Thursday, August 8, 2013

Kwa mkazi wa Kisopwa, Sinza, Manzese, Mbezi Makabe, Malambamawili, Mshikamano au Msigani; naomba usome hapa na kunipa mrejesho juu ya ardhi na mipango miji

Tarehe 12 Julai 2012 katika mchango wangu bungeni ikiwa ni sehemu ya wajibu wa kuwawakilisha wananchi na kuisimamia Serikali niliitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na mambo mengine:

Itatue mgogoro kati ya Manispaa ya Kinondoni na Halmashauri ya Kisarawe kuhusu wananchi wa Kisopwa na Mloganzila kuitwa kwamba wako Kisarawe badala ya Kinondoni.

Ichukue hatua juu ya maeneo ya wazi/umma yaliyovamiwa katika kata ya Sinza ambapo mabango yamewekwa, muda wa notisi umeisha lakini majengo bado yapo.

Imtaje wazi mwendelezaji mwenza wa Mji wa kiungani (satellite town) wa Luguruni, masharti ya mkataba na lini uendelezaji unaanza.

Itoe nakala ya mipango ya uendelezaji upya kata ya Manzese.

Iharakishe mipango ya uhakiki na urasimamishaji katika maeneo ya Mbezi Makabe, Malamba Mawili, Mshikamano na Msigani.

Mwaka mmoja umepita, kuna mambo nimepewa na majibu na kazi imefanyika na kuna masuala bado.

Kwa kuwa sasa nimeteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira nina nafasi nzuri zaidi ya ‘kuzibana’ mamlaka husika.

Naomba hali halisi ya sasa toka kwa wakazi wa Kisopwa, Sinza, Manzese, Mbezi Makabe, Malambamawili, Mshikamano na Msigani ili niweze kuendelea kuishauri na kuisimamia Serikali kuwezesha maendeleo.

Niandikie kwa kifupi kupitia ukurasa huu au kwa kina kupitia mbungeubungo@gmail.com

AMUA: Maslahi ya Umma Kwanza.

No comments: