Sunday, February 10, 2013

Waraka wa Kwanza kwa mwaka 2013 wa Mbunge kwa Wananchi


“Maji; kwa Nguvu ya Umma”:

Waheshimiwa Wananchi wenzangu, Katiba ya Nchi pamoja na ubovu wake inatamka katika Ibara ya 63 (2) kwamba “Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba”.

Hata hivyo kutokana na uzembe wa uongozi wa Bunge wa kushindwa kuzingatia na upuuzi wa wabunge wengi wa CCM kuridhia hoja ya kuondolewa hoja yangu binafsi; Bunge limeshindwa kutimiza wajibu wake wa kuisimamia Serikali kuhusu hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es Salaam.

Katiba ya Nchi ibara ya 8 (1) inatamka kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii kwa hiyo wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa katiba.

Ibara hiyo inaendelea kueleza kwamba lengo kuu la serikali ni ustawi wa wananchi, Serikali itawajibika kwa wananchi na wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao kwa mujibu wa masharti ya katiba hii.

Kwa kuwa wananchi mmekoseshwa fursa ya kushiriki kupitia mwakilishi wenu niliyewasilisha hoja binafsi kwa kuzingatia wajibu wa kibunge na mamlaka ya madaraka ya Bunge kwa mujibu wa ibara ya 63 na 100 ya Katiba ya Nchi; kwa waraka huu naiwasilisha hoja binafsi yangu kwenu wananchi muijadili na kufanya maamuzi mtayoona yanafaa.


Nawaomba mfanye maamuzi ya kuunganisha nguvu ya umma kuiwajibisha Serikali iwajibike kwenu kwa kuchukua hatua tisa za haraka, kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam na nchi nzima kama nilivyopendekeza kwenye hoja binafsi. (NIMEAMBATANISHA NAKALA).

Hoja hii kwa kuwa wameiondoa katika bunge linaloongozwa na CCM na Serikali; naiwasilisha kwenye ‘bunge’ la wananchi ambalo ndio msingi wa mamlaka na madaraka yote.

Unganisheni nguvu ya umma kwa njia zozote mtazoona zinafaa kwa kurejea katiba ya nchi hususan ibara ya 18 ya uhuru kupewa taarifa na kutoa maoni; ibara ya 20 ya uhuru kujumuika na kutoa mawazo hadharani kupitia mikutano na maandamano na ibara ya 21 ya haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayokuhusu wewe, maisha yako na yanayolihusu taifa.

Ukipata waraka huu na hoja binafsi sambaza kwa mwenzako na utujulishe maamuzi mtayofikia kupitia mbungeubungo@yahoo.com au 0768774274 au SLP 62066 Dar es Salaam ili tushirikiane kuwezesha uwajibikaji kwenye sekta ya maji kwa nguvu ya umma.

Kilichojiri kabla na wakati wa Bunge kuhusu Hoja Binafsi ya Upatikanaji Maji Safi na Ushughulikiaji wa Maji Taka Jijini Dar es Salaam:

Kutokana na umuhimu wa hoja ya Hatua za Haraka za Kuboresha Upatikanaji wa Maji Safi na Ushughulikiaji wa Maji Taka kwa maisha ya wananchi wa Dar es Salaam na Nchi kwa ujumla, tarehe 8 Januari 2013 niliwasilisha TENA taarifa ya hoja hiyo ili kutimiza masharti ya kanuni za Bunge ambayo yanaelekeza kuwa hoja isipowasilishwa na kujadiliwa taarifa yake inatenguka.

Nilitaka pia maelekezo ili kuwasilisha marekebisho zaidi na maelezo ya ziada kwa kuwa katika taarifa hiyo, nilipanua kusudio na wigo wa hoja husika kuwa nchini kwa kuzingatia yaliyojiri wakati na baada ya mkutano wa tisa wa Bunge kuhusu masuala husika.

Tarehe 10 Januari 2013 niliruhusiwa kuwasilisha mabadiliko na maelezo ya nyongeza na Ijumaa tarehe 1 Februari 2013, niliwasilisha mabadiliko ya hoja na maelezo ya nyongeza kwa kuzingatia kanuni ya 55 (10) ambayo inaruhusu mbunge kufanya mabadiliko ya hoja yake iwapo atatoa taarifa kutaka kufanya mabadiliko walau siku moja kabla ya siku ile ambapo hoja hiyo itawekwa kwenye orodha ya shughuli ili ijadiliwe.

Jumapili tarehe 3 Februari 2013 nilitafutwa jioni na kupewa barua iliyogongwa muhuri wa SIRI kuwa nimekataliwa kufanya mabadiliko na maelezo yangu ya nyongeza yamerudishwa, tafsiri yake ni kuwa nilitakiwa kuwasilisha maelezo na hoja kama yalivyokuwa Novemba 2012 kabla ya kauli ya Serikali Bungeni ya tarehe 7 Novemba 2012.

Vyanzo vyangu ndani ya Serikali, Bunge na CCM vilishanidokeza kuwa lengo lilikuwa ni kuiondoa hoja hiyo kwa majibu mepesi kuwa ina tarehe zenye kuonyesha kuwa ‘imepitwa na wakati’.

Tarehe 4 Februari 2013 asubuhi kabla ya kuingia bungeni kuwasilisha hoja hiyo niliwasilisha majibu ya barua kwa Katibu wa Bunge ya kupinga mabadiliko na maelezo ya nyongeza kukataliwa kwa kuzingatia kuwa sababu nilizoandikiwa hazikuwa za msingi na barua hiyo iliandikwa kinyume na kanuni ya 55 (12) ambayo imetoa mamlaka kwa Spika na sio Katibu wa Bunge.

Kufuatia barua hiyo niliitwa na kuelezwa kwamba naweza kuwasilisha baadhi tu ya marekebisho na mengine sipaswi kuyawasilisha. Kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda niliamua kuingia katika ukumbi wa Bunge na kujiandaa kutumia kanuni ya 55 (11) ambayo inatoa fursa hata kwa mbunge ambaye hakutoa taarifa kabla, kuwasilisha mabadiliko yake ukumbini kwa idhini ya Spika.

Yaliyotokea baada ya hapo mchana wa tarehe 4 Februari 2013 wengine mliyashuhudia kwa kuwa nilipunjwa muda, nilikataliwa kuwasilisha baadhi ya mabadiliko, nilikatishwakatishwa, nilizuiwa kusoma maelezo yangu ya nyongeza; kinyume kabisa na kanuni na inavyokuwa kwa watoa hoja wengine hususan wa Serikali.

Katika hali hiyo, nilimweleza wazi bungeni, Naibu Spika Job Ndugai kuwa nitakata rufaa dhidi ya maamuzi yake yenye mwelekeo wa kuficha uozo na ufisadi kwa kukiuka kanuni za Bunge.

Jioni ya tarehe 4 Februari 2013 Waziri wa Maji badala ya kuchangia kwa kujibu hoja kama kanuni ya 53 (6) (c) aliwasilisha hoja tofauti kwa kutumia kanuni ya 57 (1) (c) ya kuiondoa hoja yangu isiendelee kujadiliwa kwa maelezo kwamba “tayari kuna mpango maalum uliotengewa fedha nyingi na Serikali ya CCM na kwa kuzingatia kuwa utekelezaji wa mpango huo unaendelea vizuri sana”.

Waziri alikiuka kanuni za Bunge kwa kuwasilisha hoja hiyo kwa kuwa kanuni ya 57 (4) badiliko hilo lilikuwa linapingana na hoja kwa kuwa linaiondoa hoja yenyewe na kanuni ya 58 (5) ambayo inaelekeza kwamba hoja ikishawasilishwa anayeweza kuondoa hoja ni mtoa hoja mwenyewe tu tena kwa idhini ya Bunge.

Aidha, Waziri wa Maji alitoa maelezo yenye kulidanganya bunge, kujenga matumaini hewa fedha za kutosha zimetengwa na utekelezaji unakwenda vizuri sana. Hiyo ilikuwa kinyume kabisa na maelezo yake mwenyewe bungeni tarehe 10 Julai 2012, 7 Novemba 2012 na nyaraka nilizonazo za ndani ya Serikali za Januari 2013.

Pia, Waziri wa Maji hakutoa maelezo kuhusu mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya Wachina, hautoi maji huku kukiwa na upungufu katika uzalishaji, upotevu wakati wa usafirishaji, udhaifu katika usambazaji na tuhuma za ufisadi katika matumizi.

Hakujibu pia iwapo Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atafanya ukaguzi maalum wa matumizi ya fedha matumizi ya bilioni 96.4 za mradi wa maji safi na mazingira vijijini katika Jiji la Dar es salaam na Halmashauri zingine na kuwezesha hatua za ziada kuchukuliwa kutokana na matumizi mabaya ya fedha pamoja na kasoro zingine katika utekelezi wa Programu ya Maji Safi na Mazingira Vijijini (RWSSP) ikiwemo katika Manispaa za Jiji la Dar es Salaam ilipaswa kutekelezwa kuanzia mwaka 2005/2006 na kukamilika mwaka 2010/2011.

Kwa ujumla, hakueleza hatua zozote ambazo Serikali inatarajia kuchukua kutokana na hatua tisa za haraka nilizopendekeza kwenye hoja yangu na masuala niliyotaka yazingatiwe kutoka katika maelezo yangu ili kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam.

Tumefikaje katika hali hii?

Katika waraka wangu wa kwanza kwa mwaka 2012 kwenu (Ukweli ni Uhuru) wa tarehe 22 Juni 2012 nilirejea mchango wangu bungeni wa tarehe 19 Juni 2012 ambapo nilihoji kwa niaba yenu namna bajeti ya nchi ya mwaka 2012/2013 ilivyokuwa haikuzingatia vipaumbele vyenye kudhibiti mfumuko wa bei nchini na kiwango cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mzunguko na maji katika Jiji la Dar es Salaam kuwa kidogo ukilinganisha na mipango na ahadi za Serikali. Nilieleza hali hiyo imetokana na “udhaifu wa Rais, uzembe wa Bunge na upuuzi wa CCM” , kauli ambayo ilinifanya nitolewe nje ya Bunge.

Niliwaeleza madaraka makubwa juu ya wabunge aliyonayo Rais kutokana na ubovu wa katiba ya nchi ibara ya 90 na 99 kuhusu bajeti ya maendeleo na sheria ya fedha; na hivyo madaraka ya Bunge na wabunge juu ya kufanya mabadiliko kwenye bajeti ya nchi kukatazwa kupitia Kanuni ya 97 ya Kanuni za kudumu za Bunge.

Nilieleza kuwa hali hiyo ilikuwa ni matokeo pia wa uzembe wa Bunge kutokutumia ipasavyo kanuni ya 94 ya Kanuni za Kudumu za Bunge kujadili mapendekezo ya mpango wa Serikali katika mkutano wa Bunge uliofanyika mwezi Februari 2012.

Hivyo, nilishauri hatua ambazo Rais kwa nafasi yake ya mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri na Mwenyekiti wa Tume ya Mipango na kwa mamlaka yake makubwa ya kikatiba ikiwemo ya kuwa mkuu wa nchi na kiongozi wa Serikali anaweza kuzichukua kurekebisha udhaifu uliojitokeza katika Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya mwaka 2012/2013.

Niliwaahidi kuendelea kutimiza wajibu wa kibunge wa kuwawakilisha wananchi na kusimamia uwajibikaji wa Serikali ili kuwezesha maendeleo, na katika kufanya hivyo mwezi Oktoba mwaka 2012 niliwasilisha TENA taarifa ya hoja binafsi kuhusu hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es Salaam. (Taarifa hiyo nimewahi kuitoa kwa nyakati mbalimbali toka mwaka 2011 lakini sikuwahi kupewa nafasi).

Hatimaye hoja hiyo iliingizwa katika ratiba ya Mkutano wa Tisa wa Bunge hata hivyo tarehe 7 Novemba 2012 ikiwa ni siku moja kabla ya kuwasilisha hoja yangu bungeni tarehe 8 Novemba 2012, Waziri wa Maji akapewa nafasi ya kuwasilisha Kauli ya Serikali kuhusu Mpango Maalum wa kutatua tatizo la maji katika Jiji la Dar es salaam.

Hayo yalifanyika wakati hoja yangu ilipaswa kuwa siri ya Ofisi ya Katibu wa Bunge na uongozi wa Bunge uliruhusu kauli ya Serikali ambayo vyanzo vyangu mbalimbali ndani ya Bunge, Serikali na CCM vilinieleza kwamba ililenga kuondoa haja ya hoja yangu (pre-emption).

Niliomba muongozo tarehe 7 Novemba 2012 kwa kuwa pamoja na kauli hiyo bado masuala ya msingi niliyotaka Bunge iyajadili na kufanya maamuzi yalikuwa hayajapatiwa majibu katika kauli ya Serikali; hata hivyo sikuweza kupewa nafasi ya kuwasilisha hoja binafsi tarehe 8 Novemba 2012, hatua iliyonifanya niwasilishe TENA hoja hiyo tarehe 4 Februari 2013.

Kwa kuwa imeondolewa bungeni kinyemela naiwasilisha kwenu muijadili na kufanya maamuzi mtakayoona yanafaa kwa maslahi ya umma.

Maji; kwa nguvu ya umma!.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,



John Mnyika (Mb)
Bungeni-Dodoma
06/02/2013

4 comments:

Mtalii said...

eetairTumekupata,Mh.,Hoja hako hii imetupwa leo bungeni hila ni dira ya kesho.Tuombe uzima ccm awafanyi research yoyote,WAMEIFUNGIA LEO KESHO WATAWAPA WATAALAMU WAO KUIFANYIA KAZI HILI KUFI 2015 UKIULIZA WASEMA MBONA TUMETEKEREZA.Sauti wa wachache ni sauti ya mungu,unawatatea wakazi DAR,wamo marais.mawaziri,majaji,madr.wabunge,wanafunzi,na kila mmoja na idara yake,UJUMBE ULISHAFIKA SIKU NYINGI,Mungu akubalike akuzidishie afya njema,Mungu ibariki CHADEMA

Anonymous said...

mh hayo tunayajua sana na hii nikutokana na kiti cha spika kulifanya bunge liwe la chama fulani na lisiwe la wananchi kazi kubwa ya chama chetu nikuwafumbua macho watanzania ili watoe hukumu wenyewe 2015.Huwezi kuamini kuna watu tunaumia sana kiti cha spika kinavyopendelea watu flani bungeni hadi tunafikia kumchukia mtu yyte wa chama cha ufisadi. Damu ya mwangosya na ulimboka ndio mahakama ya ccm 2015

Anonymous said...

Mungu akupe afya njema unajua mtu akitaka kufa huwa anachoka hata kutumia dawa wewe hata usingeandika waraka sisi wananchi tumeshajua mchele ni upi.pumba ni zipi nachoweza kukwambia usiogope kitu wananchi tupo pamoja na chadema .sio bungeni hata huku kwetu mwnza wanatuvuluga sana ila hawatashikamana hapo 2015 tutaona hizi nguvu mbili live yaani ya shetani na nguvu ya mungu tumeona sasa wanatengeneza mtandao wa makahaba wengi kila kona ya nchi ili waje wawatumie mungu ni mwema kwa wale wamtumainie siku zote hata kama watajifungamanisha na shetani hawataweza saana watimiza unabii.ila ole wao wawatesao watu wa mungu

Anonymous said...

Mh, Mnyika umechambua vizuri udhahifu unoonyeshwa dhahiri na kiti cha spika na serikali yake kutokuwa fair kwa mkundi tofauti likiwemo upande wa upinzani katika shughuli za bunge.

Hii ni muendelezo wa kuonyesha dhahiri kuwa wabunge wa CDM wako makini kuipa taifa dira ya uongozi ikilinganisha na wabunge wa chama tawala wasiokuwa na maslahi ya taifa.

Big up Mh.

Nguvu ya umma ndiyo nguvu pekee, 2015 tutawasomea hukumu.

Jamani waTZ mshikamano muhimu... hili limekuwa likiongelewa kila mara na viongozi waandamizi wa CDM. Sio nguvu kidogo inahitajika kufurusha unyanywasaji wa utawala wa crezy green.