Saturday, February 19, 2011

Hotuba yangu Bungeni katika Mkutano wa Pili

Mchango wangu wa papo kwa papo bungeni wakati wa hoja ya kujadili Hotuba ya Rais Kikwete ya kufungua bunge jipya. Mchango huu niliutoa tarehe 11 Februari 2011 katika kikao cha nne cha mkutano wa pili wa Bunge la kumi katika hotuba hii niliwashukuru wananchi na kuzungumzia suala la viongozi kuepuka kupandikiza mbegu ya udini, haja ya kukabaliana na mfumumo wa bei unaosababisha kupanda kwa gharama za maisha, suala la kufufua viwanda na jitihada za kukabiliana na matatizo ya maji katika jimbo la Ubungo.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Na kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kutoa mchango rasmi, nichukue fursa hii kupitia Bunge lako tukufu kuingiza kwenye historia ya Taifa hili kwamba safari yangu kufika hapa ilikuwa ndefu kidogo, ilianza mwaka 2005. Lakini, kwa sababu ya udhaifu wa mifumo yetu ya kikatiba na ya kisheria ya usimamizi wa haki, safari hii imekuwa ya miaka mitano na nimefika leo hapa kwa nguvu ya umma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kuwashukuru sana wazee wa Jimbo la Ubungo bila kujali tofauti za vyama, Jimbo lenye wakazi - wapiga kura 450,000 ambao waliona wanitume mtoto wao nije kuwawakilisha. Nawashukuru vile vile wakinamama wa Jimbo la Ubungo, wanawake ambao katika kipindi kigumu sana cha kampeni walikuwa wakiniombea kwa Mwenyezi Mungu na leo nimefika hapa salama. Lakini, zaidi niwashukuru vijana wenzangu wa Tanzania nzima na Jimbo la Ubungo, vijana wa mtaani, vijana wafanyakazi na vijana wa vyuo vikuu ambao walikuwa tayari kukesha kwa siku tatu kulinda ushindi mpaka tukatangazwa. Ahadi yangu kwao ni kuwatumikia katika kipindi cha miaka mitano cha utumishi wangu.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazungumza leo tukiwa wakati pekee sana kwenye historia ya Taifa letu. Tunazungumza ikiwa ni miezi michache kuelekea kuadhimisha miaka 50 toka Taifa letu lipate uhuru. Lakini tunazungumza wakati ambapo Taifa likikabiliwa na mgawo wa umeme miaka 50 baada ya uhuru, Taifa likikabiliwa na matokeo mabovu ya wanafunzi miaka 50 baada ya uhuru, Taifa likikabiliwa na kupanda kwa hali ya juu kwa gharama za maisha ambapo kunasababisha tishio la migomo mbalimbali. Migomo ya wanafunzi wa vyuo vikuu tunazungumza leo wakiwa wamerudishwa nyumbani kwenye vyuo mbalimbali, migomo ya wafanyakazi na mambo mengine yote haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo haya yangeweza kutupa sababu ya kukata tamaa. Lakini, mimi ninayo sababu ya kuwa na matumaini. Nina matumaini kwa sababu tupo kwenye chombo hiki na natarajia kwamba hatutaendekeza itikadi na maslahi ya vyama, badala yake tutasimamia maslahi ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na upungufu wake, Ibara ya 63 inazungumza kwamba hiki ndiyo chombo kikuu kwa niaba ya wananchi waliotutuma chenye wajibu wa kuishauri Serikali na kuisimamia Serikali. Kwa hiyo, naomba nieleweke tu hapa, tunapokosoa, tunapounga mkono, ni sehemu ya kuishauri Serikali, ni sehemu ya kuisimamia Serikali. Natarajia kwamba Wabunge kwa umoja wetu hatutajigeuza kuwa na jukumu la Serikali, badala yake tutaendelea kuwa na jukumu la kuisimamia Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwanza, mimi ningeomba niishauri Serikali kwa kweli. Ili tuweze kufika Desemba 9 tukiadhimisha uhuru tukiwa na sababu ya kuadhimisha uhuru kwa maana ya kusherehekea, lazima Serikali iamue kwa dhati, Bunge lijalo la mwezi Aprili, lilete mapendekezo ya msingi wakati tunatengeneza vipaumbele vya bajeti ya safari hii. Ni mambo gani ya haraka ambayo kama Taifa tunaweza tukafanya kwa umoja wetu, kwa makubaliano yetu ili ikifika Desemba, pamoja na yote yaliyojitokeza miaka 50 iliyopita, tuseme walau hapa tuna sababu ya kujivunia; na nitasema machache:- (Makofi)


[MHE. JOHN J. MNYIKA]

Mheshimiwa Spika, nimeisoma hotuba ya Rais na nitaichangia kwa uchache wa maneno. Rais amezungumza vipaumbele mbalimbali. Ukurasa wa 12 na 13 amegusia suala la umoja wa kitaifa na hili ni jambo ambalo hatupishani kwa sababu hata Ngao ya Taifa letu inasema Uhuru na Umoja. Lakini, kuna jambo moja mimi ningependa nitoe tahadhari, suala la udini. Hotuba ya Rais ukurasa 12 inazungumza kwamba Tanzania ni moja, watu hawabaguani, kwa hiyo Tanzania hakuna mgawanyiko hata wa kidini. Lakini ukurasa wa 13 unasema kuna mpasuko wa kidini. Mimi ningeomba vyombo vya Ulinzi na Usalama vikamshauri Rais kwamba kadri viongozi wa juu tutakavyoendelea kupiga kelele nyingi sana za udini, ndiyo kadri tunavyopandikiza mbegu ya udini kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuja kwenye kikao hiki, nimezunguka vijiweni, nimekaa vijiweni, Watanzania ni wamoja kweli kweli, tusije viongozi ndiyo tukasababisha mgawanyiko miongoni mwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichangie eneo lingine: Rais amezungumza kuhusu kukuza uchumi na ukurasa wa 15 amezungumzia suala la kupanda kwa bei ya mafuta n.k kwenye Soko la Dunia na chakula kama sehemu ya matatizo ya kimaisha ambayo yalitokea mwaka 2007. Mimi ningeomba tu Serikali ituletee taarifa Bungeni kuhusu hali halisi. Takwimu hapa kwa mujibu wa hotuba ya Rais inaonyesha kwamba mfumko wa bei ni asilimia 4.2. Wakati Rais anazungumza, bei ya sukari kilo moja ilikuwa shilingi 1200/=, leo tunazungumza kilo moja imepanda mpaka shilingi 2000/=. Gharama za maisha zinapanda kwa ari, kasi na nguvu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni vizuri Serikali ikatuletea pendekezo la namna gani Tanzania inakabiliana na tatizo hili la kupanda kwa gharama za maisha. Tunaweza kuwalaumu wanafunzi kwa nini wanagoma kwamba wanalipwa 5000/= lakini wanalalamika, huku bei ya chakula inapanda! Sasa kuwalaumu wafanyakazi kwa nini wanalalamika, wanataka kuandamana, bei ya umeme imepanda, kama hatutadhibiti kupanda kwa bei, tunatengeneza mgogoro kwenye Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais amezungumza kuhusu kufufua viwanda, mimi niseme tu kwamba kazi hii ni nzito, inahitaji vile vile kama Taifa tuzungumze hivyo viwanda vilivyokufa vilikufaje. Mimi pale Jimboni kwangu Ubungo kuna Kiwanda cha Urafiki ambacho Tanzania ilikuwa inamiliki mwanzoni, sasa hivi ina hisa 49 peke yake. Kiwanda kinaelekea kufa, uzalishaji sasa hivi ninavyozungumza, wafanyakazi wamepewa likizo, tena wamepewa likizo kwa asilimia 50 tu ya malipo. Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili la Urafiki nitaliletea maelezo kwa sababu ni suala la kina sana, kuuzwa kwa mitambo n.k. Nitawaletea maelezo.

Mheshimiwa Spika, lakini, itoshe tu niingie kwenye eneo la msingi ambalo ni kero kubwa sana kwa wananchi wa Ubungo, nayo ni maji. Mheshimiwa Rais, amezungumza kuhusu ongezeko la mgawo wa fedha za bajeti kwenye maji na amezungumza kuhusu Miradi ya Benki ya Dunia. Lakini, mimi nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Maji na nimwahidi tu kwamba tulifanya kongamano la maji tarehe 31 Ubungo, tukayajua matatizo na nitaleta taarifa kamili kwake kama ambavyo tumekubaliana na nashukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa ushirikiano. Tunahitaji, pamoja na mipango ya muda mrefu ya ujenzi wa mabwawa ya Kidunda, miradi ya Kimbiji, Mpera n.k. Mheshimiwa Spika, nashukuru! (Makofi)

1 comment:

Unknown said...

Pamoja na kwamba ndo ilikua mara yako ya kwanza kutoa hoja bungeni lkn inaonekana kama ulikua na uzoefu wa miaka 50 bungeni! Hongera sana Mh John Mnyika. Hotuba yako ilikua nzuri, kwakua fupi na ya kueleweka kwa uzito wa hoja na uandishi sanifu! Mungu azidi kukupa busara na uwezo wa kujiamini hasa ktk kufanya tafiti za kusaidia Watanzania!