Tuesday, May 11, 2010

Ndoa sio fasheni

Ndoa si msukumo rika, wala kufuata mila,
Ndoa ni kukubalika, bila kufanyiwa hila,
Ndoa si kuhangaika, ili kulipa fadhila,
Ndoa ikikamilika, hutayapata madhila.

Ndoa si kuwa na gari, wala kupanda daraja,
Ndoa isiwe kamari, bali jambo la faraja,
Ndoa isiwe kwa amri, ila ni kuwa wamoja,
Ndoa haitokani na umri, bali nia ya pamoja.

Ndoa sio maigizo, haimei ka uyoga,
Ndoa isiwe likizo, ya kuanza kujikoga,
Ndoa sio bambikizo, hivyo isije kwa woga,
Ndoa ikiwa agizo, kwamwe haiwezi noga.

Ndoa suala la hiyari, si kupigiwa zumari,
Ndoa si kulipa mahari, bali ni kuwa tayari,
Ndoa inakuwa shwari, ifungwapo bila shari,
Ndoa maisha ya heri, yasiyotaka kwaheri

(JJ-8 Mei, 2010; Dar es Salaam, Tunu kwa makapera)

No comments: