Wednesday, August 31, 2011

Salaam za Eid al-Fitr

Nawatakia heri waislamu wote wa jimbo la Ubungo na watanzania kwa ujumla katika kusherehekea sikukuu ya Eid al Fitri.

Aidha nawapongeza waislamu wote ambao waliweka mstari wa mbele usafi wa kweli katika mawazo na matendo katika kipindi chote cha mwezi mtukufu wa Ramadan.

Nawashukuru viongozi wote wa kislamu tulioshirikiana katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadan kwa namna mbalimbali katika kuhamasisha maendeleo ya kiimani na ya jamii kwa ujumla hususani kwa michango katika kufanikisha mashindano ya kuhifadhi Qur’an kwa wanawake kata ya Manzese, ununuzi wa jenereta na ujenzi wa msikiti katika kata ya Saranga.

Nawaomba tuendelee kushirikiana katika kipindi chote cha mwaka kwa kuwa taasisi za dini zina mchango mkubwa katika kudumisha maadili miongoni mwa wananchi na kuchangia katika maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Wakati wote kumbukeni Aya 185 Sura 2 (Al Baqara) na maneno mengine matukufu ili kuweka mbele swala, sadaka, uvumilivu na unyenyekevu katika matendo na maisha yetu ya kila siku.

Mwenyezi Mungu abariki umoja na mshikamano wa wananchi kwa ustawi na amani ya taifa letu.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)




Sunday, August 28, 2011

"Jairo", ufisadi wa kitaasisi na ombwe Ikulu

Toka mjadala almaarufu kama wa “Jairo” uanze nimekuwa kimya bila kutoa maoni yoyote hadharani. Nilikuwa kimya kwa sababu kubwa mbili; mosi, kwa kuwa Mkutano wa Bunge ulikuwa ukiendelea kama mbunge na waziri kivuli niliona nitumie fursa ya uwakilishi bungeni kuishauri na kuisimamia serikali katika suala hili na mengine. Pili, nilikuwa mmoja wa watu ambao walihojiwa na ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu suala hili; hivyo niliona busara nisiseme chochote hadharani mpaka pale taarifa ya uchunguzi husika itakapotolewa

Kwa kuwa hivi karibuni Katibu Mkuu kiongozi na CAG wametoa baadhi ya mambo ndani ya taarifa hiyo na kwa kuwa jana mkutano wa nne wa bunge umeahirishwa nimeona nichangie mawazo machache katika mjadala huu; katika muktadha wa majibu niliyopewa jana na Waziri wa Fedha Bungeni kufuatia maelezo niliyoomba kuhusu hatua ambazo amechukua kuhusu suala hili.

Katika kikao cha jana cha bunge wakati bunge lilipokaa kama kamati ya kupitia bajeti ya Wizara ya Fedha nilishika mshahara wa Waziri na kutaka kauli yake kwa kuwa Mlipaji Mkuu wa Serikali, Mhasibu Mkuu wako chini yake na pia jana ndio tulikuwa tunapitia pia Mafungu ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Hazina na taasisi nyingine za Wizara ya Fedha.

Hata hivyo, Waziri wa Fedha akakwepa kuwajibika katika suala ambalo liko kwenye mamlaka yake kwa mujibu wa sheria kwa kisingizio kwamba anasubiria kamati teule ya bunge iundwe kuhusu suala hilo.

Kwenye mkutano huu wa bunge kuanzia vikao vya mwanzo kabisa, nimesisitiza mara kwa mara kwamba matatizo mengi katika serikali kwa sasa yanatamalaki kutokana na ombwe la uongozi katika Ofisi ya Rais na Ikulu; hali inayohitaji Rais Jakaya Kikwete kutumia kwa uthabiti na umakini mamlaka makubwa aliyonayo kwa mujibu kwa katiba na sheria.

Sakata hili la “Jairo” ni moja ya matokeo tu ya hali hiyo ambayo kama isipodhibitiwa mapema mengine zaidi yataibuka kutokana na kuyumba kwa serikali. Ikiwa Rais anachelea kutumia ipasavyo mamlaka makubwa ya urais aliyonayo; njia mbadala ya kuongeza uthabiti na udhibiti wa serikali inaweza kuwa ni kuvunja baraza la mawaziri na kulisuka upya ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazolikumba taifa kwa sasa.

Mjadala huu unaoendelea hivi sasa ungekuwa na tija ya kutosha kama tungepata nakala kamili ya taarifa ya CAG kuhusu suala hili badala ya maelezo mafupi tu yaliyotolewa na Luhanjo na Utouh mbele ya wanahabari. Binafsi nakusudia kuwaandikia kuomba taarifa husika iwekwe hadharani ili watanzania wenye kutaka kutoa mchango wao kwa kamati teule ya bunge wafanye hivyo wakiwa pia na taarifa ya awali iliyofanywa tayari kwa gharama za walipa kodi.

Kwa maoni yangu sakata la “Jairo” lisichukuliwe kama ‘tukio pweke” (isolated event) bali litazamwe kuwa ni kiashiria cha matatizo makubwa zaidi katika mifumo ya matumizi ya fedha za umma ndani ya Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali. Hata hivyo, nilishangazwa zaidi na kauli ya katibu mkuu kiongozi- hata kwa maelezo tu aliyoyatoa mwenyewe kwenye vyombo vya habari amedhihirisha kwamba kuna ukiukaji wa sheria za fedha, ubadhirifu na ufisadi wa kitaasisi katika Wizara ya Nishati na Madini. Lakini inashangaza hatimaye akatoa kauli ya kuhitimisha kuwa ni utamaduni wa kawaida katika serikali na kwamba Jairo hana hatia yoyote.

Msingi wa kutoa hitimisho hili ulianzia naamini ulianza kutokana na udhaifu wa hadidu rejea ambazo wachunguzi wa ofisi ya CAG walikuwa nazo- kwa kipindi kifupi nilichokuwa karibu na Wizara hii nafahamu idadi ya idara, vitengo, wakala, mashirika na taasisi zilizoko chini yake.Ndio maana nikatahadharisha kwamba lazima uchunguzi uhusishe mfumo mzima ikiwemo maagizo ya barua ya Jairo na matokeo badala ya kujikita kwenye kauli za Shellukindo bungeni pekee. Na nilieleza matendo yanayoshabihiana na ya Jairo yaliyofanywa pia na Wizara nyingine kuanzia wakati wa kamati za Bunge Dar es salaam mpaka katika Mkutano huu wa bunge la bajeti katika kile kinachoitwa ‘kufanikisha kupitishwa kwa bajeti’. Kwa ujumla kuna mianya katika mifumo ya fedha ambayo imewezesha ubadhirifu na ufisadi wa kitaasisi.

Kutokana na kauli ya Waziri Mkuu kiongozi kuwa matendo kama aliyoyafanya Jairo ni ya kawaida katika Serikali; Waziri wa Fedha anapaswa kuwajibika kuchukua hatua badala ya kusubiri mpaka kamati teule imalize kazi yake.


Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Umma (Public Finnance Act no 6 of 2001); wajibu na mamlaka ya Waziri wa Fedha na Hazina kwa majibu wa 5(1) (i) ni kusimamia na kufuatilia masuala yote ya fedha za umma, 5(3) kudhibiti na kutoa muongozo kwa masuala yote ya kifedha ya serikali. Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha kama Mlipaji Mkuu ndiye anayesimamia udhibiti na utoaji fedha kwa Wizara na Idara mbalimbali za serikali nzima.

Jairo anaingia katika picha kwa Wizara yake kwa kuwa sheria hiyo kifungu 8(1) kimetoa mamlaka kwa Wizara ya Fedha kuteua Afisa Masuhuli (Accounting Officer) kwa Fungu husika ambapo kwa Wizara ya Nishati na Madini ni yeye kama katibu mkuu. Hivyo, kama katibu mkuu kiongozi Luhanjo amesema kwamba matendo hayo ni ya kawaida katika serikali nilitegemea kauli nzito toka kwa ama Waziri wa Fedha au Mlipaji Mkuu au Mhasibu Mkuu wa Serikali kukanusha ama kuunga mkono.

Ni wazi, kwa Wizara ya Nishati na Madini anayepaswa kuwajibika kiutendaji ni Jairo; ingawa Waziri na Naibu nao hawawezi kukwepa kuwajibika kisiasa kutokana na kadhia hiyo hasa baada ya kutoa kauli tata na tete mara baada ya Luhanjo ‘kumsafisha’ Jairo hali inayoaishiria kwamba ‘baraka’ zao zilikuwepo kwenye barua ya Jairo na matumizi yaliyofuatia. Aidha, pamoja na kukingwa na kifungu 8(2); Watendaji wa wakala, mashirika na taasisi yaliyohusika nao wana nafasi yao ya kuwajibika katika sakata nzima. Katika muktadha huo, mnyororo huu unaelekea kuwa mrefu lakini ni muhimu hatua za msingi zikachukuliwa ili kudhibiti hali hii ambayo imeelekea kuwa ni utamaduni wa ubadhirifu na ufisadi wa kitaasisi unaoitwa ‘wa kawaida’ kwenye serikali kwa muda mrefu.

Utetezi wa Luhanjo ambao unaelekea kuungwa mkono na baadhi ya watu ndani na nje ya serikali ni kwamba ‘CAG amekagua na kukuta hakuna fedha ambazo wabunge wamepewa rushwa ili kupitisha bajeti’. (Hili la Wabunge kupewa rushwa kupitisha bajeti, naomba nisilitoleee maoni hadharani katika hatua ya sasa kwa kuwa yapo masuala ambayo niyaeleza nilipohojiwa ambayo naamini ofisi ya CAG na mamlaka zingine naamini zinaendelea kuyafanyia kazi).

Tuchukue vigezo vya kimaamuma pekee na tutumie tu maelezo ambayo yametolewa na Katibu Mkuu Kiongozi na Mkaguzi Mkuu kwa waandishi wa habari halafu tuyalinganishe na misingi ya kisheria na kikanuni inayosimamia fedha za umma na utendaji wa kazi katika serikali. Kwa hayo tu, utabaini kwamba mamlaka hizi za kiserikali zimepuuzia ubadhirifu na ufisadi wa kitaasisi unaodhihirika katika Wizara ya Nishati na Madini.
Sheria ya Ukaguzi (Public Audit Act no. 11 of 2008) kifungu cha 10(1) kinampa jukumu CAG kufanya ukaguzi wa fedha za umma kwa niaba ya bunge (Hapa unaweza kujiuliza; kwa kuwa suala lilianzia bungeni na kwa kuwa CAG hufanya ukaguzi kwa niaba ya bunge- pamoja na kuwa katika suala la Jairo aliombwa na mamlaka za kiserikali, kwa nini haikuonekana haja ya bunge kupewa taarifa ya haraka kabla ya kwenda kwenye vyombo vya habari kusafishana?).

Kifungu cha 10 (2) (c) kinaelekeza matumizi yote ya umma yawe yameadhinishwa kwa kufuata utaratibu na yatumike kwa madhumuni kwayo yalipitishwa kwa mujibu wa sheria na maelekezo (appropriation laws and directives). (d) matumizi hayo lazima yafanyike kwa kuzingatia ufanisi na tija (economy, efficiency and effectiveness). Je, ni kwa kiwango gani matumizi hayo tuliyoelekezwa yamezingatia vigezo hivyo viwili vya msingi ambavyo CAG alipaswa kuvitumia katika ukaguzi wake?

Kifungu cha 12 kimempa mamlaka CAG kutoa mapendekezo ya kuzuia au kupunguza matumizi yasiyokuwa na tija ya fedha za umma (tujiulize, ni kwanini Luhanjo kama CAG alitoa mapendekezo ya namna hiyo au la?). Aidha kifungu hicho hicho kinatoa mwanya wa kutolewa mapendekezo ya kudhibiti uzembe, ukosefu wa uaminifu, ufisadi nk.
Naelewa kwamba ukaguzi uliofanyika sio wa kawaida, hivyo wengine wametumia sababu hiyo kujenga hoja kwamba halikuwa suala la bunge katika hatua ya sasa bali la mamlaka iliyoomba ukaguzi ufanyike.

Ni vyema tukarejea tena kwenye sheria husika kifungu cha 26 (2) ambayo inaelekeza kwamba CAG anaweza kufanya ukaguzi maalum kwa maombi ya mtu au taasisi; ukiondoa ukaguzi wa kawaida unaofanywa kwa mujibu wa sheria ama kwa azimio la bunge au kamati zake za usimamizi wa fedha za umma. Hata hivyo, izingatiwe kwamba Kifungu cha 36 (1) cha Sheria hiyo hiyo kinaeleza kwamba CAG anaweza akiona kwamba kuna jambo lolote la ukaguzi wowote lina maslahi ya umma na angependa kulitaarifu bunge sheria inaelekeza kwamba anaandaa ripoti maalum anamkabidhi Rais kwa mujibu wa sheria Rais anawajibika kuipeleka ripoti husika bungeni. Kwa kuwa suala hili la Jairo lilihusu tuhuma za Bunge, likatolewa kauli na Waziri Mkuu ambayo ndiye kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni kwamba analipeleka kwa Rais, Rais badala ya kutoa maagizo mwenyewe akaikabidhi mamlaka ya nidhamu ambayo ni Katibu Mkuu Kiongozi (Hapa Rais alipaswa kutambua kwamba suala hili halikuhusu Nidhamu tu ya Jairo, lilihusu masuala ya kimfumo na kifedha ya Wizara ambayo kwa mujibu wa katiba muhusika mkuu ni yeye au watendaji aliowateua kufanya kazi kwa niaba yake mf. Waziri Mkuu, Waziri wa Fedha, Mlipaji Mkuu nk).

Ni wazi kwamba ukaguzi huu maalum haukupaswa tu kuwa wa kawaida, CAG alipaswa kutumia vizuri pia kifungu cha 28 kwa kuingiza masuala ya kukagua ufanisi (economy, efficiency, effectiveness) katika hadidu rejea (a) kuhusiana na matumizi ya fedha na rasilimali (b) kuhusu utendaji wa maafisa masuhuli husika (Accounting officer), wakuu wa idara na watendaji wakuu wa wakala, taasisi na mashirika yaliyohusika. Ukaguzi wa namna hii ungeweza kuibua masuala ambayo yangehitaji sasa kufanyika ukaguzi wa kiuchunguzi (Forensic Audit) kwa ajili ya hatua za ziada. Kamati teule ya Bunge inaweza kupanua wigo zaidi kutoka pale CAG alipoishia ili kuwezesha bunge kutimiza wajibu wa kikatiba wa kuisamia serikali kuondokana na mfumo wa ubadhirifu na ufisadi wa kitaasisi.

Wenu katika utumishi wa umma,

JJ

Thursday, August 11, 2011

Muongozo kuhusu hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu

Leo tarehe 11 Agosti 2011 katika kikao cha 48 cha Mkutano wa Nne wa Bunge la Kumi nilitaka kuomba muongozo wa Spika kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la 2007 ) kifungu cha 68 (7) kuhusu maswali na majibu ya Waziri Mkuu na nikarejea pia kanuni ya 133 (1).

Hata hivyo, kabla hata ya kutoa maelezo kamili ya kuomba muongozo wa Spika nilizuiwa na Naibu Spika Mheshimiwa Job Ndugai (Mb) bila hata ya kusikilizwa muongozo ambao nilitaka kuomba kinyume na kanuni ya 5 (1) inayotaka Spika kuongoza Bunge kwa kuzingatia kanuni na pale ambapo kanuni hazijatoa muongozo Spika anapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia katiba, sheria nyingine za nchi, kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya awali na desturi za kibunge.

Naomba kutoa taarifa kwa umma kwamba sijaridhika na uamuzi uliofanywa na Naibu Spika Mheshimiwa Job Ndugai hivyo nawajulisha kwamba ninakusudia kuwasilisha malalamiko kwa mujibu wa kanuni za Bunge kifungu 5 (4) na 7 (3) mara baada ya kupata nakala ya kumbukumbu rasmi ya Bunge (Hansard) ya kikao husika.

Mara baada ya kunukuu kanuni husika nilipoanza tu kuzungumza kwamba katika kipindi cha Maswali na Majibu kwa Waziri Mkuu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amekuwa akitoa majibu yenye upotoshaji yasiyokuwa ya kweli; baada ya kauli hiyo kabla hata ya kumaliza maelezo niweze kuomba muongozo kwa Spika; Naibu Spika alinikatisha na kuninyima fursa ya kuomba muongozo kinyume na kifungu 68 (7) na 5 (1).

Naomba umma uelewe kwamba nilikuwa naelewa kwa kina mahitaji ya kanuni za bunge kifungu cha 133 na vipengele vyake kuanzia cha kwanza mpaka cha sita; ndio maana katika kuanza kuomba muongozo nikasoma kifungu cha 133(1).

Napenda umma ufahamu kwamba muongozo ambao nilitaka kuomba kwa Spika ni kwamba kumekuwa na kawaida ya Waziri Mkuu wakati akijibu maswali ya papo kwa papo kutoa maelezo yasiyokuwa ya kweli yenye upotoshaji ambayo ni kinyume cha katiba ya nchi, sheria mbalimbali pamoja na kanuni ikiwemo kanuni za bunge hivyo nilitaka Spika atoe muongozo wenye kumpa nafasi nyingine Waziri Mkuu kutoa ufafanuzi wa kweli kuhusu masuala husika ili kuepusha uwezekano wa wabunge kupoteza imani na Waziri Mkuu kwa mujibu wa kanuni za bunge kifungu cha 133.

Katika maelezo yangu ya kuomba muongozo huo nilikusudia kutaja mifano miwili mikubwa ya majibu ya Waziri Mkuu kwenye maswali ya papo kwa papo yasiyokuwa ya kweli yenye upotoshaji kuhusu kashfa ya Meremeta na kuhusu mgogoro katika Manispaa ya Arusha.

Ikumbukwe kwamba tarehe 14 Aprili 2011 wakati wa kikao cha saba cha mkutano wa tatu wa Bunge la Tanzania wakati wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, nilimuuliza Mheshimiwa Mizengo Pinda kuwa “Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye vile vile ni Mwenyekiti wa CCM amenukuliwa akizungumzia kuhusu haja ya Chama kinachotawala kujivua gamba. Kati ya mambo aliyoyazungumza ni pamoja na kuondokana na watuhumiwa wa ufisadi. Mheshimiwa Mkuu uliwahi kulieleza Bunge hili tukufu kwamba usingetaka kabisa kuzungumzia masuala ya Meremeta kwa sababu ni siri za Jeshi. Baada ya kauli hii ya Rais na dhamira hii ya kujivua gamba kuhusiana na masuala ya ufisadi. Je, uko tayari Mheshimiwa Waziri Mkuu kutaja wahusika wa Kampuni ya Meremeta na kuelekeza Serikali kuchukua hatua zinazostahili kuhusiana na tuhuma hizo? . Waziri Mkuu katika majibu yake Mheshimiwa Mizengo Pinda hakuitumia nafasi hiyo kurekebisha kauli zake zisizokuwa za kweli zenye upotoshaji alizozitoa kwa nyakati mbalimbali katika Bunge la Tisa kuhusu kashfa ya Meremeta.

Ikumbukwe pia kwamba tarehe 10 Februari 2011 katika kikao cha tatu cha mkutano wa pili wa Bunge la kumi Waziri Mkuu Mizengo Pinda akijibu maswali ya papo kwa papo ya Mheshimiwa Freeman Mbowe (Mb) kuhusu matukio yaliyojitokeza Arusha wakati na baada ya uchaguzi batili wa Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha. Tarehe 11 Agosti 2011 katika kipindi cha Maswali ya papo kwa papo ya Waziri Mkuu kuliulizwa maswali kuhusu maamuzi ya kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA ya tarehe 6 na 7 Agosti 2011 kwa kurejea pia mazungumzo baina ya Waziri Mkuu na viongozi wa taifa CHADEMA kuhusu muafaka batili juu ya mgogoro katika Halmashauri ya Jiji la Arusha na uamuzi wa kuwafukuza uanachama madiwani watano kutokana na kukiuka maagizo ya kamati kuu. Badala ya Waziri Mkuu kuitumia nafasi hiyo kutoa majibu yenye kulenga kutoa ufafanuzi wa kurekebisha upotoshaji uliofanyika awali Waziri Mkuu Mizengo Pinda akatoa majibu mengine yasiyokuwa ya kweli kuhusu mazungumzo yake na viongozi wa CHADEMA pamoja na uamuzi wa chama wa kuwafukuza uanachama madiwani waliokiuka maamuzi ya kamati kuu ya chama.

Majibu ya Waziri Mkuu kuhusu ufisadi wa Meremeta, matukio katika halmashauri ya Jiji la Arusha na masuala mengine ya kitaifa katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo yenye uhusiano na utekelezaji wa majukumu ya Waziri Mkuu yaliyoanishwa katika ibara ya 52 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yana mwelekeo wa kuvunja sheria ya maadili ya viongozi wa umma, sheria nyingine za nchi yetu pamoja na misingi muhimu ya utawala bora kama ambavyo nitafafanua katika hatua zinazofuata. Naomba umma upuuze upotoshaji uliofanywa na Naibu Spika Job Ndugai kuhusu muongozo nilioomba mpaka pale maamuzi yatakapofanywa na Kamati ya Kanuni za Bunge kwa mujibu wa kifungu 5(5) na Bunge kujulishwa.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)
Bungeni-Dodoma
11/08/2011

Wednesday, August 10, 2011

Hatma ya Bajeti ya Nishati na Madini



LEO TAREHE 10 AGOSTI 2011 NILIOMBA MUONGOZO WA SPIKA BUNGENI KWA MUJIBU WA KANUNI 68(7) KUTAKA SERIKALI ITOE MAELEZO KWANINI AHADI YA WAZIRI MKUU YA KUZISHIRIKISHA KAMATI ZA BUNGE KATIKA KUANDAA MPANGO WA DHARURA WA UMEME NA MAELEZO KUHUSU NISHATI NA MADINI HAIJATEKELEZWA NA KUTAKA MUONGOZO KUHUSU UTARATIBU GANI UTATUMIKA KUENDELEZA MJADALA TAREHE 13 AGOSTI. UKIREJEA MAJIBU YALIYOTOLEWA UTABAINI KWAMBA SERIKALI INAKUSUDIA ‘KUFUNIKA KOMBE MWANAHARAMU APITE’ KUHUSU BAJETI YA NISHATI NA MADINI; REJEA HAPA CHINI TAMKO LANGU LA TAREHE 8/8 TUSHIKIRIANE KUISIMAMIA SERIKALI KUTIMIZA WAJIBU

Itakumbukwa kwamba tarehe 18 Julai 2011 Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa hoja bungeni ya kuahirisha mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012 kwa mujibu wa kanuni za kudumu za bunge(toleo la 2007) kanuni ya 55 (3) (b) na 69 (1).

Waziri Mkuu alilieleza bunge kuwa serikali imetoa hoja ya kuahirisha mjadala wa bajeti ya Wizara husika ili kupata muda usiozidi wiki tatu wa kutoa maelezo kuhusu michango ya wabunge hususani kwa kuwasilisha mpango wa dharura wa kuondoa mgawo wa umeme kwa kuzishirikisha kamati za bunge.

Hata hivyo, ikiwa imesalia chini ya wiki moja kufikia tarehe ya kuendelea kwa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini tarehe 13 Agosti 2011 serikali bado haijazishirikisha kikamilifu kamati za bunge hususani ya nishati na madini pamoja na fedha na uchumi kama ilivyoahidi. Hatua za haraka zisipochukuliwa na uongozi wa bunge, kamati husika na wadau wengine serikali italeta maelezo yake yakiwa yamechelewa na hivyo kukosekana kwa muda wa marekebisho ya msingi kufanyika.

Hivyo, natoa mwito kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa kuwa ndiye mwenye dhamana ya Shughuli zote za Serikali Bungeni kwa mujibu wa katiba ibara ya 52 (2) hivyo anapaswa kuwajibika kutoa maelezo bungeni kuhusu sababu za kutozihusisha kamati za bunge mpaka hivi na kutimiza wajibu wa serikali kuwasilisha mpango wa dharura pamoja na marekebisho mengine ya kibajeti kwa kamati zinazohusika mapema iwezekanavyo.

Aidha, kwa umma una matarajio makubwa kuwa serikali itafanya marekebisho ya msingi katika bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ni muhimu kwa Spika wa Bunge Anna Makinda kutoa fursa ya mjadala kuendelea mara baada ya serikali kutoa maelezo na mpango wa dharura kwa kamati zitakazohusika za bunge pamoja na kambi rasmi ya upinzani kutoa maoni kabla ya mtoa hoja kupewa nafasi ya kujibu wa mujibu wa kanuni ya 99 (9). Hii italiwezesha bunge kutekeleza kwa ukamilifu wajibu wa kikatiba uliotajwa kwenye ibara ya 63 (3) (b) na (c).

Katika mpango wa dharura na maelezo yatayotolewa natarajia Serikali itazingatia mapendekezo tuliyotoa kambi rasmi ya upinzani kupitia Bajeti Mbadala ya Nishati na Madini na kuongeza kiwango cha bajeti kwa kiwango kisichopungua bilioni 977 kwa bajeti ya maendeleo pekee kwa kutumia vyanzo vya nyongeza vya mapato tulivyovitaja. (tofauti na ile ambayo serikali ilitenga awali Sh. Bilioni 452 kwa maendeleo ya nishati na Madini-Fungu 58 na 50).


Baadhi ya vyanzo hivyo ni kupunguza misamaha ya Kodi ikiwemo kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta Kampuni za Madini peke yake kutaongeza mapato ya shilingi bilioni 59. Kutoka Vyanzo vipya vya mapato tulivyovianisha; kwa upande wa sekta ya madini kwa Kurekebisha Kodi Sekta ya Madini peke yake tunaweza kukusanya shilingi bilioni 240 katika mwaka wa fedha 2011/2012. Kupunguza fedha kwenye Wizara zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida yasiyokuwa ya lazima na kuelekeza fedha katika miradi ya maendeleo hususani ya umeme na gesi. Wizara ya Nishati na Madini peke yake imepanga kutumia Sh. Bilioni 7.9 kulipana posho ambazo zinaweza kupunguzwa na kuongezwa kwenye ujenzi wa miundombinu wa Chuo Cha Madini Dodoma na na kuongeza kiwango cha fedha katika mfuko wa wachimbaji wadogo wa madini.


Kama sehemu ya vyanzo vya mapato tunatarajia kwamba serikali itatoa maelezo ya kukamilisha majadiliano ya ubia ama mikopo toka Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na washirika wengine isiyopungua bilioni 400 kwa ajili ya miradi ya umeme na gesi asilia. Pia, serikali itaeleza namna itavyoharakisha ufilisi wa IPTL ili kupata takribani bilioni 200 zilizohifadhiwa katika katika akaunti maalum (escrow account) na kuzielekeza kwenye kuliwezesha Shirika la Umeme (TANESCO) kuwekeza katika umeme na kukamilisha utekelezaji wa mpango maalum wa kurekebisha hali ya kifedha ya shirika. Aidha, zaidi ya bilioni 100 zingine zinaweza kuongezwa katika ujenzi wa miundombinu ya umeme kutoka kwenye fungu 98 kasma 4168 ya fedha za bajeti ambazo zimepitishwa bila kupangiwa matumizi halisi.


Tunaamini kwamba ongezeko hilo la bajeti litawezesha vipaumbele vifuatavyo kuzingatiwa kwa uzito unaostahili kwa kurejea mwelekeo wa matumizi ambao tuliuwasilisha kwenye bajeti mbadala ya Nishati na Madini tarehe 15 Julai 2011: Kuwekeza fedha za kutosha kwenye mpango wa dharura wa sekta ya umeme na Gesi ili kumaliza kabisa tatizo la nishati ya Umeme na kupunguza gharama za maisha. Hatua hizo ziambatane kuwekeza katika Bomba la Gesi kutoka Mtwara, pamoja na ujenzi wa mtambo wa kutengeneza Gesi (LPG extraction Plant) ili kuwezesha gesi kutumika kwenye magari, viwandani na majumbani. Kuhakikisha tunazalisha 360MW za umeme katika mwaka wa fedha 2011/2012 ili kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo wa miaka Mitano na kumaliza tatizo la mgawo wa umeme. Pamoja na ununuzi wa mitambo mingine kipaumbele kiwekwe pia kuanza kutekeleza miradi ya Kiwira, Stiggler Gorge, Ngaka na Mchuchuma Kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya usafirishaji na usambazaji wa umeme vijijini ili kuchangia katika ukuaji wa uchumi vijijini kama tulivyoshauri katika bajeti mbadala.


Aidha kufuatia Kamati Kuu ya CCM kutoa agizo lenye kukubaliana na maoni tuliyotoa kwenye Bajeti Mbadala ya Nishati na Madini tarehe 15 Julai 2011 kuhusu ongezeko la kodi katika mafuta ya taa; serikali ipaswa kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria ya fedha katika mkutano wa bunge unaoendelea ili kupunguza gharama za maisha kwa wananchi kwa kuondoa ongezeko kubwa lililofanywa kwenye kodi ya mafuta ya taa na pia kupunguza kodi zaidi kwenye dizeli na petrol kama tulivyoshauri.

Kwa upande wa sekta ya madini, pamoja na kushughulikia masuala ya mapato kama tulivyoyaeleza natarajia kwambaWaziri wa Nishati na Madini William Ngeleja atatoa maelezo na mpango wa kushughulikia masuala yote ya ufisadi na migogoro tuliyoyaeleza kwenye hotuba ya kambi ya upinzani tarehe 15 Julai 2011. Mathalani kuhusu mauzo na mabadilishano ya umiliki yaliyofanyika baina ya kampuni ya Australia (Mantra Resources) na Kampuni ya Urusi ya ARMZ Uranium Holding kampuni tanzu ya Rosato.

Mauzo hayo ambayo yanaelezwa kimataifa kuwa yamefanyika kwa bei ya dola 1.16 bilioni ambayo ni zaidi ya shilingi trilioni 2. Mauzo hayo yamehusisha kuhamishiana umiliki wa maeneo ya Tanzania Mkuju River (Namtumbo) na Bahi Kaskazini (Dodoma) bila serikali kupata mapato yanayostahili wala wananchi wa maeneo husika kunufaika.
Pia Serikali itoe maelezo kuhusu kutokutekelezwa kikamilifu kwa ahadi ya kumaliza migogoro katika sekta ya madini baina ya wachimbaji wakubwa na wachimbaji wadogo pamoja na kuepusha migogoro ya leseni mathalani mgogoro wa wachimbaji wadogo eneo la Winza wilaya ya Mpwapwa ambao serikali iliahidi bungeni tarehe 9 Julai 2010 kuumaliza ambapo mpaka hivi sasa wanaendelea kuhamishwa kwa nguvu.

Kadhalika Serikali itoa maelezo juu ya shughuli za New Alamasi Ltd iliyochimba almasi katika eneo la Luhumbo bila leseni stahiki, kiasi cha almasi iliyochimbwa kinyemela kwa kipindi chote tokea tarehe 1 Juni 1965 hadi tarehe 8 Mei 2000 (kwa miaka 35); zilizokoenda fedha zilizotokana na mauzo haramu ya almasi na hatua zilizochukuliwa kwa wahusika na ikiukaji wa sheria.

Wenu katika utumishi wa umma,


John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
Bungeni, Dodoma-08/08/2011











Wednesday, August 3, 2011

Kuhusu maamuzi dhaifu ya CC ya CCM juu ya nishati na madini

Maamuzi yaliyofanywa na kamati kuu ya CCM katika kikao chake cha tarehe 31 Agosti 2011 kuhusu masuala mbalimbali yanayolikabili taifa hususani kuhusu nishati na madini imethibitisha ulegelege na kupoteza mwelekeo kwa serikali na chama hicho kwa ujumla.

Aidha maagizo hayo bado ni legelege na hayawezi kutoa muongozo thabiti kwa serikali katika kukabiliana na changamoto za msingi zinazolikabili taifa kwa sasa katika sekta za nishati na madini.

Kwa nyakati mbalimbali kuanzia mwaka 2005 nimekuwa nikitoa kauli za kueleza kwamba CCM na serikali yake ni legelege kiuongozi na kimaadili hali ambayo inaathiri maisha ya wananchi na mustakabali wa nchi kwa ujumla.

Hatimaye mwezi Februari mwaka 2007 wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya CCM Mwenyekiti wa chama hicho Rais Jakaya Kikwete akatambua hali hiyo na kurejea kauli ya Mwalimu Julius Nyerere kwamba “chama legelege huzaa serikali legelege’ na kueleza dhamira ya kuondoa ulegelege huo kuanzia kwenye chama na hatimaye katika serikali.
Hata hivyo, maagizo yaliyotolewa na kamati kuu katika kikao chake cha tarehe 31 Agosti 2011 kuhusu bei ya mafuta ya taa, matatizo ya umeme na masuala ya madini yamedhihirisha kwamba CCM na serikali yake bado hawajaondokana na ulegelege ambao kama usipodhibitiwa ni hatari kwa hatma ya nchi kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Ni muhimu watanzania wakatambua kwamba Mwenyekiti wa CCM Rais Kikwete ambaye ndiye aliyeongoza kikao cha kamati kuu kilichotoa maagizo kuhusu bei ya mafuta ya taa, matatizo ya umeme na migogoro migodini ndiye kiongozi mkuu wa shughuli za serikali na mwenyekiti wa baraza la mawaziri ambalo vikao vyake vimejadili masuala hayo hayo na kupitisha maamuzi mabovu.

Aidha umma ukumbuke kwamba kabla ya Mkutano wa Nne wa Bunge hili la bajeti palifanyika vikao vya vyombo vya maamuzi vya CCM hususani sekretariati, kamati kuu na halmashauri kuu ambavyo vilijadili pamoja na ajenda nyingine hali ya siasa ikiwemo maandalizi ya bajeti na kushindwa kutoa maagizo muafaka kwa serikali hali ambayo imelitumbukiza taifa katika matatizo ya sasa.

Hivyo, maagizo yaliyotolewa kwa serikali na Kamati Kuu ya chama hicho ni ya kisiasa yenye kulenga kumkosha Rais Kikwete na CCM kufuatia malalamiko ya wananchi juu ya ugumu wa maisha na tishio la maandamano ya CHADEMA kuhusu maamuzi mabovu yaliyofanywa na serikali yaliyopitishwa kwa kura za wabunge walio wengi wa CCM bila kuzingatia maslahi ya wananchi.

Ikiwa maagizo hayo yametolewa kwa dhamira ya kweli ya chama kuisimamia serikali yanapaswa kuambatana na hatua ya Rais Kikwete kuvua magamba kwa kuvunja baraza la mawaziri kwa kushindwa kumshauri vizuri katika kuiongoza serikali.

Agizo la kamati kuu ya CCM la kuitaka serikali ‘kutafuta njia ya kushusha bei ya mafuta ya taa’ ni dhaifu kwa kuwa sababu ya kupanda kwa bei ya mafuta hayo inajulikana wazi kuwa ni kupandishwa kwa kodi kulikofanywa tarehe 22 Juni 2011 hivyo; Kamati Kuu ya CCM ilipaswa kutoa agizo la kukubaliana na maoni tuliyotoa kwenye Bajeti Mbadala ya Nishati na Madini tarehe 15 Julai 2011 na kuiagiza serikali kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria ya fedha katika mkutano wa bunge unaoendelea ili kupunguza gharama za maisha kwa wananchi kwa kuondoa ongezeko kubwa lililofanywa kwenye kodi ya mafuta ya taa na pia kupunguza kodi zaidi kwenye dizeli na petroli.

Azimio la kamati kuu kueleza kusikitishwa na tatizo la umeme halionyeshi CCM kuwaomba radhi watanzania kutokana na kuliingiza taifa katika hali hiyo kutokana na uzembe, ufisadi na udhaifu wa kiuongozi. Aidha, azimio hilo halionyeshi kamati kuu kutambua uzito wa tatizo hilo kwa kulitangaza kuwa janga la taifa au hali ya dharura yenye kuhitaji uwajibikaji wa pamoja ikiwemo wa Rais Kikwete badala yake imelichukulia kuwa ni suala la kurekebisha bajeti ya nishati na madini kwa kuambatanisha mpango wa dharura. Kamati Kuu ya CCM ingetambua tatizo la ukosefu wa nishati linavyoathiri uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kuwa ni janga la taifa ingetoa maagizo ya kukabiliana na maoni tuliyotoa kwenye bajeti mbadala ya nishati na madini tarehe 15 Julai 2011 ya kutaka sio tu kufanya marekebisho ya bajeti ya nishati na madini bali pia kwa Wizara ya Fedha kuwasilisha bajeti ya nyongeza (supplementary budget) ili kurekebisha kasoro zilizotokana na kupitishwa kwa bajeti finyu tarehe 21 Juni 2011. Aidha, kamati kuu ya CCM ingetambua kwamba taifa lipo kwenye hali ya dharura lingemtaka Rais Kikwete ambaye pia na mwenyekiti wa chama hicho kuwajibika kutumia mamlaka yake ya kikatiba ikiwemo ya hali ya dharura kuwezesha hatua za haraka kuchukuliwa.

Taarifa ya kwamba kamati kuu ya CCM imejadili masuala mengine kama ‘migogoro migodini’ na ‘kuagiza serikali kuyashughulikia kwani yanatatulika’ inaonyesha ulegelege na udhaifu wa chama hicho katika kuishauri na kuisimamia serikali. Kamati Kuu ya CCM ilipaswa kutoa maelekezo mahususi ya maeneo ya migogoro migodini kwa kuzingatia maoni tuliyoyatoa kwenye bajeti mbadala ya nishati na madini tarehe 15 Julai 2011. Aidha, Kamati Kuu ya CCM imejikita katika kutoa agizo la ujumla kuhusu migogoro migodini bila kutoa maagizo kuhusu suala muhimu zaidi kuhusu mapato katika madini na ufisadi katika sekta hiyo pamoja na gesi asilia. Kamati Kuu ya CCM ilipaswa kukubaliana na maoni tuliyotoa kwenye bajeti mbadala ya nishati na madini na kuiagiza serikali kuwasilisha muswada wa marekebisho ya kitabu cha mapato na sheria ya fedha ili kuongeza wigo wa mapato kwenye sekta ya madini na pia kuchukua hatua za kushughulikia ufisadi pamoja na kupanua uwekezaji katika gesi asilia ikiwemo ujenzi wa bomba la gesi.

Watanzania warejee hotuba ya bajeti mbadala ya nishati na madini ya kambi rasmi ya upinzani bungeni ambapo tulieleza bayana vyanzo vya matatizo kwenye sekta za nishati na madini ikiwemo suala la bei ya mafuta ya taa, tatizo la umeme, migogoro migodini na changamoto zingine na kueleza kwamba matatizo yamezidi kuongezeka baada ya kupitishwa kwa bajeti mbovu tarehe 21 Juni 2011 kwa kura za ndio za wabunge wa CCM bila kutanguliza mbele maslahi ya umma.

Umma ufahamu kwamba bajeti iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha Mustapha Mkullo tarehe 8 Juni 2011 ilishindwa kutenga fedha za kutosha za kushughulia matatizo ya umeme pamoja na upungufu wa gesi asilia ilipitia katika baraza la mawaziri chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete. Hata baada ya kambi rasmi ya upinzani kuwasilisha bajeti mbadala na serikali haikukubali kuzingatia maoni yaliyotolewa kwa uzito unaostahili.
Aidha muswada wa sheria ya fedha na marekebisho yake yaliyowasilishwa tarehe 22 Juni 2011 ambao uliongeza kodi kubwa katika mafuta ya taa na kuongeza misamaha ya kodi katika madini badala ya kupanua wigo wa mapato ulitokana na serikali inayoongozwa na CCM. Ikumbukwe kwamba wakati wa kujadiliwa sheria husika niliwasilisha marekebisho kwenye muswada yenye lengo la kupunguza kiwango cha kodi ambacho serikali ya CCM ilidhamiria kuongeza kwenye mafuta ya taa lakini yalikataliwa na serikali pamoja na wabunge wa CCM.

Bajeti ya Serikali pamoja na Sheria ya Fedha vyote vilipitishwa kwa kura ya ndio na wabunge wa CCM kwa kufuata kilichoelezwa kuwa ni msimamo wa chama uliofikiwa katika kikao cha kamati ya wabunge wa chama hicho (party caucus) kwa maelezo kwamba ni utekelezaji wa sera na ilani za chama hicho.

Sehemu kubwa ya Kamati Kuu ya CCM ni wabunge ambao tayari walishapiga kura bungeni kupitisha bajeti na sheria bila kuzingatia mahitaji ya nishati na madini kwa kuongeza gharama za maisha kwa wananchi kupitia kupandisha bei ya mafuta ya taa, kupitisha bajeti isiyokidhi mahitaji ya kukabiliana na matatizo ya umeme na kushindwa kupanua wigo wa mapato katika madini.

Hivyo, ni muhimu Rais Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM akaliomba radhi taifa kutokana na hali hiyo na pia CCM ikawaagize wabunge wake kuwaomba radhi wananchi wa majimbo yao na watanzania kwa kupiga kura ya ndio kwa kutanguliza mbele maslahi ya chama badala ya maslahi ya umma.

Aidha natoa mwito kwa kamati kuu za vyama vingine vyenye uwakilishi bungeni ikiwemo CHADEMA inayoongoza kambi rasmi ya upinzani bungeni kuitisha vikao vya dharura kabla ya mkutano wa bunge unaoendelea hivi sasa kumalizika kujadili hali ya siasa ili kutoa ushauri kwa wabunge wake na serikali kwa ujumla kwa ajili ya kulinusuru taifa kwa kuwa nchi ipo katika hali tete.

Izingatiwe kuwa Kwa sehemu kubwa matatizo katika sekta za nishati na madini yamechangiwa na sababu za kibinadamu za kutowajibika ipasavyo kisera, kimaamuzi, kiusimamizi na kiutendaji kwa viongozi wa kiserikali kuanzia kwa viongozi wakuu wa nchi, wizara na watendaji wengine na hivyo kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi na kuathiri uchumi wa nchi.

Uwajibikaji unahitajika ukiambatana na hatua za haraka za kusimamia sera sahihi, uongozi makini na taasisi thabiti zenye kuelewa kwamba sekta ya nishati ni moyo wa taifa na sekta ya madini ni mtaji wetu kwa sasa na kuchukua hatua kali dhidi ya ufisadi uliofanyika katika sekta husika, kufanya mapitio ya mikataba, kuharakisha utekelezaji wa mipango kwa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
Bungeni, Dodoma-02/08/2011

Tuesday, August 2, 2011

Kauli yangu kuhusu uuzwaji batili wa hisa na mali za UDA

Tarehe 27 Julai 2011 vyombo mbalimbali vya habari vimemnukuu Meya Wa Jiji la Dar es salaam Dkt. Didas Masaburi akieleza kilichoitwa maamuzi ya Baraza la Madiwani wa Jiji kuhusu kuvunja uongozi wa Shirika la Usafiri Dar es salaam (UDA) na kuunda kamati ya kuchunguza matatizo katika shirika hilo.

Tarehe 28 Julai 2011 vyombo mbalimbali vya habari vimemnukuu Meneja wa UDA, Victor Milanzi akimjibu Meya Masaburi kwa pamoja na mambo mengine kugoma kuondoka katika nafasi hiyo na kukanusha tuhuma zilizoelekezwa juu yake kuhusu ubadhirifu wa fedha za mauzo ya hisa za shirika hilo.

Kwa nafasi yangu ya ubunge ni mjumbe katika Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es salaam ambalo lina hisa 51% katika Shirika hilo na pia nawajibika kushiriki kuisimamia serikali kuu ambayo ina hisa 49% katika kampuni hivyo inanibidi kutoa kauli kuhusu upotoshaji unaondelea kufanywa na Meya Masaburi pamoja Meneja Milanzi kuhusu kashfa hii kupitia vyombo vya habari.

Naomba wakazi wa Dar es salaam na wananchi watanzania kwa ujumla wafahamu kwamba Meya Masaburi na Meneja Milanzi wote wawili ni sehemu ya matatizo ya UDA kwa kushiriki kwa kiwango kikubwa katika kukiuka sheria, kanuni na taratibu kwenye uendeshaji wa shirika bila kuzingatia kwa ukamilifu maslahi ya wasafiri na walipa kodi.

Meya Masaburi na Meneja Milanzi wote kwa nyakati mbalimbali wameshiriki katika kuachia maamuzi ya kifisadi ya kuuzwa kwa bei chee kwa hisa za kampuni ya UDA bila ya kuzingatiwa kwa sheria, kanuni na taratibu. Meneja Milanzi ameshiriki kuanzia hatua za mwanzo za mkataba kati ya UDA na Kampuni ya Simon Group mwaka 2009 wakati Meya Masaburi ameshiriki katika kubariki utekelezaji wa mkataba huo wa kifisadi mwaka 2011 bila kuzingatia sheria, kanuni na maslahi ya wananchi wa Dar es salaam.
Meneja Milanzi na bodi ya Wakurugenzi chini ya uenyekiti wa Iddi Simba wameshiriki katika kuingia mkataba mbovu na wa kifisadi wa mauzo ya kampuni hiyo huku sehemu ya fedha za malipo zikiingizwa kwenye akaunti za watu binafsi.

Meya Masaburi ametekeleza mkataba huo kinyume cha sheria, kanuni na maslahi ya umma kwa yeye binafsi kuhamisha umiliki wa kampuni ya UDA kwa Simon Group baada ya malipo ya milioni 285 tu sawa na asilimia 12.5 ya mauzo ya hisa hizo kupitia maamuzi yake ya tarehe 10 Juni 2011 wakati UDA ina mali zenye thamani ya zaidi ya bilioni 12.

Baada ya kufanya maamuzi hayo kinyume cha sheria, kanuni na maslahi ya wananchi Meya Masaburi amejaribu kujikosha kwa maamuzi batili ya vikao haramu vya kamati ya fedha na uongozi cha tarehe 29 Juni 2011 na Baraza la Madiwani la tarehe 20 Julai 2011.
Kwa nafasi yangu ya ubunge ni mjumbe wa kamati ya fedha na uongozi na pia ni mjumbe wa baraza la Madiwani na tarehe 20 Julai 2011 nilieleza mbele ya waandishi wa habari kwamba vikao hivyo vyote viwili vilikuwa batili kwa kuwa viliitishwa bila kuzingatia sheria na kanuni pia vilifanya maamuzi haramu ambayo hayakuzingatia sheria, kanuni na maslahi ya wananchi wa Dar es salaam.

Kama nilivyoelekeza kusudio siku hiyo, nitatoa waraka kwa wananchi wa Dar es salaam na mamlaka husika wenye kueleza msingi wa kupiga kura ya HAPANA siku hiyo kwa maamuzi yote haramu yaliyofanywa na vikao hivyo batili na kueleza kwa kina vifungu vya sheria, kanuni, mkataba na taratibu zilizokiukwa pamoja na kuwataja wa majina wahusika na kiwango cha fedha kilichotolewa. Hata hivyo, kabla ya kutoa waraka huo nimeona nitoe taarifa hii kwa umma ili mamlaka zote zinazohusika ziingilie kati na kuchukua hatua za haraka kunusuru mali na mwelekeo wa shirika la UDA.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda anapaswa kuingilia kwa kuchukua hatua stahiki za kuingoza serikali kupitia upya mkataba ulioingiwa na kutekelezwa kinyume cha sheria, kanuni na maslahi ya wananchi kati ya Jiji, UDA na Simon Group Limited. Maamuzi yaliyofanywa na Meya Masaburi na vikao vyake haramu vya jiji na vya UDA yanapaswa kubatilishwa. Aidha maamuzi ya bodi ya UDA chini ya uenyekiti wa Iddi Simba kwa miaka kadhaa yanapaswa kupitiwa upya kwa kuzingatia sheria, kanuni na maslahi ya umma.

Waziri wa Fedha Mustapha Mkullo anapaswa kuingilia kati kupitia Msajili wa Hazina na CHC ili kunusuru hisa za serikali kuu katika UDA pamoja na mali za shirika kwa ujumla wake. Izingatiwe kwamba tarehe 28 Februari 2011 ofisi ya Waziri Mkuu iliandika barua yenye kumbukumbu namba CAB. 185/295/01/27 ambayo Katibu Mkuu Hazina anayo nakala yake yenye kueleza bayana kwamba uuzwaji wa hisa ambazo hazijagawiwa (unallocated shares) uliokuwa ukifanywa na UDA haukuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma na kuagiza mchakato huo usitishwe na CHC kushirikishwa. Izingatiwe kwamba katika maamuzi haramu yaliyofanywa na Meya Masaburi tarehe 10 Juni 2011 Wizara ya Fedha (hazina) na CHC wote hawakushiriki kwenye kikao kilichoitwa cha wana hisa wa UDA wakati serikali kuu imekuwa na hisa 49%.

Kamati husika za Bunge hususani ya Miundo mbinu na ya Hesabu za Mashirika ya Umma ziingilie kati kwa haraka kwa kushirikiana na ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mamlaka ya Kudhibiti Manunuzi ya Umma(PPRA) na wabunge wa mkoa wa Dar es salaam.

Hatua hizo za haraka zitaokoa mali za umma, kuweka msingi wa kuboresha usafiri katika mkoa wa Dar es salaam na kuwezesha hatua za kisheria na kinidhamu kuchukuliwa kwa wahusika wote waliofikisha jiji na taifa katika hali hiyo.

Ikumbukwe kwamba masuala ya Mashirika na Makampuni yaliyo chini ya jiji la Dar es salaam nilianza kuyahoji katika vikao hususani vya kamati ya fedha na uongozi mara baada ya kuingia katika utumishi wa umma kwenye Halmashauri ya Jiji kupitia mikutano ya mwezi Machi na Mei 2011.

Hata hivyo, badala ya Mstahiki Meya Masaburi kuchukua hatua stahiki kama ilivyoazimiwa katika vikao hivyo akaenda kufanya maamuzi binafsi ambayo yameongeza ukubwa wa matatizo badala ya kuyapunguza.

Kutokana na hali hiyo mwezi Juni nikaamua kutumia fursa za kibunge katika kushughulikia hatma ya UDA na usafiri mkoani Dar es salaam kwa ujumla wake.
Hivyo, wakati wa mjadala wa Azimio la kuliongezea muda Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) tarehe 23 Juni 2011 nilihoji kwa maandishi kuhusu mauzo ya hisa na mali za kampuni ya UDA na kutaka hatua za haraka kuchukuliwa kwa kurejea pia ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) . Hata hivyo, Waziri wa Fedha Mustapha Mkullo kwenye majumuisho yake hakutoa kauli wala kuchukua hatua za haraka pamoja na kuwa hatma ya hisa 51% za shirika hilo zinahusu Wizara yake kupitia Msajili wa Hazina.

Nikarudia tena kuhoji kwa maandishi wakati wa mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyowasilishwa tarehe 23 Juni 2011 nikipinga uuzwaji wa hisa za UDA bila maslahi ya usafiri wa wananchi wa Dar es salaam kuzingatiwa na kutaka kuwe na uhusiano baina ya hatma ya UDA na Mradi wa Mabasi yaendayo kwa Haraka (DART) ambao unaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu. Nilihoji suala hilo kama sehemu ya hitaji la kuwa na mfumo thabiti wa Usafiri wa Halaiki wa Umma (Mass Public Transit) ambao utachangia kwa kiwango kikubwa kupunguza adha ya usafiri katika jiji la Dar es salaam.

Hatahivyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika majumuisho ya bajeti yake tarehe 1 Julai 2011 hakutoa kauli wala kuchukua hatua za haraka za kunusuru hali ya mambo pamoja na kuwa yeye ndiye mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) hivyo ana wajibu wa kufuatilia masuala ya kisheria, kinanuni na kimikataba ya Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam kama ilivyo kwa halmashauri zingine.

Baada ya hapo ndipo kashfa ya UDA ikaanza kujitokeza kwenye vyombo vya habari tarehe 11 Julai 2011 ikiwa katika sura ya mzozo baina ya Meneja Milanzi na Mkurugenzi Kisena wa Simon Group Limited katika hatua za kulazimishana kuondoka ofisini.

Kufuatia hali hiyo tarehe 15 Julai 2011 baada ya majibu ya swali la msingi nililouliza Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu ukaguzi maalum wa mahesabu na ufisadi katika kituo cha Mabasi cha Ubungo (UBT) niliuliza swali la nyongeza kuhusu kashfa ya kampuni ya UDA kutokana na uhusiano wake na mradi wa DART ambapo maeneo ya UBT na UDA yatahusika. Katika swali langu nilitaka hatua za haraka kuchukuliwa na serikali kutokana na mauzo hayo kuendelea bila kuzingatia sheria, kanuni na maslahi ya wananchi hata hivyo Naibu Waziri Aggrey Mwanri hakutoa majibu ya kuridhisha wala kuchukua hatua zinazostahili kufuatia suala hilo hali ambayo ilitoa mwanya kwa Meya Masaburi kuendelea na mchakato haramu. Katika muktadha huo nitaendelea kushirikiana na madiwani wenzangu wenye kutanguliza mbele maslahi ya umma ikiwemo wabunge wa mkoa wa Dar es salaam ambao mimi ni katibu wao pamoja na mamlaka zingine za kiserikali na kibunge katika kushughulikia suala hili. Natoa mwito kwa wananchi wa Dar es salaam kutuunga mkono katika kulifuatilia kwa karibu suala hili na kuchukua hatua zinazostahili kila mmoja kwa nafasi yake.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)
Bungeni-Dodoma
31 Julai 2011