MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amehimiza kupanuliwa kwa wigo wa bima na hifadhi ya jamii kwa kuwawezesha wananchi kukabiliana na athari za umaskini wa kipato na kuongeza ustawi.
Mnyika aliyasema hayo juzi alipowahutubia wanachama wa kikundi cha Kusaidiana Kilungule Darajani (KICHAKIDA), kilichopo Kata ya Kimara, Ubungo, ambapo alikizindua rasmi kikundi hicho na ofisi yao.
Alisema mifumo ya bima na hifadhi ya jamii (social security) inahudumia zaidi watu walio kwenye sekta rasmi na kuacha sehemu kubwa ya wananchi waliopo katika sekta isiyo rasmi, hivyo kuna haja ya kufanyika kwa mabadiliko na mifumo hiyo kurekebishwa.
“Bima na hifadhi ya jamii inahudumia zaidi watu walio kwenye sekta rasmi na kuacha sehemu kubwa ya wananchi walio kwenye sekta isiyo rasmi,” alisema Mnyika.
Aidha, aliwapongeza wananchi wa eneo hilo kwa kuanzisha kikundi hicho, kwani kinatoa baadhi ya huduma za msingi zinazopaswa kutolewa na mifumo rasmi ya bima au hifadhi ya jamii.
Kadhalika, mbunge huyo aliwataka wananchi wa Ubungo kuendelea kuunga mkono hoja ya kuandikwa kwa Katiba mpya na marekebisho ya kisheria ili pamoja na mambo mengine kuwepo kwa mifumo thabiti zaidi ya bima na hifadhi za kijamii kama suluhisho la kudumu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa KICHAKIDA, alimueleza mbunge huyo kwamba kikundi hicho kina wanachama 100 ambapo kinawahudumia wategemezi zaidi ya 500 wanaotoka kwenye kaya za wanachama hao katika matatizo ya kijamii kama maradhi, misiba na mikopo ya elimu.
Chanzo: Tanzania Daima (13/01/2011)
1 comment:
Mheshimiwa Mbunge hongera,
Nimependa kuona jinsi unavyojiweka karibu na wananchi. Kwa staili hiyo utawaweza watanzania. Nimeguswa na juhudi zako za kuhamasisha ujenzi wa ofisi. Ningekushauri kuwa kama kweli una dhamira ya kuleta utawala bora basi ni vyema uhakikishe kuwa angalau kila Kata inakuwa na Ofisi ambayo ina hadhi ya Ofisi.
Hili lifanyie kazi kwa kuwashirikisha wananchi kwani huwa wako tayari kujitolea ila wanashindwa kupata watu wanaowaamini. Wako watu wengi ambao wanaweza kkuchangia ujenzi au ukarabati wa ofisi hizo lakini uchama - uccm ulikuwa unakwamisha mambo.
Ipo haja pia ya kuhakikisha kuwa serikali za Mitaa katika Kata zote jimboni kwako zinaitisha ile mikutano ya hadhara ya wananchi kwa kuzingatia utaratibu kila miezi miwili ili wananchi wapate fursa ya kujadili maendeleo yao. Kama utaweza uwe unahudhuria mikutano hii basi hapo utakuwa unarahisisha mawasiliano na wananchi.
Mwisho nimalizie kwa kusema: HIVI HII NGUVU YA UMMA YA HUKO TUNISIA MMEISIKIA? HAPA KWETU KWANINI TUNASHINDWA KUWALAZIMISHA WATU KAMA AKINA MWEMA, NAHODHA NA ANDENGENYE KUBAKIA KATIKA VITI VYAO? NCHI HII HAITABADILIKA KWA MAJADILIANO YA MEZANI.
MUNGU IBARIKI TANZANIA
Post a Comment