Mihimili miwili ya nchi yaani bunge na serikali inapaswa kutoa uongozi thabiti wenye kuwezesha Tanzania kupata wabunge wanaokubalika na umma wa Bunge la Afrika Mashariki katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kwenye mkutano ujao wa bunge.
Ili kutimiza azma hiyo Spika wa Bunge Anna Makinda anapaswa kuwezesha marekebisho ya msingi ya kanuni zinazosimamia uchaguzi husika kabla ya katibu wa bunge kutoa tangazo la uchaguzi tajwa.
Aidha, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta anapaswa kutoa kwa umma na kwa vyama vya siasa muswada wa sheria ya uchaguzi wa Afrika Mashariki wa mwaka 2011 uliopitishwa na Bunge la Afrika Mashariki ili uwe msingi wa marekebisho yanayopaswa kufanyika kabla ya uchaguzi husika kufanyika nchini.
Uchaguzi huu una umuhimu wa pekee kwa wananchi wa Tanzania ikiwemo wa Jimbo la Ubungo wakati huu ambapo jumuiya ya Afrika Mashariki ipo katika soko la pamoja na majadiliano ya kuwa na sarafu moja yanaendelea hali ambazo zina athari kwa nchi na wananchi kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Izingatiwe kuwa tarehe 10 Februari 2012 wakati wa kuahirishwa kwa mkutano wa sita wa Bunge Spika Makinda ametangaza kuwa uchaguzi wa wabunge wa kuwakilisha Tanzania kwenye bunge la Afrika Mashariki utafanyika katika mkutano wa saba wa Bunge unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 10 Aprili 2012.
Spika Makinda alitoa maelezo hayo bungeni siku chache baada ya mimi kuandika barua kwa Katibu wa Bunge tarehe 8 Februari 2012 ya kutoa mapendekezo ya kufanyika kwa mabadiliko katika kanuni za kudumu za Bunge Nyongeza ya Tatu (The East African Legislative Assembly Election Rules) zinazosimamia uchaguzi husika.
Kufuatia kauli hiyo nasisitiza kutoa mwito kwa Spika wa Bunge na Kamati ya Kanuni za Bunge watumie mamlaka ya kibunge kwa mujibu wa vipengele 3(3)(a) na (b) vya Nyongeza ya Nane chini ya Kanuni ya 115 ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la 2007 kufanya marekebisho ya msingi katika kanuni za uchaguzi kabla ya kutoa tangazo kamili la uchaguzi husika.
Suala hili ni muhimu kwa maslahi ya taifa kwa sasa kwa kuzingatia kuwa wakati wa uchaguzi wa Wabunge wa Afrika Mashariki uliofanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 2 Novemba 2006 palijitokeza malalamiko na mapendekezo mbalimbali yenye kuonyesha haja ya mabadiliko kufanyika katika Kanuni za Kudumu za Bunge Nyongeza ya Tatu.
Kuanzia mchakato wa uchaguzi wa bunge la Afrika ya mashariki kwa upande wa Tanzania ulipotangazwa mwaka 2006 baadhi ya vyama vilimuandikia barua spika katika hatua mbalimbali kutaka ufafanuzi ama kulalamikia baadhi ya taratibu. Masuala mengi ambayo vyama vilipendekeza yazingatiwe katika uchaguzi huo hayakuzingatiwa ikiwemo kuhusu utaratibu wa uteuzi wa mgombea kutoka kundi la upinzani. Lakini kwa upande mwingine ofisi ya spika ilitoa ufafanuzi kwamba vyama vya upinzani vinayoruhusa ya kusimamisha wagombea katika makundi mbalimbali katika uchaguzi huo zaidi ya kundi C ambalo limetengwa mahususi kwa vyama vya upinzani.
Barua hii ndio ilikuwa msingi wa matangazo ya mwito kwa wanachama kujitokeza kugombea na hata mchakato wa kuteua wagombea uliofanywa na vikao vya vyama. Ufafanuzi huu uliendana pia na hukumu iliyotolewa na msimamizi wa uchaguzi wa kipindi kilichopita ambaye alikuwa katibu wa bunge kipindi hicho Bwana Musa Kipenka.
Katika hoja zake alizotumia kutupilia mbali pingamizi dhidi ya mgombea mmoja wapo wakati huo aliweka bayana kuwa vyama vya upinzani vinahaki ya kugombea katika makundi mbalimbali ya uchaguzi huo. Lakini hali ilikuwa tofauti katika hatua za mwisho za uchaguzi wa mwaka 2006 ambapo maelekezo tofauti yalitolewa. Pia wagombea wa baadhi ya vyama walinyimwa fursa ya kugombea kundi la Zanzibar walilolitaka na kuhamishiwa kundi tofauti na fomu zao za kugombea.
Kadhalika, tangu mwaka 2005 mpaka 2010 masuala ya uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki yameibua migogoro na mijadala katika nchi mbalimbali za Afrika Mashariki hali ambayo Tanzania inapaswa kujifunza na kufanya marekebisho ya msingi ili kuepusha mazingira hayo kujitokeza nchini.
Kutokana na hali hiyo, Bunge la Afrika Mashariki limepitisha Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA Elections Act 2011); hivyo marekebisho ya msingi yanapaswa kufanyika katika kanuni za bunge la Tanzania zinazosimamia uchaguzi tajwa kuendana na mabadiliko ambayo yamejitokeza.
Kifungu cha 4 (3) cha muswada wa sheria hiyo kinataja kwamba uchaguzi wa wabunge unapaswa kuzingatia kadiri iwezekanavyo vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni, kambi na pande zote (shades of opionion), jinsia, makundi maalum na uendelevu na kumbukumbu ya kitaasisi (continuity and institutional memory).
Wakati kanuni za sasa za bunge nyongeza ya tatu kipengele cha 5 (5) kinaweka tu makundi manne ya wagombea yaani: wanawake, wagombea wa Zanzibar, kundi la vyama vya upinzani na wagombea wa bara. Hivyo, kanuni zinapaswa kurekebishwa kuzingatia misingi ya muswada husika na matakwa ya marekibisho yaliyohitajika tangu mwaka 2006.
Katika uchaguzi uliopita pamoja na kuwa vyama vilivyokuwa na wabunge wengi kwa upande wa upinzani vilikuwa ni CHADEMA na CUF; vyama hivyo vyote viwili havikupata hata nafasi moja ya uwakilishi katika Bunge la Afrika Mashariki. Hali hii itajirudia tena hivi sasa iwapo kanuni hazitafanyiwa marekebisho, aidha kwa kanuni za sasa uwakilishi wa kuzingatia masuala mengine ya msingi yaliyoelezwa ili kulinda maslahi ya makundi yote ya kijamii katika Bunge la Afrika Mashariki hautazingatiwa kikamilifu.
Katika muktadha huo, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samuel Sitta anapaswa kutoa kwa umma na vyama vya siasa nakala ya muswada wa sheria husika na kueleza iwapo muswada huo umeshatiwa saini na kuanza kutumika katika nchi za jumuiya husika.
Ni muhimu kwa watanzania kulipa uzito unaostahili suala hili kwa kuzingatia kwamba maandalizi ya uchaguzi kama huu kwenye nchi nyingine za Afrika Mashariki yamekuwa na migogoro ambayo imepelekea mpaka maamuzi katika mahakama ya Afrika Mashariki ya kuzuia chaguzi kuendelea mpaka kanuni katika nchi husika kuweza kufanyiwa mabadiliko.
Uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki unagusa maslahi ya wananchi wa Tanzania katika maeneo yote nchini wakati huu ambapo nchi za jumuiya zipo katika soko la pamoja na zinaendelea na majadiliano ya kuwa na sarafu moja. Hivyo, uchaguzi unapaswa kuwezesha taifa kupata wabunge wanaokubalika watakaosimamia vizuri masuala muhimu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayowagusa wananchi na nchi kwa ujumla katika jumuiya ya Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment