Monday, February 4, 2013

MAELEZO NA HOJA BINAFSI YA KUPENDEKEZA BUNGE LIJADILI NA KUPITISHA MAAZIMIO YA HATUA ZA HARAKA ZA KUBORESHA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA USHUGHULIKIAJI WA MAJI TAKA KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM KWA MUJIBU WA KANUNI YA 54 FASILI YA (1) YA KANUNI ZA KUDUMU ZA BUNGE TOLEO LA MWAKA 2007

Mheshimiwa Spika; 
Awali ya yote niungane na wote wenye mapenzi mapema katika kuomba ulinzi wa Mwenyezi Mungu wakati tukitimiza wajibu wa kibunge kwa mujibu wa ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania wa kuwawakilisha wananchi, kuisimamia serikali, kuidhinisha mipango na kutunga sheria.

Mheshimiwa Spika;
Aidha, kwa namna ya pekee ni kushukuru wewe binafsi na uongozi mzima wa Bunge kwa kunipa fursa hii adimu na adhimu ya kuwasilisha hoja binafsi kwa mujibu wa kanuni ya 54 fasili ya (1) ya kupendekeza bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam.

Mheshimiwa Spika;
Maji ni uhai, hivyo matatizo ya upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam na nchini kwa ujumla kama hatua za haraka zisipochukuliwa yatageuka kuwa janga la taifa. Katika kila watanzania katika Jiji la Dar es Salaam na nchini; kwa wastani mmoja hapati huduma ya maji safi na salama na hali ni mbaya zaidi kuhusu ushughulikiaji wa maji taka.

Wakati baadhi ya nchi duniani zikielezwa kwenye kitabu cha hivi karibuni cha Mnukuzi Maalum wa Umoja wa Mataifa (UN Special Rapporteur) kuwa katika mwelekeo unaostahili kuhusu kuhakikisha haki ya maji na usafi wa mazingira (On the right track; Good practices in realizing the rights to water and sanitation: 2012), hali ni kinyume kwa taifa letu.

Ripoti ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia masuala ya maji (WaterAid: 2011) imeiweka Tanzania katika kundi la nchi ambazo haziko katika mwelekeo unaostahili wa kuboresha upatikanaji wa maji safi, ushughulikiaji wa maji taka na usafi wa mazingira (Policy Report: Off Track, Off Target; why investments in water, sanitation and hygiene is not reaching those who need the most).

Mheshimiwa Spika;
Hoja hii inalengo la kuibua mjadala wa hatua za haraka. Kimsingi hatua hizi za haraka hazitanufaisha Mkoa mmoja pekee kwa kuzingatia kuwa Mpango Maalum wa kutatua tatizo la maji katika Jiji la Dar es salaam ni kwa ajili pia ya maeneo mengine ya miradi iliyo sehemu ya mpango huo ya Morogoro mpaka Pwani. Aidha, kujadiliwa na kupitishwa kwa mapendekezo ya hoja hii kutaongeza pia msukumo wa miradi katika maeneo mengine ya mijini na vijijini katika mikoa mbalimbali nchini.

Shukrani zangu za dhati ziwafikie wabunge wenzangu wa vyama vya upinzani na wa chama tawala kwa maoni na mapendekezo yenu yaliyoniwezesha kuirekebisha hoja hii pamoja na ushauri wa Katibu wa Bunge Dr Thomas Kashillilah na maafisa na watendaji katika ofisi ya bunge, kambi rasmi ya upinzani na ofisi ya mbunge wa Jimbo la Ubungo mlioboresha hoja hii kwa manufaa ya Jiji la Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika;
Nitumie pia nafasi hii kuwashukuru Watanzania wenzangu wa kada, hadhi na ngazi mbalimbali katika taasisi na maeneo mengi ndani na nje ya nchi mnaoendelea kuniunga mkono kwa hali na mali katika kutimiza majukumu yangu ya kibunge na nafasi nyingine ninazozitumikia.

Nawashukuru sala zenu wakati wa kesi ya msingi na rufaa ya kupingwa kwa matokeo ya ushindi wetu Jimbo la Uchaguzi la Ubungo; kwa pamoja tumeshinda, tuendelee na kazi.

Aidha, pamoja na mjadala huu wa bungeni natarajia kupokea maoni na mapendekezo yenu kuhusu hoja hii kwa njia mbalimbali za mawasiliano ikiwemo kupitia mtandao wa http://mnyika.blogspot.com kwa hatua zaidi. Kaulimbiu yetu ni ile ile: AMUA; Maslahi ya Umma Kwanza.


MAELEZO YA HOJA: 

Mheshimiwa Spika;
Maji ni mojawapo ya mahitaji ya msingi ya binadamu, maji ni uhai. Upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ni sehemu ya muhimu ya maendeleo ya nchi na maisha ya wananchi. Maji ni lazima kwa matumizi ya majumbani, maji ni muhimu ni moja ya malighafi muhimu katika kazi za uzalishaji iwe ni za viwanda, kilimo, mifugo na shughuli zingine za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni nchi ambayo imejaliwa vyanzo vingi vya maji, vinavyohusisha mito, mvua, maziwa na bahari; kuwepo kwa vyanzo hivi vya maji ni wazi kuwa nchi yetu inaweza kuepukana na shida ya maji inayoikumba jamii ya Tanzania iwapo tutaondoa udhaifu uliopo. Aidha, udhaifu huo unahusisha pia kuziweka vyanzo vyenyewe pia mashakani kwa matendo ya binadamu yenye kuathiri endelevu wa matumizi hali itayozua migogoro katika siku za usoni iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

Mheshimiwa Spika;
Upatikanaji wa maji safi na salama kwa urahisi wa bei unachangia katika kupunguza gharama za maisha; upatikanaji wa maji safi na salama karibu na makazi husaidia jamii, hususan wanawake, kutumia nguvu na muda katika uzalishaji na hivyo kuchangia katika kupunguza umaskini. Upatikanaji wa maji safi na salama ni nyenzo ya kulinda utu na afya; kinyume chake kuenea kwa magonjwa na maisha duni.

Ifahamike kuwa kadiri ya Tathmini ya Hali ya watu na Afya ya mwaka 2010 (Demographic and Health Survey 2010); ni asilimia 4.8 tu ya kaya zilizopo vijijini ndiyo zinazopata maji katika eneo lao la kaya (water on premises) wakati ni asilimia 19.4 tu ya kaya kwa mijini ndizo zenye maji katika kaya zao. Hivyo kaya nyingi za Tanzania zinawekwa katika mazingira hatarishi kwa magonjwa ya mlipuko na mengine ambayo si ya mlipuko kutokana na uhaba wa maji, hali ikiwa tete zaidi katika maeneo yasiyopimwa yenye msongamano mkubwa wa watu katika Jiji la Dar es Salaam (slums).

Mheshimiwa Spika;
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, toleo la mwaka 2005 haijataja haki ya kupata maji safi na salama; huu ni kati ya upungufu ambao wananchi wa mijini na vijijini wanapaswa kuutolea maoni katika mchakato wa katiba mpya kwa kurejea mfano wa Katiba ya Afrika Kusini, Ghana na katiba mpya ya Kenya.

Katika hatua ya sasa haki hii inapaswa kulindwa kupitia Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni (“The International Covenant on Economic, Social and Cultural Rights”, ICESCR) wa 1966. Mkataba huu unataja haki za kijamii na hivi karibuni Umoja wa Mataifa (UN) umeutafsiri kuwa ni pamoja na haki ya kupata maji safi na salama ambayo inapaswa kutiliwa mkazo katika nchi yetu.

Suala la upatikanaji wa maji safi na kuweza kushughulia maji taka ni sehemu ya makubaliano ya kimataifa ambayo nchi yetu imeridhia kuingia mathalani Malengo ya Milenia (MDGs); lengo namba saba (7) shabaha 10; la kupunguza nusu ya watu waoishi bila maji na safi ya kunywa na usafi wa msingi. Hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka ni muhimu kama sehemu ya haki za binadamu lakini lina tija pia katika uzalishaji na uchumi wa nchi kwa kuwa tafiti zinaonyesha kwamba kudumu kwa matatizo hayo kunazigharimu nchi za Afrika, Tanzania ikiwemo wastani wa asilimia sita (6) ya pato la taifa (Gross Domestic Product).

Utafiti uliofanywa kwa Stockholm Environment Institute kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo Afrika mwaka 2006 kuhusu uhusiano kati ya maji na umaskini Afrika kwa kutumia mfano wa nchi yetu (Water and Poverty Linkages in Africa: Tanzania Case Study) umebainisha namna ilivyo vigumu kupima Tanzania inavyosonga mbele katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia yanayohusu maji. Aidha, utafiti huo umeeleza namna ambavyo bila kushughulikia kwa haraka matatizo ya maji jitihada za kupambana na umaskini zitakwama.

Mheshimiwa Spika; 
Jiji la Dar es Salaam ni letu sote, ni mahali ambapo wabunge wote tunaishi kwa nyakati mbalimbali hususan wakati wa vikao vya kamati za kudumu za Bunge hivyo adha ya maji katika Jiji hili kila mmoja anaifahamu na anawajibu wa kushiriki katika kuipatia ufumbuzi.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2002 Mkoa wa Dar es salaam ulikuwa na jumla ya wakazi 2,497,940 huku ukikadiriwa kuwa na kasi ya ongezeko la watu ya asilimia 6 kwa mwaka; ikiwa ni juu ya wastani wa kitaifa wa asilimia 4.5, lakini kasi ya upatikanaji wa maji na ushughulikiaji wa maji taka ikiwa ndogo. Bunge ikiwa ni chombo cha juu cha kuisimamia Serikali linapaswa kuitafakari hali hii kwa upekee wake kwa kuwa itakuwa na athari kwa taifa kwa sasa na baadaye ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.

Hadi kufikia mwaka 2011 Jiji la Dar es Salaam linakadiriwa kuwa na watu zaidi milioni nne na laki tano likiwa na takribani nusu ya waajiriwa wote wa viwandani nchini. Hivyo kwa kurejea takwimu za ujumla za sensa zilizotolewa mwezi Desemba 2012 kwamba Tanzania kwa sasa ina watu zaidi ya milioni 44.9; hoja hii inalenga kupendekeza kwa bunge kujadili kuhusu mustakabali wa zaidi ya asilimia 10 ya Watanzania, lakini kwa kurejea utangulizi wangu maazimio ninayopendekeza yapitishwe yatakuwa na maslahi sio kwa wakazi wa Dar es salaam bali kwa taifa kwa ujumla mijini na vijijini.

Mheshimiwa Spika;
Upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es salaam miaka michache baada mwaka 1961 ulikuwa zaidi ya asilimia 68; hivi sasa miaka 50 baada ya uhuru tumerudi nyuma na upatikanaji ni kwa wastani asilimia 55 tu tena kwa mgawo.

Zipo hisia kwamba Dar es salaam inapata huduma maji safi na maji taka kuliko miji na mijiji mengine nchini, lakini uhalisia unaonyesha kwamba hali ni bora kwa wachache wakati walio wengi hususan waoishi kwenye maeneo ya wananchi wa kipato chini hali ya upatikanaji wa maji ni duni kuliko miji na majiji mengine nchini.

Jiji la Dar es Salaam ni la mwisho kwa kigezo cha wastani wa kitaifa wa upatikanaji wa maji ukilinganisha na majiji mengine ambayo yanafikia asilimia 75; hivyo hatua za haraka zinahitajika kurekebisha hali hiyo.

Hatua hizo zitawezesha kupunguza kwa haraka tatizo hilo na kuelekeza nguvu zote katika maeneo ya vijijini palipo na shida kubwa badala ya mfumo wa sasa ambapo kwa miaka zaidi ya kumi, rasilimali zinatumika lakini kunakosekana ufumbuzi endelevu maeneo yote.

Hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa kuhusu hali hii kwa kuzingatia kuwa idadi ya watu katika Jiji la Dar es salaam inaendelea kukua kwa kasi likiwa ni jiji la tatu kwa ongezeko kubwa la watu barani Afrika na la tisa duniani; matatizo ya upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika jiji kutokana na msongamano wake wa watu ni bomu la wakati.

Mheshimiwa Spika;
Mkoa wa Dar es Salam unapata maji kutoka mito na visima kwa matumizi ya nyumbani, viwanda, bustani, mifugo, usafi na Mazingira. Sehemu ya Jiji inayopata maji inahudumiwa na Kampuni ya DAWASCO (Dar es salaam Water Supply and Sewerage Company) ambayo imepewa mkataba na Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Dar es Salaam, DAWASA (Dar es Salaam Water Supply and Sewerage Authority) na maeneo yasiyo na mtandao wa DAWASA hupata maji kutoka visima vinavyoendeshwa na vyombo vya watumia maji, Taasisi na watu binafsi.

Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa Jimbo la Ubungo kama sehemu ya Jiji la Dar es salaam katika kufuatilia masuala ya maji nilianza kwa kufanya Kongamano la Maji mwanzoni mwa mwaka 2011 ili kuwakutanisha wananchi, mamlaka husika na wadau wengine katika kuunganisha nguvu kupata ufumbuzi. Nikiri kwamba katika hatua za awali ushirikiano kutoka DAWASA, DAWASCO na Wizara ya Maji ulikuwa mdogo kwa kiwango cha kuamua kuwaunganisha wananchi kupitia ‘maandamano ya maji’ kwenda DAWASCO. Toka wakati huo ushirikiano umeongezeka kwa upande wa DAWASCO ambapo nimeshafanya nao ziara ya kikazi ya kata mbalimbali ya kutembelea maeneo yenye matatizo na hatua zimechukuliwa ambazo zimewezesha baadhi ya maeneo kuanza kutoka maji. Wakati wa hatua hizo tumewaonyesha DAWASCO biashara haramu ya maji iliyokuwa ikiendelea na baadhi ya maeneo wamechukua hatua ikiwemo kwa watendaji wao; hatua zaidi zinahitajika.

Mheshimiwa Spika;
Baada ya mwito wa mara kadhaa hapa bungeni; nashukuru pia Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe alifika Jimboni Oktoba 2012 kwa ajili ya uzinduzi wa visima katika maeneo ya King’ongo, Kilungule na Mavurunza na kuona hali halisi ya ugumu wa upatikanaji wa maji katika Mkoa wa Dar es salaam.

Natambua pia jitihada zinazofanywa na wadau wengine wa maendeleo Jimboni Ubungo katika masuala ya maji hususani Shirika la Kibelgiji (BTC) katika maeneo ya Kwembe na Kibamba. Hata hivyo, yapo bado maeneo mengi yenye matatizo makubwa ya maji ikiwemo ya Msumi, Makabe, Msakuzi, Malambamawili, Msingwa, Goba na mengineyo mengi katika Jiji la Dar es salaam. Na hata yale yenye miundombinu ya maji kama Sinza, Manzese, Makurumla na mengine nayo hali ni tete. Hali iko hivyo katika Manispaa zote tatu za Ilala, Kinondoni na Temeke.

Mheshimiwa Spika;
Hata katika maeneo ya umma ya kuuzia maji, bei ipo juu kwa kuwa mamlaka zetu za kuratibu na kusimamia masuala ya bei kama EWURA imekuwa na udhaifu katika kusimamia na kuratibu bei elekezi wanazozitoa. Kwa mfano jiji la Dar es Salaam: vituo vingi vya kutoa huduma za maji chini ya DAWASCO/DAWASA maarufu kama “vioski vya maji” vimekuwa vikiongeza bei tofauti na bei elekezi toka EWURA ya Tsh 1 kwa lita moja yaani ndoo ya lita 20 kwa Sh 20 kinyume na waraka nambari 10-017 (Order No.10.017) wa Juni 8, 2010, agizo lililopaswa kuanza kutekelezwa Juni 15, 2010.

Utafiti wa Shirika lisilo la kiserikali la Twaweza uliofanywa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam uliopewa jina; “Bei ya maji Dar es Salaam Je, wanaoendesha maghati ya maji wanazingatia bei walizopangiwa?” uliweza kubainisha kukithiri kwa bei zilizoongezwa kinyume na taratibu na agizo hilo la EWURA katika maghati ya maji. Hata baada ya kurekebishwa kwa agizo hilo na bei kuongezwa kiasi bado maeneo hayo ya kuuzia maji kwa umma yamekuwa yakipandisha bei kupindukia.

Mheshimiwa Spika;
Kero kubwa zaidi iko wa wauzaji binafsi ambapo mazingira ya upungufu na ukubwa wa mahitaji umefanya maji yauzwe kama bidhaa ya anasa bila mamlaka EWURA kutunga kanuni wala kudhibiti bei, na kuachia soko holela yenye kuambana na hujuma za miundombinu katika baadhi ya maeneo ili kuongeza uhaba.

Wananchi ambao wengi wao ni wa kipato cha chini hupata huduma ya maji kwa gharama kubwa ambayo huuzwa kwa kati ya Tsh 300 hadi Tsh 500 kwa ndoo ya lita 20 kwa maeneo ya Dar es salaam.

Kuwapo pia kwa watoa huduma wasio rasmi husababisha bei ya maji kuwa kubwa ambapo inakadiriwa kuwa 68% ya wakazi wanaoishi maeneo ya mjini yenye msongamano mkubwa hupata maji kutoka kwa wauzaji wasio rasmi.

Hatua za haraka zinahitajika kudhibiti ongezeko kubwa la bei ya maji kwa wananchi wa kipato cha chini wanaotegemea kupata maji kutoka sekta binafsi ambapo wanaonunua maji kwa madumu hununua bei ambayo ni takribani mara 15 ya bei ya mteja anayepata huduma ya maji ya bomba.

Mheshimiwa Spika;
Kwa nyakati mbalimbali katika kipindi cha kati ya mwaka 2000 mpaka 2012 Serikali imekuwa ikitoa ahadi bungeni ya kumaliza tatizo la majisafi na majitaka katika Jiji la Dar es Salaam bila utekelezaji sahihi, kamili na wa haraka.

Malengo ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini wa kwanza (MKUKUTA I) yaliyoingizwa pia katika ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2005-2010 hayakuweza kutekelezwa.

Malengo mengine yameingizwa katika ilani ya CCM na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini awamu ya pili (MKUKUTA II) ya kuboresha upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira ifikapo mwaka 2015; nayo tukiwa mwaka 2013 mwelekeo unaonyesha kwamba hayatafikiwa iwapo hatua za haraka zisipochukuliwa.

Mara baada ya kupitishwa kwa Mpango Maalum wa Maji katika Jiji la Dar es salaam mwaka 2011, Rais alitangaza kwamba tatizo la maji kuwa historia mwaka 2013; ambapo ni mwaka huu. Hata hivyo, utekelezaji wa mipango hauashirii ahadi hiyo kutekelezeka na kwa mwelekeo wa sasa tatizo litaendelea mpaka baada ya mwaka 2016 iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

Mheshimiwa Spika;
Mabomba ya ‘mchina’ bila maji na miradi hewa katika maeneo ya wananchi wa kipato cha chini Jijini Dar es Salaam:

Kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP).

Mradi huo uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji huku kukiwa na upungufu katika uzalishaji, upotevu wakati wa usafirishaji, udhaifu katika usambazaji na tuhuma za ufisadi katika matumizi.

Hali hii ni kati ya matatizo yanayokera wananchi wa Jiji la Dar es salaam kwa kuwa na mabomba yasiyotoa maji kwa muda mrefu hata kwa mgawo maarufu mitaani kama mabomba ya ‘mchina’.

Serikali ilieleze bunge lako sababu ya mabomba hayo kutokutoa maji mpaka hivi sasa, lini mabomba hayo yataanza kutoa maji katika maeneo ambayo maji hayatoki mpaka sasa na hatua gani zimechukuliwa wa waliotekeleza mradi huo bila kuzingatia maandalizi ya msingi.

Ni muhimu hatua zikachukuliwa kwa wahusika kwa kuwa kitendo cha mabomba hayo kukaa muda mrefu bila kutoa maji inafanya miundombinu hiyo kuanza kuharibika au kuharibiwa ambayo ni hasara kwa taifa kwa kuwa pamoja na fedha zilizotumika kuweka mabomba hayo kupotea, fedha nyingine zitatumika katika hatua ya baadaye kufanya matengenezo kwenye maeneo yaliyoharibika.

Aidha, yapo pia malalamiko ya kwamba yapo maeneo ambayo yalitoa maji mara chache kati ya mwaka 2009 na 2010 lakini baada ya hapo maeneo hayo hayajatoa maji tena mpaka sasa, Serikali itoe maelezo ya kitaalamu kwa bunge na kwa wananchi kuhusu sababu za maji hayo kutoka wakati huo na kutokutoka tena na hatua zinazochukuliwa kurekebisha hali hiyo.

Mheshimiwa Spika;
Kasoro katika mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP); hazielezwi na wananchi pekee bali pia hata watafiti mbalimbali.

Ripoti ya karibuni kabisa mwaka 2012 ya Shirika la Kimataifa la Water Aid ya utafiti uliofanywa ukihusisha wataalamu kutoka Overseas Development Institute na Chuo kimoja cha nchini Uingereza (SOAS) iliyofuatilia uwekezaji wa miradi ya maji mijini katika nchi za Ghana, Burkinafasso na Tanzania ( Stregthening pro poor targeting of investments by African utilities in urban water and Sanitation) ikiwemo namna miradi ilivyoshindwa kuwajali maskini na maeneo na kiwango cha hali ya maji kutokupatikana kinyume na malengo yaliyowekwa wakati wa kuanza kwa mradi.

Mheshimiwa Spika;
Matatizo ya kuwa na mabomba yasiyotoa maji hayapo tu katika mabomba waliyofungiwa wananchi majumbani bali pia kwenye visima na ‘vioski’/maghati ya jumuiya. Kuna udhaifu wa kuanzisha miradi ya jamii na kuacha kusimamia uendelevu (sustainability) wake na hatimaye baada ya muda mfupi miradi hiyo iliyotumia fedha za umma inabaki kuwa ‘miradi hewa’.

Utafiti wa vituo vya maji uliofanywa June 2009 na Overseas Development Institute (ODI) chini ya udhamini wa shirika la Water Aid hapa nchini ulibainisha ni asilimia 54 tu ya vituo vya maji vilivyopo ndivyo vinatumika kwa kutoa huduma ya maji.

Hivyo kwa wastani baada ya miaka miwili tu ya kujengwa karibu nusu ya visima na vioski huwa haviendelei tena kufanya kazi. Utaratibu wa kukimbilia kutumia fedha za miradi ya maji kwa mwaka wa kibajeti mpya bila kuzingatia taarifa za utekelezaji na ufuatiliaji wa miradi ya nyuma ni hatari kwa uendelevu wa kuwepo kwa huduma ya maji kwa siku zijazo kama hatua za haraka hazitachukuliwa kuzingatia matatizo yaliyojitokeza katika miradi iliyopita na kuzingatia ubora na ufanisi katika miradi ya maji nchini.

Mheshimiwa Spika;
Utafiti uliofanywa na Economic and Social Research Foundation, umebaini utofauti wa utekelezaji wa miradi ya serikali na mashirika binafsi katika kauhakiki ubora wa matumizi ya fedha na huduma kwa jamii. Utafiti ulibaini kuwa katika miradi iliyofadhiliwa na mashirika ya maendeleo, wastani wa asilimia 67 ya vioski vilionekana kufanya kazi; wakati miradi ambayo imefadhiliwa na Serikali ni wastani wa asilimia 45 ya vioski vya maji vilikuwa vikifanya kazi katika maeneo hayo hayo. Utafiti huo ulihusu Mikoa ya Singida na Dodoma.

Hali ni mbaya zaidi kwa upande wa Dar es Salaam ambapo kwa mujibu wa utafiti mwingine wa Shirika la Water Aid uliobainisha kuwa asilimia 85 ya vioski vilivyounganishwa Jijini Dar es Salaam havitoi maji, Asilimia 10 vinatoa maji kwa kusuasua na asilimia 5 tu ndivyo ambavyo vinatoa maji kwa uhakika.

Mheshimiwa Spika;
Kasoro katika utendaji na uwajibikaji wa mamlaka na vyombo vinavyohusika na utoaji na udhibiti wa huduma ya maji:

Majukumu ya utoaji wa huduma ya maji jijini Dar es salaam na baadhi ya maeneo ya Kibaha na Bagamoyo yanafanywa na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) ambayo ni mmiliki, mkodishaji na msimamizi wa utoaji wa huduma ya majisafi na maji taka na ina wajibu wa kupanga na kugharamia utekelezaji wa miradi ya miundombinu, kuiendeleza na kugharamia matengenezo ya dharura na makubwa.

Mwaka 2005 DAWASA iliingia mkataba wa miaka kumi (10) wa uendeshaji na Shirika la Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO). Chini ya mkataba huo majumu ya DAWASCO ni kuendesha mitambo, kusimamia usambazaji wa maji na uondoshaji wa maji taka, kuuza maji kwa wateja , kutoa ankara kwa wateja, kukusanya maduhuli, kulipia gharama za uendeshaji, kutekeleza matengenezo makubwa yanayogharamiwa na DAWASA na kutekeleza uunganishaji wa maji kwa wateja wapya kwa kutumia mfuko wa maji.

Kisheria na kimkataba DAWASA ina wajibu wa kuisimamia DAWASCO iliyoingia nayo mkataba; hata hivyo kwa kuwa yote ni taasisi na mashirika ya umma ambayo bodi zake na watendaji wake wakuu huteuliwa na mamlaka zile zile na kuripoti kwa watu wale wale, hali ambayo ina athari kwenye utendaji na uwajibikaji.

Wakati umefika sasa wa mkataba huo kati ya DAWASA na DAWASCO kuwekwa wazi kwa umma; kufanyiwa tathmini ya miaka zaidi ya mitano iliyopita ya utekelezaji; kufanyiwa marekebisho kwa ajili ya kipindi kilichobaki na maandalizi kuanza ya mfumo bora unaopaswa kuanza kuandaliwa baada ya kuisha kwa mkataba huo mwaka 2015.

Utoaji wa huduma ya maji unamhusu pia mdhibiti ambaye ni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA) yenye mamlaka ya kudhibiti utoaji wa huduma, kuidhinisha bei ya huduma ya maji safi na uondoaji wa maji taka pamoja na kutoa leseni za uendeshaji. Hata hivyo, EWURA imekuwa ikitoa kipaumbele zaidi kwenye kutumia mamlaka yake kudhibiti kwa karibu sekta ya nishati, huku udhibiti kwenye sekta muhimu ya maji hususan kwa upande wa watoa huduma binafsi ukiachwa uwe katika mfumo wa soko holela na kuchangia katika ongezeko la bei ya maji pamoja na ubovu wa huduma.

Wakati umefika sasa wa Bunge kusimamia kwa karibu utekelezwaji wa The Energy and Water Utilities Regulatory Authority Act (Sura ya 414) kifungu cha 6 ambayo inaelekeza bayana kwamba wajibu wa EWURA ni pamoja na kulinda maslahi ya walaji na kuhamasisha upatikanaji wa huduma inazozidhibiti ikiwemo maji wa watumiaji wakiwemo wa kipato cha chini na walio pembezoni au katika mazingira magumu (low income and disadvantaged consumers).

Aidha kwa mujibu wa kifungu cha 7 cha sheria hiyo majukumu ya EWURA ni pamoja na kupanga viwango cha ubora, viwango vya ugavi, kufuatilia utendaji ikiwemo uwekezaji na upatikanaji, kudhibiti bei na tozo na kushughulikia malalamiko na migogoro.

EWURA itumie mamlaka yake pia kwa kutumia vifungu vya 16, 17, 18 na 19 kuhakikisha kwamba masuala ya udhibiti wa bei hashaishii tu katika mamlaka za umma na pia ianze yenye uchunguzi juu ya kuporomoka kwa kiasi na kiwango cha huduma za maji katika Jiji la Dar es salaam na nchi kwa ujumla na kupendekeza hatua za ziada za haraka zaidi kuweza kuchukuliwa.

Mheshimiwa Spika;
Mwaka 2011 Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alifanya ukaguzi wa ufanisi (performance audit) kuhusu usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini ikiwemo Dar es salaam, hata hivyo taarifa yake ya Januari 2012 baada ya kutajwa bungeni miongoni mwa hati zilizowasilishwa; hatua za kutekeleza mapendekezo yake hazikupata usimamizi wa kutosha wa kibunge.

Hivyo, ipo haja kwa kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa niaba ya Bunge ipokee maelezo ya Serikali kuhusu utekelezaji wa mapendekezo yaliyomo kwenye ripoti hiyo ambayo yalilenga kuboresha utendaji wa DAWASA, DAWASCO na Mamlaka zingine za maji katika mikoa yote nchini na hatimaye kamati hiyo iwasilishe maoni na mapendekezo yake bungeni kwa ajili ya hatua zaidi.

Mfumo duni wa ushughulikiaji wa maji taka ni bomu la wakati katika Jiji la Dar es salaam:

Mheshimiwa Spika;
Hali ni mbaya zaidi kuhusu uondoaji wa maji taka ambapo ni chini ya asilimia 10 tu ya makazi ndiyo yaliyounganishwa katika mtandao wa maji taka na hivyo kuleta uchafuzi wa mazingira hususani katika maeneo yasiyopimwa. Hata katika maeneo yaliyopimwa Jijini Dar es salaam, mitandao ya maji taka haijakarabatiwa na kupanuliwa kwa wakati kwa kuzingatia ongezeko la watu suala ambalo lisipochuliwa kwa uzito unaostahili madhara yatatokea katika siku za usoni.

Kwa mujibu wa ripoti ya EWURA ya mwaka 2009, viwango vya huduma za uondoaji maji taka katika asilimia vimewekwa katika mabano Mwanza (3.1%), Moshi (5.8%) Arusha (7.0%), Dodoma (11.6%), Tabora (1.3%) na Tanga (9.3%).

Taarifa hiyo inaeleza kuwa kwa upande wa Dar es salaam huduma za mtandao wa maji taka ni kwa kiwango cha asilimia 4.8 katika Jiji lenye msongamano mkubwa wa watu ambapo hata katika kata zilizopimwa kama ya Sinza na nyinginezo hali ni tete.

Matokeo yake ni kuwawapo wakazi ambao hukiuka sheria na kusubiri mvua zinyeshe na kutiririsha maji taka hali ambayo ni hatari kwa afya za wananchi; kwa upande wa vijijini unafuu unapitakana katika ukubwa wa maeneo ya kuweza kuchimba vyoo, kinyume na mijini ambapo kadiri gharama za kukodi magari ya maji taka kwa sekta binafsi zisizodhibitiwa zinavyozidi kuongezeka ndivyo hatari zinavyozidi katika maeneo wanayoishi wananchi wa kipato cha chini.

Udhaifu wa kiutendaji katika miradi ya maji inayosimamiwa na Halmashauri, kamati na jumuiya za watumia maji:

Katika baadhi ya Halmashauri nchini ikiwemo za Jiji la Dar es salaam yamekuwepo matumizi mabaya na udhaifu wa kiutendaji katika miradi ya maji inayosimamiwa na Halmashauri kwa kushirikiana na kamati za maji au jumuiya za watumia maji.

Kushindwa kushughulikiwa kwa matatizo ya kimfumo kuhusu uendeshaji wa miradi ya maji, kutokutekelezwa kwa wakati kwa vipaumbele vya maji kwa mujibu wa bajeti za Halmashauri iliyopitishwa na madai ya ufisadi katika miradi inayosimamiwa na kamati za maji au jumuiya za watumiaji katika baadhi ya maeneo kumesababisha wananchi kukosa huduma ya maji.

Hata hivyo, pamoja na wananchi kuwasilisha malalamiko yao Wizara ya Maji na Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa- TAMISEMI) ili kutimiza wajibu wa usimamizi na ufuatiliaji hatua za haraka zimekuwa hazichukuliwi hali inayohitaji mjadala na usimamizi wa kibunge.

Katika mjadala utakaotokana na hoja hii, naamini wabunge wenzangu mchangia uzoefu wenu katika maeneo mnayotoka; naomba kwa upande wangu nitoe mfano wa Manispaa ya Kinondoni kuhusu mradi wa maji kata ya Goba.

Tatizo la maji katika kata ya Goba limedumu sasa kwa kipindi cha miaka zaidi ya mitano, pamoja na kwamba serikali inaowajibu kulinda maslahi ya walaji na kuhamasisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa watumiaji wakiwemo wa kipato cha chini na walio pembezoni au katika mazingira magumu mamlaka zinazohusika hazijaweza kutimiza wajibu ipasavyo kuhusu kata ya Goba.

Jitihada nyingi zimefanywa zilizofanywa na wakazi wenyewe kama njia mbadala ya kupata huduma hiyo muhimu kwa maisha ya Binadamu lakini zimekuwa zikikwamishwa na baadhi ya watendaji wa Halmashauri kwa kushindwa kusimamia kwa kurejesha na kupanua huduma hiyo muhimu kwa wananchi hata baada ya kupokea malalamiko katika nyakati mbalimbali .

Mnaweza mkajiuliza sababu za suala hili kuvuka mipaka ya Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Kinondoni, mpaka Bungeni; ni muhimu ifahamike mapema kwamba jitihada katika ngazi hizo kwa miaka mingi hazijaweza kuleta ufumbuzi hali inayohitaji chombo cha juu zaidi kwa niaba ya wananchi; yaani Bunge kujadili kwa kuwa Wizara ya Maji nayo imeshindwa kuchukua hatua zinazostahili kwa wakati.

Historia ya tatizo hili inaonesha kuwa wakazi wa Goba wameshawahi kuandika barua kwa Waziri wa Maji barua ya tarehe 15/10/2009 ikieleza kero ya maji kwa wananchi na wakimtaka alipatie ufumbuzi tatizo hilo na nakala ya barua hiyo ilipelekwa kwa mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, na mkuu wa wilaya ya Kinondoni pamoja na hayo bado tatizo linaendelea kutopatiwa ufumbuzi huku wakazi wa Goba wakiendelea kukosa haki yao ya msingi kwa kuwa hakuna maisha bila maji.

Kushindwa kulipatia ufumbuzi tatizo hilo kulipelekea wananchi pia kuandika barua ya wazi kwa waziri mkuu mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda wakilalamikia mradi wa maji wa muda mrefu, pamoja na barua hiyo hakuna jitihada kamili zilizofanyika za makusudi kuondoa tatizo hilo.

Utendaji mbovu na usimamizi mbovu wa miradi ya maji kwa manispaa ya Kinondoni chini ya kamati za maji zilizosababisha maji kukatwa kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2007 na 2011 ndiyo chanzo cha ukosefu wa maji kwa kipindi chote hicho.

Katika kipindi cha karibuni, kamati ya maji Goba baada ya kukatwa kwa maji ilimwandikia barua mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni tarehe 30/08/2011 yenye kumbukumbu namba G/WP/GOBA/VOL013/11 ikimuarifu Mkurugenzi kuhusu kusitishwa kwa huduma ya Maji kwa Wananchi wa Kata ya Goba.

Katika barua hiyo ambayo mbunge nilipatiwa nakala yake, wananchi hao walimlalamikia mkurugenzi kwa kutozifanya kazi barua zao wakionesha mfano barua ya tarehe 22/05/2011 na kumuomba Mkurugenzi kuchukua hatua za haraka ili huduma ya maji irejeshwe hata hivyo Manispaa ilizembea kuchukua hatua zinazostahili.

Mnamo tarehe 21/03/2011, nilimwandikia barua Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni yenye namba : KUMB:OMU/MJ/005/2011 yenye kichwa cha barua “Hatua za Haraka zinahitajika kuhusu mradi wa Maji Goba” .

Kutokana na hatua stahili kutochukuliwa niliandika barua nyingine kwa Mkurugenzi yenye kumb. OMU/MJ/008/2011 na kupendekeza hatua za haraka kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha fedha kutoka mfuko wa Jimbo Tsh 3,000,000.00 zinapelekwa haraka katika Akaunti ya maji Goba ikiwa ni sehemu ya kuchangia katika wajibu wa manispaa za kujenga uwezo wa mradi husika na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni alifanya ziara Goba tarehe 31/01/2012 katika ziara ile mkurugenzi aliwaahidi wakazi wa Goba kurejesha huduma ya Maji ndani ya wiki moja lakini hadi sasa ni zaidi ya mwaka wananchi bado hawajapata huduma hiyo.

Tarehe 18/03/2012 niliwaandikia barua tena DAWASA yenye kumbukumbu namba OMU/MJ/006/2012 kuhusu hatua ambazo DAWASA imechukuakuhusu matatizo ya maji katika kata ya Goba, katika barua hiyo nilitaka kujua hatua ambazo DAWASA imechukua kushughulikia matatizo ya maji Goba hususani juu ya kufanya majadiliano na Manispaa ya Kinondoni ili kuwa na mfumo endelevu zaidi wa utoaji wa huduma ya maji katika kata ya Goba ambayo ina ongezeko kubwa la wakazi, makazi na mahitaji mengine mengi kwa sasa.

Wizara ya Maji na mamlaka zingine za kiserikali zinapaswa kuharakisha uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya wote waliohusika kusababisha uvunjwaji wa haki za watumiaji wa huduma ya maji, udhaifu wa usimamizi wa miradi ya maji na ukosefu wa huduma ya maji katika kata ya Goba kwenye Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es salaam ili kutoa fundisho kwa maeneo mengine.

Kwa kufanya hivyo, Serikali ifuatilie mpaka Manispaa ya Kinondoni, DAWASA na DAWASCO wawezeshe huduma ya maji kurejea kwa wananchi, kupanua kwa dharura wigo wa upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Kata ya Goba pamoja na kuboresha mfumo mzima wa upangaji, utekelezaji na usimamizi wa miradi ya maji katika Manispaa ya Kinondoni, DAWASA na DAWASCO.

Aidha ili kupata ufumbuzi wa kudumu Wizara ichukue hatua za ziada ili kata ya Goba itoke katika kupatiwa huduma ya maji chini ya Manispaa ya Kinondoni na badala yake ihudumiwe na DAWASA pamoja na DAWASCO ili kuwezesha uboreshaji mpana wa miundombinu.

Mheshimiwa Spika;
Upungufu katika usimamizi wa Sheria za maji na haja ya kuharakisha utungaji wa kanuni na marekebisho ya sheria husika:

Hatua kuhusu uboreshaji wa huduma ya maji safi na uondoaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam zinasimamiwa na sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge hili.

Baadhi ya Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji ya mwaka 2009, Sheria ya maji safi na usafi wa mazingira ya mwaka 2009, sheria ya mamlaka ya udhibiti wa nishati na maji ya mwaka 2001 na sheria ya mamlaka ya maji safi na maji taka Dar es salaam ya mwaka 2001. Hata hivyo kumekuwa na upungufu wa kusimamia utekelezaji wa sheria hizo ikiwemo katika kutunga kanuni na kuchukua hatua kwa wakati.

Serikali inapaswa kutoa maelezo bungeni ni kwanini mpaka mwezi Julai mwaka 2012 ilikuwa haijakamilisha kutunga kanuni zinazohusu uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Uwekezaji wa Maji (National Water Investment Fund) toka Sheria husika itungwe mwaka 2009. Bunge lijadili hoja hii ili pamoja na mambo mengine liisimamie Serikali mfuko huu uweze kufanya kazi kwa manufaa ya wananchi wote wenye kuhitaji uwekezaji toka mfuko huu kuondoa matatizo ya maji nchini ikiwemo Dar es salaam.

Mheshimiwa Spika;
Aidha, katika utekelezaji wa sheria umeonekana pia upungufu mwingine wa ziada unaohitaji marekebisho ya sheria mbalimbali. Mfano, ukiondoa maeneo ya mijini ambapo huduma za maji zinasimamiwa na mamlaka za maji safi na maji taka kwa upande wa Dar es salaam ikiwa ni DAWASA; maeneo ya vijijini kote nchini yanayohudumiwa na Halmashauri ikiwemo maeneo ya pembezoni ya Dar es salaam yanayohudumiwa na Manispaa, mifumo ya usimamizi ina udhaifu kutokana na upungufu wa kisheria.

Kutokana na hali hiyo kwa nyakati mbalimbali limetolewa pendekezo na wabunge kwamba paundwe Wakala wa Maji (TANWATER) kama ilivyo Wakala wa Barabara (TANROADS) hata hivyo Serikali mpaka sasa haijatekeleza pendekezo hilo ambalo utekelezaji wake utahusisha pia marekebisho ya sheria mbalimbali.

Mheshimiwa Spika;
Sheria ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam ya mwaka 2001 nayo inahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa. Kati ya mambo yanayohitajika kufanyika ni pamoja na kurekebisha ramani ya awali iliyopitishwa ikiwa ni sehemu ya sheria husika kuhusu eneo ambalo kwa mujibu wa sheria linapaswa kuhudumiwa na DAWASA (designed area) ili kuendana na ukuaji wa jiji pamoja na maeneo jirani ya Kibaha na Bagamoyo.

Aidha, marekebisho mengine yanahitajika katika utaratibu mzima wa DAWASA kutoa mikataba kwa makampuni mengine kuendesha huduma ya maji kwa niaba yake ili kuepusha kasoro zilizojitokeza wakati wa mkataba wa City Water na kasoro nyingine zinazoendelea hivi sasa katika mkataba baina ya DAWASA na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO).

Marekebisho yanayohitajika kufanyika ni pamoja na ya kubadili muundo wa Bodi ya DAWASCO ikiwemo kuwezesha uwakilishi wa Halmashauri za Manispaa za Dar es salaam katika bodi ya DAWASA.

Kwa upekee wa muundo wa Mkoa wa Dar es salaam, Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam inafanya kazi ya uratibu tu wakati ambapo sehemu kubwa ya taratibu za ardhi, mipango miji na ujenzi ziko katika Halmashauri. Halmashauri za Manispaa ndizo ambazo zinahusika kwa kiwango kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maji ukiondoa ya DAWASA katika kata na mitaa mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam.

Hata hivyo, wakati halmashauri ya Jiji la Dar es salaam inawakilishwa kati bodi ya DAWASA, Manispaa zote tatu hazina uwakilishi hali ambayo inapunguza kiungo cha mawasiliano na kuathiri nguvu za Halmashauri katika kufuatilia miradi ya maji inayotekelezwa katika maeneo yao na wakati mwingine kuchelewesha miradi husika.

Marekebisho ya sheria ya DAWASA yanapaswa kuhusisha pia kurekebisha adhabu zinazotokana na makosa ya uharibifu wa miundombinu ya maji, wizi wa maji safi na uunganishaji kinyemela wa mabomba ya maji taka; kwa kuwa adhabu zilizopo kiwango chake kimepitwa na wakati na hakilingani na kukithiri kwa makosa ya biashara haramu ya maji na hujuma katika miundombinu ya maji katika jiji la Dar es salaam.

Kasoro katika upangaji na utekelezaji wa Mpango Maalum wa kutatua tatizo la Maji katika Jiji la Dar es salaam:
Ikumbukwe kuwa katika kutafuta ufumbuzi Mwezi Machi 2011 Baraza la Mawaziri lilipitisha Mpango Maalum wa Maji Dar es salaam na Pwani wenye mgawanyo wa fedha ufuatao:

Mahitaji ya fedha Mpango Maalum 

              Mahitaji ya fedha Mpango Maalum
Na.
Kazi zitakazotekelezwa
Gharama
2010-2013
(SH.BILIONI)
Makadirio kila mwaka wa fedha  (sh. bilioni)
2010/11
2011/12
2012/13
2013/14
1
Upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu
17.25
0.45
6.00
6.00
4.80
2
Upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini
122.50
9.38
24.28
56.98
31.88
3
Kazi ya visima vya Kimbiji na Mpera
133.15
10.35
70.90
29.25
22.65
4
Ujenzi wa bwawa la Kidunda
174.75
3.00
7.80
83.70
80.25
5
Upanuzi wa mtandao wa mabomba ya maji safi
82.40
-
24.05
37.15
21.20
6
Uchimbaji na ukarabati wa visima katika maeneo yasiyo na maji.
4.00
1.50
2.50
-
-
7
Kuimarisha utoaji wa huduma ya maji
18.00
-
5.00
6.00
7.00
8
Kuboresha uondoaji wa majitaka (upanuzi wa mtandao na ujenzi wa mitambo mitatu ya maji taka)
100.60
-
-
50.30
50.30
9
Miradi mingine
0.20
0.20
-
-
-
10
Elimu kwa umma
1.00
0.50
0.20
0.20
0.10

Jumla Kuu
653.85
25.38
140.73
269.58
218.18


Katika kutekeleza mpango huu maalum, natambua kwamba upanuzi wa mfumo wa maji wa Ruvu Juu ikiwemo ujenzi wa wa Tanki la Kibamba na Bomba mpaka Kimara utafanyika na fedha za ujenzi huo kiasi cha dola milioni 132 zimepatikana ikiwa sehemu ya mkopo wa dola milioni 178 kutoka Serikali ya India. Nafahamu pia kwamba ujenzi wa kupanua intake na machujio mapya ya maji unaendelea kwa udhamini wa Shirika la Milenia (MCC) wa kiasi cha dola za kimarekani milioni 36.8. Naelewa pia kuwa ujenzi wa bomba kutoka Ruvu Chini hadi Dar es Salaam utakaogharimu shilingi bilioni 122.5 za walipa kodi wa Tanzania umeanza.

Hata hivyo, kiwango cha uwekezaji huo hakijaweza kufikisha malengo yaliyopitishwa na Baraza la Mawaziri na Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano uliopitishwa na Bunge hili; kwa kuwa jumla mpaka mwaka wa fedha 2012/2013, zilipaswa kuwa zimetumika au walau zimetengwa kiasi cha shilingi bilioni 435.67 ikiwa ni hatua ya haraka ya kuboresha upatikanaji wa maji safi na uondoaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam na mikoa mingine inayoguswa na miradi hiyo ikiwemo ya Morogoro na Pwani.

Mheshimiwa Spika;
Hivyo, pengo hilo linapaswa kuzibwa kwa haraka kupitia nyongeza ya fedha katika Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya mwaka 2013/2014 kwa kuchukua hatua za haraka. Serikali ieleze bungeni imefikia wapi katika kupata fedha za kulipa fidia ya maeneo ya hifadhi ya maji ya Kimbiji na Mpera kiasi cha shilingi bilioni 27 ambayo ilipaswa kuwa imelipwa tangu mwaka 2011 na lini hasa ujenzi utaanza.

Serikali ieleze iwapo ujenzi wa Bwawa la Kidunda Mkoani Morogoro unaokadiriwa kugharimu shilingi bilioni 175 utaingizwa katika vipaumbele vya taifa kwa mwaka 2013/2014 kwa kuzingatia umuhimu wa bwawa hilo katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ambayo yenye kufanya upatikanaji wa maji kutokuwa na uhakika katika mto Ruvu kipindi chote cha mwaka na kusababisha uhaba wa maji kwa wananchi wa Pwani na Dar es Salaam.

Hatua hizi zote zitakuwa na tija kwa wananchi wengi zaidi iwapo zitaambatana na ujenzi wa mfumo wa usambazaji wa maji katika maeneo ambayo hayakufikiwa katika awamu iliyopita; maeneo ambayo wananchi huyaita ‘yaliyorukwa katika uwekezaji wa mabomba ya mchina’ na ukarabati wa mifumo chakavu ya usambazaji wa maji. Serikali inapaswa kueleza ni lini maeneo hayo yatawekewa mtandao wa mabomba ambayo yanakisiwa kuhitaji jumla ya shilingi bilioni 82.4.

Mheshimiwa Spika;
Kwa upande mwingine, ili kuondokana na ‘bomu la wakati’ serikali ione umuhimu wa kutafuta fedha kwa haraka kiasi cha shilingi bilioni 100.6 kwa ajili ya kuboresha huduma za maji taka kama ilivyoahidi kwa nyakati mbalimbali.

Fedha hizi zinaonekana ni nyingi lakini ni matokeo ya udhaifu wa miaka mingi katika mipango miji katika Jiji la Dar es salaam hali inayosababisha gharama za usambazaji wa huduma ya maji safi na uondoaji wa maji taka kuwa kubwa. Upo umuhimu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutambua kwamba ongezeko la zaidi ya asilimia 70 ya maeneo ya makazi ambayo hayajapimwa katika Jiji la Dar es Salaam ikilinganishwa na wastani wa asilimia 30 wa miji mingine mikuu ya mikoa ni hali yenye kuathiri kwa kiwango kikubwa uchumi wa nchi na maisha kwa wananchi kwa ujumla.

Ujenzi wa miundombinu hiyo mipya na ukarabati wa ile chakavu ya usafirishaji hautakuwa na maslahi tu kwa wananchi kwa kuwawezesha kupata huduma bali pia utakuwa na tija kwa nchi kwa kupunguza upotevu wa maji mpaka asilimia 25 na hivyo kudhibiti hasara ambayo inalikumba taifa hivi sasa kutokana na kiwango cha maji kinachopotea kwa Jiji la Dar es Salaam pekee.

Bajeti ndogo ya sekta ya maji na utegemezi wa fedha kutoka nje:

Mheshimiwa Spika;
Fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwenye sekta ya maji ni kidogo na hata hizo zinazotengwa utegemezi wa wahisani kutoka nje ni mkubwa kwa kiwango cha kuathiri miradi katika Jiji la Dar es salaam na nchi kwa ujumla.

Kujibu wa ripoti ya Hali ya Umaskini na Maendeleo ya Watu mwaka 20112 (PHDR) Fedha za ndani za kutekeleza bajeti ya Sekta ya Maji imekuwa ikishuka mwaka hadi mwaka toka 57% katika mwaka wa fedha 2005/06 hadi 10% kwa mwaka wa fedha 2011/12.

Hali hii imesabababisha kukithiri kwa utegemezi katika vyanzo vya mapato toka nje na kwa wabia wa maendeleo kuwezesha miradi ya maji; fedha ambazo hazipatikani kwa wakati na kwa kiwango kinachokidhi mahitaji.

Kwa mwaka 2011/12 tumeshuhudia kutokutimizwa kwa azimio la serikali la kutenga kiasi cha Dola za Kimarekani 128 milioni kutekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Maji (WSDP) huku bajeti pangwa ikiwa ni dola za kimarekani 28 milioni tu kwa mwaka huo 2011/12.

Tufahamu kwamba kupungua huku kwa kiwango cha bajeti katika sekta ya maji kunapingana hata na azimio la Sharm el Sheikh la nchi za Umoja wa Afrika la mwaka 2008 la kutaka dhamira na azma ya kuongeza kipaumbele cha kisiasa katika utengwaji na kuwekwa wazi kwa bajeti kwa ajili ya sekta ya maji safi na maji taka.

Mheshimiwa Spika;
Utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2012/2013 umeendelea kuonesha upungufu katika utoaji wa fedha za miradi ya maendeleo katika sekta ya maji, taarifa zinaonyesha kwamba katika kipindi cha miezi sita ya kwanza Jumla ya Shilingi Bilioni 29 tu ndizo zilitolewa ikiwa ni sawa na asilimia 36 katika fedha za ndani. Hali hii ni kidogo ikizingatiwa kiwango kilichoidhinishwa na tume ya mipango kikiwa ni shilingi 48,326,792,184 kwa kipindi cha robo ya kwanza pekee.

Mheshimiwa Spika,
Mapungufu yanayojitokeza katika utekelezaji wa mipango ya serikali hususani katika ugawaji wa rasilimali fedha ambazo zimeidhinishwa na bunge katika huduma muhimu za jamii kama maji, matokeo yake ni kuwa na huduma mbovu, hivyo napendekeza bunge lijadili hali hiyo na kupitisha hatua za haraka ambazo zitanufaisha nchi kwa ujumla ikiwemo Jiji la Dar es Salaam.

Hatua hizo zitawezesha fedha za miradi ya maendeleo ya maji kutolewa kwa wakati katika miezi iliyobaki ya mwaka wa fedha 2012/2013 na kupewa kipaumbele katika Mpango wa Mwaka wa Maendeleo na Bajeti kwa mwaka 2013/2014.

Mheshimiwa Spika;

Udhaifu katika utekelezaji wa Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini:


Tangu mwaka 2000 Bunge hili limekuwa likipewa ahadi za utekelezaji wa Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RWSSP). Wakati maelezo ya kuanza kwa mpango huo yalipoletwa bungeni mwaka 2003, wakati huo ukiitwa mpango wa vijiji kumi (quick wins), yapo maeneo katika Jiji la Dar es salaam ambayo yalikuwa na vijiji na yaliingizwa katika mpango huo. Hata hivyo, mpaka leo miaka takribani kumi baadaye mwaka 2013 maeneo hayo yakiwa yameshapanda hadhi na kuwa mitaa miradi hiyo haijatekelezwa kwa ukamilifu wake.

Maeneo hayo yamekosa maji kwa pande zote, hayajahudumiwa na DAWASA na DAWASCO kwa kuwa yapo kwenye vijiji kumi; na mradi huo wa vijiji kumi haujaweza kuwafanya wananchi hao wapate huduma ya maji.

Hali hii haihusu Halmashauri za Manispaa za Jiji la Dar es Salaam za Ilala, Kinondoni na Temeke; inahusu halmashauri zote nchini ambazo mpango huo ulipaswa kutekelezwa. Naamini kujadiliwa kwa hoja hii kutawezesha wabunge wenzangu kueleza pia uzoefu katika maeneo yenu ya vijijini na mijini hatimaye kutokana na mapendekezo ya hoja hii; Bunge likapitisha maazimio ambayo yataweza kuchangia katika kurekebisha hali hii.

Mheshimiwa Spika;
Programu hii ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ilipaswa kutekelezwa kwa awamu nne, ambapo utekelezaji wa awamu ya kwanza baada ya kucheleweshwa toka mwaka 2003 ulipaswa kuanza mwaka 2005/2006 na kukamilika mwaka 2010/2011. Kwa maneno rahisi ni kwamba hadi kufikia hivi sasa ilipaswa tayari maji yawe yameshapatikana katika vijiji kumi vya kila halmashauri nchini, hata hivyo ukomo wa muda wa awali ukiwa umeshapita kwa zaidi ya mwaka mmoja; utekelezaji katika maeneo mbalimbali nchini haukufanyika hata robo.

Hali iko hivyo, wakati ambapo fedha zimetumika bila maji kupatikana; katika hatua hiyo ya kwanza jumla ya shilingi bilioni 96.4 zimetumika kwenye “quick wins” hadi kufikia mwanzoni mwa mwaka 2012 huku maji kwa sehemu kubwa kukiwa hakuna; hali ambayo ni matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

Mheshimiwa Spika;
Katika ufuatiliaji wangu kuhusu masuala ya maji katika Manispaa za Jiji la Dar es salaam, katika halmashauri zingine na katika Wizara ya Maji nimebaini kwamba hali hiyo ilisababishwa na mikataba mibovu yenye dalili za ufisadi, kukosekana kwa uwajibikaji miongoni mwa makampuni yaliyopewa zabuni katika mazingira ya utata na udhaifu katika mchakato mzima wa zabuni na usimamizi wa miradi.

Matokeo yake watafiti na wachimbaji binafsi wengi wao wakiwa hawana uwezo wa vifaa na wataalamu walipewa kazi na kulipwa fedha bila hata ya mchakato kukamilika; badala ya kuwekwa mfumo wa watafiti kuhusika pia na uchimbaji na kulipwa kwa kadiri na matokeo na hatua iliyofikiwa. Anafanya utafiti mwingine, anachukua fedha zake anakwenda; anayekwenda kufanya uchunguzi ni mwingine naye anachukua fedha zake anakwenda; anayejenga miundombinu ni mwingine, naye anaelekezwa eneo na baadaye kueleza kwamba hakuna maji huku hasara ikiwa imeshapatikana.

Ripoti ya Tathmini (Appraisal Report) ya Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Rural Water Supply and Sanitation Program) ya mwaka 2010 inaonyesha namna ambavyo awamu ya kwanza katika ya mwaka 2007 mpaka 2010 ilivyoshindwa kutekelezwa kwa ufanisi. Usimamizi wa kutosha wa kibunge unahitajika kuhakikisha awamu ya pili (RSSWP Phase II), ambayo awali ilipangwa ifanyike kuanzia mwaka 2011 mpaka 2014 inafanyika kwa kuanzia na kufanya ukaguzi wa awamu iliyopita.

Bunge lako lijadili hali hii na kupitisha maazimio yenye kuwezesha ukaguzi maalum ufanyike kwenye matumizi ya bilioni 96.4 za mradi wa maji safi na mazingira vijijini katika Jiji la Dar es salaam na Halmashauri zote nchini ili kasoro hizo zisijirudie katika awamu ya pili ya programu hiyo inayotarajiwa kuanza mwezi Juni mwaka 2014.

Mheshimiwa Spika;
Baada ya maelezo hayo sasa naomba kuwasilisha hoja kwa mujibu wa kanuni ya 54 fasili ya (1) (2) na (3) ya kupendekeza bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam.

MABADILIKO KATIKA HOJA KUHUSU HATUA ZA HARAKA ZA KUBORESHA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA USHUGHULIKIAJI WA MAJI TAKA KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM

(Kwa mujibu wa Kanuni 55 (10) ya Kanuni za Kudumu za Bunge)

Kwa kuondoa maneno kuanzia “KWA KUWA, kati ya mwaka 2003….. (yaliyo kuanzia katika ukurasa wa 42 na kuendelea mpaka ukurasa wa 45 yanapoishia maneno maneno)…….. mapendekezo ya mpango wa taifa”

Na kuingiza maneno:

KWA KUWA, Programu ya Maji Safi na Mazingira Vijijini ikiwemo katika Manispaa za Jiji la Dar es Salaam ilipaswa kutekelezwa kuanzia mwaka 2005/2006 na kukamilika mwaka 2010/2011 kwa kugharimu dola za kimarekani milioni 292 hata hivyo tathmini ya miaka miwili na nusu ya utekelezaji (mid term review) imebanisha kasoro nyingi katika utekelezaji.

KWA KUWA, Kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 Serikali ilitekeleza Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya wachina hautoi maji huku kukiwa na upungufu katika uzalishaji, upotevu wakati wa usafirishaji, udhaifu katika usambazaji na tuhuma za ufisadi katika matumizi.

NA KWA KUWA, Wizara ya Maji iliandaa waraka maalum wa kuiomba Serikali kutenga kiasi cha shilingi bilioni 653.85 Mpango Maalum 2011-2013 wa kuboresha huduma za majisafi na uondaji wa majitaka katika Jiji la Dar es salaam na kupitishwa na Baraza la Mawaziri mwezi Machi 2011 lakini utekelezaji wake unaelekea kucheleweshwa mpaka mwaka 2016.

NA KWA KUWA, katika mwaka wa fedha 2011/2012 na 2012/13 Serikali haikutenga kiwango kamili cha fedha kwa kuzingatia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ulioidhinishwa na Bunge na kwa kuzingatia mgawanyo wa Mpango Maalum wa Maji Safi na Maji Taka katika Jiji la Dar Es Salaam na kauli ya Serikali ya tarehe 7 Novemba 2012.

NA KWA KUWA, kwa mujibu wa ibara ya 62 (2) na (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 , Bunge ndicho chombo kikuu chenye madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu.

NA KWA KUWA, kwa mujibu wa ibara ya 63(3) katika utekelezaji wa madaraka yake bunge laweza kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutunga sheria pale utekelezaji unapohitaji kuwapo sheria.

NA KWA KUWA, Malengo ya Kitaifa yalikuwa ni kuwapatia wakazi wa Mjini maji kwa asilimia 90 ifikapo mwaka 2010 na kwamba malengo hayo kwa Jiji la Dar es Salaam yamesogezwa mbele na kuwekwa malengo mapya ya upatikanaji wa huduma ya maji safi kufikia asilimia 90 na uondoaji wa maji taka kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2015.

KWA HIYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali ichukue hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam:

NA KWAMBA, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi maalum wa matumuzi ya fedha matumizi ya bilioni 96.4 za mradi wa maji safi na mazingira vijijini katika Jiji la Dar es salaam na Halmashauri zingine na kuwezesha hatua za ziada kuchukuliwa.

NA KWAMBA, Kufuatia kauli iliyotolewa bungeni tarehe 7 Novemba 2012 kuhusu Mpango Maalum wa kutatua tatizo la maji katika Jiji la Dar es salaam uliopitishwa mwezi Machi 2011 Serikali izingatie makisio ya awali ya gharama za mpango huo na kuingiza mahitaji yaliyobaki kwenye Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Mwaka 2013/2014 na Bajeti ya mwaka 2013/2014.

NA KWAMBA, Mpango wa dharura wa kupunguza kero ya maji ulionza kutekelezwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na DAWASA kuanzia Juni 2010 unaohusisha uchimbaji wa visima 29 uliopaswa kukamilika Oktoba 2011 uwekewe muda wa ukomo wa kukamilika kwa dharura katika maeneo ambayo miradi haijakamilika mpaka hivi sasa ikiwemo iliyozinduliwa Oktoba 2012 yenye kuhitaji miundombinu ya ziada kufikia wananchi zaidi.

NA KWAMBA, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa thamani ukilinganisha na ufanisi (Value for Money) wa Mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) kwa kurejea ukaguzi wa kiufundi (technical Audit) uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys.

NA KWAMBA, EWURA ifanye ukaguzi wa kiufanisi (performance audit) wa miradi ya visima vya maji takribani 200 ambavyo vilichimbwa na serikali na kukabidhiwa kwa DAWASCO, jumuiya za wananchi na taasisi mbalimbali lakini haitoi huduma inavyostahili kwa kadiri ya malengo ya awali.

NA KWAMBA, EWURA iharakishe kukamilisha mchakato ulioanza wa kutunga kanuni za udhibiti wa ubora na bei ya huduma ya maji kwa upande wa sekta binafsi katika Jiji la Dar es salaam.

NA KWAMBA, Kamati husika ya Bunge ijadili taarifa ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu usimamizi wa usambazaji wa maji katika maeneo ya mijini (performance audit report on the management of water distribution in urban areas) ya Januari 2012 ili maoni na mapendekezo yazingatiwe wakati wa kujadili na kushauri kuhusu mapendekezo ya mpango wa taifa na bajeti ya nchi.

NA KWAMBA, Serikali iwasilishe bungeni haraka iwezekanavyo muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali za majisafi na majitaka (Water Supply and Sanitation Miscellaneous Amendment Bill) ili kushughulikia upungufu uliojitokeza katika utekelezaji wa sheria zilizopo na kuweka mfumo thabiti wa usimamizi wa sekta ya maji nchini.”

Naomba kuwasilisha.

………………… 

John John Mnyika(Mb) 

Jimbo la Uchaguzi-Ubungo

12 comments:

Mtalii said...

Hoja ni ya msingi sana.Kila la heli katika kupigania afya ya wakazi wa jiji ambalo wabunge,mawaziri na Rais mwenyewe wanaishi na wanapambana na kero ya maji.Kama ikishindwa kukipita wala usishangae mwakani wataitumia kutatua kero ya maji jiji,Tatizo wataona aibu kwa kuwa imewasilishwa na mbunge kambi ya upinzani.Nina hakika umewapa dira ya kesho hata wasipokubali leo.Kila la heli mungu atakuongoza na mengine mengi

facebook.com/peterhelpeterluena said...

Hoja ni nzuri na ninaimani wabunge wote wataungana ili kufanikisha hoja hii kufanyiwa kazi.

Mungu Mwenyezi liwezeshe Bunge letu Tukufu, kujadili na hatimaye kupitisha hoja hii.

Mungu Ibariki Tanzania.

fratern lassoya said...

kaka nakubaliana na kila unachokifanya bungeni, heshima kwako ila nina mashaka sana uendeshaji wa bunge ya kuwa kila hoja inayotolewa na wapinzani ina kasoro?

Anonymous said...

Cha msingi msiwe wasaliti SERA nzuri mitazamo mizuri ila HARAKATI ziwe za kweli ndo hasa watanzania tunachohitaji sio kisa mnatekeleza wajibu kama wapinzani tu kuwa mnakosoa na kuirekebisha serikali iliyo madarakani MUWE NA HARAKATI ZA KWELI

Anonymous said...

Hi, mimi nina James ubongo, nilikuwa kukwama
katika hali ya uchumi na
Mimi zinahitajika refinance na kulipa madeni yangu.
Nilijaribu kutafuta mikopo kutoka mkopo tofauti
makampuni binafsi na ushirika, lakini
kamwe mafanikio, na wengi benki
kupunguzwa mikopo yangu. Mimi ilianzishwa kwa mtu
Mungu binafsi mkopo Taasisi aliyetoa
mimi mkopo nilikuwa kutafuta bila matatizo na ucheleweshaji. ikiwa ni lazima
wasiliana makampuni yote kwa kuzingatia
mkopo unsecured, bila
mikopo hundi, katika busara kiwango na ulipaji shecdule kuwasiliana Mheshimiwa Aiden William. yeye
hawajui kuwa mimi nina kufanya hili, lakini
ni furaha sasa, na niliamua hebu
watu kujua zaidi juu yake. unaweza
kuwasiliana naye kupitia barua pepe yake.
aidenwilliamloanfirm@outlook.com

Anonymous said...

Mganga wa jadi, Sangoma na Daktari, Uchawi inaelezea, kupoteza upendo inaelezea, inaelezea Voodoo, Psychic
kuacha cheating katika mahusiano yako sasa na Spell ya upendo ulinzi, wamepoteza upendo inaelezea, inachukua 24hours kuanza kazi 100% kuhakikisha Same SIKU matokeo.
Waliopotea upendo inaelezea.
Kurejesha waliopotea Lover inaelezea
fedha inaelezea
Kisasi inaelezea.
Wamepoteza mali inaelezea
Kupata Spell mtoto.
Kivutio inaelezea.
Talaka inaelezea. Barua pepe: okpolespellcaster1@gmail.com

Anonymous said...

Salamu kwenu kutoka MASTERS GRAND JOIN
Illuminati kutoka Afrika Kusini, Marekani, au mahali popote duniani LEO, kuwa matajiri, FAMEOUS,
Na posses nguvu. New wanachama wa usajili sasa ni wazi online sasa !!!!! FAIDA aliyopewa MPYA wanachama ambao JOIN Illuminati. Ujira Fedha ya dola $ 300,000 USD CAR New Sleek Dream yenye thamani ya dola za Kimarekani $ 120,000 USD House Dream kununuliwa katika nchi ya uchaguzi yako mwenyewe Moja Mwezi likizo (kulipwa kikamilifu) kwa yako marudio ndoto utalii. Mwaka mmoja Golf Uanachama mfuko matibabu VIP katika viwanja vya ndege wote katika Dunia A jumla Maisha mabadiliko Kupata Bohemian Grove mwezi malipo ya Dola za Kimarekani $ 1,000,000 katika akaunti yako ya benki kila mwezi kama mwanachama Mwezi Mmoja mchakato Uteuzi na Viongozi wa dunia Juu 5 na Juu 5 Celebrities katika Dunia. Kama mail yangu sasa au kutuma barua pepe yako illuminatiworldwide@hotmail.com

Anonymous said...

Siku njema,

Sisi ni halali And Reputable fedha Wakopeshaji. Sisi mikopo fedha nje kwa watu binafsi katika haja ya msaada wa kifedha, sisi kutoa mkopo kwa watu kwamba wana mikopo mbaya au katika haja ya fedha za kulipia bili, kuwekeza katika business.Have Umekuwa kuangalia kwa mkopo? una wasiwe na wasiwasi, kwa sababu wewe ni katika mahali pa haki i kutoa mkopo kwa kiwango cha maslahi ya 2% hivyo kama wewe ni katika haja ya mkopo i nataka kuwasiliana tu na mimi kupitia hii ya mitaani email: mobilfunding1999@gmail.com

TAARIFA LOAN MAOMBI zinahitajika KUTOKA KWAKO.

1) Majina Kamili: ............
2) Jinsia: .................
3) Umri: ........................
4) Nchi: .................
5) Namba ya Simu: ........
6) Kazi: ..............
7) mapato ya kila mwezi: ......
8) Loan Kiasi Inahitajika: .....
9) Loan Duration: ...............
10) Madhumuni ya Mikopo: ...........

Shukrani kwa yako Ushirikiano

Kila la heri

Bill said...

Hello!

Unahitaji halali na ya haraka huduma ya mkopo?
Kwa sasa sadaka 3% Mikopo ya yote Aina mikopo ya biashara, Mikopo kibinafsi, Gari Mikopo, kilimo Mikopo, au fedha Project? Sisi kutoa mikopo kwa makampuni na watu binafsi duniani kote, konsolideringen madeni, hata kama una
alama ya chini ya mikopo na kutafuta ni vigumu kupata mikopo kutoka benki ya eneo lako au taasisi yoyote ya kifedha? , Na sasa kuwa na wakati mgumu kukabiliana na benki yako, au nyingine taasisi za fedha? Je, unahitaji haraka mkopo kama ndiyo Email yetu nyuma kupitia (ryanloaninvestment@outlook.com) sisi Kutoa kila aina ya Mikopo.

Omba Sasa na kupata fedha yako haraka!

* Kukopa kati 5000 na Euro 50,000,000
* Chagua kati ya miaka 1 hadi 30 kulipa.
* Flexible suala mkopo na masharti.

mipango hii yote na zaidi, wasiliana nasi sasa.

wasiliana nasi kupitia barua pepe: kwa ajili ya kampuni ya mkopo yeyote aliyenisaidia hapa ni maelezo yao mawasiliano (ryanloaninvestment@outlook.com)


kuhusu
Management.
Wito simu: +27 (0603170517)
Wasiliana Speedy yako Loan Sasa!

Unknown said...

Loan Kutoa @ cha 2% !!!

kampuni yetu ni shirika ya kisheria ambayo iliundwa kusaidia watu ambao wanahitaji msaada, kama vile misaada ya kifedha. sisi ni USA msingi kampuni ya fedha.
Hivyo kama wewe ni katika matatizo ya kifedha katika fujo fedha, na unahitaji fedha ya kuanzisha biashara yako yenyewe, au unahitaji mkopo kulipa madeni au kulipa bili yako, kuanza biashara nzuri, au ana Matatizo zilizokopwa zaidi ya benki za mitaa, wasiliana nasi leo Barua pepe: ohioloans85@gmail.com


Mr Scotty

Unknown said...

Je! Unahitaji mkopo wa haraka? Je! Una deni? Je! Una mikopo mbaya? Umekataliwa na benki, unahitaji mkopo kuanza biashara yako OR uwekezaji? kukutana na DIAMOND WEALTH LOAN COMPANY Tunatoa mikopo kwa watu pamoja na alama zao mbaya za mikopo. Tunatoa mikopo yako ya muda mrefu na ya kibinafsi ya biashara na ya kibinafsi na viwango vya chini vya riba kwa 2% kwa mwaka kwa watu binafsi na makampuni. Programu yetu ya mkopo ni ya haraka na ya kuaminika, iliyopitishwa leo na kupokea jibu la haraka. Mtayarishaji ni bima bora, amethibitishwa kwa wateja 100% uhakika na kiwango cha juu. Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana nasi kupitia anwani yetu ya barua pepe: (diamondcreditexpress1@gmail.com) DIAMOND WEALTH S MD / Afisa Mtendaji Mkuu.

martin maxwell said...


WELCOME TO THE GREAT BROTHERHOOD.
Do you want to be a member of Illuminati as a brotherhood
that will make you rich and famous in the world and have
power to control people in the high place in the worldwide
.Are you a business man or woman,artist, political,
musician, student, do you want to be rich, famous, powerful
in life, join the Illuminati brotherhood cult today and get
instant rich sum of. 2 million dollars in a week, and a free
home.any where you choose to live in this world
BENEFITS GIVEN TO NEW MEMBERS of ILLUMINATI.
1. A Cash Reward of USD $500,000 USD
2. A New Sleek Dream CAR valued at USD $300,000 USD
3.A Dream House bought in the country of your own choice
4. One Month holiday (fully paid) to your dream tourist
destination.
5.One year Golf Membership package
6.A V.I.P treatment in all Airports in the World 7.A total
Lifestyle change 8.Access to Bohemian Grove
account every month as a member
9.One Month booked Appointment with Top 5 world
Leaders and Top 5 Celebrities in the World.
If you are interested of joining us in the great brotherhood of illuminati CONTACT MR ROLAND or WhatsApp him +2348142587627
or email:illuminatipower666brotherhood@gmail.com