Sunday, December 30, 2012

Tume yachunguza kilio cha Maji Goba

Na Katuma Masamba

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini bado inafanyia kazi malalamiko yaliyowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) anayetaka kujua kiini cha wakazi wa Goba kutokupata maji.

Mnyika aliwasilisha barua yake yenye malalamiko kwenye Tume hiyo ili kujua tatizo linalosababisha kata ya Goba kukosa huduma ya maji tangu mwaka 2007.


Mkurugenzi wa Tume hiyo ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Francis Nzuki alisema malalamiko hayo bado wanayafanyia uchunguzi ili kubaini tatizo linalofanya kata hiyo isipate maji kwa muda mrefu sasa.

Alisema baada ya kukamilika kwa uchunguzi watatoa majibu haraka iwezekanavyo juu ya malalamiko hayo ila kwa sasa bado wanaendelea kufanyia kazi malalamiko hayo.

Wakazi wa Goba wanalalamikia ukosefu wa maji unaowaathiri wakazi kwa muda mrefu sasa ambapo hulazimika kununua ndoo moja yenye ujazo ya lita 20 kwa Sh 500 hadi Sh 700.

Naye Mnyika alisema amekuwa akijitahidi kufanya juhudi ili wapiga kura wake waondokane na tatizo hilo na kuongeza kwamba Halmashauri ya Kinondoni ndiyo inayokwamisha kata hiyo isipate maji.

Mnyika alisema anaendelea kusubiri taarifa itakayokuwa na majibu ya malalamiko yake ili ajue tatizo liko wapi kwa wananchi kukosa maji miaka yote hiyo.

Chanzo: http://www.habarileo.co.tz/index.php/habari-za-kitaifa/7727-tume-yachunguza-kilio-cha-maji-goba

No comments: