Tarehe 19 Februari 2013 Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alifanya ziara ya kikazi katika kata za Kimara na Saranga kufuatilia kuhusu matengenezo ya barabara na daraja la Golani.
Mnyika alifanya hivyo siku mbili tangu afanye mkutano wa kikazi na viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Kanuni na wananchi katika kata ya Mabibo tarehe 16 Februari 2013 kulitolewa malalamiko kuhusu Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) kutoshughulikia maombi ya wananchi yaliyowasilishwa kwa kampuni hiyo kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2010 mpaka 2012.
Ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji huo kuhusu barabara, Mnyika alikutana na wananchi ambapo walipaswa kulipwa fidia inayokadiriwa kufikia shilingi milioni 278 ili kuruhusu njia mbadala kupatikana kufuatia ujenzi wa daraja katika eneo hilo.
Aidha, Mbunge amekagua matumizi ya daraja hilo yaliyoanza kupitia njia ya zamani na athari zake katika mfumo mzima wa usafiri katika eneo husika; na kubaini kwamba daraja husika haliwezi kuzinduliwa pamoja na kuwa limeanza kukamilika mpaka ujenzi wa kingo za mito ukamilike pamoja na kupatikana kwa barabara mbadala baada ya wananchi kulipwa fidia.
Mara baada ya ziara hiyo Mbunge alikutana na uongozi wa Manispaa ya Kinondoni na kuwasilisha madai hayo ya wananchi ambao miezi zaidi ya sita imepita toka nyumba zao ziwekewe X bila hata ya kufanyiwa tathmini. Baada ya Mnyika kuwawakilisha wananchi hao uongozi wa Manispaa umeamua kutuma timu ya uthamini na mara baada ya uthamini huo, kutuma uongozi kukamilisha majadiliano na wananchi husika kabla ya tarehe 25 Februari 2013.
Itakumbukwa kwamba tarehe 6 Mei 2011 Mbunge Mnyika alitembelea kata za Saranga na Kimara kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo na kuwajulisha wananchi wa maeneo husika kwamba jumla ya shilingi milioni zaidi ya mia tano (501,973,470) zilitengwa kwenye bajeti ya Halmashauri ya Kinondoni kwa mwaka wa Fedha 2011/2012 kwa ajili ya kujenga Daraja Kubwa la Burura/Golani katika Mto Ubungo.
Baada ya ujenzi wa daraja hilo kuchelewa mbunge alichukua hatua za kufuatilia kwa mara nyingine mwezi Aprili 2012 na hatimaye mkataba wa ujenzi wa daraja husika umesainiwa kati ya Manispaa ya Kinondoni na Mkandarasi Kika Co. Ltd kwa gharama za shilingi milioni 447. Gharama za ujenzi huo zimeongezwa kwa nyakati mbalimbali mpaka kufikia milioni 672.
Ifahamike kwamba kutokuwepo kwa daraja katika eneo hilo miaka mingi kulifanya mawasiliano katika maeneo hayo kuwa magumu nyakati za mvua na kusababisha madhara ya kibinadamu na mali wananchi wanapovuka mto katika eneo hilo wakati wa mafuriko.
Baada ya mbunge kuwawakilisha wananchi kwa kushirikiana na madiwani kutaka ujenzi wa daraja hilo, liliingizwa kwenye bajeti ya Manispaa ya Kinondoni kwa mwaka wa fedha 2011/2012 kwa vyanzo vya ndani (own source).
Imetolewa tarehe 20 Februari 2013 na:
Aziz Himbuka
Katibu Msaidizi
Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo
No comments:
Post a Comment