Saturday, July 2, 2011

Kanuni zimepindishwa kumlinda Pinda

Sijaridhika na maamuzi ya Mwenyekiti wa Bunge, George Simbachawene kupindisha kanuni tarehe 29 Juni 2011 na 30 Juni 2011 kwa ajili ya kumlinda Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutekeleza wajibu wa kujibu maswali ya papo kwa papo ya wabunge kama kanuni zinavyohitaji.

Kutokana na hali hiyo nakusudia kuwasilisha malalamiko tarehe 2 Julai 2011 kwa katibu wa bunge kwa mujibu wa kanuni za bunge kifungu 5(2) na 7(3) ili sababu hizo ziwasilishwe kwa Spika aitishe kikao cha Kamati ya Kanuni za Bunge kwa kurejea kanuni 5(5) na kulijulisha bunge kuhusu uamuzi mbadala utakaotolewa.

Tarehe 30 Juni 2011 niliomba muongozo wa mwenyekiti kwa mujibu wa kanuni 68 (7) kutokana na tarehe 29 Juni 2011 Mwenyekiti wa Bunge, Simbachawene kutoa taarifa ya bunge kuwa hakutakuwepo na maswali na majibu kwa Waziri Mkuu tarehe 30 Juni 2011 kwa kuwa kanuni zilitenguliwa 22 Juni 2011 kumruhusu Waziri Mkuu kujiandaa kuwasilisha hotuba yake tarehe 23 Juni 2011.

Niliomba mwenyekiti atoe muongozo kuwa kanuni za bunge zilikiukwa tarehe 29 Juni 2011 kwa kutoa taarifa ya kupindisha kanuni kumlinda Waziri Pinda asijibu maswali ya wabunge wa papo kwa papo bila kufuata utaratibu wa kutengua kanuni.

Nikalieleza bunge kwamba kanuni ya 150 imekiukwa ambayo kipengele cha 150(1) ambacho kinaelekeza bayana kwamba ili kanuni itenguliwe kwa madhumuni mahususi ni lazima waziri, mwanasheria mkuu wa serikali au mbunge yoyote lazima atoe hoja hiyo na kifungu cha 150 (3) kinataka maelezo ya hoja hiyo yakiwemo madhumuni yatolewe jambo ambalo halikufanyika tarehe 29 Juni 2011.

Hivyo, nikalijulisha bunge kwamba kwa kuwa kuna masuala tata na tete yanayoendelea katika taifa ambayo yanahitaji kauli za serikali ilikuwa ni muhimu kwa kipindi cha maswali na majibu kwa waziri mkuu kuendelea kama kanuni zinavyohitaji tarehe 30 Juni 2011 ili Waziri Mkuu Pinda atimize wajibu wa kutoa majibu.

Mathalani nililieza bunge kwamba vyombo vya habari vimenukuu Waziri Mkuu Pinda akitoa maelekezo potofu kwa wakuu wa mikoa na wilaya kuhusu mchakato wa katiba kabla ya sheria kupitishwa. Maelekezo ambayo yalifuatiwa na uamuzi wa kuondolewa kwa muswada wa sheria ya mapitio katiba kuondolewa katika ratiba ya mkutano wa nne wa bunge kinyume mipango iliyotangazwa awali.

Pia, nililieza bunge kuwa serikali inapaswa kutoa kauli bungeni ya kumaliza mgawo wa umeme unaondelea na kuathiri taifa ikiwemo wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam. Nililieleza bunge kuwa wananchi wanakusudia kuandamana hivyo majibu kwa Waziri Mkuu Pinda kupitia maswali ya papo kwa papo yangeweza kueleza ufumbuzi wa suala hilo.

Kadhalika, nililieleza bunge kuwa vyombo vya habari vimewanukuu wakuu wa wilaya wakitoa maelekezo kwa Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) kuwabagua wanafunzi kwa misingi ya vyama vyao wakati wa kuwarejesha chuoni kwa kuanza kuwarejesha kwanza wanachuo ambao ni wanachama wa CCM. Aidha nilidokeza kuwa kauli hiyo ilifuatiwa na waraka wa Wizara ya Elimu na Ufundi ambao umetoa maelekezo maalum ya ubaguzi kwa bodi ya mikopo na UDOM. Matokeo ya maelekezo hayo ni UDOM kutoa taarifa yenye masharti magumu ya kuwataka wanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo Cha Sanaa na Sayansi za Jamii waliosimamishwa masomo kuripoti chuoni huku ikiwabagua wanafunzi 15 ambao wametajwa kwa majina.

Kutokana na masuala hayo na mengine toka kwa wabunge wengine yanayohitaji majibu toka kwa Waziri Mkuu Pinda kama kiongozi wa Shughuli za Serikali bungeni niliomba muongozo kwa mwenyekiti ili kanuni ya 30 (6) itumike kuagiza utaratibu wa kuwezesha shughuli ya maswali kwa waziri mkuu kuweza kuendelea kama kawaida.

Nilitaka muongozo kanuni za bunge zisipindishwe kumlinda Pinda kwa kuwa kifungu cha 38 (5) kinaeleza bayana kwamba hakutakuwa na maswali kwa Waziri Mkuu iwapo hayupo kwa sababu maalum na kwamba siku ya leo ya alhamisi tarehe 30 Juni 2011 Waziri Mkuu Pinda alikuwepo bungeni katika kipindi husika cha maswali. Hata hivyo, pamoja na maelezo hayo Mwenyekiti Simbachawene aliendelea kutoa miongozo yenye kukiuka kanuni za bunge hususani vifungu 5(1), 7(3), 30(6), 38(5), 150 (1) na 150 (4).

Kwa upande mwingine, naelewa kwamba kanuni za bunge zinaelekeza hoja ambazo mbunge anaweza kuziwasilisha hivyo, natoa mwito kwa Waziri Mkuu Pinda kwa kuwa kanuni zilipindishwa kuondoa kipindi cha maswali kwake atumie kipindi cha majumuisho ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kesho tarehe 1 Julai 2011 kutoa majibu ya kina kuhusu kauli zake juu ya mchakato wa katiba mpya, kauli ya serikali kumaliza mgawo wa umeme na hatma ya wanafunzi 15 wa UDOM waliobaguliwa katika taratibu za kurejeshwa chuoni.

Aidha, Waziri Mkuu Pinda atambue kwamba wanachuo wengine nao wanamalalamiko ya kupewa muda mfupi wa kurejea chuoni na masharti magumu ya malipo ambapo wanapaswa kurejea tarehe 2 na 3 Julai pekee na kutangaziwa kuanda mtihani tarehe 4 Julai 2011 siku moja baada ya kurejea; na kwamba wanafunzi ambao hawatafika na hati za malipo hawatapokelewa.

Natoa rai kwa Waziri Mkuu Pinda kuzingatia ukweli kwamba mgogoro wa wanachuo wa UDOM ulianza mwaka 2009/2010 wakati wanafunzi walipotumia njia zote za kawaida za mawasiliano na serikali na utawala wa chuo hicho kutaka madai yao ya kutaka serikali kuingiza kozi ambazo hazikuwa katika mpango wa mafunzo kwa vitendo (PT-Practical Training).

Baada ya mgomo wa wanafunzi wa tarehe 21 Disemba 2010 alikwenda Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Shukuru Kawambwa akiongozana na Waziri wa Mambo ya Ndani Shamsi Nahodha na watendaji wakuu wa mamlaka zinazohusika na elimu ya juu walifika katika Chuo hicho kuzungumza na wanachuo na kubainika kwamba wanachuo wenye kusomea shahada za Utawala wa Biashara (BBA) na Sanaa ya Lugha (BA LT) ambao kutokana na kozi zao kwa kadiri ya Prospectus walipaswa kwenda mafunzo kwa vitendo lakini serikali ilikiri kutotimiza wajibu wa kuwaingizia fedha kama ilivyohitajika. Pia, maelekezo yalitolewa kwa kozi ambazo hazijawekewa mafunzo kwa vitendo (field) kwenye bajeti zifikazo 14 ziwekewe bajeti na menejimenti iliridhia kazi hiyo kwa kutoa barua kwa wanafunzi tarehe 3 Januari 2011 na kuandaa bajeti kupitia kikao cha bodi kilichoketi tarehe 26 Januari 2011.

Hata hivyo, baadhi ya watendaji wa serikali walichochea mgogoro katika Chuo hicho kutokana na barua ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kwamba haijatoa idhini na mafunzo kwa vitendo na hivyo Seneti ya UDOM ilikaa tarehe 8 Juni 2011 na wanachuo kuelezwa kwamba hakuna fedha zitazoombwa Hazina kwa ajili ya wanafunzi kwenda kwenye mafunzo kwa vitendo kama serikali ilivyoahidi awali kupitia mawaziri na taarifa kufika kwa Waziri Mkuu.

Hali hiyo iliwachochea wanavyuo kutaka kuja Bungeni kukutana na Mawaziri husika ili kuwelezwa hatma yao lakini polisi wa kutuliza ghasia (FFU) waliwavamia njiani na kutumia nguvu kubwa kuwazuia kwa kupiga mabomu ya machozi, kuwapiga kwa vitako vya bunduki na kuwaumiza vibaya mathalani Malambo Ngata aliyevunjwa mguu wa kushoto. Pia, polisi ilikamata viongozi wa Serikali ya Wanafunzi na wanachuo wengine na kuwaweka rumande kuanzia tarehe 10 Juni 2011 hali iliyochochea wanafunzi wengine kuanza mgomo mpaka uongozi wa Chuo ulipofunga Chuo tarehe 16 Juni 2011.

Uamuzi huu ulitolewa kwa ghafla huku wanafunzi wakipewa muda mchache wa kuondoka chini ya ulinzi wa vyombo vya dola hali ambayo imesababisha wengi ikiwemo vijana wa kike kukwama Dodoma. Katika majumuisho ya Bajeti ya Wizara yake, Waziri Mkuu Pinda atoe tamko la kutekeleza ahadi ya Serikali ya kutoa fedha kwa wanafunzi kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo na pia kuwarejesha wanafunzi kuendelea na masomo bila masharti magumu ikiwemo kufuatilia hatma ya wanafunzi waliofukuzwa bila taratibu zinazohitajika kufuatwa.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)
30 Juni 2011; Bungeni, Dodoma

2 comments:

william said...

Waheshimiwa wabunge wa Chama Kitukufu cha CHADEMA tunawaamini kuwa nyie ndiyo wakombozi wa nchi hii ambayo imetekwa na hawa MAFISADI. Kazeni buti tuko nanyi. Huwa tunaumia tunapoona hoja zenu Bungeni zinapondwa na hawa MAFISADI.Msikate tamaa tunaamini ipo siku mtakuwa wakuu wa nchi hii.Mimi naiamini CHADEMA maana wabunge wake wote ni Vichwa vilivyoenda shule!Nikiwaona wewe,Mdee,Zitto,Lissu,Freeman,Rev.Msigwa,Lema na wengineo mkiwa bungeni nafarijika sana. Kejeli za CCM zisiwakatishe tamaa maana wanawaogopa na kuwaheshimu sana. Big Up and LONG LIVE CHADEMA!!!!!! ALUTA CONTINUA!!!!!!!!

Schola Mwacha said...

Hongera sana mheshimiwa kwa kazi nzuri,nakuombea MUNGU akupe afya na ulizi,swala la field naomba mzid kulieleza bunge ukwel kwan wabunge baadhi wa ccm wanalitizama kisiasa,huku wakitaka hoja nyingine kama urejeshwaj wa mikopo kufanikiwa wa2 watarejeshaje fedha bila ajira ambayo serikali inaonesha juhud za kuwapunguzia sifa kwa kuwanyima field koz kama project planning management and community delelopment,na sababu zip zinafanya vyuo vingine kama Tengeru,Mipango Waende Udom wasiende.VIVA FOREVER Chadema.