Wednesday, February 19, 2014

Mkakato wa Katiba Mpya: Wadau washirikishwe kutunga kanuni Bunge la Katiba

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), amesema atawasilisha mapendekezo ya kutaka ratiba ya Bunge Maalumu la Katiba ibadilishwe, ili wadau washirikishwe kwenye mchakato wa kutunga kanuni za Bunge hilo.

Mnyika alisema hayo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana.

Alisema ratiba iliyotolewa inaonyesha kwamba baada ya kusomwa kwa tangazo la kuitisha Bunge hilo na uchaguzi wa mwenyekiti wa muda, kazi ya kutunga kanuni itaanza.

Mnyika alisema kanuni ndiyo msingi wa kufikia mwafaka wa kuboresha rasimu ya Katiba badala ya kuchakachua na kwamaba ili zisitungwe kanuni mbovu ipo haja ya wadau wote wanaohusika na mchakato wa Katiba mpya ndani na nje ya Bunge kushiriki. 

“Nakusudia kuwasilisha mapendekezo kwamba ratiba ya Bunge ifanyiwe mabadiliko ili kuwapo na kikao cha kusikiliza umma (Public hearing), juu ya kanuni hizo ili mawazo ya wadau yazingatiwe katika maandaluzi ya kanuni kabla ya Bunge kupitisha azimio la kuridhia kanuni hizo,” alisema Mnyika.

Aidha, alisema atawasiliana na Katibu wa Bunge na Katibu wa Baraza la Wawakilishi au Mwenyekiti wa muda atakayechaguliwa ili kanuni zisitolewe nakala kwa wajumbe hao pekee, bali iwekwe kwenye tovuti za Bunge, za Baraza la Wawakilishi, za serikali ili ziwe wazi kwa wadau wazijadili.

Alisema kanuni za kawaida za Bunge zimekuwa zikitoa mamlaka makubwa sana kwa maspika kwa kiwango, ambacho wamekuwa wakifanya maamuzi mabovu na kusababisha vurugu. 

“Ni lazima Bunge la Katiba liwe na kanuni, ambazo zinatoa mamlaka zaidi kwa wajumbe na pia kuweka msingi wa kujenga mwafaka zaidi wa kitaifa kwa kuwa Katiba ni maridhiano ya wananchi na siyo ushindani wa vyama au makundi mbalimbali,” alisema Mnyika.

Alisema wajumbe ni wawakilishi tu wa kuwezesha mwafaka huo kufikiwa na kanuni ni nyenzo ya kuongoza majadiliano ya kufikia maridhiano kwa kuzingatia maoni ya wananchi na maslahi ya umma.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Katibu wa Bunge na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, leo wajumbe hao watakuwa na jukumu la kuandaa na kupitisha kanuni za Bunge Maalumu.

Rejea chanzo: http://goo.gl/0nxMuB

No comments: