Thursday, May 13, 2010

Maadili ya Uchaguzi wa Urais, Ubunge na Udiwani

Tutafakari kuhusu maadili ya Uchaguzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2010. Izingatiwe kuwa Kanuni na taratibu zinazosimamia kampeni za uchaguzi Tanzania zinafafanuliwa katika sehemu ya VI ya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 kifungu cha 51 (1-6). Hata hivyo pamoja na uwepo wa sheria hiyo kuna mapungufu kadhaa ambayo yanapaswa kujadiliwa.

Ipo changamoto ya ukiukwaji wa maadili ya uchaguzi wakati wa kampeni. Kabla ya kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 kuanza maadili ya uchaguzi yalisainiwa na vyama mbalimbali vya siasa (isipokuwa DP na NCCR-Mageuzi), tume ya uchaguzi na serikali. Kampeni za uchaguzi ziligubikwa na matatizo kadhaa ikiwemo wagombea kutumia lugha za asili katika baadhi ya maeneo, ratiba za mikutano kutofuatwa katika baadhi ya maeneo, ufanyaji wa kampeni hasi (negative campaigns) nk. Mifano ya matukio ya namna hii ni mingi, mathalani katika tukio moja wafuasi wa CCM walipita na gari wakitangaza kwamba mgombea Urais na Ubunge wa CHADEMA wote wamejitoa na kujiunga na chama chao.(Kisa hiki kimesimuliwa kwa kina katika ripoti ya uchaguzi ya TEMCO).

Pia mikutano ya kampeni hususani katika ngazi za ubunge na udiwani ilitawaliwa na siasa za kushambulia haiba ikiwemo kwa njia ya matusi badala ya sera. Matukio mengine ya ukiukwaji wa maadili ambayo yameripotiwa katika baadhi ya maeneo ni pamoja na utoaji wa taarifa za upotoshaji, uharibifu wa alama za wagombea/vyama, udini/ukabila (katika baadhi ya maeneo) na vurugu (hususani maeneo yaliyokuwa na upinzani mkali).

Katika kipindi cha 2006 mpaka 2009, hali haikubadilika katika chaguzi za marudio hususani wa kampeni za ubunge. Mathalani, uchaguzi wa Kiteto (2007 ulihusisha Mbunge wa CCM, John Komba; kuvamia Mkutano wa CHADEMA, polisi walimshusha jukwaani baada ya shinikizo. Hata hivyo, hakuna hatua za msingi zilizochukuliwa hata baada ya CHADEMA kufungua jalada polisi la kosa la jinai. Pia katika uchaguzi huo, viongozi wa CHADEMA walipigwa na kujeruhiwa na polisi kwa kushirikiana na makada wa CCM. Katika uchaguzi wa Tarime (2008), kampeni zilihusisha baadhi ya Vyama kuhutubia jukwaani na kusambaza nyaraka zikiitaja CHADEMA na viongozi wake kama ‘genge la wauaji’ waliomuua Chacha Wangwe (Mungu Amlaze Mahali Pema). Hata hivyo, hakuna hatua zozote madhubuti zilizochukuliwa na Tume ya Uchaguzi ama Vyombo vya Dola hata baada ya kiongozi mmojawapo wa CHADEMA kushtaki suala hilo polisi na jalada la uchunguzi kufunguliwa. Pia kampeni zilihusisha baadhi ya viongozi wa vya upinzani kushambuliwa kwa mawe na baadhi ya wanachama wa CHADEMA kukatwa na mapanga. Kadhalika, jeshi la polisi liliwavamia, kuwapiga na kuwakamata viongozi wa CHADEMA pamoja na mgombea ubunge na mgombea udiwani. Matuko ya namna hiyo viongozi na makada wa CHADEMA kukatwa mapanga katika kampeni za uchaguzi wa marudio za ubunge katika majimbo ya Busanda na Biharamulo mwaka 2009; hakuna hatua za kisheria zilizochukuliwa mpaka sasa pamoja na majalada ya uchunguzi wa jinai kufunguliwa polisi.

Fungamano lililokuwepo wakati wa chama kimoja kati ya chama na dola limeendelea na linaendelea. Hali hii ya kuwa na ‘chama dola’ imekuwa ikitumika kuhujumu wapinzani nyakati za uchaguzi. Katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 palikuwa na fungamano la mara kwa mara kati ya chama kwa upande mmoja na serikali na dola kwa upande mwingine. Yalitolewa maelekezo na mengine ya wazi kabisa kutoka kwa viongozi wa CCM akiwemo Mwenyekiti (wakati huo akiwa pia Rais wa nchi) kwa viongozi wa serikali kwamba watumie nguvu zote ikiwemo za dola kuhakikisha upinzani haushindi katika maeneo yao. Hivyo viongozi wa serikali hususani wakuu wa mikoa, wilaya na watendaji wa kata walikuwa mstari wa mbele kwenye kampeni za chama tawala na mahali pengine kuvitumia hata vyombo vya dola. Hii ni changamoto ambayo marekebisho ya kisheria yanayokusudiwa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 yalipaswa kuishughulikia lakini hayajafanya hivyo, na tayari kuna wimbi la matumizi haya mabaya ya madaraka kuelekea uchaguzi mkuu.

Viongozi wa serikali waliokuwa na nafasi zao mathalani mawaziri waliendelea kuzitumikia nafasi hizo sanjari na kupigia kampeni chama tawala. Miradi mbalimbali ya maendeleo ilielekezwa kuzinduliwa ama kufunguliwa kipindi cha kampeni. Taasisi za umma zilitumika kupiga kampeni mathalani matangazo ya pongezi ya kulipia yalitolewa na taasisi hizi kwa wagombea wa CCM mara baada ya kuteuliwa ndani ya chama. Vyombo vya dola yakiwemo majeshi vilitumika kukandamiza upinzani hasa Zanzibar na maeneo yaliyokuwa na upinzani mkubwa bara. Hali haikuwa tofauti katika kipindi cha kati ya mwaka 2006 mpaka 2009. Hii ni changamoto ambazo marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi yaliyofanyika mwaka 2010 hayakuzingatia kwa CCM kutumia uwingi na hodhi(monopoly) bungeni kuyakataa. Tume ya Uchaguzi inakapokaa tena mwaka huu na vyama vya siasa kuandaa Maadili ya Uchaguzi kwa ajili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2010.

No comments: