Monday, September 8, 2014

Uzinduzi wa rasimu ya ripoti ya matokeo ya utafiti kuhusu kuongeza ushiriki na uwakilishi wa wanawake,vijana na wenye ulemavu


John Mnyika, Mbunge wa Jimbo la Ubungo Akizindua rasimu ya ripoti ya matokeo ya utafiti kuhusu kuongeza ushiriki na uwakilishi wa wanawake, vijana na wenye ulemavu katika uongozi uliofanywa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD)


Akihutubia kama mgeni rasmi katika uzinduzi huo ambapo alisisitiza kwamba wasisubiri kuwezeshwa bali waanze kwa kujiwezesha na kuwezeshana ndipo watakapopata ushindi; aliwapa changamoto kwamba kama alivyoshinda 2010 ndivyo wao wanavyoweza kushinda 2015 wakijipanga kushinda badala ya kupanga kusubiri kuwezeshwa tu. Alitoa mwito kwa utafiti huo kuongezwa wigo wake kwa kutafiti juu ya mbinu za wanawake, vijana na wenye ulemavu kujiwezesha na kuwezeshana badala ya kujikita katika kutaka wawezeshwe zaidi kama rasimu ya utafiti inavyoeleza. Aidha, alieleza namna ambavyo utafiti umeeleza kuhusu vijana na urais hapa nchini na kuendeleza dhana isiyo sahihi kwamba kumewahi kujitokeza wagombea urais vijana. Alieleza kwamba katiba ya sasa kwa kutaja umri wa urais kuwa ni miaka 40 na kuendelea wakati ukomo wa umri wa ujana kwa sera ya maendeleo ya vijana na mkataba wa vijana Afrika ni miaka 35; hakuna mgombea urais yoyote kijana aliyejitokeza mpaka sasa wala haiwezekani kwa Tanzania kuwa na Rais kijana mpaka katiba ibadilishwe. Pia, alitahadharisha matumaini hewa ya wanawake, vijana na wenyeulemavu kwamba wigo wa uwakilishi wao utaongezeka 2015 kutokana na katiba mpya kwa kuwa mchakato wa katiba mpya umecheleweshwa na kuvurugwa kwa kiwango ambacho katiba mpya haiwezi kutumika katika uchaguzi 2015. Hivyo, alitoa mwito kwamba wajipange kushinda 2015 bila kusubiri katiba mpya. 


Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya wenye Ulemavu (Shivyawata) Amina Mollel akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wengine kufuatia hotuba niliyotoa katika uzinduzi huo.

No comments: