Tuesday, February 7, 2012

Mgomo wa Madaktari bungeni tena leo; nilitaka hatua hizi zichukuliwe

Leo Mbunge wa Mbozi Geofrey Zambi alitoa hoja ya bunge kujadili suala la mgomo wa madaktari kwa dharura kufuatia taarifa kuwa madaktari bingwa nao wameingia kwenye mgomo. Spika Anna Makinda alizuia hoja hiyo kwa maelezo kuwa suala hilo bado linashughulikiwa na bunge kupitia kamati yake ya huduma za jamii. Baada ya maelezo ya Spika niliomba muongozo hata hivyo sikupatiwa nafasi.

Kimsingi nilitaka kuelieza bunge kwamba maelekezo yaliyotolewa na Naibu Spika Job Ndugai yanahitaji kuongezewa maagizo ya ziada na Bunge ili wadau wote wakawa na imani kwamba suala hili linashughulikia kwa dharura na kwa mwelekeo stahiki hali ambayo itashawishi mgomo kuweza kusitishwa.

Hadidu rejea na ratiba ya kamati inapaswa iwe bayana hivyo kuna umuhimu wa uongozi wa bunge kutoa tamko lenye maelezo ya ziada kwa kuwa kimsingi madaktari walishapoteza imani na namna ambavyo serikali kupitia kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikishughulikia masuala yao.

Aidha, imani hiyo ilipoteza zaidi baada ya uamuzi wa Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii kutoa maelezo yasiyokuwa ya kweli bungeni kuhusu madai ya madaktari na hali ya mgogoro mzima. Bunge na uongozi wa bunge unapaswa kuwa makini katika mazingira ya sasa ili kuepusha uwezekano wa madaktari na wananchi kwa ujumla kupunguza imani pia na namna ambavyo mgogoro huu unashughulikiwa.


Nilitaka kuomba muongozo wa Spika ili agizo litolewe kwamba Kamati husika ya Bunge itawasilisha taarifa yake ya awali kwenye mkutano wa bunge unaoendelea; hii itajenga imani kwa madaktari na wananchi kwamba bunge lina dhamira ya kushughulikia kwa haraka suala hili. Katika mazingira ya sasa ya ratiba kutokuwa bayana ya lini kamati inatarajia kukamilisha kazi yake, madaktari na wananchi wanaweza kuwa na mashaka kwamba taarifa ya kamati italetwa bungeni katika mikutano ijayo ya bunge kuanzia mkutano wa saba mwezi Aprili.

Aidha, kwa kuwa imeonyesha bayana kwamba madaktari hawana imani na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Katibu Mkuu wa Wizara husika na Mganga Mkuu wa Serikali ni muhimu Kamati ya Bunge ikalitafakari suala hili na kama bado ni kikwazo; inashauri serikali mapema ili watendaji husika waweze kuondolewa ili majadiliano yaendelee katika msingi wa maelewano.

Pia; katika kauli yake bungeni serikali pamoja na kukataa sehemu kubwa ya madai ya msingi ya madaktari haikutoa kauli yenyewe ni nini iko tayari kutoa hivyo kuweka msingi wa majadiliano. Ikiwa tayari serikali imeweka mezani misingi ya majadiliano ni muhimu Spika wa Bunge airuhusu kamati husika itoe mrejesho ama kwa madaktari kupitia kwa wawakilishi wao, au kwa bunge ili kujenga imani kwamba bunge tayari limeanza kuchukua hatua za haraka ili madaktari na umma kuwa na imani kuwa ufumbuzi wa mgogoro unaelekea kupatikana mapema.

Naungana na wote ambao pamoja na kutaka bunge kuharakisha usuluhishi wa mgogoro baina ya madaktari na serikali na kuisimamia serikali kutatua madai ya msingi ya madaktari; nawaomba pia madaktari na watumishi wengine wa afya katika utumishi wa umma wahakikishe wanaendelea kuokoa na kulinda maisha ya wananchi wasio na hatia.

John Mnyika (Mb)

07/02/2012



2 comments:

Anonymous said...

Tunashukuru kwa mrejesho huu Mh Mbunge. Kwe kweli ina huzunisha kuona jinsi wananchi wanapata tabu katika mgogoro huu wakati wao ni nyasi tuu kwenye uwanja wa mapambano kati ya Madaktari na Serikali.

Ni vigumu mtu kuupata uchungu huu wanaoupata wenzetu hadi pale utakapompeleka mwanao, mkeo, baba, mama, kaka, dada nk akiwa hoi ukitegemea kupatiwa matibabu na kukosa hivyo mgonjwa wako akakufia mikononi just like that!

Ningetegemea kuona matamko mbalimbali toka vyama vya siasa, ngo na taasisi mbalimbali za kiraia juu ya suala hili lakini nao wamekaa kimya kama serikali yenyewe. Hivi ni raia wangapi wanatakiwa kupoteza maisha ili hatua za dhati zichukuliwe? Jamani mnafanya usanii hata kwenye uhai wa watu?

Natumaini mahalipengine watu wangeshajaa mitaani. Inasikitisha.

Anonymous said...

Ni aibu hata kwa CHADEMA ambao tunajipambanua kuwa tunaongozwa na nguvu ya umma halafu hatufanyi chochote kwa umma unaopotea. Labda tuanze kuainisha kuwa umma wetu ni ule wa wenye uwezo wa kupiga kura tu na wenye afya njema. Wabunge mnakaaje bungeni kujadili mafuta na gesi halafu mnasahau roho za watu zinazoteketea kila siku? Mbona ni ajabu hii! Hatuna hata vipaumbele? au na wabunge ni wachawi tu...ndo maana huku wenzetu wanakufa wabunge mnadai posho? Please, suala hapa ni utaifa sio UCHADEMA watanzania wanakufa na hivyo lazima tuahirishe jukumu lolote ili kuokoa hali hiyo. its not fair Ndg. Mnyika you have to do something with your party.