Wednesday, November 27, 2013

Taarifa kwa umma kuhusu serikali kupandisha bei ya umeme

Gazeti la Tanzania Daima Toleo na. 3280 la tarehe 26 Novemba 23 limenukuu kauli iliyotolewa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini George Simbachawene wakati akizungumza na kipindi cha Kumepampazuka kilichorushwa na Redio One juu ya Serikali kupandisha bei ya umeme kama Shirika la Umeme (TANESCO) lilivyoomba.

Katika habari hiyo Simbachawene amenukuliwa akisema kwamba endapo kuna mwananchi yeyote atakayeona gharama za umeme ni kubwa ni vema akaamua kuwasha kibatari au akae giza. 

Rais Jakaya Kikwete anapaswa kumwagiza Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospter Muhongo kuwaomba radhi wananchi kwa kauli hiyo iliyotolewa na Naibu Waziri Simbachawene kwa niaba ya wizara anayoiongoza.

Aidha, ni vyema Rais Kikwete kwenye hotuba yake kwa taifa ya mwisho wa mwezi huu akawaeleza wananchi iwapo uamuzi huo wa kupandisha kwa mara nyingine bei ya umeme ndio utekelezaji wa ahadi ya maisha bora aliyoitoa kwa watanzania kuanzia kwenye uchaguzi wa mwaka 2005.

Hii ni kwa sababu kupandisha bei ya umeme kuna athari ya kuchangia katika ongezeko la gharama na ugumu wa maisha kwa kuwa shughuli za uzalishaji na maisha ya kila siku zinategemea kwa kiwango kikubwa nishati.

Thursday, November 21, 2013

Mgao wa umeme na uongo nyuma yake!

Mgawo huu wa umeme ni wa ufisadi wa kimikataba Songosongo/PAT na udhaifu wa Mpango wa Dharura wa Umeme; Bungeni Muhongo alinijibu uongo.

Mgawo wa Umeme ufisadi wa PAT na udhaifu wa ukarabati wa visima ulijulikana toka Julai na Novemba 2011; Prof Muhongo alisema uongo kuficha.

Trilioni 1 ilitumika kuficha uongo wa Prof Muhongo Mgawo wa Umeme kwenye manunuzi ya mafuta mazito; Ufisadi, PAT, visima, gesi umemshinda.

MgawowaUmeme Prof Muhongo alisema uongo mara 2 bungeni; 1. 28 Julai 2012 baada ya kumhoji kwenye hotuba 27 Jul http://mnyika.blogspot.com/2012/07/hotuba-ya-kambi-rasmi-ya-upinzani.html

Uongo wa mara ya 2 wa Prof Muhongo bungeni kuhusu MgawowaUmeme ni wa Mei 23 nilipohoji baada ya hotuba ya 22 Mei: http://mnyika.blogspot.com/2013/05/hotuba-ya-msemaji-wa-kambi-rasmi-ya.html

Halafu kwa maagizo ya IMF/WB wanataka kupandisha bei ya umeme kufidia ufisadi kukodi mitambo ya dharura/ununuzi mafuta na mikataba mibovu.

Thursday, October 24, 2013

Wednesday, October 16, 2013

Ujenzi wa Kisima cha Maji Safi-Msigani!


Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika alipotembelea ujenzi wa kisima cha maji kilichojengwa katika mtaa wa Msigani, Kata ya Msigani, ujenzi wa kisima hicho umechangiwa na fedha za mfuko wa jimbokiasi cha Tsh 3.5 milioni katika kumalizia ujenzi huo.

Thursday, September 12, 2013

Mnyika ahoji ziliko fedha za DECI

na Shehe Semtawa

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amemtaka Gavana wa Benki Kuu, Benno Ndulu, kuwaeleza waliokuwa wanachama wa Kampuni ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI) fedha zao zilizotaifishwa na serikali kutoka kwenye taasisi hiyo ziko kwenye akaunti gani.

Mnyika alisema kuwa wakati sakata la DECI linaanza mwaka 2009, serikali ilitaifisha jumla ya sh bilioni 19, sawa na asilimia 40 ya fedha zote ambazo wanachama wa taasisi hiyo iliyokuwa ikiendesha na kusimamia mchezo wa upatu walikuwa wakidai.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara juzi Mtaa wa Mavurunza, Kata ya Kimara baada ya kuulizwa swali na mmoja wa wananchi aliyetaka kujua hatima ya fedha zao, Mnyika alitoa tahadhari kuwa danadana inayotaka kufanywa na serikali inaweza kutia shaka kuwa fedha hizo hazipo.

”Sasa naomba nimjibu yule mwananchi aliyetaka kujua hatima ya fedha za DECI. Mtakumbuka hili suala nimekuwa nikitaka majibu yake bungeni, lakini kila mara wanatumia kisingizio kuwa suala hili liko mahakamani.

Tuesday, September 10, 2013

Mnyika: Serikali imalize tatizo la maji

na Abdallah Khamis

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika, ameitaka serikali kuhamisha nguvu na kasi zilizotumika katika ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kuelekea jijini Dar es Salaam na kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi hususan katika Jimbo la Ubungo.

Mnyika alitoa kauli hiyo juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Kimara, Mtaa wa Mavurunza na kusisitiza hakuna suala muhimu kama maji kwa wananchi na kwamba kunahitajika ufumbuzi wa muda mfupi na mrefu, ikibidi kwa hali ya dharura.

Alisema kama serikali inaweza kutumia muda mfupi kujenga na kutandaza bomba hilo kwa nini ishindwe kufanya hivyo kwa mabomba ya maji, ambayo ni uhai wa wananchi.

“Tunaendelea kupambana kuhakikisha tatizo la maji tunalipunguza na kuliondoa kabisa, ninachowaomba ni sauti zenu na mshikamano wenu, suala hili ni uhai wa watu, kama maji ni tatizo maana yake uhai wa binadamu uko shakani,” alisema Mnyika.

Wednesday, August 28, 2013

Uzinduzi wa Kampeni ya Kuchangia Maabara na Madawati chini ya Shirika la UDI



Mhe. John Mnyika akishirikiana na Mratibu John Mallya kuonyesha bango lenye ujumbe wa harambee ya kuchangia maabara na maktaba iliyozinduliwa Agosti 21, 2013

Thursday, August 15, 2013

Leo Agosti 15, 2013: Sengerema na Mwanza Mabaraza ya wazi ya Katiba Mpya

Sengerema: Endeleeni kutoa maoni kwa maneno na maandishi kwenye baraza letu la katiba linaloendelea uwanja wa Wenje kata ya Nyamburukano

Mwanza: Baraza la wazi la Jiji likijumuisha pamoja Wilaya za Ilemela na Nyamagana litaanza saa 9 alasiri Uwanja wa Magomeni kata ya Kirumba.

Mwenyekiti Mbowe na mimi tutashiriki katika michakato hiyo.

Maslahi ya Umma Kwanza!!

Monday, August 12, 2013

Leo Agosti 13, 2013 Busega, Maswa, Meatu, na Bariadi; tukutane tushiriki mabaraza ya wazi ya katiba.

Leo Agosti 13, 2013 Busega, Maswa, Meatu, na Bariadi; ni kushiriki kikamilifu baraza la wazi la katiba. Mwenyekiti Mbowe na mimi tutajumuika nanyi kupitia rasimu ya katiba mpya.

Busega: Baraza la wazi la katiba leo litaanza saa 3 asubuhi.

Maswa: Wanachana na wapenzi hudhurieni baraza la wazi la katiba kuanzia saa 5 kamili

Meatu: mtaanza baraza la wazi la katiba saa 7 mchana. Wanachama na waalikwa mkifika anzeni kutoa maoni yenu juu ya rasimu; tuko pamoja!

Bariadi: ni haki na wajibu kushiriki baraza la wazi la katiba leo tarehe 13 Agosti kuanzia saa 9 alasiri.

Shime tushiriki kikamilifu na kuitumia fursa hii kwa maslahi ya taifa letu.

Thursday, August 8, 2013

Salamu za Eid-Al-Fitr na kutembelea kata ya Malamba Mawili!

Saa 5 mpaka 8 mchana nitakuwa pamoja na viongozi wenzangu Malamba Mawili (Eneo la Stendi Mwisho). Tutagawa zawadi kwa watoto pamoja na kutoa salamu za Eid-Al-Fitr. Tutasambaza nakala za rasimu ya katiba mpya vijiweni na kwa wawakilishi wa makundi ya kijamii yenye malengo yanayofanana.

Tunaanza muda huo ili kuheshimu wajib wa salaat ya Eid na sunnah ya khutbah asubuhi. Imekuwa ni kawaida kwa siku ya Eid kuwa pia ni wasaa kwa kusikiliza hotuba juu ya wajibu kwa Allah lakini pia kwa binadamu wengine. Ni wakati wa ummah kukumbushwa masuala muhimu katika jamii. Tunamaliza mapema kutoa fursa ya mikusanyiko mingine.

Nitazungumza na umma kuhusu mchakato wa katiba na kutoa pia mrejesho juu ya masuala ya maendeleo ikiwemo juu ya ujenzi/matengenezo ya Barabara ya Kinyerezi-Malamba Mawili Mbezi, kuhusu maji na juu ya masuala mengine muhimu ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Kwa wakazi wa maeneo jirani yanayozunguka Malamba Mawili ya Kifuru, King’azi, Msingwa, Msigani na mengineyo mnaweza kuja kujumuika nasi. 

Kwa maelezo zaidi na maelekezo naomba muwasiliane na Ali Makwilo 0715/0784691449.

Eid Mubarak!

Kwa mkazi wa Kisopwa, Sinza, Manzese, Mbezi Makabe, Malambamawili, Mshikamano au Msigani; naomba usome hapa na kunipa mrejesho juu ya ardhi na mipango miji

Tarehe 12 Julai 2012 katika mchango wangu bungeni ikiwa ni sehemu ya wajibu wa kuwawakilisha wananchi na kuisimamia Serikali niliitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na mambo mengine:

Itatue mgogoro kati ya Manispaa ya Kinondoni na Halmashauri ya Kisarawe kuhusu wananchi wa Kisopwa na Mloganzila kuitwa kwamba wako Kisarawe badala ya Kinondoni.

Ichukue hatua juu ya maeneo ya wazi/umma yaliyovamiwa katika kata ya Sinza ambapo mabango yamewekwa, muda wa notisi umeisha lakini majengo bado yapo.

Imtaje wazi mwendelezaji mwenza wa Mji wa kiungani (satellite town) wa Luguruni, masharti ya mkataba na lini uendelezaji unaanza.

Itoe nakala ya mipango ya uendelezaji upya kata ya Manzese.

Iharakishe mipango ya uhakiki na urasimamishaji katika maeneo ya Mbezi Makabe, Malamba Mawili, Mshikamano na Msigani.

Mwaka mmoja umepita, kuna mambo nimepewa na majibu na kazi imefanyika na kuna masuala bado.

Mkazi wa Mabibo na maeneo jirani nakutaarifu kuwa nitahutubia mkutano wa hadhara kwenye eneo la Sahara leo siku ya 8/8 kuanzia saa 9 alasiri mpaka 11 jioni ulioandaliwa na chama. Njoo na waalike na wengine.

Mkutano huo una malengo matatu: Mosi; kuwasilisha mrejesho wa kazi jimboni za utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyogharamiwa na Mfuko wa Jimbo katika maeneo yenu.

Pili; nitafanya kazi ya kuuchambua mchakato wa mabadiliko ya katiba unaoendelea ikiwemo kuhusu rasimu ya katiba mpya.

Tatu; kupokea maoni/mapendekezo ya masuala muhimu ya kuyazingatia katika kazi ya kuwawakilisha wananchi kwenye vikao vya kamati za Bunge vinavyoanza wiki ijayo na Mkutano wa Bunge unaoanza mwishoni mwa mwezi huu.

Itakumbukwa kwamba tarehe 21 Julai 2013 nilitaka kutimiza azma hiyo kwenye eneo tajwa lakini Jeshi la Polisi lilizuia mkutano kwa maelezo yasiyokuwa ya kweli kwamba kulikuwa na ziara ya Makamu wa Rais katika Jimbo la Ubungo.

(Msaidizi katika Ofisi yangu ameeleza hapa kwa kirefu: http://www.youtube.com/watch?v=VyHF5O-P-Vk&feature=c4-overview&list=UUs0TcFkgqs2OYd6x5E68nhg ).

Nitashiriki kwenye Iftar nyumbani kwa Marehemu Mbwana Masoud Makurumla leo 8/8 jioni; wasiliana na Aziz (OMU) 0784/0715-379542 kutuunga mkono kwa hali na mali. Ramadan Kareem.

Kwa ndugu zangu na wenzetu waislamu, ni siku ya 30 ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadan. Siku ya 30 ni kati ya siku kumi za mwisho za mfungo ambazo wapo wanaomini kwamba usiku ni siku ya “usiku wa nguvu”. Siku na usiku ambao Mtume Muhammad (SAS) alipokea ufunuo wa kwanza wa Q’uran yaani Laylat al-Qadr.

Katika siku hii ya 30 nitaungana pamoja na familia ya Marehemu Mbwana Masoud, majirani zake wakazi wa Kata ya Makurumla na wengine mtakaojumuika nami katika Iftar nyumbani kwa familia ya marehemu . Jioni tutaanza na tende na futari itafuata baada ya swala ya maghrib.

Marehemu Mbwana Masoud alikuwa ni mmoja wa wanachama wa CHADEMA walijitolea kusafiri kwenda Igunga kwa ajili ya kuwa wakala kwenye uchaguzi uliofanyika tarehe 2 Oktoba 2011.

Monday, July 29, 2013

Hali tete na tata ya kituo cha mabasi cha Ubungo (UBT)- Hatua ambazo nimeanza kuzichukua

Katika siku za karibuni nimepokea malalamiko kuhusu hali tete na tata katika Kituo cha Mabasi cha Ubungo (UBT) kinachosimamiwa na kuendeshwa na Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam. 

Kufuatia malalamiko hayo, nimechukua hatua zifuatazo mpaka sasa: Mosi, tarehe 15 Julai 2013 nilifanya ziara ya ghafla kujionea hali halisi, sehemu ya ziara hiyo inaweza kutazamwa kupitia: 
http://www.youtube.com/watch?v=JuPGoz-JI-I , ambapo nilibaini kwamba hatua za haraka zinahitajika. 

Nimeshuhudia hali ya uchafu ikiwemo utiririkaji wa maji machafu ndani ya Kituo cha Mabasi ambayo yanatuama na hadi kubadilika rangi na kuwa ya kijani ambapo ni hatarishi kwa abiria na watu wanaofanya shughuli zao ndani ya kituo. Pia, kuna vyoo vichache ukilinganisha na idadi ya abiria na watumiaji wengine wa Kituo. Hali hiyo inaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko.

Nimejulishwa hali ya usalama ndani ya kituo ni tete; usalama ndani ya kituo ni mdogo sana kwa abiria na nimepewa taarifa za matukio ya uhalifu ambayo yamesababisha pia madhara kwa abiria.

Nimetembelea kituo na kukuta kuna usumbufu mkubwa sana kwa abiria na watumiaji wengine wa Kituo baada ya maeneo ya awali ya kupumzikia kwa abiria na wasindikizaji kubomolewa. 

Thursday, July 25, 2013

Chenge (Mb) amesema kodi ya kadi za simu (SimCardTax) ni sahihi kwa utafiti wao; aulizwe kupitia 0754782577 atoe maelezo zaidi na vielelezo vya ziada

Leo tarehe 25 Julai 2013 chombo kimoja cha habari kimemnukuu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Andrew Chenge (Mb) akisema kwamba uamuzi kuhusu kodi/tozo ya kadi/laini za simu haukuwa wa kubahatisha. Chenge amesema kwamba kamati yake ilifanya utafiti wa kina na kisha kufikia uamuzi wa kuona tozo hiyo ni sahihi.

Ni muhimu akatakiwa kupitia namba yake 0754782577 atoe maelezo zaidi kuhusu usahihi wa tozo hiyo na aeleze ni wapi wananchi na wadau mbalimbali wanaweza kupata vielelezo vya utafiti walioufanya.

Aidha, wenye maswali kuhusu nini hasa kilijiri kwenye kamati ya bajeti mpaka kamati hiyo ikakataa jedwali la marekebisho nililowasilisha tarehe 27 Juni 2013 kabla ya muswada wa sheria ya fedha kupitishwa bungeni tareheb 28 Juni 2013 kwa kuwa yeye ambaye ndiye msemaji wa kamati ameanza kutoa majibu. 

Pia, aeleze iwapo yupo tayari kumshauri Spika aruhusu kamati ya bajeti ikutane kwa dharura wiki ijayo kufanya kazi ya kupitia matumizi ya Serikali kwa lengo la kuanisha maeneo ambayo Serikali inaweza kubana matumizi kwa haraka kufidia pengo la bilioni 178 zinazotafutwa kwenye tozo hiyo ya simu. Hatua hii itawezesha kodi hiyo kuacha kutozwa bila ya kulazimika hata kuongeza vyanzo vingine vya fedha iwapo Serikali inasuasua kupanua wigo wa mapato.

Friday, July 19, 2013

Kufuatia kauli za Serikali magazetini kuhusu mimi na kodi ya umiliki wa kadi za simu; nijibu tu kwa ujumla kwamba SITAACHA. Badala yake naomba kuwapatia namba zao: Makamba 0767783996 na Mgimwa 0754/0684765644, tunachohitaji ni kauli ya Serikali kuwa kodi imesitishwa na itaondolewa na sio siasa chafu.

Kwa mliotaka msimamo wangu juu ya kauli ilinukuliwa jana tarehe 18 Julai 2013 na Gazeti la Majira kwamba Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Januari Makamba kwamba; “Mnyika anaangalia upepo unakoelekea, akiona watu wanalalamika ndipo anaongea namsihi aache kufanya siasa katika jambo hili”, naomba kutumia mtandao huu kutoa majibu ya ujumla kwa maswali na masuala yote kama ifuatavyo:

Nieleze kwamba sitaacha kufanya siasa kwenye jambo hili mpaka kodi hiyo itakapofutwa kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kubaki na fedha walau kidogo kwa maendeleo.

Sitaacha kufanya siasa kwa sababu ndio kazi yangu ambayo wananchi walinichagua kuifanya ya kuwawakilisha na kuisimamia Serikali ambayo yeye Makamba ni sehemu yake. Sitaacha kufanya siasa kwa sababu Mwalimu Nyerere alisema ili nchi yetu iendelee inahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Ambacho sitafanya ni siasa chafu kama hizo ambazo Makamba amefanya za kusema uongo, kwa kuwa naamini anafahamu kabisa kwamba sijaanza kuongea kuhusu suala hili baada ya malalamiko ya wananchi bali jambo hili nilianza kulishughulikia bungeni mara baada ya Waziri wa Fedha kuwasilisha jedwali la marekebisho la kuanzisha kodi lukuki za simu ikiwemo hii. Katika mchango wangu bungeni, nieleza kwamba muswada huo wa sheria ya fedha kwa kupandisha kodi kwenye mafuta na simu ni ‘muswada wa majanga ya kuwaongezea mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi.

Wednesday, July 17, 2013

Kodi ya kadi ya simu (SimcardTax): Maoni ya awali ya wananchi juu ya hatua za kuchukuliwa

Nawashukuru kwa maoni ambayo mmenitumia kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa kufuatia kuanzishwa kwa ushuru wa bidhaa kwa kadi za simu (sim card) kwa wamiliki wa simu za kiganjani/mkononi.

Bado naendelea kuchambua maelfu ya maoni yaliyotolewa katika mijadala na niliyotumiwa kwa barua pepe. Nitoe mrejesho wa awali kwamba kwa muktasari mapendekezo niliyoyachambua mpaka sasa yanapendekeza hatua zifuatazo kuchukuliwa:

Monday, July 15, 2013

Mnyika aponda sera za michezo za CCM

Na Mwandishi Wetu

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika amesema ukosefu wa maandalizi ya mapema katika micheo kunatokana na sera za Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndiko kunakoibua matokeo mabovu katika sekta hiyo hususan kwa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars.

Mnyika ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, aliyasema hayo jana wakati akizindua michuano ya Mama Kevin Cup kwenye viwanja vya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Chang’ombe (DUCE), jijini Dar es Salaam.

Mnyika alisema katika ilani ya uchaguzi ya Chadema 2010, waliahidi masualaya michezo hususan Tanzania kucheza fainali za Mataifa ya Afrika na Kombe la Dunia Brazil mwakani endapo wangekabidhiwa cnchi, lakini kutokana na baadhi ya maeneo kutowataka waingie serikali mpya, hayo yameshindikana chini ya sera mbovu za CCM.