Thursday, August 8, 2013

Mkazi wa Mabibo na maeneo jirani nakutaarifu kuwa nitahutubia mkutano wa hadhara kwenye eneo la Sahara leo siku ya 8/8 kuanzia saa 9 alasiri mpaka 11 jioni ulioandaliwa na chama. Njoo na waalike na wengine.

Mkutano huo una malengo matatu: Mosi; kuwasilisha mrejesho wa kazi jimboni za utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyogharamiwa na Mfuko wa Jimbo katika maeneo yenu.

Pili; nitafanya kazi ya kuuchambua mchakato wa mabadiliko ya katiba unaoendelea ikiwemo kuhusu rasimu ya katiba mpya.

Tatu; kupokea maoni/mapendekezo ya masuala muhimu ya kuyazingatia katika kazi ya kuwawakilisha wananchi kwenye vikao vya kamati za Bunge vinavyoanza wiki ijayo na Mkutano wa Bunge unaoanza mwishoni mwa mwezi huu.

Itakumbukwa kwamba tarehe 21 Julai 2013 nilitaka kutimiza azma hiyo kwenye eneo tajwa lakini Jeshi la Polisi lilizuia mkutano kwa maelezo yasiyokuwa ya kweli kwamba kulikuwa na ziara ya Makamu wa Rais katika Jimbo la Ubungo.

(Msaidizi katika Ofisi yangu ameeleza hapa kwa kirefu: http://www.youtube.com/watch?v=VyHF5O-P-Vk&feature=c4-overview&list=UUs0TcFkgqs2OYd6x5E68nhg ).

Na kwamba hawakuwa na askari wa kutosha wa kulinda mkutano (lakini walikuwa na askari na silaha za ziada za kuzuia mkutano).

Itakumbukwa pia katika mkutano huo nikiwa jirani na gari la polisi nikizungumza na bomu la machozi lilifyatuka kutoka kwenye gari hilo (Mungu ndiye Mlinzi) likapita na kwenda kujeruhi mwananchi mmoja aliyesimama mbali.

(Unaweza kusikiliza ushuhuda wake hapa: http://www.youtube.com/watch?v=SBu5P8cG1gE&feature=c4-overview&list=UUs0TcFkgqs2OYd6x5E68nhg ).

Polisi walisema bomu hilo lilipuka kwa bahati mbaya , hakuna aliyejeruhiwa na ni bomu lisilokuwa na madhara! (Tukumbuke Mwangosi aliuwawa kwa bomu la machozi, Ali Singano Zona aliuwawa kwa ‘kitu kizito kinachoruka’).

Nimerejea yaliyojiri sio kwa dhamira ya kuwapa hofu ya kuhudhuria mikutano bali kwa dhima ya kuwapa dira kwamba huku tukichukua hatua za kudhibiti hali hii, hatupaswi kukwepa wajibu wetu wa kikatiba, kidemokrasia na kimaendeleo.

Milipuko ya mabomu imewahi kutokea pia katika makanisa na misikiti iwe hapa nchini au nchi nyingine; lakini haijawahi kufanya watu kuacha kukutana kwa sala na swala.

Hivyo hivyo, matukio yanayojitokeza kwenye shughuli halali za kisiasa zinazofanywa na CHADEMA, viongozi na wanachama wake yasitusahaulishe maneno ya Mwalimu Nyerere kwamba ili nchi iendelee inahitaji pamoja na mambo mengine; siasa safi.

Tusishiriki siasa chafu za uoga, uongo, ubaguzi, unyama na ufisadi. Tushiriki kwenye siasa safi za ujasiri, ukweli, umoja, utu na uadilifu. 

Kwa maelezo au maelekezo kuhusu eneo la mkutano huo wasiliana na Mwenyekiti wa CHADEMA Kata ya Mabibo Omar Pilingu 0653025322. 

AMUA: Maslahi ya Umma Kwanza.

No comments: