Waziri Mkuu,Mizengo Pinda, ametakiwa kutoa tamko ikiwa ofisi yake kupitia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imeamua kuzigawa kata na tarafa za wilaya ya Kinondoni jijini Dares Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Kinondoni katika kanda maalum ya Dar es Salaam, John Mnyika, alisema hayo jana katika taarifa yake kwa Nipashe.
“Ni muhimu kufanya hivyo sasa ili kama kuna kata mpya zinaundwa vyama vya siasa viweze kujiandaa kwa uchaguzi na wagombea waweze kutangaza nia,” alisema.
Mnyika alisema inapaswa kuzingatiwa kwamba kwa mujibu wa sheria, wakati mamlaka ya kugawa majimbo yako chini ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), mgawanyo wa kata uko Tamisemi.
“Tume imeshatangaza mgawo wa majimbo lakini Tamisemi haijatangaza hadharani kama kuna kata imezigawa au la kwenye halmashauri ya Kinondoni,” alisema.
Kwa mujibu wa Mnyika, Oktoba 2008 baadhi ya wilaya ikiwemo Kinondoni, ziliwasilisha mapendekezo ya mgawo wa kata na tarafa kwa Tamisemi.
Alisema Mei na Desemba mwaka jana, halmashauri ya Kinondoni ilipitisha tena mapendekezo hayo yaliyopitishwa na vikao vya mkoa Januari mwaka huu.
Mnyika alisema kwa mujibu wa muundo wa sasa wa serikali, pamoja na kuwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Celina Kombani, mwenye dhamana ya kutoa tamko hilo ni Waziri Mkuu akiwa mwenye dhamana.
Alidai kuwa kwa upande wa Kinondoni, mapendekezo yaliyopitishwa na Baraza la Madiwani na kuwasilishwa Tamisemi miezi kadhaa iliyopita, yanataka kuundwa kata mpya saba na tarafa kuongezwa kutoka nne mpaka saba.
“Haya ndiyo madhara ya sheria kutoa mamlaka kwa kiongozi wa serikali ambaye chama chake na yeye mwenyewe ni wagombea kupanga taratibu nyeti zenye athari za uchaguzi kama mipaka ya kata,” alisema.
Mnyika alisema ukimya wa Tamisemi kuhusu suala hilo unaweza kuibua hisia za kuwepo hujuma zinazopangwa kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana, na kwamba suluhu pekee ni kutolewa kwa tamko la Waziri Mkuu.
Jitihada za kumpata Kombani kupitia simu yake ya mkononi jana, ili atoe ufafanuzi kuhusu suala hilo, zilishindikana kutokana na kuita pasipo kupokewa.
CHANZO: NIPASHE(Tarehe 10 Mei 2010)
No comments:
Post a Comment