Sunday, August 28, 2011

"Jairo", ufisadi wa kitaasisi na ombwe Ikulu

Toka mjadala almaarufu kama wa “Jairo” uanze nimekuwa kimya bila kutoa maoni yoyote hadharani. Nilikuwa kimya kwa sababu kubwa mbili; mosi, kwa kuwa Mkutano wa Bunge ulikuwa ukiendelea kama mbunge na waziri kivuli niliona nitumie fursa ya uwakilishi bungeni kuishauri na kuisimamia serikali katika suala hili na mengine. Pili, nilikuwa mmoja wa watu ambao walihojiwa na ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu suala hili; hivyo niliona busara nisiseme chochote hadharani mpaka pale taarifa ya uchunguzi husika itakapotolewa

Kwa kuwa hivi karibuni Katibu Mkuu kiongozi na CAG wametoa baadhi ya mambo ndani ya taarifa hiyo na kwa kuwa jana mkutano wa nne wa bunge umeahirishwa nimeona nichangie mawazo machache katika mjadala huu; katika muktadha wa majibu niliyopewa jana na Waziri wa Fedha Bungeni kufuatia maelezo niliyoomba kuhusu hatua ambazo amechukua kuhusu suala hili.

Katika kikao cha jana cha bunge wakati bunge lilipokaa kama kamati ya kupitia bajeti ya Wizara ya Fedha nilishika mshahara wa Waziri na kutaka kauli yake kwa kuwa Mlipaji Mkuu wa Serikali, Mhasibu Mkuu wako chini yake na pia jana ndio tulikuwa tunapitia pia Mafungu ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Hazina na taasisi nyingine za Wizara ya Fedha.

Hata hivyo, Waziri wa Fedha akakwepa kuwajibika katika suala ambalo liko kwenye mamlaka yake kwa mujibu wa sheria kwa kisingizio kwamba anasubiria kamati teule ya bunge iundwe kuhusu suala hilo.

Kwenye mkutano huu wa bunge kuanzia vikao vya mwanzo kabisa, nimesisitiza mara kwa mara kwamba matatizo mengi katika serikali kwa sasa yanatamalaki kutokana na ombwe la uongozi katika Ofisi ya Rais na Ikulu; hali inayohitaji Rais Jakaya Kikwete kutumia kwa uthabiti na umakini mamlaka makubwa aliyonayo kwa mujibu kwa katiba na sheria.

Sakata hili la “Jairo” ni moja ya matokeo tu ya hali hiyo ambayo kama isipodhibitiwa mapema mengine zaidi yataibuka kutokana na kuyumba kwa serikali. Ikiwa Rais anachelea kutumia ipasavyo mamlaka makubwa ya urais aliyonayo; njia mbadala ya kuongeza uthabiti na udhibiti wa serikali inaweza kuwa ni kuvunja baraza la mawaziri na kulisuka upya ili kuongeza uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazolikumba taifa kwa sasa.

Mjadala huu unaoendelea hivi sasa ungekuwa na tija ya kutosha kama tungepata nakala kamili ya taarifa ya CAG kuhusu suala hili badala ya maelezo mafupi tu yaliyotolewa na Luhanjo na Utouh mbele ya wanahabari. Binafsi nakusudia kuwaandikia kuomba taarifa husika iwekwe hadharani ili watanzania wenye kutaka kutoa mchango wao kwa kamati teule ya bunge wafanye hivyo wakiwa pia na taarifa ya awali iliyofanywa tayari kwa gharama za walipa kodi.

Kwa maoni yangu sakata la “Jairo” lisichukuliwe kama ‘tukio pweke” (isolated event) bali litazamwe kuwa ni kiashiria cha matatizo makubwa zaidi katika mifumo ya matumizi ya fedha za umma ndani ya Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali. Hata hivyo, nilishangazwa zaidi na kauli ya katibu mkuu kiongozi- hata kwa maelezo tu aliyoyatoa mwenyewe kwenye vyombo vya habari amedhihirisha kwamba kuna ukiukaji wa sheria za fedha, ubadhirifu na ufisadi wa kitaasisi katika Wizara ya Nishati na Madini. Lakini inashangaza hatimaye akatoa kauli ya kuhitimisha kuwa ni utamaduni wa kawaida katika serikali na kwamba Jairo hana hatia yoyote.

Msingi wa kutoa hitimisho hili ulianzia naamini ulianza kutokana na udhaifu wa hadidu rejea ambazo wachunguzi wa ofisi ya CAG walikuwa nazo- kwa kipindi kifupi nilichokuwa karibu na Wizara hii nafahamu idadi ya idara, vitengo, wakala, mashirika na taasisi zilizoko chini yake.Ndio maana nikatahadharisha kwamba lazima uchunguzi uhusishe mfumo mzima ikiwemo maagizo ya barua ya Jairo na matokeo badala ya kujikita kwenye kauli za Shellukindo bungeni pekee. Na nilieleza matendo yanayoshabihiana na ya Jairo yaliyofanywa pia na Wizara nyingine kuanzia wakati wa kamati za Bunge Dar es salaam mpaka katika Mkutano huu wa bunge la bajeti katika kile kinachoitwa ‘kufanikisha kupitishwa kwa bajeti’. Kwa ujumla kuna mianya katika mifumo ya fedha ambayo imewezesha ubadhirifu na ufisadi wa kitaasisi.

Kutokana na kauli ya Waziri Mkuu kiongozi kuwa matendo kama aliyoyafanya Jairo ni ya kawaida katika Serikali; Waziri wa Fedha anapaswa kuwajibika kuchukua hatua badala ya kusubiri mpaka kamati teule imalize kazi yake.


Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Umma (Public Finnance Act no 6 of 2001); wajibu na mamlaka ya Waziri wa Fedha na Hazina kwa majibu wa 5(1) (i) ni kusimamia na kufuatilia masuala yote ya fedha za umma, 5(3) kudhibiti na kutoa muongozo kwa masuala yote ya kifedha ya serikali. Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha kama Mlipaji Mkuu ndiye anayesimamia udhibiti na utoaji fedha kwa Wizara na Idara mbalimbali za serikali nzima.

Jairo anaingia katika picha kwa Wizara yake kwa kuwa sheria hiyo kifungu 8(1) kimetoa mamlaka kwa Wizara ya Fedha kuteua Afisa Masuhuli (Accounting Officer) kwa Fungu husika ambapo kwa Wizara ya Nishati na Madini ni yeye kama katibu mkuu. Hivyo, kama katibu mkuu kiongozi Luhanjo amesema kwamba matendo hayo ni ya kawaida katika serikali nilitegemea kauli nzito toka kwa ama Waziri wa Fedha au Mlipaji Mkuu au Mhasibu Mkuu wa Serikali kukanusha ama kuunga mkono.

Ni wazi, kwa Wizara ya Nishati na Madini anayepaswa kuwajibika kiutendaji ni Jairo; ingawa Waziri na Naibu nao hawawezi kukwepa kuwajibika kisiasa kutokana na kadhia hiyo hasa baada ya kutoa kauli tata na tete mara baada ya Luhanjo ‘kumsafisha’ Jairo hali inayoaishiria kwamba ‘baraka’ zao zilikuwepo kwenye barua ya Jairo na matumizi yaliyofuatia. Aidha, pamoja na kukingwa na kifungu 8(2); Watendaji wa wakala, mashirika na taasisi yaliyohusika nao wana nafasi yao ya kuwajibika katika sakata nzima. Katika muktadha huo, mnyororo huu unaelekea kuwa mrefu lakini ni muhimu hatua za msingi zikachukuliwa ili kudhibiti hali hii ambayo imeelekea kuwa ni utamaduni wa ubadhirifu na ufisadi wa kitaasisi unaoitwa ‘wa kawaida’ kwenye serikali kwa muda mrefu.

Utetezi wa Luhanjo ambao unaelekea kuungwa mkono na baadhi ya watu ndani na nje ya serikali ni kwamba ‘CAG amekagua na kukuta hakuna fedha ambazo wabunge wamepewa rushwa ili kupitisha bajeti’. (Hili la Wabunge kupewa rushwa kupitisha bajeti, naomba nisilitoleee maoni hadharani katika hatua ya sasa kwa kuwa yapo masuala ambayo niyaeleza nilipohojiwa ambayo naamini ofisi ya CAG na mamlaka zingine naamini zinaendelea kuyafanyia kazi).

Tuchukue vigezo vya kimaamuma pekee na tutumie tu maelezo ambayo yametolewa na Katibu Mkuu Kiongozi na Mkaguzi Mkuu kwa waandishi wa habari halafu tuyalinganishe na misingi ya kisheria na kikanuni inayosimamia fedha za umma na utendaji wa kazi katika serikali. Kwa hayo tu, utabaini kwamba mamlaka hizi za kiserikali zimepuuzia ubadhirifu na ufisadi wa kitaasisi unaodhihirika katika Wizara ya Nishati na Madini.
Sheria ya Ukaguzi (Public Audit Act no. 11 of 2008) kifungu cha 10(1) kinampa jukumu CAG kufanya ukaguzi wa fedha za umma kwa niaba ya bunge (Hapa unaweza kujiuliza; kwa kuwa suala lilianzia bungeni na kwa kuwa CAG hufanya ukaguzi kwa niaba ya bunge- pamoja na kuwa katika suala la Jairo aliombwa na mamlaka za kiserikali, kwa nini haikuonekana haja ya bunge kupewa taarifa ya haraka kabla ya kwenda kwenye vyombo vya habari kusafishana?).

Kifungu cha 10 (2) (c) kinaelekeza matumizi yote ya umma yawe yameadhinishwa kwa kufuata utaratibu na yatumike kwa madhumuni kwayo yalipitishwa kwa mujibu wa sheria na maelekezo (appropriation laws and directives). (d) matumizi hayo lazima yafanyike kwa kuzingatia ufanisi na tija (economy, efficiency and effectiveness). Je, ni kwa kiwango gani matumizi hayo tuliyoelekezwa yamezingatia vigezo hivyo viwili vya msingi ambavyo CAG alipaswa kuvitumia katika ukaguzi wake?

Kifungu cha 12 kimempa mamlaka CAG kutoa mapendekezo ya kuzuia au kupunguza matumizi yasiyokuwa na tija ya fedha za umma (tujiulize, ni kwanini Luhanjo kama CAG alitoa mapendekezo ya namna hiyo au la?). Aidha kifungu hicho hicho kinatoa mwanya wa kutolewa mapendekezo ya kudhibiti uzembe, ukosefu wa uaminifu, ufisadi nk.
Naelewa kwamba ukaguzi uliofanyika sio wa kawaida, hivyo wengine wametumia sababu hiyo kujenga hoja kwamba halikuwa suala la bunge katika hatua ya sasa bali la mamlaka iliyoomba ukaguzi ufanyike.

Ni vyema tukarejea tena kwenye sheria husika kifungu cha 26 (2) ambayo inaelekeza kwamba CAG anaweza kufanya ukaguzi maalum kwa maombi ya mtu au taasisi; ukiondoa ukaguzi wa kawaida unaofanywa kwa mujibu wa sheria ama kwa azimio la bunge au kamati zake za usimamizi wa fedha za umma. Hata hivyo, izingatiwe kwamba Kifungu cha 36 (1) cha Sheria hiyo hiyo kinaeleza kwamba CAG anaweza akiona kwamba kuna jambo lolote la ukaguzi wowote lina maslahi ya umma na angependa kulitaarifu bunge sheria inaelekeza kwamba anaandaa ripoti maalum anamkabidhi Rais kwa mujibu wa sheria Rais anawajibika kuipeleka ripoti husika bungeni. Kwa kuwa suala hili la Jairo lilihusu tuhuma za Bunge, likatolewa kauli na Waziri Mkuu ambayo ndiye kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni kwamba analipeleka kwa Rais, Rais badala ya kutoa maagizo mwenyewe akaikabidhi mamlaka ya nidhamu ambayo ni Katibu Mkuu Kiongozi (Hapa Rais alipaswa kutambua kwamba suala hili halikuhusu Nidhamu tu ya Jairo, lilihusu masuala ya kimfumo na kifedha ya Wizara ambayo kwa mujibu wa katiba muhusika mkuu ni yeye au watendaji aliowateua kufanya kazi kwa niaba yake mf. Waziri Mkuu, Waziri wa Fedha, Mlipaji Mkuu nk).

Ni wazi kwamba ukaguzi huu maalum haukupaswa tu kuwa wa kawaida, CAG alipaswa kutumia vizuri pia kifungu cha 28 kwa kuingiza masuala ya kukagua ufanisi (economy, efficiency, effectiveness) katika hadidu rejea (a) kuhusiana na matumizi ya fedha na rasilimali (b) kuhusu utendaji wa maafisa masuhuli husika (Accounting officer), wakuu wa idara na watendaji wakuu wa wakala, taasisi na mashirika yaliyohusika. Ukaguzi wa namna hii ungeweza kuibua masuala ambayo yangehitaji sasa kufanyika ukaguzi wa kiuchunguzi (Forensic Audit) kwa ajili ya hatua za ziada. Kamati teule ya Bunge inaweza kupanua wigo zaidi kutoka pale CAG alipoishia ili kuwezesha bunge kutimiza wajibu wa kikatiba wa kuisamia serikali kuondokana na mfumo wa ubadhirifu na ufisadi wa kitaasisi.

Wenu katika utumishi wa umma,

JJ

No comments: