Tuesday, November 15, 2011

Sheria ya Manunuzi!

Sheria ya Ununuzi: Wabunge wapunguza nguvu za Rais
Monday, 14 November 2011 21:41

Kizitto Noya, Dodoma
MUSWADA wa Sheria ya Ununuzi wa Umma jana ulipita kwa mbinde baada ya wabunge kuibana Serikali na kuilazimu kuufanyia marekebisho kwenye baadhi ya vipengele, ikiwemo kuondoa kipengele kinachotaka Rais athibitishe ununuzi.

Mbali na kuibana Serikali kubadili kipengele hicho, wabunge pia walitaka ufafanuzi wa kina kuhusu kifungu cha 104 kinachoelezea adhabu ya mtu anayeisababishia Serikali hasara katika mchakato wa ununuzi pamoja na kifungu cha 66 kinachopendekeza ununuzi wa vifaa vilivyotumika, hatua ambayo ilimfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuagiza vipengele hivyo kurudishwa kwenye Kamati ya Sheria Ndogo za Bunge, kwa ajili ya majadiliano zaidi.

Muswada huo ambao awali ulipangwa kupitishwa jana mchana, ulilazimika kusubiri katika kikao cha jioni baada ya kutokea malumbano makali ya hoja kati ya wabunge waliopinga vipengele hivyo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema ambaye alikuwa akivitetea.Malumbano hayo yalijitokeza wakati Bunge lilipokuwa limekaa kama kamati kwa ajili kupitisha sheria hiyo mpya.

Wabunge waliotawala mjadala huo walikuwa John Mnyika wa Ubungo (Chadema), Luhaga Mpina wa Kisesa (CCM) na Godfrey Zambi wa Mbozi Mashariki (CCM).

Kwa nyakati tofauti, wabunge hao walipinga adhabu iliyopendekeza mtu anayepatikana na hatia ya kuisababishia Serikali hasara katika mchakato wa ununuzi, kufungwa miaka mitano na kulipa faini ya kuanzia Sh5milioni hadi Sh10 milioni wakisema ni ndogo na inapaswa kuongezwa.

“Mheshimiwa Mwenyekiti mimi naona adhabu hiyo ni ndogo, mtu wa aina hiyo anapaswa kufungwa siyo zaidi ya miaka 30 na baadaye afilisiwe mali zake kulipa hasara aliyoisababishia Serikali,” alisema Mpina na baadaye kuungwa mkono na wabunge wengine watano: Seleman Jafu (Kisarawe), Christina Mughwai (Viti Maalumu), Alphaxard Lugola (Mwibara), Dk Mahmoud Mgimwa (Mufindi Kaskazini) na Mnyika.

Katika kuunga mkono hoja hiyo, wabunge hao walisema si sahihi wala haki mtu aliyeisababishia Serikali hasara ya mabilioni ya shilingi kufungwa jela kwa kipindi kisichozidi miaka mitano na kulipa faini isiyopungua Sh10 milioni au zaidi wakisisitiza kuwa mtu huyo anapaswa kufungwa miaka isiyopungua 20 na isiyozidi 30 na baadaye afilisiwe mali zake zote kulipa deni.

Hata hivyo, Werema alipinga mapendekezo hayo ya wabunge kwa maelezo kuwa adhabu hiyo ni kubwa mno kwa watu ambao mfumo, uliwadhamini kuitumikia jamii.

“Waheshimiwa wabunge, katika kutunga sheria tusiwe na hasira kwa sababu hasira ni pango la shetani. Nakubaliana kwamba tatizo hilo linahitaji adhabu kali lakini, adhabu hiyo inapaswa kuwa ya uwiano na kosa lenyewe. Kosa tunalotaka kulifanya tuliwahi kulifanya mwaka 1983 katika Sheria ya Uhujumu Uchumi. Sheria ile tuliitunga kwa hasira, kwa ushauri wangu adhabu hiyo inatosha,” alisema Jaji Werema.

Kauli hiyo ya Jaji Werema, iliwaamsha wabunge kadhaa na Makinda kumchagua Mpina kuzungumza ambaye alisema: “Ninachoweza kusema hapa ni kwamba Mwanasheria Mkuu hana uzoefu na manunuzi.”

“Kwa nini tuwe na sheria za upendeleo? Tumetunga sheria kwamba raia akionekana kwenye mbuga za wanyama hata kama hana silaha, akamatwe na watu wanapigwa risasi. Lakini tunapokuja kutunga sheria kwa ajili ya watendaji tunataka ziwe laini, kwa faida ya nani?”

Malumbano hayo yalimfanya Spika Makinda ambaye wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge zima, kuifunga hoja hiyo akisema: “Sasa naagiza kifungu hicho kirudishwe kwenye kamati ili kikajadiliwe upya.”

Hoja nyingine iliyozua mjadala katika kikao hicho ni ile aliyoitoa Mnyika kutaka kanuni zitakazotungwa na waziri kwa ajili ya utekelezaji wa sheria hiyo, zipitiwe upya na Bunge pamoja na kutaka kufutwa kabisa kifungu cha 66 kinachotaka kuruhusiwa ununuzi wa vifaa vilivyotumika.

Mkulo
Awali, akifunga mjadala huo, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo alisema Serikali imeridhia mapendekezo ya wabunge kufanyia marekebisho kipengele kinacholihusisha Baraza la Mawaziri kushiriki katika kuidhinisha ununuzi wa umma.
“Tumekubaliana na mapendekezo ya wabunge kwamba Rais asihusishwe kuidhinisha ununuzi, badala yake sasa kazi hiyo itafanywa na Waziri wa Fedha baada ya kushauriwa na kamati maalumu atakayoiunda.”

Waziri Mkulo aliwaomba wabunge kuondoa hofu ya mwanya wa ufisadi katika sheria hiyo, akisema Serikali imejipanga vya kutosha kukabiliana na hali hiyo kwa kuja na kanuni zitakazodhibiti mianya yote ya rushwa.

Alitaja baadhi ya kanuni hizo kuwa ni zile zinazotaka wataalamu kukagua mali inayotaka kununuliwa, mmiliki kuwasilisha nyaraka zinazoonyesha kifaa husika kimetengenezwa lini, ulinganifu wa ubora wa vifaa pamoja na taasisi zisizoridhika na mchakato kutoa taarifa (Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA).

Kupitisha muswada
Kabla ya kupitishwa kwa muswada huo jana jioni, Jaji Werema alifafanua kwamba Serikali imekubaliana na hoja ya Mpina ya kukifanyia marekebisho kifungu cha 104 kinachohusu adhabu kwa watuhumiwa ambacho kinatoa mamlaka ya mtuhumiwa aliyesababishia Serikali hasara katika ununuzi kuhukumiwa adhabu ya miaka zaidi ya saba na kufidia hasara hiyo au kukamatwa na kutaifishwa kwa mali zake.

Jaji Werema alisema anaamini kwamba adhabu hizo zitaongeza uwajibikaji na umakini katika kusimamia na kutekeleza Sheria ya Ununuzi ili kuliepusha taifa na hasara na kuongeza kwamba Serikali pia ilikubaliana na hoja ya Mnyika aliyeonyesha shaka juu ya mamlaka ya waziri katika utekelezaji wa kanuni ambayo pamoja na mambo mengine, ataweza kuunda timu ya wataalamu ambayo itamshauri katika baadhi ya vitu muhimu vinavyohitaji ununuzi kisha naye kuamua.

Hata hivyo, baadaye muswada huo ulipitishwa na utakapotiwa saini na Rais, Sheria ya Ununuzi ya mwaka 2011 itachukua nafasi ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004, inayotumika sasa.

Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz/habari/49-uchaguzi-mkuu/17501-sheria-ya-ununuzi-wabunge-wapunguza-nguvu-za-rais

No comments: