Kumbukizi
maalum ya tarehe 20 Machi 2015 ya wanafunzi watano wa Chuo Kikuu cha Dar Es
Salaam (UDSM) waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani imetukumbusha msiba
mkubwa wa watu 50 katika ajali moja ya basi na lori ya tarehe 11 Machi 2015.
Wakati
tukiendelea kuwaombea marehemu na majeruhi na kutoa pole kwa wafiwa na wahanga
wakati umefika sasa tutangaze #AjaliBarabaraniJangalaTaifa tuwajibike
kuzipunguza.
Kumbukizi
katika ukumbi wa Nkurumah ilihusisha ibada, nyimbo maalum na kusomwa kwa wasifu
wa wanafunzi walioaga dunia wakiwa wadogo familia zao na taifa likiwahitaji na
hatimaye salamu kutoka makundi mbalimbali.
Niliguswa
na salamu za Chuo cha Fani za Jamii zilizosomwa na Mkuu wa Chuo cha Fani za
Jamii aliyeeleza kwamba mabasi sasa yanaua kuliko magonjwa mengi. Alipendekeza
utafiti ufanyike UDSM kuchangia kupunguza hali hiyo kwa kuzingatia kwamba Chuo
Kikuu hicho kina fani mbalimbali (multi disciplinary).
Alieleza
kwamba kwa upande wa uhandisi waangalie iwapo teknolojia ya mabasi yenye spidi
inawiana na barabara zetu kuu ambazo nyingi ni za njia moja. Huku fani ya jamii
iangalie masuala ya maadili kufanya madereva wa mabasi kujifunza kwamba
wanabeba binadamu sio wanyama.
Nakubali
kwamba kuna umuhimu wa kuendelea na utafiti lakini tujiulize ni wananchi wangapi
wataendelea kupoteza maisha wakati tukisubiri matokeo ya utafiti mpya.
Hivyo,
kuna haja ya UDSM kuitisha Kongamano Maalum kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa
cha Usafirishaji (NIT) ili matokeo ya tafiti zilizofanyika tayari yajadiliwe na
mapendekezo ya hatua za dharura yatolewe.
Pamoja na tafiti zilizofanywa na wasomi, Waziri wa
Uchukuzi Samuel Sitta awasilishe matokeo ya Ripoti ya kamati iliyoundwa
kutathmini na kutoa mapendekezo ya hatua ya kuchukua ili kupunguza ajali za
barabarani ambayo ripoti yake ilikabidhiwa kwa aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Dr
Harrison Mwakyembe Novemba 2014.
UDSM
iende mbele zaidi ya kufanya utafiti kwa kuzingatia dhima iwezeshe msukumo wa
kisomi na kimkakati katika huduma kwa umma.
Natambua
pia katika salamu kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar Es Salaam (DUCE)
zilizosomwa kwa niaba ya Mkuu wa Kitivo cha Sayansi Fani na Sayansi Jamii
(DUCE) Serikali iliombwa kuongeza juhudi za kupunguza ajali.
Lakini
maombi pekee hayatoshi kuna haja ya kutaka utekelezaji na uwajibikaji na
Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salam isibaki nyuma katika kukabiliana na #AjaliBarabaraniJangalaTaifa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi amenukuliwa
kwenye vyombo vya habari kwamba chanzo cha ajali ya basi la Majinja Express na
lori ni ubovu wa barabara katika eneo la ajali na mwendo kasi.
Picha kutoka eneo la tukio zinaonyesha kulikuwepo na shimo
kubwa la muda mrefu katika barabara kuu. Lakini pamoja na hali hiyo hakuna
kiongozi yoyote wa Wakala wa Barabara (TANROADS) au mamlaka zingine
zinazohusika aliyewajibika au kuwajibishwa mpaka hivi sasa.
Baada ya Ikulu kusambaza taarifa ya salamu za rambirambi za
Rais ni vyema sasa ikasambaza tena taarifa nyingine ya kueleza umma hatua
ambazo Rais ameelekeza kuchukuliwa kwa waliosababisha hali hiyo.
Aidha, Waziri wa Uchukuzi atakiwe kuwasilisha kupitia
Mkutano wa 19 wa Bunge unaoendelea hivi sasa kauli ya Serikali kuhusu mkakati
wa kushughulikia kukithiri kwa ajali za barabarani nchini.
John Mnyika (Mb)
25 Machi 2015