Monday, September 1, 2014

Rais Kikwete, Waziri wa Maji Prof Maghembe na Bodi mpya ya DAWASCO

Tarehe 13 Agosti 2014 Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe alizindua Bodi mpya ya Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar Es Salaam (DAWASCO) na kutoa kauli mbalimbali mbele ya vyombo vya habari ambazo zinaendeleza udhaifu ule ule badala ya kuchukua hatua za haraka kunusuru wananchi katika shida kubwa ya upatikanaji wa maji.

Ni suala lililo wazi kwamba kuzindua bodi mpya ya DAWASCO pekee haitoshi, kwa kuzingatia kuwa majukumu makuu ya kuwezesha hatua za haraka yapo chini ya Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar Es Salaam (DAWASA) ambayo nayo inahitaji bodi mpya.

Natoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kuvunja bodi iliyopo ya DAWASA na kuunda bodi mpya. Aidha, namkumbusha Rais Kikwete kuitisha kikao ikulu pamoja na DAWASCO, DAWASA na Wizara ya Maji kama alivyoahidi mbele ya wananchi mwezi Machi mwaka 2013.

Juzi wakati Waziri Maghembe anazindua bodi hiyo, alisema kwamba sasa uvumilivu juu ya wizi wa maji unaochangia ukosefu wa maji umefikia kikomo. Ni vyema Rais Kikwete akajua kwamba hii si mara ya kwanza kwa waziri huyo kutamka kauli ya namna hiyo; aliitoa pia tarehe 21 Februari 2013 mbele ya wajumbe wa bodi na wafanyakazi wa DAWASCO na DAWASA .

Rais Kikwete achukue hatua katika mamlaka yake kuwezesha kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji kuongezeka na atambue kwamba iwapo akiingilia kati kabla hata ya kukamilika kwa miradi hiyo huduma ya maji inaweza kuongezeka kwa wananchi ikiwa wizi wa maji utadhibitiwa na ufanisi wa DAWASA na DAWASCO utaongezeka.

Waziri Maghembe ameipa bodi mpya muda wa mwezi mmoja kushughulikia wizi wa maji wakati alipaswa kueleza kwanza ni hatua gani alichukua dhidi ya bodi iliyotangulia na watendaji waandamizi wa DAWASCO kwa kushindwa kutekeleza agizo la awali la mwezi mmoja alilolitoa zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Waziri Maghembe ameagiza bodi kuunda mara moja kitengo cha kiintelejensia kitakachoripoti juu ya wizi wa maji wakati alipaswa kueleza kwanza matokeo kikosi kazi alichoagiza tarehe 21 Februari 2013 kuwa kingeundwa kushughulikia wizi huo huo.

Waziri Maghembe alishasema mbele ya vyombo vya habari zaidi ya mwaka mmoja uliopita kwamba wezi wa maji wanafahamika na kwamba baadhi ya viongozi wa DAWASCO wanatoa mgawo wa maji kwa upendeleo kwa kupewa rushwa na wezi hao. Hivyo, anapaswa kuwataja kwa majina watuhumiwa hao wa wizi na ufisadi ndani ya DAWASCO wanaoshirikiana nao na kuwachukulia hatua za haraka ili wananchi wasiendelee ‘kuhangaikia’ uhai kutokana na ukosefu wa maji. 

Waziri Maghembe ametaka bodi itoe maoni juu ya marekebisho ya sheria kwa mwezi mmoja, bila ya kuweka wazi kwa umma maoni yaliyotolewa na bodi iliyotangulia na kwanini hadi sasa hajatekeleza ahadi yake aliyoitoa tarehe 21 Februari 2013 kwamba atawasilisha muswada wa sheria bungeni mwaka jana.

Udhaifu wa DAWASCO ulioueleza Waziri Maghembe juu ya upotevu wa maji wa asilimia 56, DAWASCO kudai taasisi za Serikali zaidi ya bilioni 27 kwa mwaka, makusanyo madogo ya bilioni 4.2 badala ya bilioni 9.5 kwa mwezi, udhaifu wa Sheria za maji ikiwemo ya DAWASA, DAWASCO kudaiwa madeni makubwa ikiwemo ya kudaiwa na TANESCO bilioni 10 na hivyo umeme kukatwa na wananchi kukosa huduma ya maji ni ushahidi kwamba hoja binafsi niliyowasilisha bungeni kwa niaba ya wananchi ilipaswa kukubaliwa na hatua za haraka kuchukuliwa.

Hata hivyo, kinyume na kauli zake za sasa za kukiri ukubwa wa matatizo, Waziri Maghembe alilidanganya Bunge tarehe 4 Februari 2014 kwa kutoa maelezo kwamba utekelezaji unakwenda vizuri ikiwemo unaohusu DAWASCO na alikiuka kanuni kwa kutoa hoja iliyofanya udhaifu huo usijadiliwe hali iliyochochea vurugu bungeni.

Itakumbukwa kwamba baada ya hoja binafsi juu ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka Jijini Dar Es Salaam na Nchini kuondolewa bungeni nilieleza kusudio la kuitisha maandamano ya wananchi kwenda Wizara ya Maji kutaka majibu. 

Kufuatia kusudio hilo Waziri aliamua kutoa majibu kwa baadhi ya masuala ambayo alikwepa kukiri udhaifu bungeni hata hivyo yapo maazimio mengine ambayo mpaka sasa Serikali haijachukua hatua za haraka zinazohitajika.

Wakati tukisubiri kikao na Rais kuhusu maji, bodi mpya ya DAWASCO chini ya uenyekiti wa Meja Jenerali Mstaafu Samweli Kitundu iipitie hoja binafsi niliyowasilisha bungeni kwa niaba ya wananchi tarehe 4 Februari 2013 na kutoa taarifa kwa umma juu ya hatua za haraka ambazo bodi mpya itasimamia zichukuliwe.

Aidha, bodi mpya ya DAWASCO ipitie ripoti ya ziara tuliyofanya na Naibu Waziri wa Maji Amos Makalla Julai 2014 na kuchukua hatua za haraka kwa kushirikiana na DAWASA juu ya masuala tuliyobaini. Niko tayari kukutana na bodi hiyo kwa ajili ya kuwapatia maelezo zaidi na vielelezo vya ziada ili kushirikiana na kuwezesha upatikanaji wa maji kwa wananchi kuendelea kuongezeka.

Wenu katika utumishi wa umma,
John Mnyika (Mb)
15 Agosti 2014

No comments: