Baada ya habari kutolewa jana na leo juu
ya uamuzi wa Spika kuhusu tuhuma kwamba baadhi wa wabunge na wajumbe wa kamati
ya Nishati na Madini walijihusisha na vitendo vya rushwa katika kutekeleza kazi
zao za kibunge, nimeulizwa na baadhi ya wanahabari na wananchi kwa simu na
kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii sababu za kusimama bungeni tarehe 9
Novemba 2012 mara baada ya Spika kutoa uamuzi huo na kutaka kuomba muongozo.
Nalazimika kutoa ufafanuzi huu nje ya
bunge baada ya mkutano wa bunge kuahirishwa bila Spika kunipa fursa ya kusema
jambo hili bungeni kwamba nilitaka muongozo wake kwa mujibu wa Kanuni ya 5(1)
na 5 (2) kuwa nakusudia kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake kutokana na kuwa na
maudhui kadhaa yasiyozingatia katiba ya nchi, sheria mbalimbali za nchi, kanuni
za kudumu za bunge, maamuzi ya awali ya maspika wa Bunge pamoja na mila na
desturi za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu
wa bunge letu.
Hata hivyo kwa kuzingatia kuwa rufaa
huchukua muda kusikilizwa nilitaka niombe muongozo wake kabla ya Mkutano wa
Bunge kuahirishwa kwa kuwa katika uamuzi wake hakueleza hatma ya Kamati ya
Nishati na Madini ilivyovunjwa, hivyo Spika anapaswa bado kueleza kwa umma
iwapo kamati hiyo inarejeshwa au inaundwa kamati nyingine au kuelekeza kamati
nyingine ya kudumu ya Bunge inayopaswa kuisimamia Serikali wakati huu ambapo
nchi inakabiliwa na matatizo mengi kwenye sekta za nishati na madini yenye
athari kwa maisha ya wananchi wakiwemo wa Jimbo la Ubungo.
Kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa
Nishati na Madini nasisitiza kwamba Spika anapaswa kurejea barua yangu ya toka
mapema Oktoba ambayo mpaka sasa haijapatiwa majibu, hoja niliyoiwasilisha
bungeni na kuungwa mkono ya jambo lililohusu haki za bunge na miongozo niliyoomba bungeni kuhusu masuala
ya nishati kwa nyakati mbalimbali katika mkutano wa Bunge uliomalizika na kutoa kauli kwa umma.
Kwa kuwa katika uamuzi wake Spika wa
Bunge ameeleza kwamba Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake Eliackim Maswi
wametoa maelezo yasiyokuwa kweli kwa nyakati mbalimbali uwepo wa kamati ya
bunge kwa ajili ya kuisimamia Wizara hiyo kwa niaba ya bunge ni suala linalohitaji
uamuzi wa haraka.
Aidha, katika uamuzi wake Spika zaidi
ya kutoa onyo kali kwa Katibu Mkuu na Wabunge hakutoa onyo kwa Waziri wa
Nishati na Madini wala hakueleza chochote
iwapo alipokea ushauri kutoka kwa Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka
ya Bunge kuhusu ukiukwaji wa kanuni uliofanywa na Spika mwenyewe bungeni wakati
wa kadhia nzima.
Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Spika
anaweza kutoa taarifa bungeni wakati wowote
na taarifa yake haijadiliwi hivyo sehemu kubwa ya taarifa ya tarehe 9 Novemba
2012 ilikuwa ni maelezo kuanzia sehemu ya kwanza mpaka sehemu ya pili.
Uamuzi wa Spika unapatikana sehemu ya
tatu ya maelekezo hususan kifungu cha 6.12 ya kwamba “tuhuma husika hazikuweza
kuthibitishwa” na baadaye kufuatiwa na uamuzi wa Spika kuhusu watoa tuhuma
katika vipengele (a), (b), (c) na (d).
Nakusudia kukata rufaa ili taarifa
kamili ya Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iweze kuwasilishwa
kwa ukamilifu wake kwenye kamati husika ya kudumu ya Bunge na hatimaye taarifa
kamili kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni ili ‘mbivu na mbovu’ zijulikane na
masuala yanayohitaji kufanyiwa uchunguzi wa ziada na vyombo vingine vya nje ya
Bunge yaendelee kwa hatua zaidi badala ya uamuzi huu wa ‘funika kombe’.
Yapo masuala ya ziada ambayo binafsi
niliyaeleza mbele ya kamati ndogo chini ya kiapo ambayo sitakiwi kuyaeleza nje
ya bunge kwa mujibu wa kanuni na sheria husika , hata hivyo taarifa kamili
ikiingia bungeni kutakuwa na uhuru wa majadiliano kwa mujibu Kwa Ibara ya 100
ya Katiba ya Nchi.
Aidha, nitaka rufaa kwa kuwa kiwango
cha ‘adhabu’ kilichotolewa kwenye uamuzi wa Spika hakilingani na ‘makosa’
ambayo yameelezwa kuwa na uzito wenye
kuathiri “kwa kiasi kikubwa hadhi ya Bunge kama taasisi na heshima ya wabunge
waliohusishwa”.
Spika amefanya uamuzi wake chini ya
Kanuni ya 5(1) na 72 (1) lakini hakuzingatia kuwa kanuni ya 72 (3) inaeleza
kuwa iwapo mbunge ameshindwa kuthibitisha ukweli Spika amepewa fursa ya
kumsimamisha mbunge huyo kuhudhuria vikao vya Bunge visivyozidi vitano.
Aidha nitakata rufaa kwa kuwa
waliodaiwa kutoa kutoa tuhuma bila ushahidi walipaswa kujieleza kwa tuhuma hizo
kabla ya kuhukumiwa kwa misingi ya kanuni za haki ya asili zilizopo pia katika
katiba ya Nchi na kwa kuzingatia matakwa ya kanuni za kudumu za Bunge; hata hivyo
Spika amefikia uamuzi wa moja kwa moja wa kutoa adhabu ya ‘onyo kali’ kinyume
na masharti ya kanuni ya 5 (1).
Ikumbukwe kwamba Spika katika maelezo
yake amesisitiza kuwa Kamati Ndogo ilipewa hadidu rejea moja tu, “Kuchunguza na
kumshauri Spika iwapo tuhuma kwa baadhi ya wabunge na wajumbe wa Kamati ya
Nishati na Madini kujihusisha na vitendo vya rushwa ni za kweli au hapana”,
baada ya kuchunguza kwa mujibu wa hadidu rejea hiyo na kuwasilisha ripoti yake
Spika alipaswa kama kuna ukiukwaji mpya wa kanuni uliobainika kutokana na
uchunguzi huo kuanzisha mchakato wa adhabu.
Binafsi niliitwa kwa maandishi kuisaidia
kamati ndogo katika uchunguzi wake kutokana na maoni niliyowasilisha bungeni ya
kwamba “….Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inafahamu kwamba kuna kampeni kubwa inafanywa ndani na nje ya Bunge ili
uamuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ubatilishwe kwa maslahi ya Makampuni
yaliyokosa zabuni kuiuzia TANESCO mafuta ya kuendesha mitambo ya kufua umeme…”.
Sijawahi kuandikiwa au kuitwa popote
kutakiwa kujieleza kwa ‘kuisemea tuhuma bungeni bila ya kufanya utafiti kupata
ukweli’ na maelezo hayo niliyoyatoa bungeni hayakukiuka kanuni yoyote ya bunge
kama ambavyo nitathibitisha wakati nitakapokata rufaa.
Kwa upande mwingine nitakata rufaa kwa
kuwa adhabu aliyopewa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi
hailingani na ukubwa wa makosa anayodaiwa kuyafanya, ikiwa ni kweli amevunja
haki za bunge kwa kuzusha tuhuma za uongo dhidi ya wabunge kwa ajili ya
kujihami dhidi ya baadhi ya wajumbe wa kamati ya Bunge ya Nishati na Madini
waliokuwa wanahoji kuhusu utendaji wa Wizara yake.
Kwa kosa hilo ikiwa maelezo ya Spika
kuhusu matokeo ya uchunguzi wa Kamati ni sahihi anapaswa kufunguliwa mashtaka
kwa mujibu wa Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge na kupewa adhabu ya
zaidi ya onyo ikiwemo hata faini au kifungo au walau kutakiwa kuwajibika.
Kadhalika kwa Spika ameeleza kuwa mbinu
aliyotumia ni pamoja na kutaka kuwalipa fedha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya
Nishati na Madini shilingi milioni mbili kwa kila mjumbe madai haya ni ya
jaribio la kufanya ufisadi wa fedha na matumizi mabaya ya madaraka kama
ilivyokuwa kwenye kashfa ya Katibu Mkuu aliyemtangulia David Jairo hivyo Spika
alipaswa kupendekeza kwa mamlaka ya uteuzi wake kuchukua hatua za kinidhamu na
kisheria.
Uamuzi wa Spika ‘kufunika kombe’ hauna
tofauti na maamuzi yaliyotangulia ambayo yamesababisha mpaka sasa Serikali
haijawasilisha bungeni ripoti ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge kufuatia
uchunguzi uliofanywa na kamati teule ya Bunge.
Ni vizuri ikakumbukwa kwamba katika
hotuba yangu bungeni kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tarehe 27
Julai 2012 nilisisitiza kwamba “ili
ukweli wa kina uweze kujulikana Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa bunge
liazimie kuunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza masuala yote ya ukiukwaji wa
sheria, matumizi mabaya ya madaraka na tuhuma za ufisadi katika utekelezaji wa
mpango wa dharura wa umeme na ununuzi wa mafuta wa ajili ya mitambo ya umeme.
Uchunguzi huo uhusishe pia mkaguzi mkuu
kufanya ukaguzi wa kiuchunguzi (Forensic Audit) kwa malipo yaliyofanywa na
makampuni ya BP (Sasa PUMA Energy), Oryx na Camel Oil ili kubaini iwapo kuna
vigogo zaidi wa serikali waliojinufaisha kwa kisingizio cha dharura ya umeme.
Izingatiwe kwamba masharti ya ibara ya 27(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania inamtaka kila mtu “… kutunza
vizuri mali ya Mamlaka ya Nchi na ya pamoja (na) kupiga vita aina zote za
uharibifu na ubadhirifu….”.
Mchakato huu ungewezesha kupata ukweli
wa ziada kibunge kuliko utaratibu uliotumiwa na Kamati Ndogo na Spika.
Nitaeleza masuala ya ziada
nitakayoyakatia rufaa na kauli yangu kuhusu maelezo na uamuzi wa Spika juu ya
Waziri na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini.
John Mnyika (Mb)
10/11/2012
No comments:
Post a Comment