Kutoka Bungeni: Hadhi ya Barabara DSM; mgomo wa madaktari ; Uchaguzi Afrika Mashariki; Sheria ya Fedha Haramu; utalii na ajira pori la Pande
Katika kuendelea kuwawakilisha wananchi nimeendelea kuisimamia serikali katika masuala yafuatayo:
Leo 08/02/2011 nimeulizwa swali la nyongeza kuhusu barabara za Dar es salaam kwa lengo la kuharakisha uboreshaji wa miundombinu ya pembezoni na kuchangia kupunguza foleni. Kwa muda mrefu kikwazo cha ujenzi wa barabara, madaraja na mifereji kimekuwa ni kiwango kidogo cha fedha ambacho TANROADS Mkoa wanatengewa. Nimetoa mfano wa mfereji wa Malapa Ilala Bungoni ulihitaji tu 2.3 Bilioni kukamilika lakini toka mwaka 2009 mpaka leo ujenzi bado unaendelea ukisuasua; nikata Wizara ya Ujenzi ieleze ni lini barabara za Dar es salaam zitapandishwa hadhi kwa orodha ambayo tulishawasilisha serikalini miaka kadhaa iliyopita ili ziongezewe bajeti ujenzi uweze kuharakishwa? Waziri Magufuli amekiri kweli fedha zilikuwa zikitengwa kidogo, amekubali kuwa ameshapokea orodha ya barabara husika na ameahidi kwamba wataalamu wake wanazipitia na karibuni atatoa taarifa ya barabara zilizopandishwa hadhi. (Swali hili nimeuliza kufuatilia masuala niliyowahi kuyazungumza hapa: http://mnyika.blogspot.com/2012/01/kuhusu-msongamano-wa-magari-dsm-na.html
Aidha, nimeandika barua kwa Spika kuhusu mgomo wa madaktari kama ambavyo mlishauri jana nilipoandika ujumbe huu: http://mnyika.blogspot.com/2012/02/mgomo-wa-madaktari-bungeni-tena-leo.html; kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge cha dharura kinaendelea hivi; nimeshauri hayo mapendekezo saba niliyoyatoa kwenye hiyo barua yazingatiwe na bunge litoe taarifa ya haraka kuhusu hatua ambazo zimechukuliwa mpaka sasa. Aidha, nimetoa mwito kwa Rais kuweza kutaarifiwa naye kuweza kuingilia kati kwa mujibu wa mamlaka yake ya kikatiba ya kwenye ibara ya 34 na 35.
Pia; nimewasilisha mapendekezo kwa Katibu wa Bunge kutaka kufanyika kwa mabadiliko katika kanuni za Kudumu za Bunge nyongeza ya tatu juu ya The East African Legislative Assembly Election Rules; kwa kurejea upungufu ambao ulijitokeza kwenye uchaguzi uliopita tarehe 2 Novemba 2006 kama nilivyoyaeleza kwenye tamko hili: http://www.chadema.or.tz/tamko/tamko.php?id=8&pg=41 na pia kwa kuzingatia sheria mpya EALA Elections Act 2011. Suala hili ni la haraka ili kuepusha migogoro kuhusu uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki kama ilivyotokea kwa nchi nyingine jirani hadi kufikia hatua ya mahakama ya Afrika Mashariki kuagiza baadhi ya chaguzi kusimamishwa mpaka kanuni zifanyiwe marekebisho (Rejea: Ruling of the Court Dated 30/11/2011 ya case. No. 6 of 2001).
Juzi 06/02/2011 niliomba muongozo wa Spika kwa mujibu wa kutokana na kukiukwa kwa kanuni ya 86, 88 na 91 kubadilishwa kinyemela kwa maamuzi ya bunge baada ya marekebisho ya sheria niliyowasilishwa na kukubaliwa ya kuongeza ukubwa wa adhabu katika makosa ya fedha haramu kama ambavyo nilieleza hapa: http://mnyika.blogspot.com/2012/02/kutoka-bungeni-sheria-ya-fedha-haramu.html. Kimsingi Serikali ilikubaliana nami kuwa kulikuwa na kasoro kwa kuwa mwenyekiti kufuta kauli yake hakubatilishi uamuzi wa bunge; hivyo Naibu Spika akaagiza kamati ya kanuni ikutane mapema iwezekanavyo. Kamati ya Kanuni itakutana leo.
Pia, nimeuliza swali la msingi maswali ya nyongeza kuhusu Pori la Akiba la Pande kuhakikisha kwamba linaendelezwa kwa ajili ya kuinua utalii na utafiti kwa mapato ya serikali na kuongeza ajira hususan kwa vijana. Nimetaka Pori hilo liendelezwe kwa ajili ya kujenga Animal Park kama ilivyo Nairobi na miji mingine duniani. Nimetaka hatua pia zichukuliwe kuhakikisha migogoro inaepushwa kati ya hifadhi na maeneo ya jirani ya Mbopo, Msumi, Mpiji Magoe na Msakuzi katika jimbo la Ubungo ili isije ikawa kama ilivyo katika wilaya ya Urambo, Meatu na nyinginezo.
2 comments:
Mnyika upo so transparent and responsible kwa watu wa Ubungo,Dar es salaam na tanzania kwa ujumla,sasa kama ikiwezekana basi upitishwe muswada, kuwa wabunge wengine pia wawe wanakuwa transparent kiasi hiki.100 thumbs up and keep it this way
nikweli tena nikweli kabisaaa,Mungu alikupa mamlaka ufanye hivyo,ila inakupasa uiheshimu nafasi hiyo,Loooo,mlitest ikaonekana inalipa,sasa mnapiga kabisaa,ok.nimgomo wa madaktari,unajua kunawatu wanakufa,wanazidi kupoteza maisha,kunawengine wewe ndo umepewa mamlaka uyakomboe,nakuambia wanakata roho,hakika wengine ni ndugu zako mwenyewe bila kujijua wanapotea,Pesa ambayo inaonyesha haipatikani kwa sasa Yanini kuing'ang'ania? kweli Nimtanzania huyu anahitaji makaratasi meeengi ili ale ashibe,jamani embu turudishe ule moyo wa kusaidiana.pesa zipo tu.kunawatu wanaishi maisha magumu sana kuliko wewe daktari,nikuambie!!!! niyule aliye kuonyesha wewe namna yakushika kalamu,ila mpaka sasa bado haja goma.rudi kazini,fanya kazi tena kwa bidii na kasi kubwa,ili kumwonyesha bwana mkubwa siku akiupenda awape na asipo penda basi utaacha kazi,walau na yeye ajipange kwakuwa mamia wanapoteza maisha,hatakama utajifariji kwani ulishika kisu ukamchoma mtu,no ila majibu unayo,roho inakuuma.usifurahie hali ni mbaya.Kweli wewe ni muhimu,wanaumia maskini,Jameni wanaharakati,watu wa haki za binadamu,mapadri,wachungaji,masheghe,mpo upande wa naniiiii??? mbona hatu msikii hata mmoja,inashangaza, tunawaomba wanajamii ingilieni kati jambo hili,msinyamaze tu eti serikali ndo iyamalize wakati hali si nzuri,semeni jambo nasi tuwaone mnazingatia haki za watu wote.
Post a Comment