Thursday, December 6, 2012

Balozi Sefue na Yambesi watoe kauli iwapo Serikali imetoa waraka wa maagizo kwa watumishi wa umma kutoa taarifa katika mikutano ya CCM kinyume cha maadili




Katibu Mkuu Mkuu Kiongozi (Ofisi ya Rais-Ikulu) Balozi Ombeni Sefue na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi (Ofisi ya Rais) Menejimenti ya Utumishi wa Umma George Yambesi watoe kauli kwa umma iwapo Serikali imetoa waraka mpya kwa watumishi wa umma kuhudhuria mikutano ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoa taarifa kama sehemu ya kazi zao kama walivyotakiwa na chama hicho katika tamko lake la tarehe 2 Disemba 2012.

Kwa sasa utumishi wa umma katika nchi yetu unaongozwa na Sheria ya Utumishi wa Umma na. 8 ya mwaka 2002 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2007 pamoja na kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003 kama zilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2009 na kanuni za maadili ya utendaji katika utumishi wa umma za mwaka 2005.

Itakumbukwa kwamba awali utumishi wa umma Tanzania ulikuwa ukiongozwa na Sheria ya Utumishi Serikalini namba 16 ya mwaka 1989 na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma Toleo la 1994 pamoja na marekebisho yake. Kifungu cha 4(1) cha Sheria hiyo kilimpa mamlaka Mkuu wa Utumishi wa Umma, ambaye ni Katibu Mkuu kiongozi kutoa waraka kuhusu taratibu mbalimbali za utumishi wa umma.

Chini ya Mamlaka hayo, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Martem Y.C. Lumbanga tarehe 26 Juni, 2000 alitoa Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma na. 1 wa mwaka 2000 wenye kumb. Na. SHC/C.180/2/113 uliohusu maadili ya Watumishi wa Umma katika mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Waraka huo unawataka watumishi wa umma kutekeleza wajibu wao wa utumishi bila kufanya upendeleo wala ubaguzi wa chama chochote cha siasa. Waraka huo unawakataza watumishi wa umma kuzungumza na kutoa taarifa kwenye mikutano ya vyama vya siasa na haujatoa ruhusa kwa watumishi hao kuzungumza katika mikutano ya CCM pekee; hivyo Balozi Sefue na Yambesi wanapaswa kutoa kauli kwa umma iwapo Serikali imetoa waraka mwingine kwa siri wenye kuagiza watumishi wa umma kutoa taarifa katika mikutano ya CCM.

Izingatiwe kwamba kanuni za maadili ya utendaji katika utumishi wa umma hazielekezi watumishi wa umma kuwa na utii au kuwajibika kwa CCM bali zinaeleza kwamba watumishi wa umma watawajibika kwa umma na watakuwa na utii kwa Serikali na sio chama kinachotawala na zimeweka mipaka ya matumizi sahihi ya taarifa za kiserikali wanazowajibika kuzitoa kwa nafasi zao.

Izingatiwe kuwa mapendekezo ya Tume ya Nyalali ya mwaka 1991 na marekebisho ya Katiba ya mwaka 1992 kuingia katika mfumo wa vyama vingi na marekebisho ya sheria yaliyofuata yameweka uhuru wa watumishi wa umma katika kujiunga na vyama vya siasa (isipokuwa watumishi wa kada maalum) na mipaka ya mahusiano kati ya kazi zao za kiserikali na shughuli za vyama vya siasa kikiwemo chama kinachotawala.

Hivyo maagizo au waraka wenye kuwalazimisha watumishi wa umma kuhudhuria mikutano ya CCM na kutoa kutoa taarifa ni kinyume cha uhuru wa kikatiba, sheria za nchi, kanuni za utumishi wa umma na misingi ya utawala bora.

Imetolewa na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
05/12/2012

1 comment:

Anonymous said...

KUNA HALI KUBWA SANA YA UBABE UNAOFANYWA NA CCM KAMA CHAMA NA HATA IMEFIKIA MAHALI WANAJIHISI WAO NI SERIKALI NA SERIKALI NI WAO KUMBE WAO NI 'WATOA SERA' TU.

HII NDIO SABABU WANATOA MAAGIZO YA KIJESHI AU KIASKARI KWA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA KUPIGA NA HATA KUUA RAIA(REJEA MIKUTANO YA CHADEMA MOROGORO NA IRINGA).

NAFIKIRI UMEFANYA UUNGWANA KUMWULIZA HUYU BWANA SEFUE AJUE SIKU SI NYINGI ATAWAJIBIKA KWA MATENDO YAKE (AKINYAMAZA ITAMAANISHA KARUHUSU UHALIFU HUO) KWANI CCM WANASEMA TENA KWA KUJIDAI KUWA WATAENDELEA KUTUMIA RASILIMALI ZA UMMA/SERIKALI BILA WOGA KWANI WAO NDIO WATAWALA...SASA SIJUI KAMA KUWA MTAWALA INAMAANISHA UNAJIFANYIA MAMBO KINYUME CHA KATIBA, SHERIA,KANUNI NA TARATIBU ZA NCHI AU TUUITE HUO NI UASI WA CCM KWA SERIKALI WANAYOIONGOZA?

RAHA YA UBABE NI MOJA:LEO WEWE NI MBABE,KESHO MWENZIO TENA OMBA MUNGU UBABE WAKE UWE UNA MIPAKA,VINGINEVYO ATALIPIZA VYOTE ULIVYOMFANYIA....CCM LEO ENDELEENI NA UBABE LAKINI MJUE MNATUFUNDISHA NASI JINSI YA KUWARUDI MUDA SI MREFU...KAENI CHONJO!!!