Wednesday, February 27, 2013

NCHI IMEINGIA TENA KWENYE MGAWO WA UMEME, SERIKALI IELEZE WANANCHI UKWELI NA HATUA KUHUSU UDHAIFU KWENYE UTEKELEZAJI WA MPANGO WA DHARURA

Nchi imeingia tena katika mgawo wa umeme kinyume na ahadi iliyotolewa na Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo bungeni tarehe 28 Julai 2012. 

Hali hiyo ni matokeo ya Serikali kutozingatia tahadhari niliyoitoa bungeni tarehe 27 Julai 2012 kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani na kwa nyakati mbalimbali kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini juu ya hali tete iliyotarajiwa kuwepo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme. 

Ikiwa ni sehemu ya wajibu wa kibunge wa kuisimamia Serikali nawataka viongozi na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuacha kuficha hali ya mambo na kuwaeleza ukweli wananchi kuhusu mgawo wa umeme uliojitokeza na hatua za haraka zinazochukuliwa kurekebisha hali hiyo. 

Iwapo Wizara na TANESCO hawatatoa matangazo ya ukweli kwa wananchi, kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini nitaeleza vyanzo vya mgawo wa umeme uliojitokeza ili hatua ziweze kuchukuliwa wakati huu ambapo wajumbe wa kamati ya nishati na madini wenye wajibu wa kuisimamia Serikali kwa niaba ya Bunge katika sekta hizo nyeti hawajateuliwa.

Monday, February 25, 2013

Mnyika amuweka Maghembe kitanzini

NA RICHARD MAKORE

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, amemuweka katika wakati mgumu Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, baada ya kutoa hadharani namba ya simu ya waziri huyo ili wananchi wamuulize ni lini atatekeleza ahadi ya kuwapatia huduma ya maji wananchi wa jimbo hilo.

Mnyika alitoa namba ya simu ya Profesa Maghembe na Naibu wake, Dk. Binillith Mahenge, wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Goba mwisho na kuwataka wananchi kuwauliza viongozi hao wakuu wa Wizara ya Maji ni lini watapatiwa huduma ya maji ambayo imekosekana kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

Mnyika alisema Profesa Maghembe akihututubia wananchi hao aliwapa namba ya simu ‘feki’ na kwamba alifanya hivyo kutokana na kuwadharau.

Februari 17 mwaka huu, Profesa Maghembe akihutubia mkutano wa hadhara eneo la Goba mwisho alikaririwa akisema kwamba huduma ya maji ingeanza kupatikana Februari 20, mwaka huu, lakini hadi kufikia juzi ahadi hiyo haijatekelezwa.

Profesa Maghembe alikaririwa akisema serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiyo ina funguo za kufungua maji ama kuyafunga na kuwataka wananchi wa Kata ya Goba kumuamini kwamba Februari 20, mwaka huu wangepata maji.

Mnyika alisema ni aibu kwa Waziri akiwa na viongozi wa kitaifa wa CCM kutoa ahadi hewa na kwamba ataongoza maandamano makubwa ya wananchi wa jimbo lake kuvamia ofisi za Profesa Maghembe kwenda kudai maji.

Sunday, February 24, 2013

UFUMBUZI WA MADAI YA FIDIA MILIONI 278 KWENYE UJENZI WA BARABARA NA DARAJA GOLANI SUCA

Tarehe 19 Februari 2013 Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alifanya ziara ya kikazi katika kata za Kimara na Saranga kufuatilia kuhusu matengenezo ya barabara na daraja la Golani. 

Mnyika alifanya hivyo siku mbili tangu afanye mkutano wa kikazi na viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Kanuni na wananchi katika kata ya Mabibo tarehe 16 Februari 2013 kulitolewa malalamiko kuhusu Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) kutoshughulikia maombi ya wananchi yaliyowasilishwa kwa kampuni hiyo kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2010 mpaka 2012. 

Ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji huo kuhusu barabara, Mnyika alikutana na wananchi ambapo walipaswa kulipwa fidia inayokadiriwa kufikia shilingi milioni 278 ili kuruhusu njia mbadala kupatikana kufuatia ujenzi wa daraja katika eneo hilo. 

Aidha, Mbunge amekagua matumizi ya daraja hilo yaliyoanza kupitia njia ya zamani na athari zake katika mfumo mzima wa usafiri katika eneo husika; na kubaini kwamba daraja husika haliwezi kuzinduliwa pamoja na kuwa limeanza kukamilika mpaka ujenzi wa kingo za mito ukamilike pamoja na kupatikana kwa barabara mbadala baada ya wananchi kulipwa fidia. 

Mara baada ya ziara hiyo Mbunge alikutana na uongozi wa Manispaa ya Kinondoni na kuwasilisha madai hayo ya wananchi ambao miezi zaidi ya sita imepita toka nyumba zao ziwekewe X bila hata ya kufanyiwa tathmini. Baada ya Mnyika kuwawakilisha wananchi hao uongozi wa Manispaa umeamua kutuma timu ya uthamini na mara baada ya uthamini huo, kutuma uongozi kukamilisha majadiliano na wananchi husika kabla ya tarehe 25 Februari 2013. 

Saturday, February 23, 2013

Ziara Kimara: Ukaguzi ulipaji fidia, upanuzi wa barabara na kuhakiki ujenzi wa daraja!


Mbunge wa Ubungo, John Mnyika akizungumza na mkazi wa Kimara Korogwe, Richard Paul wakati mbunge huyo alipokutana na wakazi hao kutaka kujua fidia wanazotaka kulipwa kutokana na upanuzi wa barabara, pia alitembelea ujenzi wa daraja katika eneo hilo. 



Tuesday, February 19, 2013

BAADA YA HOJA BINAFSI NA KUSUDIO LA MAANDAMANO; WAZIRI WA MAJI NA MKUU WA WILAYA WAENDA GOBA NA MAENEO MENGINE KUFUATILIA MIRADI YA MAJI

Nitafuatilia ahadi alizotoa Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe tarehe 17 Februari 2013 kuwa maji yataanza kutoka kata ya Goba tarehe 20 Februari 2013 na ziara ya Mkuu wa Wilaya Jordan Rugimbana kwenye kata hiyo. 

Hata hivyo, ni vizuri umma ukatambua kuwa pamoja na mabadiliko ya hoja kwa kuongeza maneno ya kupendekeza hoja kuondolewa yaliyofanywa na Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe kinyume na kanuni za Bunge tarehe 4 Februari 2013, maelezo na hoja binafsi niliyowasilisha bungeni yameongeza uwajibikaji wa Waziri wa Maji, Mkuu wa wilaya ya Kinondoni na Halmashauri kuhusu masuala ya maji. 

Siku chache baada ya kutangaza tarehe 10 Februari 2013 kwenye mkutano wa hadhara kuipa Serikali wiki mbili, Mkuu wa Wilaya na Meya wa Halmashauri ya Kinondoni waliitisha mkutano na viongozi wa mitaa pamoja na kamati za miradi ya maji ya jumuiya na leo tarehe 18 Februari 2013 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Jordan Rugimbana ameanza ziara ya ufuatiliaji wa miradi ya maji katika Jimbo la Ubungo. 

Sunday, February 17, 2013

HALI TETE YA UPATIKANAJI WA MAJI JIJINI DSM; DAWASA NA DAWASCO WAWAJIBISHWE

Kwa nyakati mbalimbali kuanzia mwezi Januari mpaka Februari 2013 pametokea matatizo ya kuharibika kwa baadhi ya mitambo na kupungua kwa uzalishaji wa maji katika vyanzo vya mto Ruvu na hivyo kusababisha matatizo ya maji kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo yanayohudumiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) katika Mkoa wa Pwani. 

DAWASA imeingia mkataba wa uendeshaji na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO) wa kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kuendesha mitambo, kusimamia usambazaji wa maji na kufanya matengenezo na kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa. Aidha, DAWASCO wanapaswa kuzingatia mikataba ya huduma kwa wateja ambayo inaitaka kutoa taarifa kwa umma pale kunapotokea matatizo ya maji. 

Kwa kuzingatia mikataba hiyo, DAWASA na DAWASCO wanapaswa kutoa matangazo kwa umma kuhusu matatizo mapya yaliyojitokeza mwezi Januari na Februari 2013 ili kuepusha matatizo hayo kuhusishwa na hatua ya kuwasilishwa na kuondolewa bungeni kwa hoja binafsi niliyoiwasilisha tarehe 4 Februari 2013 juu ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam. 

Kwa wakazi wa Kibamba, Kwembe, Msigani, Mbezi, Saranga na Kimara ni muhimu wakatambua kwamba nimefuatilia na kujulishwa kwamba palikuwa na tatizo la kupungua kwa uzalishaji wa maji katika chanzo cha Ruvu Juu ambalo limerekebishwa tarehe 12 Februari 2013 hivyo maji yataendelea kupatikana kwa mujibu wa ratiba ya mgawo kama ilivyokuwa awali katika maeneo ambayo yalikuwa yakipata maji tangu mwaka 2012. 

Kwa wateja ambao bado watakuwa na matatizo katika maeneo yao wawasiliane na DAWASCO kupitia namba ya huduma kwa wateja 022 55 00 240 au 0779090904 au info@dawasco.com ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa. 

Monday, February 11, 2013

Sunday, February 10, 2013

Waraka wa Kwanza kwa mwaka 2013 wa Mbunge kwa Wananchi


“Maji; kwa Nguvu ya Umma”:

Waheshimiwa Wananchi wenzangu, Katiba ya Nchi pamoja na ubovu wake inatamka katika Ibara ya 63 (2) kwamba “Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba”.

Hata hivyo kutokana na uzembe wa uongozi wa Bunge wa kushindwa kuzingatia na upuuzi wa wabunge wengi wa CCM kuridhia hoja ya kuondolewa hoja yangu binafsi; Bunge limeshindwa kutimiza wajibu wake wa kuisimamia Serikali kuhusu hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es Salaam.

Katiba ya Nchi ibara ya 8 (1) inatamka kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii kwa hiyo wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa katiba.

Ibara hiyo inaendelea kueleza kwamba lengo kuu la serikali ni ustawi wa wananchi, Serikali itawajibika kwa wananchi na wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao kwa mujibu wa masharti ya katiba hii.

Kwa kuwa wananchi mmekoseshwa fursa ya kushiriki kupitia mwakilishi wenu niliyewasilisha hoja binafsi kwa kuzingatia wajibu wa kibunge na mamlaka ya madaraka ya Bunge kwa mujibu wa ibara ya 63 na 100 ya Katiba ya Nchi; kwa waraka huu naiwasilisha hoja binafsi yangu kwenu wananchi muijadili na kufanya maamuzi mtayoona yanafaa.

Monday, February 4, 2013

MAELEZO NA HOJA BINAFSI YA KUPENDEKEZA BUNGE LIJADILI NA KUPITISHA MAAZIMIO YA HATUA ZA HARAKA ZA KUBORESHA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA USHUGHULIKIAJI WA MAJI TAKA KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM KWA MUJIBU WA KANUNI YA 54 FASILI YA (1) YA KANUNI ZA KUDUMU ZA BUNGE TOLEO LA MWAKA 2007

Mheshimiwa Spika; 
Awali ya yote niungane na wote wenye mapenzi mapema katika kuomba ulinzi wa Mwenyezi Mungu wakati tukitimiza wajibu wa kibunge kwa mujibu wa ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania wa kuwawakilisha wananchi, kuisimamia serikali, kuidhinisha mipango na kutunga sheria.

Mheshimiwa Spika;
Aidha, kwa namna ya pekee ni kushukuru wewe binafsi na uongozi mzima wa Bunge kwa kunipa fursa hii adimu na adhimu ya kuwasilisha hoja binafsi kwa mujibu wa kanuni ya 54 fasili ya (1) ya kupendekeza bunge lijadili na kupitisha maazimio ya hatua za haraka zaidi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam.

Mheshimiwa Spika;
Maji ni uhai, hivyo matatizo ya upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam na nchini kwa ujumla kama hatua za haraka zisipochukuliwa yatageuka kuwa janga la taifa. Katika kila watanzania katika Jiji la Dar es Salaam na nchini; kwa wastani mmoja hapati huduma ya maji safi na salama na hali ni mbaya zaidi kuhusu ushughulikiaji wa maji taka.

Wakati baadhi ya nchi duniani zikielezwa kwenye kitabu cha hivi karibuni cha Mnukuzi Maalum wa Umoja wa Mataifa (UN Special Rapporteur) kuwa katika mwelekeo unaostahili kuhusu kuhakikisha haki ya maji na usafi wa mazingira (On the right track; Good practices in realizing the rights to water and sanitation: 2012), hali ni kinyume kwa taifa letu.

Ripoti ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia masuala ya maji (WaterAid: 2011) imeiweka Tanzania katika kundi la nchi ambazo haziko katika mwelekeo unaostahili wa kuboresha upatikanaji wa maji safi, ushughulikiaji wa maji taka na usafi wa mazingira (Policy Report: Off Track, Off Target; why investments in water, sanitation and hygiene is not reaching those who need the most).

Mheshimiwa Spika;
Hoja hii inalengo la kuibua mjadala wa hatua za haraka. Kimsingi hatua hizi za haraka hazitanufaisha Mkoa mmoja pekee kwa kuzingatia kuwa Mpango Maalum wa kutatua tatizo la maji katika Jiji la Dar es salaam ni kwa ajili pia ya maeneo mengine ya miradi iliyo sehemu ya mpango huo ya Morogoro mpaka Pwani. Aidha, kujadiliwa na kupitishwa kwa mapendekezo ya hoja hii kutaongeza pia msukumo wa miradi katika maeneo mengine ya mijini na vijijini katika mikoa mbalimbali nchini.

Shukrani zangu za dhati ziwafikie wabunge wenzangu wa vyama vya upinzani na wa chama tawala kwa maoni na mapendekezo yenu yaliyoniwezesha kuirekebisha hoja hii pamoja na ushauri wa Katibu wa Bunge Dr Thomas Kashillilah na maafisa na watendaji katika ofisi ya bunge, kambi rasmi ya upinzani na ofisi ya mbunge wa Jimbo la Ubungo mlioboresha hoja hii kwa manufaa ya Jiji la Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika;
Nitumie pia nafasi hii kuwashukuru Watanzania wenzangu wa kada, hadhi na ngazi mbalimbali katika taasisi na maeneo mengi ndani na nje ya nchi mnaoendelea kuniunga mkono kwa hali na mali katika kutimiza majukumu yangu ya kibunge na nafasi nyingine ninazozitumikia.

Nawashukuru sala zenu wakati wa kesi ya msingi na rufaa ya kupingwa kwa matokeo ya ushindi wetu Jimbo la Uchaguzi la Ubungo; kwa pamoja tumeshinda, tuendelee na kazi.

Aidha, pamoja na mjadala huu wa bungeni natarajia kupokea maoni na mapendekezo yenu kuhusu hoja hii kwa njia mbalimbali za mawasiliano ikiwemo kupitia mtandao wa http://mnyika.blogspot.com kwa hatua zaidi. Kaulimbiu yetu ni ile ile: AMUA; Maslahi ya Umma Kwanza.


MAELEZO YA HOJA: 

Mheshimiwa Spika;
Maji ni mojawapo ya mahitaji ya msingi ya binadamu, maji ni uhai. Upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ni sehemu ya muhimu ya maendeleo ya nchi na maisha ya wananchi. Maji ni lazima kwa matumizi ya majumbani, maji ni muhimu ni moja ya malighafi muhimu katika kazi za uzalishaji iwe ni za viwanda, kilimo, mifugo na shughuli zingine za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni nchi ambayo imejaliwa vyanzo vingi vya maji, vinavyohusisha mito, mvua, maziwa na bahari; kuwepo kwa vyanzo hivi vya maji ni wazi kuwa nchi yetu inaweza kuepukana na shida ya maji inayoikumba jamii ya Tanzania iwapo tutaondoa udhaifu uliopo. Aidha, udhaifu huo unahusisha pia kuziweka vyanzo vyenyewe pia mashakani kwa matendo ya binadamu yenye kuathiri endelevu wa matumizi hali itayozua migogoro katika siku za usoni iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

Friday, January 25, 2013

Salamu za Maulid na Barua ya wazi kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba

Nawatakia heri katika Maulid an-Nabi, ni siku ya kukumbuka kuzaliwa na maisha ya Mtume Muhammad (S.A.W)! Ifuatayo ni barua ya wazi kwa tume ya mabadiliko ya Katiba;


BARUA YA WAZI KWA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA 

Mwenyekiti, 

Tume ya Mabadiliko ya Katiba, 

Dar es Salaam 

Mheshimiwa, 

YAH: KUPANUA WIGO WA KUKUSANYA MAONI YA WANANCHI BINAFSI KWA SIMU ZA MKONONI NA MAKUNDI YA WANANCHI KATIKA MABARAZA YA KATIBA 

Nakuandikia nikirejea maelezo yako kwenye mkutano wako na waandishi wa habari tarehe 5 Januari 2013 kuhusu mchakato wa ukusanyaji maoni ya mabadiliko ya katiba. 

Maelezo uliyotoa yanadhihirisha upungufu katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi binafsi unaoelezwa kukamilika kwa kuwa na idadi ndogo ya watu waliotoa maoni mpaka sasa ambapo mpaka awamu nne zinakamilika jumla ya watu 318,223 tu ndio waliotoa maoni; kwa tafsiri yangu hii ni sawa na asilimia 0.7 ya wananchi wote zaidi ya milioni 44.9. 

Upungufu huo uko zaidi katika utoaji maoni kwa simu za mkononi ambapo kwa mujibu wa maelezo yako wananchi waliotoa maoni kwa njia hiyo ni 16,261 tu; kwangu mimi hii ni sawa na asilimia 0.08 ya idadi ya wateja wa makampuni ya simu za mkononi ambao watajwa kuwa zaidi ya milioni 20 (mobile phone subscribers).

Thursday, January 24, 2013

Nimemwandikia Spika Bunge liwezeshe ufumbuzi wa mgogoro wa gesi asilia

BUNGE LIINGILIE KATI KUWEZESHA UFUMBUZI WA MGOGORO WA GESI MTWARA. SPIKA ATUMIE MAMLAKA YAKE KUELEKEZA KAMATI ITAYOKUTANISHA SERIKALI NA WANANCHI. RAIS NA SERIKALI WAJISAHIHISHE NA KUONDOA UDHAIFU BADALA YA KUENDELEA KULAUMU NA KUPOTOSHA 

Nimemwandikia barua Spika atumie mamlaka na madaraka yake kutoa nafasi Bunge liingilie kati kuwezesha ufumbuzi wa mgogoro unaoendelea kati ya Serikali na wananchi kuhusu utafutaji, uvunaji, usafirishaji na utumiaji wa gesi asilia kutoka Mtwara.

Katika hatua ya sasa Serikali ni kupitia Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake ni sehemu ya watuhumiwa na washutumiwa hivyo ni muhimu majadiliano kati ya Serikali na wananchi kuwezesha ufumbuzi wa mgogoro huo yakasimamiwa na muhimili mwingine kwa dola.

Rais naye tayari ameshachukua upande bila kusikiliza kwa kina na kuyaelewa madai ya wananchi hivyo katika hali ya sasa ni muhimu kurejea katika madaraka na mamlaka ya wabunge kwa mujibu wa katiba ya nchi kuwezesha ufumbuzi wa mgogoro huu kuepusha hali tete inayoweza kuzuka na kuathiri uchumi na usalama katika maeneo husika.

Katiba ya Nchi Ibara ya 63 (2) inaelekeza kwamba sehemu ya pili ya Bunge (inayoundwa na wabunge) itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba.

Monday, January 21, 2013

SPIKA ASILINDE UFISADI KIWANDA CHA URAFIKI NA WAZIRI KIGODA ASIKWEPE KUTOA MAJIBU

Tarehe 21 Januari 2012 gazeti la Tanzania Daima limemnukuu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda na Biashara akieleza kuwa wameunda Kamati Ndogo ya Uchunguzi kuhusu ufisadi wa miaka mingi wa Kiwanda cha Nguo cha Urafiki lakini wanasubiri idhini ya Spika kamati hiyo ianze kazi. Habari hiyo imeeleza kuwa Spika ndiye anayekataa uchunguzi huo kufanyika.

Nikiwa mbunge wa Jimbo la Ubungo, mahala kilipo Kiwanda cha Urafiki nasisitiza umuhimu wa Spika kutoa kauli kwa umma kuhusu hatua alizochukua ikizingatiwa kwamba hata kabla ya kamati ndogo ya uchunguzi kuundwa nilishawasilisha kwa Spika wa Bunge maelezo binafsi kuhusu ufisadi huo na mpaka sasa hajatoa idhini yashughulikiwe.

Aidha, majibu ya Waziri wa Viwanda na Biashara Dk Abdalah Kigoda kuwa anafuatilia suala hilo Wizarani hayajitoshelezi kwa kuzingatia kuwa zaidi ya nusu mwaka umepita toka atoe ahadi ya kufuatilia Wizarani; wafanyakazi wa Urafiki na wananchi kwa ujumla wanachohitaji kuelezwa ni hatua zilizochukuliwa mpaka sasa.

Sunday, January 20, 2013

HOTUBA YA JOHN MNYIKA (MB) ALIYOITOA TAREHE 20 JAN, 2013 KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO WA BARAZA LA WANAWAKE WA CHADEMA (BAWACHA) JIMBO LA UBUNGO ULIOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA MATUNGUCHA KATA YA SARANGA

Viongozi wa BAWACHA Taifa,

Waheshimiwa Wabunge wa viti maalum,

Viongozi wa CHADEMA Jimbo la Ubungo,

Viongozi wa BAWACHA Jimbo la Ubungo,

Waheshimiwa Madiwani wa kata na viti maalum,

Viongozi wa BAWACHA toka kata zote za Jimbo la Ubungo.

Niungane nanyi katika kumshukuru Mungu kwa kutupa uzima na kuendelea na kazi katika mwaka mpya wa 2013. Kwa wale ambao hatujakutana mwezi huu wa Januari, nitumie fursa hii kuwatakia mwaka mpya mwema wenye upendo na uwajibikaji.

Nawashukuru kwa kunialika kuzungumza machache kwenye Mkutano huu wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) Jimbo la Ubungo na niwapongeze waandaaji kwa kuweza kuwakutanisha pamoja viongozi kutoka kata zote na wawakilishi wa wanachama kutoka katika matawi na misingi na BAWACHA katika mitaa mbalimbali ya Jimbo la Ubungo.

Mwezi Disemba 2012, CHADEMA taifa kiliutangaza 2013 kuwa ni mwaka wa ‘nguvu ya umma’. Kufuatia tamko hilo la Kamati Kuu, viongozi mbalimbali wa CCM walianza propaganda chafu kupitia vyombo vya habari kuwa CHADEMA imetangaza mwaka wa ‘vurugu’.

Propaganda hizo zinalenga kutisha umma, hususan wanawake wasiunge mkono vuguvugu la mabadiliko (M4C), kujiunga kwenu kwa wingi katika Jimbo la Ubungo kunadhihirisha kuwa wanawake hamko tayari kudanganywa kwa siasa chafu na mnaendelea kuiunga mkono CHADEMA; asanteni sana.

Saturday, January 19, 2013

Ziara Jimboni: KATA YA MANZESE 08 Desemba, 2012

Ziara ndani ya Jimbo: muendelezo wa kutembelea maeneo mbalimbali ya jimboni. Jana, Desemba 08, 2012 ziara kubwa ilifanyika katika kata ya MANZESE.

Ziara ilimudu kutembelea ofisi ya kata (Kilimani), kufungua misingi katika mitaa ifuatayo; Kilimani, Chakula bora, Mvuleni, Midizini, Mwembeni, na Mnazi Mmoja.

Kisha mkutano wa hadhara na wananchi wa mtaa wa Mnazi Mmoja.


Shirika la Umeme (TANESCO) linakabiliwa na ufisadi na uzembe unaoongeza gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme kwa upande mmoja na uendeshaji wa shirika kwa upande mwingine. Ufisadi na uzembe huo unapunguza uwezo wa TANESCO kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na unaongeza gharama na bei ya upatikanaji wa umeme hali inayoathiri uchumi wa nchi na maisha ya wananchi kwa kuchangia katika mfumuko wa bei na ongezeko la gharama za maisha. Mzigo wa ufisadi na uzembe katika TANESCO unajitokeza zaidi katika mikataba mibovu pamoja na ukiukwaji wa sheria za ununuzi wa umma, ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63 sehemu ya pili ya bunge (inayoundwa na wabunge) ndio chombo kikuu chenye madaraka na mamlaka kwa niaba ya wananchi ya kuisimamia serikali. Hata hivyo, katika kipindi cha kati mwaka 2008 mpaka 2012 maazimio ya Bunge kuhusu sekta ya nishati ikiwemo kuhusu umeme yamekuwa hayatekelezwi kwa wakati na kwa ukamilifu hali inayofanya tuhuma za ufisadi na uzembe kuendelea kujirudiarudia. Katika muktadha huo, ni muhimu kwa kuwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi ibara ya 8 madaraka na mamlaka ni ya umma (serikali inafanya kazi kwa niaba tu) ipo haja ya kuanza kuunganisha ‘nguvu ya umma’ katika kushinikiza hatua kuchukuliwa kwa wahusika wa ufisadi na uzembe ili kuweka misingi bora ya uwajibikaji katika sekta ya nishati.

Friday, January 18, 2013

Rais na Mawaziri wanadharau wabunge kuhusu mabadiliko ya mzunguko wa Bajeti

Yaliyojiri na yanayoendelea kujiri ndani ya Baraza la Mawaziri na Wizara ya Fedha kuhusu mabadiliko ya mzunguko na mchakato wa bajeti yanaashiria kwamba Rais na Serikali wanadharau mamlaka na madaraka ya Bunge na wabunge.

Aidha, kutokana na umuhimu wa mzunguko na mchakato wa bajeti katika kuwezesha uwajibikaji kwenye mapato na matumizi ya rasilimali za umma; Waziri wa Fedha anatakiwa aweke wazi kwa umma mabadiliko hayo yaliyofanyika ili wananchi na wadau waweze kutoa maoni na Bunge liweze kuyazingatia wakati wa marekebisho ya kanuni za Bunge yanayotarajiwa kufanywa katika mkutano wa kumi wa Bunge.

Wakati Katibu wa Bunge amenukuliwa tarehe 17 Januari 2013 akisema kwamba pendekezo la mabadiliko ya mzunguko na mchakato wa bajeti bado linajadiliwa na kwamba iwapo litaafikiwa, uamuzi utatangazwa mapema mwezi ujao (Februari 2013) wakati wa mkutano wa Bunge; upande wa Rais na Wizara ya Fedha wameshapitisha na kuanza kutekeleza mzunguko na mchakato mpya wa bajeti kuanzia mwezi Disemba 2012.

Tuesday, January 15, 2013

Sera ya majimbo ni siri ya maendeleo ya nchi na wananchi

Na John J.Mnyika

Mwaka 2007 miaka miwili baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 palijitokeza mjadala kuhusu sera ya majimbo. Mwaka 2012 ikiwa ni miaka miwili tena toka uchaguzi wa mwaka 2010 pameibuka kwa mara nyingine mjadala kuhusu sera ya majimbo kufuatia maandamano ya wananchi wa Mtwara juu ya madai ya gesi. Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospter Muhongo amenukuliwa na gazeti moja tarehe 29 Disemba 2012 akiponda sera ya majimbo ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa ni mbovu na haitumiki kokote duniani; kauli ambayo haina ukweli kama nitavyoeleza katika makala hii. Amedai madai ya rasilimali za wananchi wa eneo hayana msingi na kuwaita wote wenye kujenga hoja hiyo kuwa wanataka kuigawa nchi vipande vipande, majibu ambayo ni mwendelezo wa propaganda chafu.

Prof. Muhongo badala ya kujibu hoja za waandamanaji na wananchi wa Mtwara ameamua kuibua ‘vioja’ vya kuishambulia CHADEMA na sera yake ya majimbo. Wakati hata kwa sera za CCM na serikali ya sasa, maandamano ya wananchi wa Mtwara kutaka majibu toka kuhusu manufaa ya miradi ya gesi asili inayotoka katika maeneo yao ni matokeo ya madai ya ufisadi wa baadhi ya viongozi na udhaifu wa Serikali katika kuushirikisha umma katika michakato ya maamuzi ya kisera na kitaasisi kuhusu rasilimali na miradi muhimu ya maendeleo. Aidha, ni matokeo pia Bunge kutokuisimamia kikamilifu Serikali kwa niaba ya wananchi kwa mujibu wa ibara ya 63 ya katiba wakati serikali inapoacha kufafanua masuala yanayohojiwa na wabunge na inapokwepa kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu sekta ya nishati ikiwemo sekta ndogo ya gesi asili.

Saturday, January 5, 2013

Nimewasilisha Muswada Binafsi wa Sheria ya kuunda Baraza la Taifa la Vijana


Jana tarehe 4 Januari 2012 niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge taarifa ya muswada binafsi wa Sheria ya kuunda Baraza la Taifa la Vijana (The National Youth Council Bill, 2013) kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (1) na Taarifa ya Muswada huo kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007).

Nimechukua hatua hiyo kwa kuwa kwa miaka zaidi ya kumi Serikali imekuwa ikiahidi karibu kila mwaka bungeni kuwa itawasilisha muswada wa kuunda baraza la vijana la taifa lakini haijawahi kutekeleza ahadi hiyo; nimeamua kuitekeleza ahadi hiyo kwa kupeleka bungeni muswada binafsi wa kuunda baraza la vijana la taifa.

Katika taarifa hiyo ya muswada nimewasilisha madhumuni, sababu pamoja na nakala ya muswada wenyewe wa sheria ya kuanzisha Baraza la Vijana la Taifa kwa madhumuni ya kuanzisha chombo cha kuwaratibu vijana wa Tanzania katika kutekeleza shughuli zao kijamii, kuuchumi, kiutamaduni na kimichezo, na kuchagiza hali ya utambulisho wa Kitaifa wa pamoja na uzalendo.

Friday, January 4, 2013

Washindi wa Shindano la Ujasiriamali Jimbo la Ubungo wapatikana

Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo kwa ushirikiano na shirika la Maendeleo Ubungo; Ubungo Development Initiative (UDI) waliendesha shindano la kuwainua wajasiriamali wadogo wadogo na hususan vijana wasio na ajira (na walio katika mazingira magumu) kwa kuwataka kuandaa mchanganuo namna gani watatumia Tsh 200,000/- katika kuanzisha au kuiendeleza biashara zao. Washindi waliopatikana ni;
Mshindi wa Kwanza: Joseph R. Shindo (22) kutoka Kata ya Kimara Tsh 200,000/-

Thursday, January 3, 2013

Hatua kuhusu matumizi ya dola milioni 164.6 za “mabomba ya mchina” na mikataba ya miradi ya sasa ya maji jijini Dar es salaam

Tarehe 3 Januari 2013 kwa kutumia kifungu cha 10 cha sheria ya haki, kinga na madaraka ya Bunge nimetaka Wizara ya Maji inipatie nakala ya ripoti ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotekelezwa kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 jijini Dar es salaam.

Nimetaka ripoti hiyo ili kubaini matumizi ya dola milioni 164.6 zinazoelezwa kutumika katika mradi huo maarufu kama wa ‘mabomba ya mchina’ kwa kuwa mpaka sasa mwaka 2013 sehemu kubwa ya mabomba yaliyowekwa wakati wa mradi huo katika Jiji la Dar es salaam hayatoi maji huku kukiwa na upungufu katika uzalishaji, upotevu wakati wa usafirishaji, udhaifu katika usambazaji na tuhuma za ufisadi katika matumizi.

Pamoja na kutaka ripoti ya utekelezaji wa mradi huo, nimetaka pia nakala ya ripoti ya ukaguzi wa kiufundi (technical Audit) uliofanywa na kampuni ya Howard Humphreys kuhusu mradi huo.

Nimetaka pia kupatiwa ripoti za ukaguzi uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Kampuni ya Maji Dar es salaam- DAWASCO (Dar es salaam Water Supply and Sewerage Company) na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka-DAWASA (Dar es Salaam Water Supply and Sewerage Authority) kwa mwaka miaka mitatu ya 2009/10, 2010/2011, 2011/2012 ili kuweza kufuatilia hatua zinazostahili kuchukuliwa.