Wednesday, February 15, 2012

Kuhusu Kauli za Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma

Kufuatia Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutangaza katika vyombo mbalimbali vya habari tarehe 15 Februari 2012 kwamba wameanza kuhakiki fomu za tamko la mali na madeni kwa baadhi ya viongozi tuliojaza fomu husika, mjadala umeibuka jimboni na katika jamii kuhusu suala hilo na baadhi mmeomba maoni yangu juu ya mchakato huo.

Umma ufahamu kuwa nilitimiza masharti ya kuwasilisha fomu kwa wakati na kutoa tamko kwa mujibu wa sheria, uhakiki ni utaratibu wa kawaida. Pamoja uhakiki, natoa mwito kwa Sekretariati kufanya uchunguzi juu ya viongozi wa umma wenye tuhuma mbalimbali ambao tumewataja kwa majina kwa nyakati mbalimbali. Aidha, kuhusu kufanya marekebisho ya sheria ya maadili ya umma kwa ajili ya kuweka mipaka kati ya biashara na siasa, sekretariati badala ya kurudia tena kufanya utafiti irejee kauli ya serikali bungeni kuwa waraka wa marekebisho ulishaandaliwa tayari na itoe mapendekezo kwa serikali yenye kuwezesha muswada kuwasilishwa katika mkutano ujao wa bunge.

Pamoja na uhakiki wa kawaida, sekretariati ifanye uchunguzi kwa watuhumiwa:

Ni vizuri ikazingatiwa kuwa nilitimiza masharti yanayotakiwa kwa mujibu kifungu cha 9 cha Sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995 ya kujaza fomu za tamko la mali na madeni na ni jambo la kawaida kwa sekretariati kufanya uhakiki wa fomu tajwa na kabla ya kuwa mbunge nimekuwa nikitoa mwito wa mara kwa mara kwa sekretariati kutimiza wajibu husika.

Ni muhimu sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma ikapanua wigo wa uhakiki iongeze orodha ya viongozi wa umma ili walau kwa mwaka iweze kuhakiki sampuli isiyopungua 10% ya viongozi wote wa umma na taarifa ya uhakiki huo iweke wazi kwa umma kuhusu wote wasiotangaza mali kwa mujibu wa sheria au ambao watabainika kutoa taarifa zenye kasoro.


Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 132 imeweka msingi wa kuundwa kwa Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma na kwamba Ibara ya 70 kuwasilisha taarifa ya mali na kifungu cha 71 kinataja sababu za kukoma kuwa mbunge kutokana na kukiuka masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa umma; hivyo sekretariati inapaswa kupanua wigo wa kutimiza majukumu husika ya kikatiba.

Kwa hiyo, pamoja na kufanya zoezi la kawaida la kuhakiki fomu za tamko la mali na madeni kwa viongozi wa umma; kwa kuwa sekretariati imetangaza kuwa itafanya kazi kwa uwazi na kwa kuzingatia sheria basi iweke kipaumbele katika kutumia mamlaka iliyonayo kwa mujibu wa sheria husika vifungu 18(4) na 22 (4) kufanya mchakato muhimu zaidi wa kufanya uchunguzi wa tuhuma juu ya ufisadi uliofanywa na unaoendelea kufanywa na viongozi wa umma ambao wametajwa kwa nyakati mbalimbali kwenye mikutano na katika vyombo vya habari.

Izingatiwe kuwa pamoja na uchunguzi wa awali unaoweza kufanywa na Sekretariati kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 kifungu 22(2); uchunguzi kamili unafanywa na baraza ambalo kwa mujibu wa kifungu 26(5) linapaswa kufanya uchunguzi wake hadharani ili umma uweze kufahamu.

Kuibuka kwa mjadala huu kumenifanya nikumbuke mjadala mwingine ambao uliibuka ulijitokeza mwanzoni mwa mwaka 2010 baada ya kauli zangu nilizotoa kwenye kipindi cha Kipima Joto kilichorushwa katika kituo cha luninga cha ITV ijumaa tarehe 19 Februari 2010 na kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari tarehe 21 Februari 2010.

Mjadala huo uliongezeka zaidi kufuatia tarehe 24 Februari 2010 Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Rais- Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutoa taarifa kwa umma kujibu kauli zangu nilizotoa na kuchapa matangazo kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuanzia tarehe 26 Februari 2010 mpaka tarehe 5 Machi 2010.

Kutokana na taarifa hiyo tarehe 7 Machi 2010 nilitoa tamko ambalo linaweza kurejewa kupitia: http://www.chadema.or.tz/habari/habari.php?id=111 ambalo nilihimiza masuala ambayo Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma inapaswa kuyazingatia na kurejea kuweka mkazo wa kauli ambazo nilitoa awali kuhusu ufisadi na hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa kwa viongozi wenye tuhuma ambao niliwataja kwa majina.

Waraka ulishaandaliwa; muswada wa marekebisho ya sheria uletwe bungeni

Kwa upande mwingine, Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma imenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari leo tarehe 15 Februari 2012 ikileza kuwa ‘itafanya utafiti kabla ya kutoa mapendekezo ya kubadili sheria inayotenganisha biashara na uongozi ili kuweka nidhamu kwa viongozi wa umma’.

Ni vyema Sekretariati ifanya mawasiliano na mamlaka zingine za kiserikali ili kuepusha kurudia utafiti ambao umekwishafanyika na badala yake ikaelekeza nguvu zake kwenye kutoa mapendekezo ya kuwezesha marekebisho ya sheria husika yakawasilishwa katika mkutano wa saba wa bunge unaotarajiwa kuanza tarehe 10 Aprili 2012.

Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma izingatie kuwa suala ililolizungumzia lilishajadiliwa bungeni na bunge kupitisha azimio no. 11 mwezi Februari 2008 kwamba “Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya Mwaka 1995 (The Public Leadership Code of Ethics Act), ifanyiwe marekebisho makubwa ili kudhibiti utaratibu unaoonekana wa kawaida sasa wa Viongozi Waandamizi wenye dhamana ya kisiasa kuendelea na biashara zao binafsi wakiwa madarakani, jambo ambalo lina mgongano wa kimaslahi. Serikali ianze rasmi maandalizi ya majadiliano ya kina kuhusu suala hili ndani na nje ya Bunge kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali.”

Mwezi Februari 2010 Bunge lilitaarifiwa kuhusu utekelezaji wa Serikali juu ya marekebisho ya sheria husika kwamba kikundi kazi (Task Force) kiliundwa ambacho kiliandaa waraka wenye mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, (Sura 398) ambao ulikuwa katika ngazi ya kujadiliwa na Kamati ya Makatibu Wakuu (IMTC). Aidha, Bunge lilielezwa kuwa serikali ilitarajia kuwasilisha muswada husika katika mkutano wa kumi na tisa wa Bunge la tisa hali ambayo ilionyesha serikali na vyombo vyake tayari walishakamilisha utafiti kuhusu suala husika. Hata hivyo, Muswada huo haukupitishwa katika Bunge la tisa kama ilivyoshauriwa na kamati na mpaka sasa muswada huo bado haujawasilishwa kwa bunge la kumi.

Hali hii imetokana na kufungwa kwa mjadala juu ya utekelezaji wa maazimio ya bunge juu ya mkataba kati ya TANESCO na Richmond Development Company kabla ya maazimio kukamilika hivyo, na msukumo kuhusu utekelezaji wa maazimio husika ikiwemo la kufanya marekebisho ya sheria tajwa ungeongezeka iwapo hoja binafsi niliyoiwasilisha kutaka uamuzi ubadilishwe ingejadiliwa.

Ikumbukwe kwamba miaka miwili imepita bila ya utekelezaji kamili wa maazimio 10 kati ya 13 yaliyobaki hususan Maazimio Nambari: Nambari 3,5,7,8,9,10,11,13,14 na 18; toka mjadala kuhusu Richmond ufungwe bungeni mwezi Februari 2010; na ni miaka minne toka bunge lipitishe maazimio mwezi Februari 2008. Kama kwa miaka minne, taifa limeshindwa kukamilisha utekelezaji wa maazimio ya bunge kwenye suala moja, haiwezekani umma ukaamini kwamba utekelezaji wa maazimio mengine ya bunge mathalani ya Novemba 2011 uchunguzi wa sekta ndogo ya gesi asili au utekelezaji wa maamuzi ya serikali kuhusu uchunguzi ulioanzishwa hivi sasa juu ya watendaji waandamizi katika Wizara ya Afya kufuatia mgomo wa madaktari.

Hivyo bunge na serikali lazima kwa pamoja vyombo vyote vionyeshe kwa vitendo kumaliza masuala haya ili kuweka misingi ya uwajibikaji katika masuala mengine; Sekretariati ya Maadili ya Viongozi wa Umma nayo ni mamlaka ya kuweza kuwachukulia hatua waliokiuka sheria ya maadili ya viongozi wa umma katika masuala hayo na mengine.

Hivyo, narudia kusisitiza kwamba uwepo wa sheria na kanuni za maadili pekee hauwezi kusaidia iwapo kanuni hazisimamiwi, na pia hauwezi kusaidia iwapo kanuni ni mbovu. Mwaka 2010 nilieleza kwamba Sheria na kanuni husika hazina meno ya kutosha lakini hata yale meno kidogo yaliyopo hayang’ati; kwa kuwa hakuna hatua stahili zinazochokuliwa.

Wakati huo nilieleza bayana kuwa Sekretariati haijawahi kutoa taarifa ya yoyote kuhusu aliyewahi kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kutokutangaza mali zake ama kutoa taarifa za zisizokuwa za kweli katika fomu husika; hivyo kutolewa kwa taarifa ya sasa kuwa uhakiki umeanza iwe ni hatua ya mwanzo tu kwa ajili ya mamlaka husika kuchukua hatua zaidi. Pamoja na udhaifu wa sheria, changamoto kubwa zaidi ni kutokusimamiwa kwa utawala wa sheria ambao katika suala hili la maadili wahusika wakuu katika kusimamia sheria husika ni ofisi ya Rais na sekretariati ya maadili ya viongozi wa umma.

John Mnyika (Mb)

15/02/2012



2 comments:

Midladjy Maez said...

Anko Katika Sheria mimi ninaitaka ukiachia Sheria Mpya Mama ( Katiba)hii ya Kutenganisha Biashara na Uongozi wa Kisiasa nina isubiri kwa hamu kwa hali ya sasa lazima iharakishwe! Tunajua kuna watu watajaribu kuihujumu kwa vile inakinzana na utashi wao wa kisiasa lakini lazima iwepo kama vile hewa , maji na ardhi kwa binadamu! Najua itapata matatizo kutekelezeka....lakini angalizo kupitshwa sheria ni jambo moja na utekelezaji wake ambao ndio hatua muhimu sana ni jambo lenye changamoto kuubwa sana...! Kwa sisi ambao hatujaonja 'utamu' wa Biashara na 'Ukwasi' tunaona jambo jepesi....! Lakini kuna wautu hvii sasa matumbo moto...! Njoo sheria dhidi ya ufisadi na Ufisadi Utokomee kuzimu..!

Midladjy Maez said...

Anko Katika Sheria mimi ninaitaka ukiachia Sheria Mpya Mama ( Katiba)hii ya Kutenganisha Biashara na Uongozi wa Kisiasa nina isubiri kwa hamu kwa hali ya sasa lazima iharakishwe! Tunajua kuna watu watajaribu kuihujumu kwa vile inakinzana na utashi wao wa kisiasa lakini lazima iwepo kama vile hewa , maji na ardhi kwa binadamu! Najua itapata matatizo kutekelezeka....lakini angalizo kupitishwa sheria ni jambo moja na utekelezaji wake ambao ndio hatua muhimu sana ni jambo lenye changamoto kuubwa sana...! Kwa sisi ambao hatujaonja 'utamu' wa Biashara na 'Ukwasi' tunaona jambo jepesi....! Lakini kuna watu hivi sasa matumbo moto...! Njoo sheria dhidi ya ufisadi na Ufisadi utokomee hukoo.. kuzimu..! Yote ni Changamoto kwetu sote...!