Tuesday, August 2, 2011

Kauli yangu kuhusu uuzwaji batili wa hisa na mali za UDA

Tarehe 27 Julai 2011 vyombo mbalimbali vya habari vimemnukuu Meya Wa Jiji la Dar es salaam Dkt. Didas Masaburi akieleza kilichoitwa maamuzi ya Baraza la Madiwani wa Jiji kuhusu kuvunja uongozi wa Shirika la Usafiri Dar es salaam (UDA) na kuunda kamati ya kuchunguza matatizo katika shirika hilo.

Tarehe 28 Julai 2011 vyombo mbalimbali vya habari vimemnukuu Meneja wa UDA, Victor Milanzi akimjibu Meya Masaburi kwa pamoja na mambo mengine kugoma kuondoka katika nafasi hiyo na kukanusha tuhuma zilizoelekezwa juu yake kuhusu ubadhirifu wa fedha za mauzo ya hisa za shirika hilo.

Kwa nafasi yangu ya ubunge ni mjumbe katika Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es salaam ambalo lina hisa 51% katika Shirika hilo na pia nawajibika kushiriki kuisimamia serikali kuu ambayo ina hisa 49% katika kampuni hivyo inanibidi kutoa kauli kuhusu upotoshaji unaondelea kufanywa na Meya Masaburi pamoja Meneja Milanzi kuhusu kashfa hii kupitia vyombo vya habari.

Naomba wakazi wa Dar es salaam na wananchi watanzania kwa ujumla wafahamu kwamba Meya Masaburi na Meneja Milanzi wote wawili ni sehemu ya matatizo ya UDA kwa kushiriki kwa kiwango kikubwa katika kukiuka sheria, kanuni na taratibu kwenye uendeshaji wa shirika bila kuzingatia kwa ukamilifu maslahi ya wasafiri na walipa kodi.

Meya Masaburi na Meneja Milanzi wote kwa nyakati mbalimbali wameshiriki katika kuachia maamuzi ya kifisadi ya kuuzwa kwa bei chee kwa hisa za kampuni ya UDA bila ya kuzingatiwa kwa sheria, kanuni na taratibu. Meneja Milanzi ameshiriki kuanzia hatua za mwanzo za mkataba kati ya UDA na Kampuni ya Simon Group mwaka 2009 wakati Meya Masaburi ameshiriki katika kubariki utekelezaji wa mkataba huo wa kifisadi mwaka 2011 bila kuzingatia sheria, kanuni na maslahi ya wananchi wa Dar es salaam.
Meneja Milanzi na bodi ya Wakurugenzi chini ya uenyekiti wa Iddi Simba wameshiriki katika kuingia mkataba mbovu na wa kifisadi wa mauzo ya kampuni hiyo huku sehemu ya fedha za malipo zikiingizwa kwenye akaunti za watu binafsi.

Meya Masaburi ametekeleza mkataba huo kinyume cha sheria, kanuni na maslahi ya umma kwa yeye binafsi kuhamisha umiliki wa kampuni ya UDA kwa Simon Group baada ya malipo ya milioni 285 tu sawa na asilimia 12.5 ya mauzo ya hisa hizo kupitia maamuzi yake ya tarehe 10 Juni 2011 wakati UDA ina mali zenye thamani ya zaidi ya bilioni 12.

Baada ya kufanya maamuzi hayo kinyume cha sheria, kanuni na maslahi ya wananchi Meya Masaburi amejaribu kujikosha kwa maamuzi batili ya vikao haramu vya kamati ya fedha na uongozi cha tarehe 29 Juni 2011 na Baraza la Madiwani la tarehe 20 Julai 2011.
Kwa nafasi yangu ya ubunge ni mjumbe wa kamati ya fedha na uongozi na pia ni mjumbe wa baraza la Madiwani na tarehe 20 Julai 2011 nilieleza mbele ya waandishi wa habari kwamba vikao hivyo vyote viwili vilikuwa batili kwa kuwa viliitishwa bila kuzingatia sheria na kanuni pia vilifanya maamuzi haramu ambayo hayakuzingatia sheria, kanuni na maslahi ya wananchi wa Dar es salaam.

Kama nilivyoelekeza kusudio siku hiyo, nitatoa waraka kwa wananchi wa Dar es salaam na mamlaka husika wenye kueleza msingi wa kupiga kura ya HAPANA siku hiyo kwa maamuzi yote haramu yaliyofanywa na vikao hivyo batili na kueleza kwa kina vifungu vya sheria, kanuni, mkataba na taratibu zilizokiukwa pamoja na kuwataja wa majina wahusika na kiwango cha fedha kilichotolewa. Hata hivyo, kabla ya kutoa waraka huo nimeona nitoe taarifa hii kwa umma ili mamlaka zote zinazohusika ziingilie kati na kuchukua hatua za haraka kunusuru mali na mwelekeo wa shirika la UDA.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda anapaswa kuingilia kwa kuchukua hatua stahiki za kuingoza serikali kupitia upya mkataba ulioingiwa na kutekelezwa kinyume cha sheria, kanuni na maslahi ya wananchi kati ya Jiji, UDA na Simon Group Limited. Maamuzi yaliyofanywa na Meya Masaburi na vikao vyake haramu vya jiji na vya UDA yanapaswa kubatilishwa. Aidha maamuzi ya bodi ya UDA chini ya uenyekiti wa Iddi Simba kwa miaka kadhaa yanapaswa kupitiwa upya kwa kuzingatia sheria, kanuni na maslahi ya umma.

Waziri wa Fedha Mustapha Mkullo anapaswa kuingilia kati kupitia Msajili wa Hazina na CHC ili kunusuru hisa za serikali kuu katika UDA pamoja na mali za shirika kwa ujumla wake. Izingatiwe kwamba tarehe 28 Februari 2011 ofisi ya Waziri Mkuu iliandika barua yenye kumbukumbu namba CAB. 185/295/01/27 ambayo Katibu Mkuu Hazina anayo nakala yake yenye kueleza bayana kwamba uuzwaji wa hisa ambazo hazijagawiwa (unallocated shares) uliokuwa ukifanywa na UDA haukuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma na kuagiza mchakato huo usitishwe na CHC kushirikishwa. Izingatiwe kwamba katika maamuzi haramu yaliyofanywa na Meya Masaburi tarehe 10 Juni 2011 Wizara ya Fedha (hazina) na CHC wote hawakushiriki kwenye kikao kilichoitwa cha wana hisa wa UDA wakati serikali kuu imekuwa na hisa 49%.

Kamati husika za Bunge hususani ya Miundo mbinu na ya Hesabu za Mashirika ya Umma ziingilie kati kwa haraka kwa kushirikiana na ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mamlaka ya Kudhibiti Manunuzi ya Umma(PPRA) na wabunge wa mkoa wa Dar es salaam.

Hatua hizo za haraka zitaokoa mali za umma, kuweka msingi wa kuboresha usafiri katika mkoa wa Dar es salaam na kuwezesha hatua za kisheria na kinidhamu kuchukuliwa kwa wahusika wote waliofikisha jiji na taifa katika hali hiyo.

Ikumbukwe kwamba masuala ya Mashirika na Makampuni yaliyo chini ya jiji la Dar es salaam nilianza kuyahoji katika vikao hususani vya kamati ya fedha na uongozi mara baada ya kuingia katika utumishi wa umma kwenye Halmashauri ya Jiji kupitia mikutano ya mwezi Machi na Mei 2011.

Hata hivyo, badala ya Mstahiki Meya Masaburi kuchukua hatua stahiki kama ilivyoazimiwa katika vikao hivyo akaenda kufanya maamuzi binafsi ambayo yameongeza ukubwa wa matatizo badala ya kuyapunguza.

Kutokana na hali hiyo mwezi Juni nikaamua kutumia fursa za kibunge katika kushughulikia hatma ya UDA na usafiri mkoani Dar es salaam kwa ujumla wake.
Hivyo, wakati wa mjadala wa Azimio la kuliongezea muda Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) tarehe 23 Juni 2011 nilihoji kwa maandishi kuhusu mauzo ya hisa na mali za kampuni ya UDA na kutaka hatua za haraka kuchukuliwa kwa kurejea pia ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) . Hata hivyo, Waziri wa Fedha Mustapha Mkullo kwenye majumuisho yake hakutoa kauli wala kuchukua hatua za haraka pamoja na kuwa hatma ya hisa 51% za shirika hilo zinahusu Wizara yake kupitia Msajili wa Hazina.

Nikarudia tena kuhoji kwa maandishi wakati wa mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyowasilishwa tarehe 23 Juni 2011 nikipinga uuzwaji wa hisa za UDA bila maslahi ya usafiri wa wananchi wa Dar es salaam kuzingatiwa na kutaka kuwe na uhusiano baina ya hatma ya UDA na Mradi wa Mabasi yaendayo kwa Haraka (DART) ambao unaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu. Nilihoji suala hilo kama sehemu ya hitaji la kuwa na mfumo thabiti wa Usafiri wa Halaiki wa Umma (Mass Public Transit) ambao utachangia kwa kiwango kikubwa kupunguza adha ya usafiri katika jiji la Dar es salaam.

Hatahivyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika majumuisho ya bajeti yake tarehe 1 Julai 2011 hakutoa kauli wala kuchukua hatua za haraka za kunusuru hali ya mambo pamoja na kuwa yeye ndiye mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) hivyo ana wajibu wa kufuatilia masuala ya kisheria, kinanuni na kimikataba ya Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam kama ilivyo kwa halmashauri zingine.

Baada ya hapo ndipo kashfa ya UDA ikaanza kujitokeza kwenye vyombo vya habari tarehe 11 Julai 2011 ikiwa katika sura ya mzozo baina ya Meneja Milanzi na Mkurugenzi Kisena wa Simon Group Limited katika hatua za kulazimishana kuondoka ofisini.

Kufuatia hali hiyo tarehe 15 Julai 2011 baada ya majibu ya swali la msingi nililouliza Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu ukaguzi maalum wa mahesabu na ufisadi katika kituo cha Mabasi cha Ubungo (UBT) niliuliza swali la nyongeza kuhusu kashfa ya kampuni ya UDA kutokana na uhusiano wake na mradi wa DART ambapo maeneo ya UBT na UDA yatahusika. Katika swali langu nilitaka hatua za haraka kuchukuliwa na serikali kutokana na mauzo hayo kuendelea bila kuzingatia sheria, kanuni na maslahi ya wananchi hata hivyo Naibu Waziri Aggrey Mwanri hakutoa majibu ya kuridhisha wala kuchukua hatua zinazostahili kufuatia suala hilo hali ambayo ilitoa mwanya kwa Meya Masaburi kuendelea na mchakato haramu. Katika muktadha huo nitaendelea kushirikiana na madiwani wenzangu wenye kutanguliza mbele maslahi ya umma ikiwemo wabunge wa mkoa wa Dar es salaam ambao mimi ni katibu wao pamoja na mamlaka zingine za kiserikali na kibunge katika kushughulikia suala hili. Natoa mwito kwa wananchi wa Dar es salaam kutuunga mkono katika kulifuatilia kwa karibu suala hili na kuchukua hatua zinazostahili kila mmoja kwa nafasi yake.

Wenu katika utumishi wa umma,

John Mnyika (Mb)
Bungeni-Dodoma
31 Julai 2011

4 comments:

Anonymous said...

Jamaniii ONLY in Tanzania you can do that...watu wa Dar es Salaam tuko wapi kusimama nyuma ya Mnyika?? tuwe nyuma ya Mnyika tuokoe hii nchi.

Anonymous said...

2po pamoja na wbunge wanaolitetea taifa katika ufisad na mambo mengine yenye maslai kwa taifa.mh 2naziona juhud zako 2po nyuma yako.upo mkini katika mambo yako endelea na moyo huo huo na MWENEZI MUNGU atakujaalia.wing wao bungeni usiwachoshe endeleen na moyo huohuo sisi tupo nyuma yenu!!hakuna kitakachoishinda nguvu ya umma...

Anonymous said...

kaka na mheshimiwa mimi kama mtanzania niliyechoka na UFISADI niko nyuma yako nakuombea wewe pamoja na wabunge wengine wenye msimamo kama wako, OMBI tujaribu kuwaelimisha watu wavijijini kwani ndiko tunakoanguka tufanye mikutano huko mara kwa mara ilikuwatoa kwenye giza la ujinga

Anonymous said...

DAWA NI KUKOMAA MPAKA KIELEWEKE NIVIZURI KUWEKA MAMBO SAWA MUDA NDOO HUU CCM INAPUNGUA UMAARUFU NA TENA VIONGOZI NA WANACHAMA WAMEPAGAWA HAWAJUI WAPI WASHIKE ILI KURUDISHA IMANI KWA WANANGHI MIMI KAMA MWAKATAGE NAOMBA TU TUWENA MSIMAMO ISTOKEE SISI KURUMBANA TUKAWAPA SIFA MAFISADI KUTUONGELEA NIMIMI MWAKATAGE CHADEMA DAMU