Thursday, August 8, 2013

Nitashiriki kwenye Iftar nyumbani kwa Marehemu Mbwana Masoud Makurumla leo 8/8 jioni; wasiliana na Aziz (OMU) 0784/0715-379542 kutuunga mkono kwa hali na mali. Ramadan Kareem.

Kwa ndugu zangu na wenzetu waislamu, ni siku ya 30 ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadan. Siku ya 30 ni kati ya siku kumi za mwisho za mfungo ambazo wapo wanaomini kwamba usiku ni siku ya “usiku wa nguvu”. Siku na usiku ambao Mtume Muhammad (SAS) alipokea ufunuo wa kwanza wa Q’uran yaani Laylat al-Qadr.

Katika siku hii ya 30 nitaungana pamoja na familia ya Marehemu Mbwana Masoud, majirani zake wakazi wa Kata ya Makurumla na wengine mtakaojumuika nami katika Iftar nyumbani kwa familia ya marehemu . Jioni tutaanza na tende na futari itafuata baada ya swala ya maghrib.

Marehemu Mbwana Masoud alikuwa ni mmoja wa wanachama wa CHADEMA walijitolea kusafiri kwenda Igunga kwa ajili ya kuwa wakala kwenye uchaguzi uliofanyika tarehe 2 Oktoba 2011.


Marehemu alitoweka katika mazingira ya kutatanisha wakati zoezi la kusambaza mawakala kwenye vituo likiendelea.

Baada ya jitihada za viongozi wa chama kumtafuta marehemu kushindikana nilitoa taarifa polisi tarehe 3 Oktoba 2011 na kufungua jalada RB/748/2011.

Tarehe 9 Oktoba 2011 wananchi wilayani Igunga walikuta mwili wa marehemu ukiwa porini katika eneo ambalo linajulikana zaidi kama msitu wa magereza.

Siku hiyo hiyo, nilitembelea nyumbani kwa marehemu katika mtaa wa Kwa Jongo Kata ya Makurumla kuifariji familia ya marehemu na kukubaliana na ndugu wa marehemu kutuma wawakilishi wa chama na familia kwenda Igunga kuhakiki mwili uliopatikana.

Tarehe 10 Oktoba 2011 wawakilishi wa familia wakiwa pamoja na mwakilishi wa chama walishuhudia mwili husika na kuthibitisha kuwa ni wa marehemu Mbwana Masoud.

Tarehe 11 Oktoba 2011 mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi wa kidaktari (post mortem) kuweza kubaini chanzo cha kifo na ripoti wamepatiwa jeshi la polisi. Mazingira ya kifo chake na uchunguzi wake yaliashiria kwamba marehemu aliuwawa.

Mpaka sasa, zaidi ya mwaka mmoja na miezi nane jeshi la polisi halijatoa taarifa yoyote kwa umma juu ya uchunguzi walioufanya wala hakuna mtu yoyote aliyekamatwa kwa kuhusika na kifo hicho.

Marehemu ameacha mzazi na mtoto ambao wanahitaji upendo na mshikamano wetu kila tunapopata nafasi.

Ramadan ni mwezi wa kufunga, kujinyima, kuswali, tafakuri ya kiroho na kutenda yaliyo mema. Kati ya matendo hayo ni pamoja na kuwajali maskini au wenye madhila mbalimbali. Kuwajali huko ni kwa ukarimu wa hiyari (sadaqah) au wa lazima (zakaat); shirikiana nasi kwa hali na mali kuikirimu familia ya Marehemu Mbwana Masoud.

Kwa wale ambao mtapenda kufuturisha na kufuturu pamoja nasi katika mjumuiko huo wa kijamii naomba muwasiliane na Katibu Msaidizi Ofisi ya Mbunge Ubungo Aziz Himbuka 0784379542 au 0715379542 kwa maelezo zaidi na maelekezo ya ziada.

Ramadan Kareem.

No comments: