Sunday, December 9, 2012

Maadhimisho ya Miaka 51 ya Uhuru: Uwajibikaji, Uadilifu na Uzalendo ni nguzo ya Maendeleo ya Taifa


Leo ni kumbukumbu ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanganyika (sasa Tanzania Bara), maadhimisho yanayoendelea yamenifanya nikumbuke, waraka niliouandika mwaka 2011 (“Uhuru na Mabadiliko”) wakati wa kumbukumbu ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika.

Kwamba “Ili uhuru wetu uweze kuwa wenye matokeo kwenye maisha yetu na ya taifa letu tunahitaji kuungana kufanya mabadiliko ya kweli. Changamoto kubwa ambayo nimeiona ni kwamba kuna udhaifu katika mifumo yetu ya kiserikali kwenye ngazi mbalimbali hali ambayo inakwaza hatua za haraka za kuleta mabadiliko.

Kwa pamoja tunapaswa kuendelea kulitoa taifa letu katika kufilisika kimaadili na kiitikadi na kukubaliana tunu za kitaifa zenye kuwezesha misingi ya uwajibikaji. Uhuru wa kweli wa kisiasa utakuja kwa kuwa na uongozi wenye maono (vision) na maadili (values) na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha kuanzia sasa na kuendelea kutuwezesha kunufaika na rasilimali zetu: iwe ni vipaji vyetu, kodi zetu au maliasili za nchi yetu.”.


Mara baada ya maadhimisho yanayoendelea katika Uwanja wa Taifa, nitakuwa kwenye mitaa mbalimbali ya kata ya Ubungo kwenye mikutano na wananchi tukitafakari kuhusu nchi yetu na kuhamasisha umma kuunganisha nguvu kuchukua hatua dhidi ya ufisadi na uzembe katika muktadha wa kauli mbinu ya Maadhimisho ya Miaka 51 ya Uhuru iliyotolewa na Serikali mwaka huu wa 2012 ‘Uwajibikaji, Uadilifu na Uzalendo ni nguzo ya Maendeleo ya Taifa’.

Lengo likiwa kuendelea kuunga mkono vuguvugu la mabadiliko kwa ajili ya kuleta uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya Jimbo letu na Taifa letu kwa ujumla.

Nawatakia  upendo, furaha na mafanikio  katika kumbukumbu ya uhuru huku tukiweka mstari wa mbele ukweli, uadilifu, na uwajibikaji katika maisha yetu.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)
09/12/2012

No comments: