Tuesday, May 4, 2010

Rais Kikwete na Wafanyakazi

Madai ya wafanyakazi kutaka nyongeza ya mshahara yalianza muda mrefu, kiwango hicho ambazo Rais Kikwete amekitaja leo kwa dhihaka kilianza kuzungumziwa toka mwaka 2007; ni hatua gani serikali yake ilichukua toka wakati huo mpaka wakati huu?
Hotuba ya Rais imenifanya nikumbuke makala hii ambayo niliindika mwaka 2007: http://www.chadema.or.tz/makala/makala.php?id=51

Katika makala hiyo nilinukuu kipande cha hotuba ya Nyerere ambacho ni muhimu nikakirejea hivi sasa katika muktadha wa Hotuba ya Kikwete.
Mwalimu Nyerere yeye alikabiliana moja kwa moja na wahuhusika na kuwaeleza: “Mna haki mnapozungumzia mishahara…..mishahara yetu ipo juu sana. Mnataka niipunguze? (makofi)…..mnataka nianzie na mshahara wangu? Ndio, naanza kuukata wa kwangu (vilio vya ‘hapana’). Nitapunguuza hii mishahara katika nchi hii. Wangu naukata kwa asilimia ishirini kuanzia sasa…..hii mishahara hii. Hii mishahara ndio inajenga huu mtazamo kwa wasomi, wote kabisa. Mimi na wewe. Tuko katika tabaka la wanyonyaji. Niko katika tabaka lenu. Ambapo nafikiri paundi mia tatu na themanini kwa mwaka (kiwango cha chini cha mshahara uliokuwa ukilipwa katika Jeshi la Kujenga Taifa) ni kambi ya gereza, ni kufanyishwa kazi kwa shuruti. Tuko katika tabaka la juu la wanyonyaji. Je hiki ndicho ambacho taifa letu kilipigania? Je hiki ndicho tulichokihangaikia? Ili tuendeleze tabaka la juu la wanyonyaji?....mko sawa, mishahara ipo juu sana. Kila mtu katika nchi hii anahitaji paundi ya ziada. Kila mtu isipokuwa mkulima masikini. Anawezaje kutaka? Haijui lugha…je ni nchi ya namna gani tunajenga?” (tafsiri yangu toka nukuu ya hotuba ya kingereza ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliitoa papo kwa papo akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Dar es Salaam baada ya maandamano ya wanafunzi Oktoba mwaka 1966)
Nyerere wakati huo alikwenda kuihutubia hadhira muafaka kwa suala alilolizungumzia, lakini kwa Kikwete yeye alikwenda kuwahutubia wazee na kuhusu ‘wafanyakazi’; je, alikuwa anapeleka mashtaka au alikuwa anatafuta kupigiwa makofi na hadhira isiyohusika ama ni ishara ya hofu ya kuogopa kukabiliana na wafanyakazi ana kwa ana?
Kuhusu Hotuba la Rais kusema kwamba mgomo ni batili anapewa taarifa nusu nusu au anapotoshwa ama ameamua kuupotosha umma. Ni vizuri serikali ikarejea na kukumbuka kuwa kusudio la mgomo lilitolewa siku nyingi nyuma kama sheria inavyohitaji; na wafanyakazi walieleza wazi kwamba walirejea kwenye majadiliano kwa maombi ya umma huku kusudio lao likiwepo pale pale. Hivyo, ni muhimu serikali ikaepusha mgomo kwa kushughulikia madai ya msingi ya wafanyakazi ambayo ni nyongeza ya mshahara hususani kima cha chini, punguzo la makato ya kodi na uboreshaji wa pensheni wakati wa kustaafu. Nilisoma tangazo la baraza husika ambalo limeshapwa na serikali katika magazeti mbalimbali hivi karibuni lilieleza bayana kwamba katika suala la kiwango cha kima cha chini 'wamekubaliana kutokukubaliana'; hivyo nimeshangazwa na kauli ya Rais Kikwete ya kwamba majadiliano yalifikia makubaliano kuhusu kiwango.

Tafsiri ya matukio haya ni ama kuna ufa mkali ndani ya serikali ama serikali imekerwa na kutoalikwa Mei Mosi huku ikijaribu kutumia kila mbinu kuficha aibu ya mgomo wa wafanyakazi wakati nchi ikiwa mwenyeji wa World Economic Forum-Africa(mbinu waliyoitumia kupanda miti mikubwa ya haraka haraka along Sam Nujoma Road).

Lakini naamini Rais anatambua kwamba watu wachache wanaweza kudanganywa kwa muda mchache, lakini sio watu watu wakati wote. Jaribio la hotuba ya Rais kuwatweza viongozi wafanyakazi linaweza likaishia kuwakweza zaidi, jaribio la kuwachangonanisha wafanyakazi kuwa wanataka mishahara mikubwa wakati serikali inahitaji fedha za kutoa huduma kwa jamii ili wananchi wawajie juu wafanyakazi kuwa wanajipendelea nalo limeelekea kushindwa. Jaribu la kuwachonganisha wafanyakazi kwa wafanyakazi, wafanyabiashara kwa wafanyakazi( kwa kutumia mifano ya mwenye baa na mifano ya house girl) nalo limeelekea kupuuzwa. Taasisi ya Urais sio idara ya propaganda za kutumia kejeli ama uchonganishi; Rais alipaswa kujenga hoja, kutoa matumaini na kutoa uongozi mbadala.

Hasira alizozionyesha kwa TUCTA ndio amekuwa amezionyesha kwa kiwango hicho hicho kwa mafisadi, na nguvu hizo hizo za kuzima hoja angekuwa amezitumia kwenye kutoa uongozi bora na kusimamia vizuri rasilimali za taifa mapato ya serikali yangewezesha kuwa na nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi na ukuaji wa uchumi ungewezesha hata kukuka kwa kipato katika sekta binafsi huku mfumuko wa bei ungedhibitiwa kwa kiwango cha kuridhisha. Wakati wafanyakazi wanaendelea kutozwa kodi kubwa(dai ambalo Rais hakulizungumzia), ni serikali yake hii ambayo iko mstari wa mbele kutoa katika mazingira ya utata misamaha mikubwa ya kodi.

Kama divide and rule hii ikiindelea kwa kiwango cha wafanyakazi kushindwa kushikamana, bado kila mmoja anayo fursa ya kugoma kumpa kura (kwanza ameshatangaza mwenyewe kuwa kura hazitaki). Upo msemo kwamba madaraka hulevya, na madaraka zaidi hulevya zaidi; unapokuwa na taifa lenye hodhi (monopoly) ya chama kimoja katika vyombo vya maamuzi; si ajabu kupata kauli za namna hii. Hii ndio athari ya kura zilizoitwa za mafiga matatu; lakini ipo fursa bado ya kubadili mfumo wa utawala ili tuwe na uwajibikaji wa kutosha si kwenye sererikali tu, hata kwenye taasisi zingine ikiwemo vyama vya wafanyakazi vyenyewe.

Kwa walio nje ya ajira zenye malipo duni suala hili wanaweza wakaona haliwahusu, lakini ukweli ni kuwa kuna uhusiano mkubwa katika ya ubovu wa huduma tunazozipata kwenye sekta mbalimbali na hali duni katika sekta hizo; hili ni bomu la wakati. Wafanyakazi wa Tanzania wamekuwa wawafanyi migomo rasmi kama nchi nyingine duniani, lakini aina ya mgomo unaoendelea chini kwa chini nchini ni mbaya zaidi kwa mustakabali wa nchi yetu. Tanzania kuna mgomo wa kutokuwajibika, katika hususani katika utumishi wa umma; wapo wanaokwenda kazini mwaka mzima lakini wanafanya kazi masaa machache au siku chache; muda mwingine kwenye warsha/semina kufidia kipato duni wanachopata ama muda mwingi zaidi kwenye shughuli zao binafsi. Mfano; walimu wenye wanaofundisha masomo ya ziada (tuition) ama kufanya biashara za visheti kwa wanafunzi shuleni; ama daktari anayetumia muda mwingi zaidi kwenye shughuli binafsi kuliko ndani ya hospitali ya umma, sasa 'consultancy' ndani ya serikali kwa serikali ndio zimekuwa utamaduni wa kawaida.

Rais atangaze mshahara wake hadharani na atueleze baraza lake la mawaziri limeshughulikiaje madai makuu matatu ya wafanyakazi toka aingine madarakani mwaka 2005 badala ya kukimbilia kuwapa jina baya viongozi wa wafanyakazi kuwa 'wanatumiwa'. Kama kweli wanatumiwa atueleze wanatumiwa na nani kwa kwanini? Na yeye na serikali yake waulizwe 'wanatumiwa na nani' au wanamtumikia nani?

No comments: