UTANGULIZI:
Kwa
nyakati mbalimbali kumekuwepo na mijadala kwenye mitandao ya kijamii kuhusu
utendaji kazi wangu katika kuwezesha maendeleo Jimboni Ubungo. Mijadala hiyo imeshika
kasi jana tarehe 20 Agosti 2012 siku nzima baada ya habari kwenye ukurasa wa
mbele wa gazeti la Tanzania Daima “Mnyika kinara bungeni” ambayo imerejea
rekodi za bunge na kuniweka katika orodha ya wachangiaji wa mara kwa mara
bungeni.
Napokea
kwa unyenyekevu pongezi zilizotolewa na wachangiaji mbalimbali lakini
izingatiwe kuwa michango yangu bungeni ni matokeo ya heshima mliyonipa ya
kuwawakilisha. Aidha yapo maoni machache ambayo yametoa tafsiri tenge kuhusu
kazi ya mbunge na wengine mmetaka nieleze nimefanya kazi gani za maendeleo
jimboni Ubungo.
Tarehe
kama ya leo 21 Agosti 2005 nilianza mchakato wa kuwa kugombea ubunge nikiwa
kwenye chakula na watoto yatima, tarehe kama hiyo mwaka 2010 nilianza kampeni
za uchaguzi mitaani Ubungo, tarehe hii hii kwa mwaka huu wa 2012 naomba
niitumie kutoa taarifa fupi ya utekelezaji kwa masuala ya maendeleo katika
mwaka wa fedha 2011/2012 uliomalizika tarehe 30 Juni 2012; taarifa ya kina ya
utekelezaji nitaitoa nitakapotimiza miaka miwili ya utendaji.
AHADI NILIZOTOA WAKATI WA UCHAGUZI WA MWAKA 2010
Kabla
ya kueleza kazi nilizofanya katika kutimiza majukumu ya kibunge katika
kuwezesha maendeleo jimboni ni muhimu nikawapa rejea ya ahadi nilizotoa wakati
wa uchaguzi wa mwaka 2010 ili kupata msingi
wa kupima utekelezaji.
Wakati
wa kampeni nilitoa ahadi chache na kuelekea mwishoni mwa kampeni niliorodhesha
ahadi zote na kuziweka kwenye maandishi ikiwa ni mkataba kati ya mbunge na
wananchi wa kutumika kama rejea katika kipindi cha miaka mitano ya utumishi
2010 mpaka 2015.
Ahadi
hizo ziko katika kipeperushi cha AMUA ambacho tulikisambaza kwenye kaya
mbalimbali jimboni wakati wa kampeni, ahadi hizo nilizirudia mara baada ya
kuchaguliwa na zinapatikana hapa: http://mnyika.blogspot.com/2010/11/ujumbe-wa-mbunge-shukrani-twende-kazi.html
UTEKELEZAJI KATIKA KIPINDI CHA MWAKA MMOJA NA NUSU
Toka
kuapishwa mwezi Novemba 2010 mpaka mwezi Juni 2012 ni takribani mwaka mmoja na
na miezi tisa ya kuwatumikia wananchi wa
Ubungo kwa nafasi niliyochaguliwa ya mbunge wa Ubungo; hizi ni baadhi katika
orodha ya za maendeleo ambazo nimeshiriki jimboni:
ELIMU:
Akili
na vipaji ambavyo kila mwanadamu amejaliwa ndiyo mtaji mkuu wa kujikwamua kimaisha.
Katika muktadha huo katika kipindi husika nimesimamia yafuatayo kuwezesha elimu
bora:
Mbunge amefuatilia kupitia vikao vya
manispaa ya Kinondoni na kupitia ziara jimboni, maswali bungeni ili kuhakikisha
ruzuku ya bajeti ya elimu kwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari, inafika
na kuboresha upatikanaji wa vifaa vya elimu na huduma zingine za muhimu katika
Jimbo la Ubungo, katika mwaka 2012/2013 nitafuatilia kwa karibu zaidi kasoro
zilizobainika katika mwaka 2011/2012 .
Katika kipindi husika mbunge ameendelea
kutetea haki na maslahi ya walimu na wanafunzi wakiwemo wa elimu ya juu wa
Jimbo la Ubungo. Aidha, nimeshiriki katika kuwezesha uamuzi wa kuhamisha fedha
katika mafungu mengine yasiyokuwa ya lazima kuelekeza katika matengenezo ya
madawati kwa shule za msingi na sekondari ambapo zaidi ya madawati 7,000
yamesambazwa katika Jimbo la Ubungo kutoka Manispaa ya Kinondoni, Mfuko wa
Maendeleo ya Jimbo (CDCF) na kutoka Sekta Binafsi. Kwa ushirikiano na madiwani
tumefuatilia kuhakikisha mgawo wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na vyoo
katika shule za msingi na sekondari katika kata mbalimbali kutoka katika
Manispaa ya Kinondoni na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF), orodha ya shule na
viwango vya fedha vilivyotumika inaweza kupatikana katika Ofisi ya Mbunge.
Mbunge amependekeza sehemu ya fedha za
mfuko wa kuchochea maendeleo ya jimbo (CDCF) kutumika kutoa elimu maalum ya
kuwawezesha wananchi kujua haki zao, fursa zilizopo na namna ya
kujiendeleza, haswa kwa akina mama,
vijana na walemavu. Mfano; haki za mirathi kwa wajane na kukuza vipaji kwa
vijana. Hata hivyo, utekelezaji wa kazi hii haukuwezekana kwa kutumia CDCF
kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 kutokana na utata kuhusu tafsiri ya shughuli za
kuchochea maendeleo zinazoweza kutengewa fedha kutoka kwenye mfuko, hivyo
shughuli hiyo itazingatiwa kwa ukamilifu kwenye mwaka wa fedha 2012/2013 baada
ya kibali kupatikana.
Ili kuziba pengo nje ya CDCF katika
mwaka 2011/2012 kupitia ofisi ya mbunge Ubungo na Asasi ya Maendeleo Ubungo
(UDI) tumefanya programu ya “Toa Kitabu Kisomwe” na pia kuunganisha vijana na
wanawake na elimu maalum kupitia taasisi zingine.
Mbunge
amechangia asilimia 20 (20%) ya mshahara wake kwa mwezi
kwenye masuala mbalimbali ya elimu, orodha ya baadhi ya michango kwa shughuli
za elimu kwa wanafunzi na walimu wa msingi, sekondari na vyuo inaweza kurejewa
katika Ofisi ya Mbunge (majina ya waliopewa michango yamehifadhiwa kulinda
faragha).
Kazi hizi zitapanuliwa zaidi katika
mwaka wa fedha 2012/2013 kupitia Mfuko wa Elimu Ubungo tutakaouzindua karibuni.
AJIRA:
Katika kuwezesha upatikanaji wa mitaji
kwa vijana na wanawake kuweza kujiajiri mbunge alifanikiwa kushawishi Manispaa
ya Kinondoni kuongeza fedha za mikopo kwa vikundi vya kina mama na vijana
ambapo awali zilikuwa zikitengwa milioni 20 tu, na hivyo milioni zaidi ya 200.
Orodha ya vikundi vilivyopatiwa mikopo
na mitaji mpaka sasa katika Jimbo la Ubungo inapatikana kwenye Ofisi ya Mbunge.
Aidha, mbunge ametetea wafanyabiashara wadogo kuendelea kutengewa maeneo ya
biashara na katika mwaka 2011/2012 amewezesha kamati maalum inayohusisha
wafanyabiashara na Manispaa kuundwa kwa ajili ya kuwezesha wafanyabiashara wa
Ubungo kupatiwa maeneo katika masoko yaliyotengwa. Katika mwaka 2012/2013 hatua
zitaendelea kuchukuliwa kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo ndogo ambao
hawajapata maeneo mpaka sasa.
Mbunge amefanya ziara ya kikazi katika
kiwanda cha nguo cha Urafiki ili kuzungumza na wafanyakazi na menejimenti
katika kuisimamia serikali kushughulikia matatizo yaliyojitokeza katika kiwanda
na kuathiri ajira na ujira bora. Matokeo ya ziara ya mbunge na ufuatiliaji
bungeni yamefanya kiwanda hicho kutembelewa pia na kamati ya bunge na mawaziri
husika ambapo hatua zimeanza kuchukuliwa, katika mwaka wa fedha 2012/2013. Mbunge
ataendelea kufuatilia kwa karibu matatizo yanayoendelea kuhusu ufisadi na
uwekezaji katika kiwanda husika.
Aidha, mbunge amefuatilia pia masuala ya
ajira katika viwanda vilivyofunguliwa kwenye maeneo ya uwekezaji wa kiuchumi
(EPZ/SEZ) yaliyopo katika jimbo la Ubungo ikiwemo kutaka kutengwa kwa maeneo maalum
ya wawekezaji wadogo.
Katika kupanua wigo wa ajira mbunge
amefuatilia pia kuhusu viwanda vingine vilivyobinafsishwa au
kuuzwa miaka ya nyuma katika Jimbo la Ubungo mathalani Ubungo Garments; Ubungo Spinning Mill; Polysacks Ltd; Tanzania Sewing Thread;
Coastal Diaries (Maziwa) na Kiwanda cha
Zana za Kilimo (UFI); na hatimaye serikali imemjibu kuwa waraka utawasilishwa
kwenye baraza la mawaziri ili kurejesha viwanda vilivyodidimizwa kinyume cha
masharti ya mikataba. Katika utekelezaji wa hatua hiyo, mbunge amependekeza
kuwa miongoni mwa maeneo ya viwanda yatakayorejeshwa kutengwe eneo maalum kwa
ajili ya wenye viwanda vidogo vidogo katika jimbo la Ubungo ili kupanua wigo wa
ajira hususan kwa vijana katika mwaka wa fedha 2012/2013.
Mbunge ameunga mkono jimboni na ndani ya
bunge madai ya ujira bora na stahili za wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi
kama walimu, madaktari/manesi, polisi, madereva nk. Hata baada ya nyongeza
ndogo ya mishahara iliyopatikana kufuatia shinikizo la migomo kutoka vyama vya wafanyakazi,
mbunge ataendelea kuungana na wafanyakazi na wabunge wengine katika kutaka
kuboreshwa kwa maslahi ya wafanyakazi na mazingira ya utoaji huduma hususan
katika sekta za elimu, afya, usalama na mahakama. Katika ya masuala ambayo
aliyapata kipaumbele katika mwaka wa fedha 2011/2012 ni nyongeza ya posho ya
lishe (rationing allowance) kwa askari polisi kutoka laki moja mpaka laki moja
unusu suala ambalo serikali imelitekeleza katika bajeti ya mwaka wa fedha
2012/2013.
MIUNDO MBINU:
Msimamo wangu katika kipindi chote
umekuwa kwamba pamoja kuunga mkono uwekezaji kwenye upanuzi wa barabara kuu,
ujenzi wa miundombinu ya mradi wa mabasi yaendayo haraka na ujenzi wa fly
overs, miradi hii kwa ujumla wake iliyotengewa zaidi ya bilioni 240 inachukua
muda wa kati na muda mrefu hivyo kukamilika kwake ni mpaka mwaka 2015 au zaidi.
Hivyo ili kupunguza msongamano katika barabara kuu ya Morogoro, pamoja na mbinu
zingine mbunge amekuwa mstari wa mbele kutaka barabara za pembezoni zijengwe
kwa haraka; hatimaye baada ya ufuatiliaji wa mara kwa mara kupitia ziara
jimboni, vikao vya manispaa, vikao vya bodi ya barabara, ziara jimboni,
mawasiliano kwa barua na mamlaka husika na kuhoji bungeni Serikali imekubaliana
na mapendekezo tuliyowasilisha hivyo maamuzi yamefikiwa kuwa barabara husika
zihudumiwe na Serikali kuu (TANROADS) badala ya Manispaa.
Jumla ya shilingi bilioni 10.5
zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara zifuatazo: Mbezi Luis kupitia Goba mpaka Mbezi Tangi
Bovu; Mbezi kwa Yusuph- Msakuzi- Mpiji Magohe mpaka Tegeta/Bunju;
Mbezi-Malambamawili-Kinyerezi, Kimara-Mavurunza-Bonyokwa; Ubungo
Maziwa-External, Kimara-Kilungule-Makoka-Makuburi, Kimara-Matosa-Mbezi;
Ubungo-Msewe-Chuo Kikuu na nyingine katika maeneo mengine.
Katika mwaka wa fedha 2012/2013 Mbunge
ataendelea kuisimamia serikali ili itenge bilioni 100 kujenga kwa kiwango cha
lami barabara tajwa za pembezoni za kupunguza msongamano haraka zaidi na pia
kuboresha usafiri wa maeneo ya pembezoni kwa kuwa baadhi ya barabara hizo
zilitengenezwa kwa kiwango cha changarawe kwenye mwaka wa fedha 2011/2012
lakini zimeharibika tena baada ya mvua zilizonyesha katika jiji la Dar es
salaam.
Katika mwaka wa fedha 2011/2012
tumefuatilia madaraja mbalimbali kujengwa ikiwemo Daraja Golani, Msewe, Matosa
nk pia kupitia mfuko wa maendeleo ya Jimbo (CDCF) vivuko kwa watembea kwa miguu
vimejengwa Makurumla na Msigani; orodha zaidi ya matengenezo ya barabara
yaliyofanyika inaweza kurejewa katika Ofisi ya Mbunge.
Kufuatia ufuatiliaji wa karibu kwa njia
mbalimbali hatua imechukuliwa ya kupeleka umeme katika eneo la Goba Matosa
(hata hivyo bado kuna malalamiko ya eneo lilirukwa la Mgeni Chongo) ambalo
tunaendelea kufuatilia.
Aidha, miradi iliyokuwa imekwama kwa
muda mrefu ya kupeleka umeme katika miradi ya maji ya King’ongo na Kilungule
inaendelea kutekelezwa kwa haraka zaidi. Mbunge amefuatilia mara kwa mara ahadi
ya Rais ya kupunguzwa kwa gharama za umeme na hatimaye ahadi imetolewa ya
utekelezaji kuanza kuanzia Januari 2013, pia kanuni za Februari 2011 zimetungwa
kuhusu kurejeshwa kwa gharama kwa wateja wanaolazimika kuvuta umeme zaidi ya
umbali wa kawaida.
Katika mwaka 2012/2013 mbunge ataendelea
kuisimamia serikali kurekebisha kanuni hizo kwa kuwa zina vifungu
visivyotekelezeka na kutaka pia gharama za nguzo na nyinginezo ziwekwe kwenye
bili ya mteja kama umeme uliolipiwa kabla. Orodha
ya maeneo mengine katika Jimbo la Ubungo ambayo ufuatiliaji umefanyika kuhusu
kusambaziwa umeme inapatikana katika Ofisi ya Mbunge.
MAJI:
Katika kufuatilia masuala ya maji
nilianza kwa kufanya Kongamano la Maji katika Jimbo la Ubungo mwanzoni mwa
mwaka 2011 ili kuwakutanisha wananchi, mamlaka husika na wadau wengine katika
kuunganisha nguvu kupata ufumbuzi.
Hatua nyingine zote nilizochukua baada
ya hapo zilikuwa ni za ufuatiliaji kuwezesha utekelezaji wa haraka. Nikiri
kwamba katika hatua za awali ushirikiano kutoka DAWASA, DAWASCO na Wizara ya
Maji ulikuwa mdogo kwa kiwango cha kuamua kuwaunganisha wananchi kupitia
‘maandamano ya maji’ kwenda DAWASCO. Toka wakati huo ushirikiano umeongezeka kwa
upande wa DAWASCO ambapo nimeshafanya nao ziara ya kikazi ya kata mbalimbali ya
kutembelea maeneo yenye matatizo na hatua zimechukuliwa ambazo zimewezesha
baadhi ya maeneo kuanza kutoka maji.
Pia, wakati wa hatua hizo nimewaonyesha
DAWASCO biashara haramu ya maji iliyokuwa ikiendelea na baadhi ya maeneo
wamechukua hatua ikiwemo kwa watendaji wao. Hata hivyo, udhaifu wa kimfumo
uliopo ni mkubwa kuliko hatua ambazo zimeweza kuchukuliwa mpaka sasa. Katika
mazingira hayo nilianza pia kutaka hatua za DAWASA na tayari nao nimefanya nao
ziara ya kikazi kwenye vyanzo vya maji pamoja na matenki ya maji, na kutaka
hatua za haraka za ushirikiano kati ya DAWASA na DAWASCO.
Kwa maana ya miradi ya muda mrefu ya
mwaka 2013/2014 kumetengwa fedha kuanzia mwaka 2012/2013 zaidi ya bilioni 200
kutokana na fedha za MCC na Mkopo wa India kwa ajili ya upanuzi wa vyanzo vya
Ruvu Juu na Ruvu Chini, ujenzi wa Bwawa la Kidunda na ujenzi wa mabomba mengine
miradi ambayo itagusa wananchi wa Ubungo. Hata hivyo, hatua hizi za muda mrefu
hazileti matumaini bila hatua za haraka ambazo zilipaswa kuchukuliwa katika
mwaka wa fedha 2011/2012.
Katika kuwezesha hatua za haraka kwa
mwaka wa fedha 2011/2012 nilifuatilia ratiba ya mgawo wa maji kuweza kutolewa
kwa mbunge na kwa ngazi za kata na mitaa na kufuatiliwa ili mgawo uwezeshe
kuheshimiwa bila ya upendeleo wa baadhi ya maeneo au hujuma kwa ajili ya
kuwezesha biashara haramu ya maji. Ofisi ya mbunge wakati wote imetaka kupatiwa
taarifa pale mamlaka husika au ngazi tajwa zinaposhindwa kufuatilia ratiba
husika ili kuweza kuingilia kati. Kuanza kuweka miundombinu ya maji katika
maeneo yaliyorukwa kwenye awamu ya kwanza ya uwekaji wa mabomba, tayari
utekelezaji umeshaanza katika maeneo ya Mbezi na maeneo mengine utafanyika
kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2013 kwa mujibu wa ahadi zilizotolewa na
DAWASCO/DAWASA kwa mbunge.
Katika kutekeleza ahadi ya kuhamasisha
ujenzi wa visima kwenye maeneo ambayo hayafikiki kirahisi na mtandao wa maji ya
bomba kama suluhisho la muda, huku tukifuatilia ufumbuzi wa kudumu katika
maeneo hayo, mbunge amefuatilia uchimbaji wa visima uliokuwa umesimama katika
maeneo ya Mavurunza/Bonyokwa, Kilungule na King’ongo kwa kwenda maeneo husika,
kuziandikia mamlaka zinazohusika na kuhoji kwenye vikao vya manispaa, bungeni
na kufanya ziara za ukaguzi wa maendeleo ya miradi.
Uzinduzi kwa miradi ya Mburahati
ulifanyika mwanzoni mwa mwaka 2011 na hatimaye sasa uzinduzi wa maeneo
yaliyotajwa utafanyika katika mwaka huu wa 2012 kwa kuratibiwa na DAWASA na
Wizara ya Maji.
Aidha, uchimbaji wa visima kama hivyo
unaendelea katika maeneo ya Saranga na Malambamawili. Aidha, kupitia miradi ya
Manispaa ikiwemo mradi unaofadhiliwa na benki ya dunia mbunge amefuatilia
uchimbaji katika maeneo ya Mpiji Magohe, Msakuzi, Makoka na Msumi ambao unasuasua
kutokana na udhaifu wa kiutendaji.
Mbunge ameunga mkono jitihada
zinazofanywa na wadau wengine wa maendeleo Jimboni Ubungo katika masuala ya
maji hususani Shirika la Kibelgiji (BTC) katika maeneo ya Kwembe na Kibamba na
amewasiliana na DAWASA/DAWASCO kwa ajili ya hatua za kusaidia miradi husika na
TANESCO kwa upande wa kuweka transfoma yenye uwezo mkubwa zaidi ili kuwezesha
pampu za maji kwenye maeneo husika ziweze kufungwa. Orodha ya maeneo mengine yaliyochimbwa visima vidogo ipo katika Ofisi
ya Mbunge.
Mbunge amefanikiwa kufanya suala la maji
kuwa moja ya masuala yanayojadiliwa mara kwa mara kwenye vikao vya Manispaa ya
Kinondoni hali ambayo haikuwepo kabla. Aidha alipendeza na hatimaye ukafanyika
ufuatiliaji wa miradi iliyo chini ya jamii au mamlaka za ngazi ya chini
iliyokwama kwa muda mrefu na hivyo kukosesha wananchi maji katika maeneo
mbalimbali ambayo hayapewi huduma ya moja kwa moja na DAWASA/DAWASCO. Kati ya
miradi hiyo baadhi imefufuliwa kama wa Msewe Golani na mingi inaendelea
kusuasua ikiwemo ya kata ya Goba. Mbunge amependekeza kwa DAWASA kwamba maeneo
ambayo hayakuwa yakihudumiwa na DAWASCO ikiwemo ya kata ya Goba yachukuliwe
moja kwa moja na mamlaka husika kwa kuwa kutokana na ongezeko la watu maeneo
hayo hayawezi kuhudumiwa kwa ufanisi na kamati za maji kama ilivyokuwa miaka ya
zamani.
Mbunge amefuatilia pia masuala ya bei na
ubora wa maji na kuitaka bei ya maji inayotozwa kwenye Viosk inaendana na
viwango vilivyopangwa na mamlaka husika (EWURA), kufuatia hatua hizo operesheni
zimefanyika katika maeneo ambayo yanatoza maji kinyume na bei iliyotangazwa na
DAWASCO imeingia mikataba na waendeshaji wa vioski husika kuhusu bei elekezi.
Hata hivyo, changamoto imeendelea kuwa ni usimamizi wa utawala wa sheria katika
kuhakikisha bei inayotozwa ni ile inayopaswa kutoswa kwa mujibu wa maagizo ya
EWURA. Katika kipindi husika mbunge ametaka pia EWURA itoe bei elekezi kwa
upande wa maji katika jiji la Dar es salaam kwa upande wa sekta binafsi ili
kudhibiti pia biashara holela ya maji ya kwenye malori. Katika mwaka wa fedha
2011/2012 EWURA iliahidi kutoa kanuni za kudhibiti biashara husika hatua ambayo
mpaka sasa haijachukuliwa, suala ambalo mbunge atalifuatilia katika mwaka wa
fedha 2012/2013.
UWAJIBIKAJI:
Mbunge amekuwa mstari wa mbele katika
kupambana na ufisadi na matumizi mabaya ya fedha ngazi mbalimbali ili kuchangia
katika kuhakikisha fedha nyingi
zinazopatikana kila mwaka zinatumika kuwahudumia wananchi, ikiwemo kwa kutaka kushughulikiwa
kwa mapungufu yaliyoanishwa na wakaguzi wa hesabu katika vipindi vilivyopita.
Mathalani mbunge amefuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya Ukaguzi Maalum
(Special Audit) ya Kituo cha Mabasi cha Ubungo uliofanyika mwaka 2009 lakini
utekelezaji wa matokeo ulikuwa ukisuasua. Alifanya hivyo kupitia bungeni na
katika vikao vya halmashauri ya Jiji la Dar es salaam na hatimaye baadhi ya
mapendekezo yametekelezwa ikiwemo kumwondoa mkandarasi aliyekuwa akikusanya
mapato chini ya kiwango; aidha mbunge ataendelea kufuatilia mapendekezo mengine
kuhusu mikataba mibovu iliyoingiwa katika kituo husika.
Mbunge amefanya hivyo vile vile kuhusu
vitega uchumi vingine vya Jiji la Dar es salaam ikiwemo Shirika la Usafiri Dar
es salaam (UDA). Aidha, kwa kushirikiana na madiwani amefuatilia pia miradi
hewa au ya chini ya kiwango iliyofanyika katika miundombinu, elimu na maji na
hatua mbalimbali zimechukuliwa kama zinavyoelezwa katika Taarifa za Ofisi ya
Mbunge.
Mbunge kupitia uwakilishi bungeni na
kupitia hatua zingine nje ya bunge amezifuatilia mamlaka za serikali kuhusu
masuala mbalimbali yanayowagusa wananchi wa Ubungo, mathalani EWURA katika
nishati/mafuta, SUMATRA katika usafiri na TANESCO katika umeme.
Katika mwaka wa fedha 2012/2013 mbunge
atafanya ziara za kikazi pamoja na mamlaka husika katika maeneo mbalimbali
yenye kero ili kuziwezesha kuendelea kuchukua hatua zaidi kuhusu maeneo hayo
kwa ajili ya kuchangia katika maendeleo ya wananchi na nchi kwa ujumla.
Mbunge amefanya mikutano na wananchi
katika kata zote 14 za Jimbo la Ubungo kwenye maeneo mbalimbali ya kiserikali
na ya kichama kwa ajili ya kutimiza wajibu wa uwakilishi kabla na baada ya
vikao vya bunge.
Aidha mbunge ameshiriki katika mikutano
ya wakazi ya masuala ya maendeleo jimboni kama ambavyo imetajwa katika Taarifa
ya Utendaji. Mbunge amewezesha ofisi ya mbunge kuwa vitendea kazi pamoja na
wasaidizi wawili wakati wote baada ya kukwama kupata vifaa kutoka kwenye mfumo
wa kawaida wa kiserikali.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2011/2012
maombi ya mbunge kupata ofisi ya kutumia jimboni kutoka kwenye majengo ya
manispaa au ya wilaya yalikataliwa na katika mwaka 2012/2013 mbunge ataweka
mkazo katika kufuatilia eneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya mbunge.
Aidha, mbunge amewajibika katika
kuisimamia serikali bungeni na kushiriki katika kutunga sheria. Rejea katika
ofisi ya Mbunge kuhusu kazi za mbunge bungeni inaeleza masuala ambayo mbunge
ameisimamia serikali bungeni, hatua zilizochukuliwa na serikali kupitia mchango
wake na pia sheria ambazo amewasilisha majedwali ya marekebisho katika vifungu
mbalimbali vilivyokubaliwa na vilivyokataliwa.
USALAMA:
Mbunge amechangia katika harambee ya
ujenzi wa Kituo cha Polisi Mavurunza ambapo vifaa vya awali vilichangiwa na
Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo (CDCF) lakini pia fedha taslimu zilichangwa na
mbunge kutoka mfuko wake binafsi. Aidha, kupitia CDCF mbunge amechangia pia
kwenye ujenzi wa Kituo kidogo cha Polisi Golani Msewe na pia kituo cha Polisi
Kata ya Sinza.
Pia, mbunge ameanza ufuatiliaji wa
ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kimara katika eneo lenye nafasi
tofauti na eneo la sasa la barabarani la Mbezi kwa Yusuph; kufuatia ufuatiliaji
wa mbunge tayari Wizara ya Mambo ya Ndani imeiandikia barua Manispaa ya
Kinondoni kuomba eneo.
Kadhalika, mbunge amefuatilia kuhusu
eneo la ujenzi wa kituo cha Polisi kata ya Goba ambapo kwa mujibu wa taarifa
toka ngazi ya kata eneo limekwishapatikana. Katika mwaka wa fedha 2012/2013
mbunge ataweka kipaumbele katika kazi ambazo zilianza kwenye mwaka wa fedha
2011/2012 ili ziweze kukamilika.
Mbunge ameshirikiana na polisi na
viongozi wa kata/mitaa kufanya harambee kuhakikisha doria inakuwepo ili kupunguza
vitendo vya wizi, ukabaji na ujambazi hususani kwenye maeneo yenye vitendo
vingi vya uhalifu mathalani ya Kimara B kupitia ulinzi shirikishi na polisi
jamii.
Aidha, ili kuwe na mfumo endelevu wa
kuhudumia vikundi vya ulinzi shirikishi mbunge alipendekeza kwamba masuala ya
ulinzi na usalama kuwa sehemu ya vipaumbele vya maendeleo katika mapato ya
ndani ya Manispaa kama ilivyo kwa sekta za elimu, afya, barabara nk. Kwa
usimamizi wa Meya pendekezo hilo liliingizwa kwenye baraza la madawani na
kutakiwa kutekelezwa kupitia fedha zinazobaki katika kata kutokana na ufanisi
katika makusanyo ya ndani ili kuimarisha ulinzi na usalama.
AFYA:
Mbunge
aliguswa na kasi ya kupungua kwa fedha za wahisani katika bajeti ya afya kwa
masuala ya matibabu kwa wanaoishi na UKIMWI/VVU, Wazee, Walemavu na wagonjwa wa
kifua kikuu, hivyo pamoja na kuhoji bungeni na kutaka nyongeza ya bajeti kwenye
Wizara ya Afya amechukua hatua jimboni kwenye ngazi ya Manispaa kwa kupendekeza
kiwango cha fedha toka vyanzo vya ndani kuongezwa hatua ambayo imeanza
kuchukuliwa kwa ajili ya mwaka wa fedha 2012/2013.
Kwa ajili ya afya mazingira mbunge
alipendekeza kwamba tathmini ifanyike kuhusu mfumo mzima wa uzoaji taka katika
kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo na Manispaa ya Kinondoni kwa ujumla kutokana
na kukithiri kwa uchafu katika maeneo mbalimbali. Kufuatia pendekezo hilo Meya
alifanya mkutano na wenyeviti wa mitaa na watendaji wengine ambapo maazimio ya
hatua mbalimbali yalifikiwa ambayo yameboresha uzoaji taka katika maeneo
machache. Hata hivyo, matatizo ya uchafu yameendelea katika maeneo mengi, hivyo
katika mwaka wa fedha 2012/2013 mbunge ataendelea kuisimamia serikali kuu na
serikali za mitaa katika kuchukua hatua kubwa zaidi kuhusu udhaifu wa kimfumo
ambao ulishababainishwa tayari unaochangia kasi ndogo ya uzoaji taka ngumu na
uondoaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam.
ARDHI:
Mbunge amefuatilia kwa ajili ya
kuhakikisha wananchi wa eneo la Ubungo Maziwa wanapewa fidia stahiki. Aidha,
mbunge amefuatilia na hatimaye fidia imeanza kulipwa kwa wananchi eneo la
Riverside wanaopaswa kubomolewa kupisha njia mbadala ya kwenda Kibangu.
Hata hivyo, suala la fidia ya ardhi kwa
upande wa wananchi wa Kwembe kupitisha ujenzi wa Chuo Kikuu eneo la Mlongazila
limekwama kwa Serikali kuchukua msimamo wa kutoa fidia ya maendelezo/mali pekee.
Mbunge anaendelea kufuatilia suala hilo katika mwaka wa fedha 2012/2013 kwa
kushirikiana na wananchi waliofungua kesi mahakamani wakati utekelezaji wa
mradi ukiendelea. Kwa upande mwingine, kiasi cha shilingi bilioni 10 kimeweza
kutengwa kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wa Ubungo walio karibu na
mitambo ya umeme ambao walikuwa wanadai fidia toka mwaka 2004.
Mbunge amesisitiza kupitia vikao vya Mkoa,
halmashauri ya Jiji, Manispaa na bunge kuhusu haja ya serikali kuweka
kipaumbele katika kusimamia mpangilio mzuri wa makazi na kuhamasisha upimaji wa
viwanja ili wananchi wapate hati na leseni za makazi kwa urahisi na kwa bei
nafuu kutokana na matatizo ya gharama kubwa na ucheleweshaji yaliyoko hivi
sasa. Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi amemjibu mbunge kuwa wizara
itawekwa mfumo ili hati iwe inatolewa kwa haraka katika muda usiozidi miezi
sita. Mbunge amefuatilia mradi wa urasimishaji unaofanywa na Ofisi ya Rais
(MKURABITA) katika eneo la Kimara Baruti, aidha mbunge ametaka elimu kutolewa
kwa wananchi na madiwani na watendaji wengine kuhusu namna fursa za upimaji na
urasimamishaji zinavyoweza kutumiwa katika maeneo yao.
Mbunge amefuatilia vile vile taarifa
kuhusu mji wa kiungani (Sattellite town) ya Luguruni na maeneo jirani ya mji
huo na kubaini kasoro kama zinavyoelezwa katika Taarifa ya Utendaji, aidha
Wizara imeahidi kwamba muendelezaji mwenza wa mji huo amepatikana na kwamba
kasoro zinazoendelea zitarekebishwa.
Mbunge amefuatilia kupitia hoja binafsi
na maswali katika manispaa na bungeni kuhakikisha viwanja vya umma vilivyouzwa
kinyume na taratibu na viwanja vya wazi vilivyovamiwa, vinarejeshwa. Mfano:
viwanja vya Makurumla, Sinza, Ubungo, Makuburi, Mbezi nk. Kufuatia hatua hizo,
sehemu ya viwanja hivyo imejadiliwa kwenye baraza la madiwani la manispaa ya
Kinondoni na pia Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi ametembelea kata ya
Sinza na kuweka mabango kwa ajili ya wahusika kubomoa. Katika mwaka wa fedha
2012/2013 mbunge ataendelea kufuatilia kwa karibu ili ubomoaji uanze.
HITIMISHO:
Nihitimishe
kwa kurejea msimamo wangu kuhusu kazi za mbunge ambao nimekuwa nao miaka mingi
kabla ya kuingia kwenye siasa na niliurudia mwanzoni mwaka 2010 wakati
natangaza nia ya kugombea Ubunge:
“Naamini kwamba mbunge (ambaye pia kwa nafasi yake
ni diwani katika halmashauri) ana wajibu katika maeneo makuu manne (kwa kadiri
ya umuhimu) katika kuwezesha maendeleo Jimboni kwake na kwa taifa kwa ujumla:
Mosi; kusikiliza na kuwakilisha wananchi, Pili; kuisimamia na kuiwajibisha serikali na viongozi wake, Tatu; kushiriki katika kutunga sheria, Nne; kuhamasisha upatikanaji wa huduma.
Hata hivyo, sehemu kubwa ya wabunge wetu hawaweki kipaumbele katika majukumu ya kwanza matatu ambayo ndio msingi wa ubunge wenyewe. Matokeo yake ni matakwa ya wananchi kutokuwakilishwa kikamilifu, ufisadi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na mikataba mibovu; uwepo wa sheria dhaifu na kutetereka kwa utawala wa sheria na mifumo ya haki masuala ambayo yanakwaza jitihada za maendeleo za wananchi binafsi za taifa kwa ujumla.
Wabunge wengi wanawaza kwamba jukumu kubwa la mbunge ni kutoa bidhaa na huduma kwa wananchi; wakiacha taifa katika lindi la umasikini na kufanya sehemu ya wananchi kujenga mazoea ya kutegemea hisani toka kwa viongozi wa umma na wafadhili wao.
Mwaka 2005 pamoja na majukumu hayo makuu matatu, nilizungumzia suala la mfuko wa maendeleo ya jimbo. Lakini si katika mwelekeo wa mfuko wa sasa uliopitishwa kuwa sheria. Kwa hiyo, wakati nikiunga mkono jukumu la mbunge kuhamasisha maendeleo na kushiriki kwenye shughuli za kijamii, siamini katika mazoea na mfumo wowote unaomfanya mbunge kuwa “mtoa bidhaa na huduma” (mithili ya ATM) kwani unarutubisha ufisadi wa kisiasa na kuhatarisha mwelekeo mzima wa utawala bora. Kama ambavyo siamini pia katika siasa chafu za rushwa, uongo na aina nyingine ya upofu wa kimaadili katika kampeni na uongozi kwa ujumla.
Haiwezekani wakati ambapo makisio yanaonyesha kwamba zaidi ya trilioni mbili (sawa na milioni milioni mbili) zinapotea kila mwaka kupitia misamaha ya kodi, upangaji bei hovyo kwa bidhaa za Tanzania, biashara haramu kati ya Tanzania na nchi za nje au makampuni ya kimataifa halafu wananchi wakubali kupumbazwa na bidhaa za milioni chache zinatolewa na viongozi wa umma walioshindwa kurekebisha hali hii”, Mwisho wa kunukuu. Msingi wa msimamo huu unaweza kurejewa kwa ukamilifu hapa: http://mnyika.blogspot.com/2010/03/natangaza-rasmi-dhamira-ya-kugombea.html
Mosi; kusikiliza na kuwakilisha wananchi, Pili; kuisimamia na kuiwajibisha serikali na viongozi wake, Tatu; kushiriki katika kutunga sheria, Nne; kuhamasisha upatikanaji wa huduma.
Hata hivyo, sehemu kubwa ya wabunge wetu hawaweki kipaumbele katika majukumu ya kwanza matatu ambayo ndio msingi wa ubunge wenyewe. Matokeo yake ni matakwa ya wananchi kutokuwakilishwa kikamilifu, ufisadi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na mikataba mibovu; uwepo wa sheria dhaifu na kutetereka kwa utawala wa sheria na mifumo ya haki masuala ambayo yanakwaza jitihada za maendeleo za wananchi binafsi za taifa kwa ujumla.
Wabunge wengi wanawaza kwamba jukumu kubwa la mbunge ni kutoa bidhaa na huduma kwa wananchi; wakiacha taifa katika lindi la umasikini na kufanya sehemu ya wananchi kujenga mazoea ya kutegemea hisani toka kwa viongozi wa umma na wafadhili wao.
Mwaka 2005 pamoja na majukumu hayo makuu matatu, nilizungumzia suala la mfuko wa maendeleo ya jimbo. Lakini si katika mwelekeo wa mfuko wa sasa uliopitishwa kuwa sheria. Kwa hiyo, wakati nikiunga mkono jukumu la mbunge kuhamasisha maendeleo na kushiriki kwenye shughuli za kijamii, siamini katika mazoea na mfumo wowote unaomfanya mbunge kuwa “mtoa bidhaa na huduma” (mithili ya ATM) kwani unarutubisha ufisadi wa kisiasa na kuhatarisha mwelekeo mzima wa utawala bora. Kama ambavyo siamini pia katika siasa chafu za rushwa, uongo na aina nyingine ya upofu wa kimaadili katika kampeni na uongozi kwa ujumla.
Haiwezekani wakati ambapo makisio yanaonyesha kwamba zaidi ya trilioni mbili (sawa na milioni milioni mbili) zinapotea kila mwaka kupitia misamaha ya kodi, upangaji bei hovyo kwa bidhaa za Tanzania, biashara haramu kati ya Tanzania na nchi za nje au makampuni ya kimataifa halafu wananchi wakubali kupumbazwa na bidhaa za milioni chache zinatolewa na viongozi wa umma walioshindwa kurekebisha hali hii”, Mwisho wa kunukuu. Msingi wa msimamo huu unaweza kurejewa kwa ukamilifu hapa: http://mnyika.blogspot.com/2010/03/natangaza-rasmi-dhamira-ya-kugombea.html
Hivyo,
ufanisi wa ubunge wangu upimwe kwa kuzingatia msimamo huo ambao niliwaeleza
wananchi wakati wa uchaguzi hivyo nilichaguliwa ikifahamika wazi kuwa huo ndio
wajibu ambao nitautekeleza katika kipindi cha miaka mitano.
Bado
naendelea kuamini kwamba jimbo la Ubungo na taifa kwa ujumla tutapiga hatua ya
haraka zaidi ya maendeleo kupitia mabadiliko katika mifumo yetu ya mgawanyo wa
rasilimali na usimamizi wa matumizi ya fedha za umma na pia kwa kuweka mazingira
bora ya kisera, kisheria na kiutendaji wa sekta binafsi.
Tuliyoyafanya
mpaka sasa ni sehemu tu katika mahitaji makubwa ya maendeleo kutokana na pengo
la miaka 50 ukilinganisha na fursa ambazo taifa letu linazo; hata hivyo naamini
miaka mitatu iliyobaki itafanya miaka mitano ya kuisimamia Serikali iliyopo
madarakani hivi sasa pamoja na udhaifu wote uliokuwepo kuleta tofauti katika
maendeleo majimboni. Ni katika muktadha huo wakati mwingine tunazimika
kuwakilisha na kuwasilisha matakwa ya wananchi namna hii: http://www.youtube.com/watch?v=ES4OMOD_xME
tukiamini kwamba watawala wenye dhamana kwa sasa ya kukusanya kodi watasikiliza
na kuzingatia vipaumbele vya maendeleo vya wananchi.
Aidha,
baada ya kazi mkutano wa nane wa bunge naomba kutumia fursa mjadala
utakaofuatia taarifa hii kupata maoni yenu kuhusu masuala ninayopaswa kuyapa
kipaumbele katika kuwawakilisha na kuwatumikia jimboni katika kipindi cha mwezi
Septemba mpaka Oktoba 2012 kabla ya kuanza kwa mkutano wa tisa wa bunge na pia
kuhusu maandalizi ya mwaka 2013. Kero nyingi zinazoendelea kuwepo kwa sasa ni
neema iliyojificha (blessing in disguise) ili tuendelee kuunganisha nguvu ya
umma kuendeleza wimbi la mabadiliko.
Narudia tena kuwakumbusha kuwa nguvu ile ile
tuliyoitumia kwenye kutafuta kura na kulinda kura ndio naiomba toka kwenu
katika hatua hii ya kufanya kazi za kuwezesha maendeleo kwa kutimiza wajibu
kila mmoja wetu kwa nafasi yake, kuisimamia serikali na kuunganisha rasilimali
za wadau wengine;
Maslahi ya Umma Kwanza.
Nimeandika
taarifa hii leo tarehe 21 Agosti 2012 siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwangu.
Wenu
katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
Jimboni-Ubungo
7 comments:
Kamanda hongera sana na Mungu akujalie. Napenda sana michango yako yenye mantiki pamoja na utendaji wako Bungeni na Jimboni kwako. Pia naomba umfikishie Mch.Msigwa salaam zangu hasa katika mchango wake alioutoa Bungeni ambao ulitugusa sana sisi wazalendo wa nchi hii. Ule mchango wake ni wa kipekee sana kwani haukuwa na elements zozote za ushabiki unaoharibu nchi yetu hasa Bunge letu la JMT. Hongera sana Mh.Mnyika.
Okangi.
nikupongeze kwa ufuatiliaji wako bungeni kwenye vikao mbalimbali. ongeza bidii kwenye suala la maji na barabara
Nakupongeza kwa uwakilishi mzuri na uwajibikaji. Pamoja na yote uliyoyasimamia, hususan maji, sinza D - madukani yote hadi Vatican bado maji ni tatizo, je, kwenye hili unalisemeaje ? Hatua gani zimechukuliwa na hali ikoje ? Mama Ipyana
Mheshimiwa Mbunge kwanza nakupongeza kwa kutoa taarifa juu ya utekelezaji wa ahadi zako. Very few MP do provide feedbacks. Pili nakuomba ujitahidi kuwasiliana na mamlaka husika ili kuweza kupanua huduma za zahanati ya Kimara, kwakweli inahudumia watu wengi sana, haina nafasi ya kutosha. Angalau ingeongezewa hadhi iweze hata kulaza wagonjwa. Pia kuna baadhi ya wilaya kuna kitu kinaitwa Community Health Fund (CHF) au mfuko wa afya ya jamii. ebu fuatilia suala hili ili wananchi wakowaweze kufaidika na huduma hii.
Tunakuamini, Tupo nyuma yako.
MDAU, Chuo Kikuu Ardhi.
Hongera sana Mh. JJ. Kama mwananchi mtarajiwa wa Msakuzi nikuombe tu kuwa mjadala wako angalau katika vikao vya manispaa pamoja na mambo mengine mengi yanayohusiana na maendeleo ya Jimbo letu, basi usisitize na kuiimiza serikali basi kuwa SIKU ZOTE WATU HUFUATA HUDUMA NA SI HUDUMA KUFUATA WATU. Hivyo, umeme na maji kwa maeneno hasa yanayokua Msakuzi, Kibamba, Kwembe, Mpigi n.k. TANESCO wasambaze nguzo ili kushawishi watu wahamie kwa haraka zaidi na kupunguza hadha za upangaji wa kihuni unaoathiri shughuli zetu za kila siku za kimaisha hapa mjini. Ni hayo tu Mh.
Inshallah, 2015 U A THE HERO with M4C YES WE CAN
Mheshimiwa mbunge, naomba kama unaweza jaribu kufuatialia barabara ya kutoka kwa Msuguri kwenda Msingwa ambayo ilijengwa kwa kuweka kifusi hafifi ili ccm watushawishi tuwapigie kura iligharimu shilingi ngapi za kitanzania. Kama unakumbuka hii barabara ilijengwa mwezi wa kumi kama sijakosea ilikuwa ni kipindi cha uchaguzi mkuu. juzi juzi walileta greda likaparuza kiaina pia ikumbukwe unapoleta greda na kuparuza unaondoa kokoto yote ambayo inazuia uterezi. kwa sasa makaravati mengi yapo kwenye hari ya kututenganisha na upande wa pili lakini yanaangaliwa tuu bila ya kuchukua hatua za makusudi ya kutengeneza.
Maji kwetu ni janga la kitaifa kwani tunalazimika kununua maji kwa bei ya juu sana yaani ndoo kwa sasa ni Tshs 500/=
Kuna malalamiko juu ya transforma inayopeleka umeme Msingwa kuwa ni ndogo sana kulinganisha na wakazi wa sasa wa msingwa. mbali na malalamiko hayo hakuna juhudi zozote zinazochukuliwa na Tanesco juu ya hili tatizo kibaya zaidi wanazidi kuunganishia wateja wakati transforma haitoshi. Amini usiamini jioni umeme ni low voltege mpaka kufikia 100/105 hii ni hatari kwa maisha ya vifaa vyetu.
Pia kun malalamiko kuhusu kamati ya maji ya Msingwa kuwa mapato ya maji hayako wazi! Kama ukiweza hebu jaribu kufatilia hayo.
Ahsante sana nakutakia kazi njema ya ujenzi wa Taifa lenye rasilimali lakini maskini wa kutupwa kwa sababu ya viongozi dhaifu!
Post a Comment