWURA na kampuni ya Global Fluids International (T) Ltd kuhusu ufanisi na gharama za kuweka vinasaba na kuleta vifaa maalum vya kupima ubora (XRF).

Mheshimiwa Spika, ukiondoa kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na ukubwa wa kodi zinazotozwa na serikali bei ya mafuta inakuwa juu kutokana na mfumo mzima wa uagizaji, usafirishaji, uingizaji na usambazaji. Mfumo uliopo sasa unanufaisha makampuni makubwa mengi yakiwa ya kigeni na wafanyabiashara wachache wa ndani pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali wasiokuwa waadilifu kwa kulinyonya taifa na kuongeza gharama za maisha kwa watanzania walio wengi.

Mheshimiwa Spika; Hali hii ndiyo iliyokwamisha kwa muda mrefu kuanza kwa mfumo wa uagizaji na uingizaji wa mafuta ya pamoja (Bulk Procurement System) ili kupunguza gharama; suala ambalo Julai 2010 serikali ilisema liko katika hatua za mwisho na Julai 2011 mwaka mmoja baadaye bado serikali bado inatumia lugha ile ile. Aidha Serikali iwajibike kwa kutoanzisha hifadhi ya mafuta mpaka hivi sasa wakati mwaka 2010 ilitoa kauli ya kufufua kampuni ya taifa ya mafuta (COPEC); kwa ujumla kupanda kwa gharama ya mafuta kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na udhaifu wa serikali wa kutochukua hatua zinazostahili kwa wakati.

Kama imeshindwa kufufua kampuni ya taifa ya mafuta itekeleze pendekezo lililotolewa na kambi rasmi ya upinzani la kuchukua hisa 100% katika kampuni ya BP ambayo serikali ina hisa na kuigeuza kuwa chombo cha kutimiza azma husika. Aidha Wizara ya Nishati na Madini ieleze hatua mahususi za kulinda maslahi ya nchi katika kampuni ya TIPER ambayo serikali ina hisa 50% katika hatua za uingizaji na uhifadhi wa mafuta.

Mheshimiwa Spika; Ili kuongeza tija na ufanisi wa TPDC, kambi rasmi ya upinzani inaitaka Serikali itoe maelezo kuhusu hatua iliyofikiwa katika kutekeleza ushauri wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma wa kulifanyia marekebisho shirika hilo ili kuwa na mamlaka itakayohusika na kutoa vibali kwenye leseni na kusimamia uchimbaji wa mafuta na gesi na kampuni itakayoshiriki katika biashara ya mafuta na gesi.

Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upizani Bungeni inaendelea kusikitishwa na uamuzi uliofanywa wa tarehe 22 Juni 2011 wa kuondoa msamaha wa kodi ya mafuta kwa kampuni za utafutaji ya mafuta na Gesi. Uzoefu kutokana na misamaha ambayo imekuwa ikitolewa kwa makampuni ya madini unadhihirisha kwamba makampuni mengi yanatumia mwanya huo kuleta mafuta yasiyo na kodi na kuyaingiza kwenye soko la ndani la reja reja. Mathalani takwimimu zimedhihirisha kuwa kupitia misamaha iliyotolewa kwa makampuni matano tu ya madini ni karibu robo ya mafuta yote ya Dizeli yaliyoingia nchini na kampuni hizi zililipa dola laki mbili tu.

Mheshimiwa Spika; Misamaha hii haina maslahi ya taifa na ni mianya mingine ya uhujumu uchumi; hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kufikiria upya uamuzi huo na kuleta marekebisho ya sheria ya fedha ili kuufuta msamaha hiyo kwa kuwa kampuni za utafutaji mafuta na gesi zinayofursa kwa mujibu wa mikataba (PSA) kurejeshewa gharama zao mara baada ya mafuta kupatikana. Aidha, uamuzi huu uhusishe pia kampuni za madini bila kujali mikataba (MDA) kwa kuwa imethibitika kampuni hizi zote hutengeneza faida nono bila kulipa kodi inavyostahili.

Madini

Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa sekta ya madini mwaka 2010/2011 kumekuwa na ongezeko la uzalishaji huku mauzo ya nje ya madini yakiwa yameongezeka; dhahabu pekee ikifikia thamani ya dola 1,516.6. Hata hivyo mchango kwenye mauzo ya nje umeendelea kuwa ule ule wa asilimia 3.3 wa mwaka 2009/2010 na mchango kwenye pato la taifa ni asilimia 7.1 tu licha ya maelezo matamu ya serikali kuwa mapato yameongezeka kutokana na kutungwa kwa sheria mpya ya madini.

Mheshimiwa Spika, Nyaraka ambazo kambi rasmi ya upinzani inazo toka vyanzo vya kiserikali yanaonyesha kwamba sehemu kubwa ya makampuni yenye mikataba yamekataa kukubaliana na serikali. Hatua za haraka zinahitajika kulinusuru taifa na hali hii ambapo utajiri wetu unaendelea kuondoka huku watanzania wakiendelea kuwa masikini; hatua ambazo zitahusisha mwingiliano baina ya sekta ya madini na sekta nyingine.

Mheshimiwa Spika; Ukirejea kitabu cha kwanza cha mapato ya serikali kwa mwaka 2011/2012, nchi yetu itakusanya bilioni 99.5 tu; hii ni aibu ya taifa ukilinganisha na mauzo ambayo sekta hii inauza nje hasa kwa kuzingatia sehemu kubwa ya kampuni hizo hazilipi kodi inavyostahili.

Kambi ya Rasmi ya Upinzani inaishauri Wizara ya Nishati na Madini kuwasiliana na Wizara ya Fedha ili kuboresha mfumo wa utoaji wa taarifa za malipo ya kodi kwa kampuni za madini ili malipo ya kila kampuni na mchangunuo wake yafahamike kwa umma badala ya mfumo wa sasa ambapo hurundikwa pamoja katika takwimu za idara ya walipa kodi wakubwa. Aidha, Wakala wa Madini (TMAA) ufanye ufuatiliaji maalum wa madini ya Tanzanite; ambapo bei katika soko iko kati ya dola 250-400 na zaidi kwa kwa karati wakati viwango vinavyotumiwa na mamlaka husika kukadirani vidogo hali inayosababisha upotevu wa mapato.

Mheshimiwa Spika; Ili kuongeza kiwango cha mapato ikiwemo ya kodi kutokana na uchimbaji wa madini; kambi rasmi ya upinzani inaitaka serikali kutekeleza mikakati ya kupenya kuta za umiliki na mitaji (capital and ownership structures) zilizojengwa kwa muda mrefu na makampuni ya kimataifa kwa kutumia mianya ya udhaifu wa kisheria na ushawishi wa kifisadi uliosababisha mikataba mibovu katika sekta ya madini nchini.

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kueleza bayana hatua ambazo imechukua kufuatia ripoti ya tume/kamati mbalimbali ambazo ziliundwa na serikali kwa nyakati mbalimbali kwa kutumia fedha nyingi za walipa kodi lakini mapendekezo yake bado hayajatekelezwa kwa ukamilifu wake. Mathalani ripoti za karibuni za Kamati ya Masha na ile ya Bomani (2008) zilieleza bayana namna ambavyo makampuni makubwa ya madini yamekuwa yakitumia sehemu kubwa ya uwekazaji wao kama mkopo (debt financing).

Kambi Rasmi ya Upinzani, inatambua kwamba makampuni hayo yamekuwa yakitumia mianya hiyo ya kisheria na kimikataba kuwezesha wamiliki na wanahisa kupata faida mapema kuliko kuweka mtaji kwa kuwa riba ya mikopo huondolewa katika kukokotoa kodi.

Kambi Rasmi ya Upinzani inataka serikali iwaeleze watanzania ni trilioni ngapi za mapato tumezikosa kati ya mwaka 1995 mpaka 2010 katika kipindi cha miaka 15 ya kuachia mianya ya upotevu wa mapato kwa kuruhusu asilimia kubwa ya mikopo kuwa mitaji. Aidha, ni hatua gani zimechukuliwa kwa waliohusika kuliingiza taifa katika mikataba mibovu iliyoruhusu makampuni hayo kujitangazia hasara kila mwaka huku yakipata faida kubwa.

Mheshimiwa Spika; ukipitia kitabu cha mapato serikali imeweka malengo madogo ya mapato kwa upande wa Wizara ya Nishati na Madini hali ambayo inadhihirisha kwamba inakusudia kuendelea kutoza mrabaha wa asilimia 3; tofauti na mapendekezo ya Kamati ya Bomani ya asilimia 5 na Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ambayo inaitaka serikali kutoza asilimia 4. Kwa upande mwingine bado serikali inaachia mianya kwa makampuni ya madini kutotoa mrabaha baada ya kuondoa gharama za usafiri (net back value) badala ya kutoa kwenye mahesabu ya ujumla (gross); Hatua hizi zikichukuliwa zinaweza kuongeza mapato ya serikali kufikia zaidi ya bilioni 200.

Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti hali hii ya ukwepaji kodi na kuongeza mapato ya serikali katika mwaka wa fedha 2011/2012 kambi Rasmi ya Upinzaniinaitaka Wizara ya Nishati na Madini ieleze hatua mahususi ambazo itazichukua kutekeleza mapendekezo yafuatayo yaliyotolewa kwenye bajeti mbadala:

Kutunga Sheria ya kuhakikisha kwamba mikopo kwenye makampuni ya uwekezaji wa madini katika mahesabu ya kodi isizidi 70% ya mtaji; Kutunga Sheria kuhakikisha kwamba riba ya mikopo kwenye makampuni yanayohusiana haitaondolewa kwenye mahesabu ya kodi; Kufanya marekebisho ya sheria kuhakikisha kwamba kodi ya mtaji (capital gains) inatozwa katika mauziano ya makampuni yote ya madini ambayo mali zake au uwekezaji wake uko nchini hata kama mauziano hayo yamefanyika nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kuendelea kuporomoka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania; kambi rasmi ya upinzani inaishauri Wizara ya Nishati na Madini kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Fedha katika kuweka mikakati na usimamizi wa kuhusisha sekta ya madini katika kuimarisha fedha yetu. Kwa kuwa mauzo ya madini yetu yanaongezeka huku shilingi ikishuka;

Kambi Rasmi ya Upinzani, inaitaka Wizara ieleze hatua ilizochukua za kushirikiana na Wizara ya Fedha katika kuwezesha Benki kuu kutunza sehemu ya hifadhi yetu ya fedha za kigeni katika mfumo wa madini ya dhahabu. Wizara ya Nishati na Madini ishirikiane na benki kuu kuweka mfumo wa kununua dhahabu kwa wachimbaji wadogo na pia kutoza sehemu ya mrabaha wa dhahabu kwa ajili ya uhifadhi kama ilivyoshauriwa na Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma. Taratibu hizi ziende sambamba na kusimamia mfumo wa kuhakikisha kwamba makampuni hayo yanatunza sehemu kubwa ya fedha za nje (walau 60%) kwenye benki za ndani ili kusaidia kudhibiti kuporomoka kwa shilingi ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika; Sheria ya Madini ya mwaka 2010 imeipa majukumu muhimu STAMICO ya kuwa mwakilishi na msimamizi wa rasilimali za madini nchini kwa niaba ya serikali. Kambi Rasmi ya Upinzani hairidhishwi na kasi ya kuliwezesha shirika hili muhimu kutekeleza wajibu wake. Mwaka mmoja umepita bila ya serikali kukamilisha mchakato wa marekebisho ya STAMICO kuweza kukidhi haja. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ieleze ni kwa nini marekebisho ya sheria ndogo iliyoanzisha STAMICO (Establishment order) katika mwaka wa fedha 2010/2011 kama ilivyoahidiwa na kurejesha fedha za nyumba nne za STAMICO ambazo ziliuzwa na wakala wa majengo Tanzania (TBA)?

Mheshimiwa Spika, Mkakati wa Msingi katika sekta ya madini ni kuhakikisha watanzania wanaumiliki katika miradi mikubwa ya madini ama kupitia hisa za makampuni hayo kuwekwa katika soko la ndani (DSE) au kwa kampuni ya umma kushikilia sehemu kubwa ya uwekezaji hasa katika madini nyeti ikiwemo urani. Hivyo, ni lazima mtaji wa STAMICO uongezwe haraka kwa kurekebisha sheria na kanuni lakini pia kuongeza mtaji wa shirika. Ukiondoa albaki ya bilioni 5.25 bilioni Serikali ieleze hatua ambazo inakusudia kuongeza mtaji wa STAMICO katika mwaka wa fedha 2011/2012.

Mheshimiwa Spika; tunatambua kwamba Wakala Jiolojia (GST) anaendelea na utekelaji wa mradi wa kutambua maeneo ya madini. Kambi ya upinzani inataka mradi huu uende sambamba na kufanya tathmini ya kina (mineral appraisal) ya madini yetu na kupendekeza mabadiliko ya kisheria na kimikataba ambayo yatawezesha utajiri wa madini yetu kutumika kama mtaji na dhamana katika hatua ya kuhakikisha taifa letu linanufaika na rasilimali zake.

Pia; ili kuongeza uwezo wa GST kutimiza wajibu wake malipo yote yanayopaswa kutolewa kwa mujibu wa sheria ndogo iliyounda wakala husika (Establishment Order) yafanyike kwa mujibu wa taratibu kuanzia mwaka wa fedha 2011/2012. Aidha; ramani na ripoti zinazotokana na utafiti na uchunguzi huo zitolewe kwa uangalifu ili kuhakikisha maslahi ya taifa yanalindwa katika hatua zote.

Mheshimiwa Spika; tunasikitishwa na maamuzi ya serikali ya kuendelea na hatua za mbele katika utafutaji na uchimbaji wa madini ya urani bila kukamilisha maandalizi ya kisera, kisheria, kikanuni na kitaasisi yanayohitajika suala ambalo litaachia mianya ya upotevu wa mapato kwa taifa kama ilivyokuwa kwenye madini mengine na pia itahatarisha usalama.

Kambi ya Rasmi ya Upinzani inataka maelezo ya kina kuhusu mauzo na mabadilishano ya umiliki yaliyofanyika baina ya kampuni ya Australia (Mantra Resources) na Kampuni ya Urusi ya ARMZ Uranium Holding kampuni tanzu ya Rosato. Mauzo hayo ambayo yanaelezwa kimataifa kuwa yamefanyika kwa bei ya dola 1.16 bilioni ambayo ni zaidi ya shilingi trilioni 2. Mauzo hayo yamehusisha kuhamishiana umiliki wa maeneo ya Tanzania Mkuju River (Namtumbo) na Bahi Kaskazini (Dodoma).

Mheshimiwa Spika, Iwapo tungepata asilimia 30 tu ya mauzo hayo kama kodi taifa letu lingepata 600 bilioni ambayo ni fedha nyingi kuliko bajeti nzima ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka. Izingatiwe kwamba eneo husika lina madini ya urani takribani paundi 108 milioni sawa na asilimia 77 ya uchimbaji wote wa urani kwa mwaka jana. Hii ni aibu kwa taifa linalokwenda nje kuomba huku ikiachia bwerere fursa za rasilimali za ndani na kufikia hatua hata ya mbuga za wanyama kuvamiwa kwa uchimbaji usio kuwa na tija ya moja kwa moja kwa watanzania walio wengi.

Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kusimamisha kwa muda taratibu zinazoendelea za uchimbaji wa urani mpaka maandalizi ya msingi yafanyike yatakayohakikisha umiliki, manufaa na usalama.

Mheshimiwa Spika; pamoja na ahadi ya serikali kumaliza migogoro katika sekta ya madini baina ya wachimbaji wakubwa na wachimbaji wadogo pamoja na kuepusha migogoro ya leseni mathalani mgogoro wa wachimbaji wadogo eneo la Winza wilaya ya Mpwapwa ambao serikali iliahidi bungeni tarehe 9 Julai 2010 kuumaliza.

Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kauli ya serikali kuhusu mgogoro huo kwa kuwa tayari wachimbaji wadogo wameanza kuhamishwa kwa nguvu toka maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, pia migogoro ya wafanyakazi katika makampuni ya madini. Wizara ya Nishati na Madini ilieleze taifa hatua ilizochukua kushirikiana na Wizara nyingine husika kutatua malalamiko ya wafanyakazi wa Tanzanite kuhusu ongezeko la wafanyakazi wageni; Wafanyakazi walioachishwa katika kampuni ya Bulyankulu; kampuni ya Caspiani katika mgodi wa Mwadui Shinyanga ambayo yapo Wizarani kwa muda mrefu bila hatua za msingi kuchukuliwa.

Mheshimiwa Spika, Mnamo tarehe 25 Mei 1946 kampuni iitwayo Alamasi Limited ilipewa leseni ya kuchimba madini ya almasi kaskazini ya kijiji cha Luhumbo katika eneo la Mwadui, Wilaya ya Shinyanga. Leseni hiyo ijulikanayo kama Hati ya Uchimbaji (Mining Lease) Na. 224 ilitolewa chini ya Sheria ya Madini ya mwaka 1929 iliyokuwa inatumika wakati huo na ilihusu eneo la ukubwa wa ekari 3007. Ili kuchimba almasi katika eneo hilo, Alamasi Ltd. ilipewa Hati Milki ya ardhi Na. 5954. Muda wa leseni hiyo ulikuwa miaka ishirini na moja kuanzia tarehe 14 Juni 1944 na ulitakiwa kwisha tarehe 31 Mei 1965.

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa leseni hiyo, Alamasi Limited ilitakiwa kulipa kodi ya ardhi ya senti hamsini kwa ekari moja kwa nusu ya mwaka 1944 iliyokuwa imebakia, na baadae kodi ilitakiwa kupanda hadi shilingi moja kwa ekari kwa mwaka 1945; shilingi moja na thumni kwa mwaka 1946; shilingi mbili kwa mwaka 1947 na baada ya hapo kodi ilitakiwa kuwa shilingi mbili na thumni kwa ekari kwa kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, Ilipofika Januari Mosi 1963, Alamasi Ltd. ilihamisha umiliki wa leseni hiyo kwa muda uliobakia kwa kampuni mpya iitwayo New Alamasi (1963) Limited. Uhamisho wa milki hiyo ulithibitishwa na Msajili wa Hati Msaidizi mnamo tarehe 23 Mei 1963 baada ya taratibu zote za kisheria za uhamisho kukamilika. Kwa mujibu wa taarifa ya Msajili wa Hati Mkuu Msaidizi Mary J. Mziray iliyotolewa tarehe 30 Januari 2006, milki ya leseni ya New Alamasi (1963) Ltd. ilikwisha muda wake tarehe 31 Mei 1965, na eneo la leseni hiyo lilirudishwa katika milki ya Rais.

Kwa sababu hiyo, kwa mujibu wa barua ya Kamishna wa Madini ya tarehe 27 Machi 2006, Leseni Na. 224 Hati Milki Na. 5954 ilifutwa katika rejesta ya leseni za madini.

Mheshimiwa Spika, Licha ya muda wa leseni Na. 224 kwisha na leseni yenyewe kufutwa katika rejesta ya leseni za madini, New Alamasi (1963) Ltd. iliendelea kuchimba madini ya almasi katika eneo hilo na kuyauza nchi za nje bila ya kuwa na leseni yoyote ile kwa miaka thelathini na tano! Aidha, kwa kipindi chote hicho, hakuna takwimu zozote zinazoonyesha kiasi cha almasi iliyochimbwa kinyume cha sheria na wala fedha zilizopatikana kutokana na mauzo ya almasi hiyo na zilikoenda fedha hizo.

Mheshimiwa Spika, tunaitaka Serikali itoe kauli rasmi juu ya shughuli za New Alamasi Ltd., uhalali wa shughuli zake za uchimbaji almasi katika eneo la Luhumbo, kiasi cha almasi iliyochimbwa kwa kipindi chote tokea tarehe 1 Juni 1965 hadi tarehe 8 Mei 2000 na zilizokoenda fedha zilizotokana na mauzo ya almasi hiyo! Aidha, Serikali ieleze ni kwa nini kampuni iliruhusiwa au iliachwa kuendesha shughuli za uchimbaji haramu wa almasi kwa miaka thelathini na tano na hatua ambazo zimechukuliwa au zinatarajiwa kuchukuliwa dhidi ya wale wote waliohusika na ukiukaji huu mkubwa wa sheria za Tanzania.

Mheshimiwa Spika, Mnamo tarehe 9 Mei 2000, Waziri wa Nishati na Madini wakati huo Mh. Dr. Abdallah Omari Kigoda aliipatia New Alamasi (1963) Ltd. leseni Na. ML. 71/2000 kwa ajili ya kuchimba almasi katika eneo hilo hilo kwa kipindi cha miaka ishirini na tano. Kwa mujibu wa Kamishna wa Madini kwa barua yake ya tarehe 21 Machi 2006, tarehe 25 Mei 2005, “eneo lililokuwa na leseni hiyo liliunganishwa pamoja na maeneo mengine na kuwa leseni ya uchimbaji Na. SML 216/2005 ya Williamson Diamond Ltd. kwa maombi ya wamiliki wa leseni hiyo ya awali.”

Hii ina maana kwamba wamiliki wa New Alamasi (1963) Ltd. waliomba leseni yao iunganishwe na maeneo mengine na leseni hiyo mpya kukabidhiwa kampuni ya Williamson Diamond Ltd. ambayo imekuwa ikichimba almasi katika eneo la Mwadui kwa zaidi ya miaka sitini.

Mheshimiwa Spika, Kuna shaka kubwa na ya kimsingi juu ya uhalali wa milki hii mpya ya leseni ya uchimbaji almasi katika eneo la Luhumbo. Kwanza, kwa mujibu wa kifungu cha Sheria ya Madini ya mwaka 1998 iliyokuwa inatumika wakati huo, leseni pekee inayoweza kutolewa kisheria kwa ajili ya uchimbaji almasi ni Leseni ya Uchimbaji wa Mawe ya Vito (Gemstone Mining Licence). Leseni ya Uchimbaji (Mining Licence) hutolewa tu kwa madini yasiyokuwa mawe ya vito au dhahabu. Hii ndio kusema kwamba ML. 71/2000 isingeweza kuwa leseni halali kwa uchimbaji wa almasi katika eneo la Luhumbo au eneo lingine lolote nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa barua ya Kamishna wa Madini ya tarehe 27 Machi, 2006, ML. 71/2000 iligeuzwa na kuwa Leseni Maalum ya Uchimbaji (Special Mining Licence) Na. 216/2005 mnamo tarehe 25 Mei 2005. Hii ndio inayosemekana kuwa leseni ya Williamson Diamond Ltd. na ina ukubwa wa kilometa za mraba 29.73. Hata hivyo, kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya 1998, madini ya almasi hayawezi kuchimbwa kihalali kwa kutumia Leseni Maalum ya Uchimbaji kwani leseni ya aina hii hutumika tu kwa uchimbaji wa madini ya vyuma (metals) kama vile dhahabu na sio kwa mawe ya vito.

Mheshimiwa Spika, madai yaliyotolewa kwa maandishi na Kamishna wa Madini kwamba ML. 71/2000 iliunganishwa na leseni nyingine na kugeuzwa kuwa SML. 216/2005 yanaelekea kutokuwa na ukweli wowote. Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa barua ya Kamishna wa Madini ya tarehe 19Aprili 2008, leseni pekee ambayo Williamson Diamond Ltd. wanayo katika eneo la Mwadui ni Leseni ya Uchimbaji namba ML 02/92 iliyotolewa tarehe 20 Mei 1992 na aliyekuwa Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Luteni Kanali Jakaya Mrisho Kikwete.

Eneo la leseni hiyo ni kilometa za mraba 12.33. Kwa mujibu wa barua nyingine ya Kamishna wa Madini ya tarehe 21 Aprili 2008, ML 02/92 bado ‘iko hai’ na “haijaunganishwa na eneo au maeneo ya mining licence nyingine”!

Mheshimiwa Spika, Miezi mitatu baadae, Kamishna wa Madini alipigilia msumari wa mwisho katika madai haya alipoandika ifuatavyo mnamo tarehe 24 Julai 2008: “Hapakuwa na leseni ya uchimbaji madini ya Williamson Diamond Limited iliyotumika kuunganishwa na leseni namba ML 71/2000 na kuwa moja Special Mining Licence SML 216/2005”! Ni wazi, kwa nyaraka hizi za Serikali, kwamba kuna jambo ambalo limefichwa kuhusiana na shughuli za uchimbaji almasi za New Alamasi (1963) Ltd. na uhalali wa shughuli hizo.

Kambi ya Upinzani ,Tunaitaka Serikali itoe kauli rasmi ya kufafanua mustakabali wa sasa wa eneo la iliyokuwa Hati ya Madini Na. 224. Tunaitaka Serikali ifafanue utaratibu wa kisheria ambao umeiruhusu Williamson Diamond Ltd. kuendelea kuchimba almasi katika eneo la Luhumbo wakati haina leseni halali katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika; Ni nani hasa walikuwa wamiliki na wakurugenzi wa New Alamasi Ltd? Kwa mujibu wa waraka wa Msajili Msaidizi wa Makampuni katika Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) juu ya kampuni hiyo, wamiliki wa New Alamasi Ltd. walikuwa ni mabwana Sylvanus Mipawa aliyekuwa na hisa tatu na Phares Kitanzi Songo aliyekuwa na hisa na Williamson Diamonds Ltd. iliyokuwa na hisa 96!

Aidha, kampuni hiyo ilikuwa na mtaji wa shilingi za Tanzania 2000 ikiwa na maana kwamba kila hisa ilikuwa na thamani ya shilingi ishirini tu! Waraka huu wa BRELA uliandikwa tarehe 22 Septemba, 2006. Kufuatana na waraka huu, kuanzia mwaka 2002 New Alamasi (1963) Ltd. ilipeleka fomu za annual returns ambazo hazikukamilika. Aidha, “... wenye hisa wawili Sylvanus Mipawa na Phares Kitanzi Songo hawaonekani katika returns na maelezo na utaratibu wa kutoka katika kampuni haukuzingatiwa.”

Mheshimiwa Spika, Vile vile, kwa mujibu wa waraka wa Msajili Msaidizi Mwandamizi wa Makampuni wa BRELA wa tarehe 13 Julai 2007, kati ya mwaka 1965 na 1970, wakurugenzi wa kampuni hiyo walikuwa mabwana George Faulkner Hunt, Gabriel Jacobus Du Toit na Ian David Livingstone. Kati ya mwaka 1970 na 1972, wakurugenzi walikuwa George Faulkner Hunt, Gabriel Jacobus Do Toit na Alexander John Prescott.

Aidha, kati ya mwaka 1973 na mwaka 1983 watu waliopata kuwa wakurugenzi wa kampuni hiyo ni pamoja na Samuel Lweyemamu Lwakatare, Robert Macbain Bisset, Ignace Herack Marandu, Jeremias Norbert Rweyemamu, William Henry Manning, John Robert Dawson Kiwia na Phares Kintazi Songo. Kwa mujibu wa waraka wa BRELA wa Septemba 2006, wakurugenzi wa kampuni hii wanaonekana tofauti “... lakini utaratibu wa mabadiliko haukufuatwa.” Tunaitaka Serikali itoe maelezo sahihi ya kuhusu wamiliki na wakurugenzi wa kampuni hii na kwa nini taratibu za kisheria hazijafuatwa kwa miaka mingi. Aidha, tunaitaka Serikali itoe maelezo iliwezekanaje kwa kampuni yenye mtaji wa shilingi 2000 imeweza kuchimba almasi kwa zaidi ya miaka arobaini!

Mheshimiwa Spika, Uhusiano kati ya New Alamasi (1963) Ltd. na Williamson Diamonds Ltd. umegubikwa na utata mkubwa. Hii ni kwa sababu mnamo tarehe 21 Machi, 2006, wakati akijibu swali la mwandishi wa habari wa gazeti la Uhuru aliyetaka kujua uhusiano wa makampuni haya mawili, Kamishna wa Madini alidai kwamba yeye hatunzi kumbu kumbu za makampuni hivyo “... siwezi kujua uhusiano wa New Alamasi (1963) Ltd. na Williamson Diamonds Ltd. Na kama tulivyoona, taarifa zilizotolewa na BRELA Septemba 2006 zinaonyesha kwamba Williamson Diamonds Ltd. ina 96% ya hisa zote za New Alamasi (1963) Ltd.

Hata hivyo, katika tarehe isiyojulikana ya mwaka 1992, New Alamasi (1963) Ltd. iliingia mkataba na Williamson Diamonds Ltd. ambao kwayo New Alamasi (1963) Ltd. ilifutwa kwa hiari na kuhamisha hisa na mali zake zote “zilizoko kwenye Hati ya Madini Na. 224 Hati Milki Na. 5954” kwa Williamson Diamonds Ltd. Mkataba huu unaelekea ulisainiwa na Sylvanus Mipawa kwa upande wa New Alamasi na watu watatu wasiojulikana kwa niaba ya Williamson Diamonds Ltd.

Mheshimiwa Spika; Mkataba huu kati ya New Alamasi (1963) Ltd. na Williamson Diamonds Ltd. umezua maswali mengi ambayo yanahitaji majibu kutoka kwa Serikali. Kwanza, mkataba huu unatamka kwamba kinachohamishwa ni Hati ya Madini Na. 224 na mali zilizoko kwenye eneo hilo ambavyo kama tulivyoonyesha ilikwisha muda wake tarehe 31 Mei 1965.

Pili, mkataba huu unataja Hati Milki ya Ardhi Na. 5954 ambayo nayo ilikwisha kurudi kwenye milki ya Rais tangu mwaka 1965 leseni ya uchimbaji ilipokwisha muda wake! Tatu, mkataba huu unaonyesha ulifanyika chini ya Mining Ordinance ya mwaka 1929 ambayo ilikwisha kufutwa tangu mwaka 1979 wakati Sheria ya Madini ya mwaka huo ilipotungwa! Nne, makubaliano haya yanataja makubaliano mengine ya kuhamisha haki za New Alamasi (1963) Ltd. yanayodaiwa kufanyika tarehe 31 Januari 1967, 17 Januari 1972 na 14 Februari 1978.

Mheshimiwa Spika, Hata hivyo, hakuna ushahidi wowote wa makubaliano ya aina hiyo kati ya makampuni haya mawili kwa vipindi vilivyotajwa. Aidha, makubaliano yanadai kwamba New Alamasi (1963) Ltd. walipewa leseni ya eneo hilo tarehe 25 Mei 1965 kwa kipindi cha miaka kumi na sita kuanzia tarehe 13 Juni 1965 “ambayo ilisajiliwa na Idara ya Madini.” Hata hivyo, kama tulivyoona, Idara ya Madini yenyewe imekanusha madai hayo kwa kuonyesha kwamba Hati ya Madini Na. 224 ilikwisha muda wake tangu tarehe 31 Mei 1965!

Mheshimiwa Spika; Taarifa tulizonazo zinaonyesha kwamba mkataba kati ya New Alamasi (1963) Ltd. sio halali bali uligushiwa kwa lengo la kuwezesha uchimbaji wa almasi kuendelea katika eneo hilo kinyume cha sheria na ili kuendeleza wizi wa rasilimali ya nchi yetu ambao umeendelea kwa miaka zaidi ya arobaini! Tunaitaka Serikali itoe kauli rasmi na sahihi juu ya uhusiano huu kati ya makampuni haya mawili.

Mheshimiwa Spika, Mamia ya wananchi waishio maeneo jirani na eneo la New Almas wamekuwa wakinyanyaswa kwa miaka mingi na vyombo vya dola kama vile polisi, mahakama na vyombo vya utawala kwa madai kwamba ni wavamizi wa eneo la leseni ya New Alamasi. Watu kadhaa wameuawa na askari polisi na mgambo baada ya kukutwa ndani ya eneo hilo.

Wengi wengine wamepigwa na kuteswa katika vituo vya polisi na wengine wengi wamefungwa kwa tuhuma za uongo za kuvamia eneo la Mgodi wa New Alamasi (1963) Ltd. na kwa kutumia hati za kugushi za kuonyesha umiliki wa eneo hilo. Wote hawa walioteswa namna hiyo na/au ndugu zao wanastahili sio tu kuombwa msamaha kwa mateso ya miaka mingi na ya bure, bali pia wanastahili kulipwa fidia kwa madhara yote waliyoyapata katika muda huo.

Kambi ya Upinzania , Tunaitaka Serikali itoe kauli kama iko tayari kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanapata haki zao kutokana na uovu waliotendewa na vyombo vya serikali. Aidha, Serikali itoe taarifa rasmi juu ya hatua inazotarajia kuzichukua dhidi ya Williamson Diamonds Ltd. kwa kushiriki katika kugushi nyaraka za kuiwezesha kuchimba almasi kinyume cha sheria.

HITIMISHO Mheshimimiwa Spika; kambi rasmi ya upinzani inapenda kuhitimisha kwa kusisiza kwamba kwa sehemu kubwa matatizo katika sekta za nishati na madini yamechangiwa na sababu za kibinadamu za kutowajibika ipasavyo kisera, kimaamuzi, kiusimamizi na kiutendaji kwa viongozi wa kiserikali kuanzia kwa viongozi wakuu wa nchi, Waziri mwenye dhamana na watendaji wengine na hivyo kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi na kuathiri uchumi wa nchi; wahusika wanapaswa kuwajibika.

Mheshimiwa Spika; uwajibikaji huo unapaswa kufuatiwa na hatua za haraka za kusimamia sera sahihi, uongozi makini na taasisi thabiti zenye kuelewa kwamba sekta ya nishati ni moyo wa taifa na sekta ya madini ni mtaji wetu kwa sasa na kuchukua hatua kali dhidi ya ufisadi uliofanyika katika sekta husika, kufanya mapitio ya mikataba, kuharakisha utekelezaji wa mipango kwa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi na kwa ujumla kuwajibika.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba bunge lako lijadili makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa kuzingatia maoni tuliyoyatoa ya kuongeza bajeti ya wizara husika; kupokea mapendekezo yatayopelekea kufanyika kwa mabadiliko katika sheria ya fedha na kupitisha maazimio mahususi ikiwemo ya kukabiliana na upungufu wa nishatia mbao sasa ni janga la taifa pamoja na kuhakikisha taifa letu linanufaika na madini; aidha iwapo Serikali haitakubali hoja hizi za msingi za kuinusuru nchi yetu kuzifanyia kazi, basi tutaunganisha nguvu ya umma kupitia maandamano na kitaeleweka. Kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha,


John Mnyika (Mb)

Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani

Wizara ya Nishati na Madini

15/07/2011

2 comments:

Anonymous said...

Michael, nimeisikiliza hotuba ya mh. Mnyika, nakubaliana na hoja zake za msingi.. nangojea majibu ya mh. Ngeleja... natumaini hatatoa majibu mepesi juu ya hoja zilizotolewa na wabunge mbali mabli.. Nyirenda

william said...

Hotuba ya Mh.Mnyika ilikuwa nzuri sana,ila hawa CCM nashindwa kuwaelewa kwanini hawataki kukubali mazuri yanayopendekezwa na CHADEMA....Tafadhari suala la kampuni ya gesi ya Pan Africa mlikazanie ili ukweli ueleweke. tumechoshwa na wizi wa maliasili zetu. Kwanini Viongozi wa Tz hawana huruma kwa wananchi wao????CHADEMA msilale mpaka kieleweke...ccm wakiwakejeli msiwajali maana hawana la maana.