Monday, May 17, 2010

Kikwete Abanwa

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemtaka Rais Jakaya Kikwete akanushe kauli ya kubariki rushwa katika uchaguzi, vinginevyo chama hicho kitamuumbua.
Mkurugenzi wa Vijana wa CHADEMA, John Mnyika, alitoa kauli hiyo jana alipokuwa anachukua fomu ya kugombea ubunge wa Ubungo; akasema kitendo cha Rais Kikwete kutetea rushwa kwa kisingizio cha takrima, ni ishara kuwa hakuwa na dhamira ya kweli ya kudhibiti matumizi makubwa ya fedha katika uchaguzi.

Mnyika alisema kuwa Rais Kikwete asipokanusha kauli yake hiyo, aliyoitoa Ijumaa wiki iliyopita mbele ya viongozi wa dini, atakuwa amelithibitishia taifa kuwa haheshimu utawala wa sheria.

Rais Kikwete aliwaambia viongozi wa dini kuwa takrima haikwepeki katika uchaguzi, licha ya uamuzi wa mahakama kuu iliyofuta vifungu vya sheria vilivyokuwa vinatetea takrima katika hukumu yake ya Aprili 24, 2006.

Akihutubia wananchi waliojitokeza kushuhudia akichukua fomu ya kugombea ubunge jana, Mnyika, alisema: “Wananchi wa Ubungo na Watanzania kwa ujumla puuzeni kauli za wanasiasa walioshindwa kuongoza nchi vizuri na kutumbukiza nchi katika katika mfumuko wa bei na kuzorotesha huduma za jamii huku wakiwaacha mafisadi wakivuna mamilioni ya fedha za umma.”

Alisema kauli ya Rais Kikwete ni kinyume cha sheria maana inachochea rushwa kwenye uchaguzi.

Mnyika alichukua fomu za kuwania ubunge katika ofisi za chama hicho jimbo la Ubungo na kukabidhiwa fomu hizo na Katibu wa CHADEMA Jimbo la Ubungo, Nasor Balozi.

Aidha, alisema amechukua fomu ya CHADEMA kwa kuwa anaamini ni chama mbadala na tumaini jimpya la Watanzania.

“Nachukua fomu kugombea ubunge kwa lengo la kushiriki katika kuleta mabadiliko ya kweli kwenye jimbo letu na taifa kwa ujumla kupitia siasa safi na uongozi.

“Nachukua fomu ya kugombea kwa lengo la kuchangia katika maendeleo ya nchi kwa kuondoa hodhi na nguvu ya chama kimoja bungeni na kwenye baraza la madiwani ambayo imesababisha kukosekana kwa uwajibikaji na hivyo wananchi kubaki na kero mbalimbali.

“Mimi naamini mbunge ni mwakilishi na mtumishi wa wananchi wenzake, hivyo pamoja na kuwa ninayo maadili na maono ya nini nakusudia kufanya natambua umuhimu wa kusikiliza. Sikubaliani na wanasiasa wanaopenda kusikilizwa badala ya kusikiliza, hivyo kabla sijatoa ilani yangu ya uchaguzi na ahadi zangu kwa wapigakura na wananchi kwa ujumla ningependa kusikiliza kwanza kutoka kwao,” alisema Mnyika.

Pamoja na hayo, Mnyika aliwahimiza watu wengine kujitokeza kugombea udiwani jimbo la Ubungo, ili halmashauri ya Kinondoni iwe na madiwani wa vyama mchanganyiko, kwani sasa hivi Dar es Salaam nzima inaongozwa na chama kimoja, jambo linaloifanya idorore.

Chanzo: Betty Kagonga- Tanzania Daima: http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=15748

No comments: