Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika ameendelea kufuatilia kuhusu fidia
ya ardhi ya wananchi wa kata ya Kwembe waliohamishwa baada ya kulipwa fidia ya
maendelezo pekee kupitisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Muhimbili (MUHAS) kampasi
ya Mloganzila.
Kwa upande mwingine, Mbunge Mnyika ameendelea pia kuhoji katika mamlaka
mbalimbali juu ya kauli za viongozi wa Serikali kutamka kwamba eneo hilo lipo
katika Mkoa wa Pwani badala ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar Es Salaam.
Tarehe 19 Januari 2014 Mbunge Mnyika alifika katika kata ya Kwembe na
kukutana na wananchi kusikiliza malalamiko yao na mara baada ya mkutano huo
alizikutanisha kamati mbili zinazofuatilia suala hilo.
Kufuatia hatua hiyo, Mbunge Mnyika aliwasiliana na Waziri Mkuu Mizengo
Pinda na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwakumbusha kutekeleza
ahadi zao za kuupatia ufumbuzi mgogoro huo kufuatia hatua ya mbunge kuhoji
suala hilo bungeni kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2011 mpaka 2013.
(Baadhi ya rejea kutoka Kumbukumbu Rasmi za Bunge-Hansard zimeambatanishwa).
Ofisi ya Mbunge inalazimika kutoa taarifa hii kwa umma kwa kuwa Ofisi ya
Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
zimeshindwa kutimiza wajibu wa kutoa majibu ya barua hata baada ya ofisi ya
mbunge Jimbo la Ubungo kwenda katika ofisi zao mara kwa mara kufuatilia suala
hilo.
Kutokana na hali hiyo, Mbunge Mnyika amechukua uamuzi wa kumshauri Rais
Jakaya Kikwete kuingilia kati na kutoa kauli kwa umma kuhusu fidia ya ardhi kwa
wananchi hao. Rais awezeshe kutekelezwa kwa ahadi ya kuwapatia shilingi milioni
9 za fidia ya ardhi au viwanja mbadala kama ilivyoahidiwa kwa nyakati mbalimbali
kati ya mwaka 2009 na 2010.
Itakumbukwa kwamba tarehe 11 Disemba 2012 Rais Kikwete katika hotuba yake
ya uzinduzi wa jengo la huduma za mama na mtoto katika hospitali ya Sinza, Rais
alitoa maelezo yasiyokuwa sahihi kwamba wananchi wameshalipwa fidia zote ila
wanadai fedha za ziada za usumbufu kutokana na kuchochewa na wapinzani.
Tarehe 12 Disemba 2012 Mbunge Mnyika alieleza umma kwamba Rais alipotoshwa
kuhusu suala hilo na kwamba malipo ya fidia kwa wananchi bado hayajakamilika na
kukumbusha kwamba ahadi za kutoa fidia
hizo haikutolewa na upinzani bali
Serikali kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
John Chiligati na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Patrick Rutabanzibwa.
Kadhalika kamati ya wananchi nayo iliandika barua kwa Rais yenye maelezo na
vielelezo juu ya madai ya msingi ya wananchi ambayo tangu mwaka 2013 mwanzoni
mpaka sasa haijapatiwa majibu na ikulu hivyo ni wakati muafaka sasa wa Rais
Kikwete mwenyewe kufuatilia na kuagiza hatua kuchukuliwa kwa manufaa ya
wananchi.
Ofisi ya Mbunge inasisiza kwamba Mnyika au kamati za wananchi au mtu
mwingine yeyote anapofuatilia suala hili isionekane kuwa ni uchochezi bali ni
sehemu ya uwakilishi na uwajibikaji kuwezesha haki kutendeka na miradi ya
maendeleo kutekelezeka kwa ufanisi.
Imetolewa tarehe 22 Februari 2014 na:
Aziz Himbuka
Katibu Msaidizi
Ofisi ya Mbunge
VIELEZO VYA KUREJEA:
No comments:
Post a Comment