Monday, December 10, 2012

ORODHA YA UFISADI NA UZEMBE TANESCO AWAMU YA KWANZA NA MWITO WA KUTOA MAONI KUHUSU KUSUDIO LA KUPANDISHA BEI YA UMEME KWA MARA NYINGINE


Shirika la Umeme (TANESCO) linakabiliwa na ufisadi na uzembe unaoongeza gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme kwa upande mmoja na uendeshaji wa shirika kwa upande mwingine.  Ufisadi na uzembe huo unapunguza uwezo wa TANESCO kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na unaongeza gharama na bei ya upatikanaji wa umeme hali inayoathiri uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kwa kuchangia katika mfumuko wa bei na ongezeko la gharama za maisha. Mzigo wa ufisadi na uzembe katika TANESCO unajitokeza zaidi katika mikataba mibovu pamoja na ukiukwaji wa sheria za ununuzi wa umma, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63 sehemu ya pili ya bunge (inayoundwa na wabunge) ndio chombo kikuu chenye madaraka na mamlaka kwa niaba ya wananchi ya kuisimamia serikali. Hata hivyo, katika kipindi cha kati mwaka 2008 mpaka 2012 maazimio ya Bunge kuhusu sekta ya nishati ikiwemo kuhusu umeme yamekuwa hayatekelezwi kwa wakati na kwa ukamilifu hali inayofanya tuhuma za ufisadi na uzembe kuendelea kujirudiarudia. Katika muktadha huo, ni muhimu kwa kuwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi ibara ya 8 madaraka na mamlaka ni ya umma (serikali inafanya kazi kwa niaba tu) ipo haja ya kuanza kuunganisha ‘nguvu ya umma’ katika kushinikiza hatua kuchukuliwa kwa wahusika wa ufisadi na uzembe ili kuweka misingi bora ya uwajibikaji katika sekta ya nishati.

Ili umma uweze kuungana kuchukua hatua ni muhimu masuala yote ya ufisadi na uzembe yakaelezwa kwa uwazi kwa umma hivyo, katika mfululizo huu nitaweka hadharani orodha za watuhumiwa wa ufisadi na uzembe katika sekta ya nishati. Orodha hizi zinatolewa kwa awamu zikigusa kwa kuanzia mashirika na taasisi zilizochini ya Wizara ya Nishati na Madini na baadaye Wizara yenyewe na hatimaye Serikali kwa ujumla. Aidha, orodha hizi zitatolewa kwa awamu masuala kwa masuala na matukio kwa matukio, ngazi kwa ngazi.

Katika orodha ya awamu ya kwanza nitaanza na TANESCO kuhusu masuala na matukio yaliyohusu kampuni ya M/S SANTA CLARA SUPPLIES COMPANY LIMITED pamoja na kampuni ya M/S McDONALD LIVE LINE TECHNOLOGY LIMITED. Orodha nyingine zitafuata katika awamu ya baadaye iwapo vyombo na mamlaka husika hazitachukua hatua ikiwemo juu ya tuhuma za ufisadi na uzembe katika matumizi ya dola milioni 54 (zaidi ya bilioni 86) katika ununuzi wa mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya IPTL.


Nimetoa majina haya hadharani ili umma uunganishe nguvu kwa njia mbalimbali kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya ufisadi na uzembe ili kuhakikisha nchi inaongozwa kwa utawala wa sheria na maadili katika utumishi wa umma.

Mamlaka zinazopaswa kuchukua hatua ni pamoja na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Sekretariati ya Maadili ya Umma zote kila moja kwa nafasi yake zichunguze ukiukwaji wa sheria katika masuala yaliyo kwenye majukumu yao na kuchukua hatua za ziada kwa kuzingatia pia ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo nimeitumia kama rejea kwenye baadhi ya masuala katika orodha hii.

Aidha, kwa kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeitisha Mkutano wa Taftishi Juu ya Marekebisho ya Bei ya Umeme za TANESCO ambao inakusudiwa bei ya umeme kupandishwa tena, ni muhimu masuala ya ufisadi na uzembe ndani ya TANESCO yakajadiliwa kwa upana na umma, ili kupinga gharama zinazotokana na hali hiyo zisiingizwe katika mahesabu ya kukokotoa bei.

Ikumbukwe kwamba tarehe 9 Novemba 2011 EWURA ilipokea Ombi la Dharura toka TANESCO na kupandisha bei kwa wastani wa asilimia 155 kuanzia tarehe 1 Januari 2012 na niliunganisha umma kupinga na hatimaye EWURA ikapunguza asilimia hiyo na kuruhusu nyongeza ya wastani wa asilimia 40.29 ambayo ndiyo inayotumika hivi sasa.

Hivyo, nitumie nafasi hii kuhimiza pia umma kujitokeza tarehe 10 Disemba 2012 kuanzia saa 4 asubuhi katika Ukumbi wa Karimjee Dar es salaam kwenda kutoa maoni kwa kuzingatia Taarifa ya Gharama za Huduma ya Umeme (Cost of Service Study) na zaidi kwa kupinga kuingizwa kwenye bei ya umeme gharama za uzembe na ufisadi ili kupunguza athari katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi miaka 51 baada ya Uhuru.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,


John Mnyika
Mbunge wa Jimbo la Ubungo
09/12/2012

No comments: