Friday, February 10, 2012

Kutoka Bungeni: Sheria ya Katiba; Maji Ubungo na Kiwanda cha Urafiki

Kutoka Bungeni: Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba; Maji Jimboni Ubungo mitaa ya pembezoni na Hatma ya Kiwanda cha Nguo cha Urafiki

09/02/2012 nilichangia kwa maandishi muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2011; katika mchango wangu nilirejea pia msingi wa mapendekezo niliyoyatoa awali wakati wa kuwasilisha taarifa ya hoja binafsi kuhusu mchakato wa katiba mpya na uchambuzi niliofanya mara baada ya kuchapwa kwa muswada wa sheria husika kwa mara ya kwanza: http://mnyika.blogspot.com/2011/04/tamko-la-awali-kuhusu-muswada-wa.html. Nashukuru kwamba hatimaye harakati tulizoanza miaka mingi na zikapata msukumo mwezi Disemba 2010 ya kutaka mchakato wa katiba kuanzia bungeni kupitia kwa bunge kutunga sheria juu ya tume shirishi ya katiba, bunge maalum la katiba na hatimaye katiba kuhalalishwa kwa kura ya maoni zimepiga hatua nyingine kwa marekebisho ya sheria kuwasilishwa bungeni. Hata hivyo izingatiwe kuwa marekebisho ya sheria yaliyowasilishwa bungeni tarehe 09 Februari 2011 ni awamu ya kwanza, kuhusu tume na mchakato wa kukusanya maoni pamoja na kuandaa rasimu. Bado mabadiliko yanahitajika katika awamu ya pili na ya tatu; kuhusu bunge maalum la katiba na hatua ya kutunga katiba na kura ya maoni na mchakato wake kusimamiwa na tume ya uchaguzi. Katika mchango wangu nimeeleza pia kwamba bado kifungu cha 21 pamoja na adhabu kupunguzwa bado ziko juu; hivyo nimeendelea kutaka makosa yatenganishwa kati ya makosa ya kijinai ambayo yanaweza kuhukumiwa kwa kutumia sheria ya adhabu (penal code) na makosa ya kawaida katika mchakato wa kutoa elimu juu ya mabadiliko ya katiba na kukusanya maoni. Adhabu ya makosa ya kawaida inapaswa kuwa ndogo ya kawaida ili kutokufanya wananchi wapate hofu ya kushiriki kwa uhuru kwenye mchakato wa katiba na pia ili kulinda haki za msingi za kikatiba za kupata taarifa na kutoa maoni. Nasikitika kwamba sikuwepo jana jioni na leo asubuhi wakati bunge limekaa kama kamati kuhusu muswada husika kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu; hata hivyo kwa kuwa awamu nyingine zitafuata za marekebisho ya sheria husika, bado ipo nafasi ya kuendelea kufanya marekebisho mengine ya ziada.



09/02/2012 Katika kuendelea kuisimamia serikali kuhusu kero ya maji katika kata mbalimbali za jimbo la Ubungo kama nilivyoeleza hapa: http://mnyika.blogspot.com/2011/06/mbunge-awataka-dawasco-kutoa-maelezo.html nimeuliza swali la nyongeza kutokana na uwepo wa taarifa za miradi ya maji ya visima virefu na vifupi katika maeneo mbalimbali ya pembezoni kutokufanya kazi kutokana na matatizo ya kiutendaji chini ya Manispaa ya Kinondoni na Serikali za Mitaa ya muda mrefu toka 2000-2010; hivyo nimetaka kwamba maeneo yote hayo ikiwemo Goba, Makoka, Kibwegere, Bonyokwa/Mavurunza, Msakuzi, Mpiji Magoe nk ambayo awali yalikuwa yakihesabika kama vijijini na hivyo kuhudumiwa na miradi ya maji vijijini chini ya Manispaa; mabadiliko ya kisera na kitaasisi yafanyike kwa haraka ili sasa yote yahudumiwe moja kwa moja na maji ya Bomba ya DAWASA/DAWASCO kwa mujibu wa sheria. Ofisi ya Waziri Mkuu imekubali kufanyia kazi mapendekezo niliyotoa; nitaendelea kufuatilia kwa ajili ya hatua kuendelea kuchukuliwa ikiwa ni sehemu ya wajibu wa kibunge wa kuisimamia serikali.

09/02/2012 nimefuatilia pia suala la Kiwanda cha Nguo cha Urafiki kwa ajili ya kulinda rasilimali za umma na pia kuchangia katika kupanua wigo wa ajira hususan kwa vijana ikiwemo wa jimbo la Ubungo. Rejea kauli yangu: http://mnyika.blogspot.com/2011/12/kuhusu-serikali-kulinda-viwanda-vya.html. Nimekabidhi kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara taarifa kwamba hisa asilimia 49 za serikali na mali za umma katika kiwanda cha Nguo cha Urafiki zimeanza kuuzwa katika mchakato ambao unafanyika kinyemela hivyo nimetoa mwito kwao waweze kuingilia kati. Nitaendelea kuchukua hatua zingine za kibunge na kutoa taarifa kwa umma.



No comments: