Katika Mkutano wa 14
Kikao cha 15 tarehe 21 Disemba 2013 ulisomwa Bungeni Muswada Binafsi wa Mbunge
wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa wa mwaka 2013 uliowasilishwa na John
Mnyika (Mb).
Baada ya muswada huo
kusomwa, Bunge lilielezwa na Mheshimiwa Spika, naomba kununukuu “ Waheshimiwa
wabunge, muswada binafsi…. sasa utaanza kuwepo kwenye website ya Bunge na
utakuwa public mpaka utakapopangiwa tarehe ya kujadiliwa na utapelekwa kwenye
kamati zitakazohusika wakati muafaka”.
Hata hivyo, mpaka sasa maelekezo
hayo ya Spika hayajatekelezwa hivyo; Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo inataka
Spika wa Bunge Anna Makinda kutoa kauli ya: Mosi, kuueleza umma sababu ya
maelekezo yake ya muswada huo kuwepo kwenye tovuti ya bunge kwa ajili ya kuwa
wazi kwa umma mpaka sasa kutokutekelezwa, Pili, ni lini muswada huo utapangiwa
tarehe ya kujadiliwa; Tatu, ni kwanini mpaka sasa muswada huo haujapelekwa
kwenye kamati zinazohusika; Nne, ni upi
wakati muafaka alioutaja kwenye maelezo yake.
Ofisi ya Jimbo la Ubungo
inawakumbusha vijana na wadau wote wa maendeleo yao kwamba kutokuwepo kwa
chombo kinachowaunganisha vijana wote bila kujadili itikadi kufuatilia masuala
ya maendeleo ya vijana kunafanya Wizara
mbalimbali za kisekta kutokuzingatia masuala yaliyokipaumbele kwa maendeleo ya
vijana.
Mathalani, katika
Mkutano huu wa Bunge katika Fungu la 65 la Wizara ya Kazi na Ajira Kitabu cha
Nne Cha Miradi ya Maendeleo Kifungu cha 2002, pamoja na wabunge na vijana
kupewa matumaini kwamba zimepitishwa bilioni tatu kwa ajili ya mikopo na mitaji
kwa vijana ukweli ni kwamba fedha hizo zimepangiwa matumizi ambayo kusipokuwa
na chombo cha kuyafuatilia kutakuwa na udhaifu, ufisadi na ubadhirifu kama
ilivyojitokeza katika fedha za mifuko ya maendeleo ya vijana kati ya mwaka 1993/1994 mpaka 2013/2014.
Kwa mujibu wa Kasma za
Kifungu hicho cha 2002 cha Bajeti iliyopitishwa ya Fungu 65 Wizara ya Kazi na
Ajira, fedha hizo zinazopaswa kuwa za mikopo na mitaji kwa vijana zitatumika
milioni 700 kwa ajili ya kulipia utaalamu elekezi (consultancy fees) kwa ajili
ya kutoa mafunzo kwa vijana 200 tu; milioni 150 zitatumika kununulia magari
Wizarani, milioni 60 zitatumika kwenye matangazo na orodha ndefu nyingine
ya matumizi yasiyo ya lazima ambayo
kutokana na ufinyu wa muda sitaendelea kuyataja.
Aidha, katika mjadala
wa bajeti hiyo wabunge waliweka bayana kwamba kiwango kinachotengwa katika
Mifuko ya Maendeleo ya Vijana iwe ni kwa Serikali Kuu na hata Halmashauri ni
kidogo ukilinganisha na uwezo wa nchi, mahitaji ya vijana na mafungu mengine yasiyo
na matumizi muhimu yanavyotengewa fedha nyingi katika baadhi ya Wizara.
Hivyo, ili Baraza la
Vijana la Taifa na Benki ya Vijana ambavyo ni vyombo muhimu kwa maendeleo ya
vijana viweze kuanzishwa kwa wakati, Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ubungo inamkumbusha
Spika wa Bunge kuelekeza muswada binafsi uliokwisha wasilishwa kwa Bunge kwa
kamati zinazohusika kwa ajili ya kuanza
kuujadili. Suala hili ni muhimu likapata majibu ya mapema ili muswada
huo uweze kuwasilishwa Bungeni katika Mkutano wa 16 wa Bunge unaotarajiwa
kufanyika mwezi Novemba mwaka 2014.
Ofisi ya Mbunge Jimbo
la Ubungo inatoa mwito pia kwa vijana na wadau wa maendeleo ya vijana kuingilia
kati suala hili na kuisimamia Serikali kwa kuzingatia kwamba katika majumuisho
ya Bajeti ya Wizara yenye dhamana ya vijana kwa mwaka 2013/2014 tarehe 21 Mei
2013 mkutano wa 11 kikao cha 30; Serikali ilitumia kisingizio kwamba ‘ni bunge
la bajeti’ kukwepa kuwasilishwa kwa muswda Bunge. Hata hivyo, ahadi ya Serikali
ya kuwasilisha muswada haikutekelezwa kwenye mikutano mitatu uliyofuatia ya 12,
13, 14 na 15; hivyo mkutano huu wa 16 ni muafaka kuwezesha maamuzi kufanyika
kwa ajili ya maendeleo ya vijana nchini.
Ofisi ya Mbunge Jimbo
la Ubungo inaukumbusha umma kwamba Sera ya zamani ya maendeleo ya vijana ya
mwaka 1996 ilitamka kwamba kutaanzishwa
Baraza la Vijana na suala hilo kurudiwa katika Sera mpya ya mwaka 2007;
hata hivyo Serikali imekuwa ikiwepa kuhakikisha kwamba matakwa hayo ya sera
tajwa yanatekelezwa pamoja na kuwa suala hilo linahusu mustakabali wa maendeleo
ya vijana nchini.
Imetolewa tarehe 24
Septemba 2014 na:
Aziz Himbuka
Katibu wa Mbunge
Jimbo la Ubungo
No comments:
Post a Comment