Wednesday, November 7, 2012

Sera ya gesi itafsiriwe kwa Kiswahili

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika amemtaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuwaagiza maofisa wake kuitafsiri sera ya gesi asili iliyoandikwa kwa kiingereza badala ya Kiswahili ili wananchi wengi waweze kuifahamu na kuitolea maoni.

Hatua hiyo ya Mnyika imekuja baada ya wizara ya Nishati na Madini kutoa matangazo kwenye magezeti kuhusu rasimu ya sera ya gesi asilia ikiwa katika lugha ya Kiingereza.

“Napinga hatua ya wizara kutoa rasimu ya sera hiyo kwa kiingereza pekee, natoa wito kwa Waziri Muhongo atoe kauli kwa umma kuwa rasimu hiyo itatolewa haraka kwa lugha ya Kiswahili na kuchapwa katika vyombo vingine vya habari,” alisema Mnyika ambaye ni Waziri Kivuli wa wizara ya Nishati na Madini.

Alhamisi iliyopita, uliibuka mjadala mkali Bungeni wakati wa kupitishwa kwa azimio la kuridhia itifaki ya uanzishaji wa kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo Tanzania ilihimizwa kutumia lugha ya Kiswahili katika taarifa zake kwa wananchi zikiwemo sera na sheria.

Mnyika alisema zikichapwa kwa Kiswahili wananchi wengi mijini na vijijini watapata fursa ya kutoa maoni kwa sababu wataelewa kilichoandikwa kwa kuwa ni wananchi wengi wanaofahamu lugha ya Kiingereza.

Alisema tafsiri hiyo ifanyike haraka kwa sababu muda uliotolewa kwa ajili ya kukusanya maoni na mapendekezo unamalizika Novemba 22 mwaka huu.

Mnyika pia Profesa Muhongo kutoa kwa umma ripoti ya awali ya upitiaji upya wa mikataba 26 ya utafutaji wa gesi asilia ili udhaifu uliojitokeza utumiwe na wananchi katika utoaji wa maoni katika kuboresha sera ya gesi.

Pia Mnyika alitaka wizara hiyo kueleza kwanini dola 20.1 milioni zilizopunjwa na kampuni ya Pan African Energy Tanzania (PAT) hazijarejeshwa Serikalini.

Chanzo: http://www.hakingowi.com/2012/11/john-mnyikasera-ya-gesi-itafsiriwe-kwa.html

No comments: